Thursday 5 June 2014

UMUHIMU WA SWALA


Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wata‘ala), Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake. Swala na salamu zimuendee kipenzi cha ummah Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Ndugu wa kiislamu, kama tunavyofahamu kuwa swala ndio nguzo ya pili katika Uislamu na ni ibada iliyotiliwa mkazo na ni yenye umuhimu mkubwa kwetu sisi Waislamu, kwani ni ibada pekee ambayo Allah (subhanahu wata‘ala) hakuifaradhisha kwa kumletea wahyi tu Mtume wetu Muhammad kupitia Jibril (alayhi salam) bali alimuandalia safari maalum ya kiroho na kimwili ili kuweza kumkabidhi jukumu la ibada hii kama tunasoma katika kisa cha Israa na Miraj.

Ndugu wa kiislamu, maana ya swala kilugha ni dua kama ilivyokuja katika Quran pale Allah (subhanahu wata‘ala) aliposema:

“... na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao ...” [At-Tawbah 9 : 103].
Ama kisheria ni vitendo na kauli maalum zinazoanzwa kwa Takbir na kumaliza kwa salam.

Swala ni katika aina za ibada ambazo walifaradhishiwa Mitume yote iliyopita kwani ni ibada ambayo humkurubisha mja kwa Mola wake na humpa fursa ya kuzungumza na kueleza shida zake kwa Mola wake. Allah alimfaradhishia swala Nabii Mussa (alayhi salam) pale aliposema: “Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.” [Twaha 20 : 14].

Swala inayoswaliwa ndani ya wakati wake ndiyo ‘amali bora kuliko ‘amali zote kama alivyosema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) katika hadith iliyosimuliwa na Ibn Masoud (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nilimuuliza Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) ni ipi ‘amali iliyobora? Akasema: “Swala katika wakati wake” Nikasema kisha ipi? Akasema: “Kuwafanyia wema wazazi wawili” Nikasema kisha ipi? Akasema “Jihadi katika njia ya Allah”. Bukhary na Muslim.

Allah (subhanahu wata‘ala) humuwepesishia rizki zake mwenye kuswali, kwani yeye si muhitaji wa swala bali sisi ndio wahitaji. Na kwa kupitia swala Allah ameahidi kumruzuku kwa was‘a yule mwenye kuswali kama Anavyosema: “Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchaMungu.” [Taha 20 : 132].

Pia imethibiti katika hadithil Qudsi kuwa Allah (subhanahu wata‘ala) Amesema: “Ewe Mwanaadamu, kuwa tayari kutekeleza ibada zangu, nami nitajaza katika moyo wako utajiri, na nitauziba mlango wa ufakiri kwako, na kama hutafanya hivyo nitajaza shughuli katika moyo wako, na mlango wa ufakiri sitoufunga kwako.” Ahmad na Tirmidhy.

Ndugu wa kiislamu, Allah (subhanahu wata‘ala) akazidi kuonyesha umuhimu wa swala kwa kututaka sisi waja wake tushikamane nayo na tuihifadhi zaidi pale Aliposema: “Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).” [Al-Baqara 2 : 238].

Swala tano na Ijumaa mpaka Ijumaa hufuta dhambi ndogo zilizomo baina yao. Imesimuliwa na Ibn Masoud kuwa mtu mmoja alimbusu mwanamke na akaja kwa Mtume kumpa khabari hiyo (kwa kutaka kujua hukmu yake). Basi Allah (subhanahu wata‘ala) akateremsha “Na shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu” Akasema yule mtu: ni kwa ajili yangu mimi tu hili? Akasema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Ni kwa ajili ya ummah wangu wote.” Bukhary na Muslim.

Pia Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nimemsikia Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) Akisema: “Mnaonaje ikiwa mto (wa maji) upo chini ya mlango wa mmoja wenu naye akawa anakoga humo mara tano kwa siku jee utabakia uchafu katika mwili wake?” Wakasema (maswahaba): “Hautabakia uchafu katika mwili wake.” Akasema: “Huo ndio mfano wa swala tano, Allah hufuta madhambi yalipo baina yake.” Bukhary na Muslim.

Vile vile swala inayoswaliwa vilivyo humkataza mtu na mambo maovu na machafu na kumkurubisha katika rehma za Allah kama Anavyosema Allah katika Quran: “... na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. ...” [Al-Ankabut 29 : 45].

Ndugu wa kiislamu hayo ni katika baadhi tu ya fadhila za swala kwetu. Hivyo tujihimu katika kuitekeleza na kuisimamisha kisawa sawa kwani khasara iliyoje kwa mwenye kuacha swala! Swala ndiyo ‘amali ya kwanza mja atakayohesabiwa na kutengenea kwake ndiko kutakopelekea kutizamwa ‘amali zake nyengine la sivyo atakuwa mja huyo ni katika waliyohiliki ndani ya mashimo ya moto wa Jahannam (Allah atuhifadhi).

Pia kuacha swala kunampelekea mtu kuingia katika ukafiri kama ilivyothibiti hadithi kutoka kwa Buraydah (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Ahadi iliyopo baina yetu na baina yao (makafiri na wanafiq) ni swala, mwenye kuiacha hakika amekufuru.” Tirmidhy.

Na katika hadithi nyengine Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Hakika baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swala.” Muslim.

Hivyo ndugu wa kiislamu khassa wale waliokuwa hawatekelezi ibada ya swala, turudini haraka kwa Mola wetu  ili tuwe miongoni mwa waislamu na tuepukane na ukafiri na adhabu kali inayotusubiri siku ya Qiyama, kama Allah anavyotukhabarisha : “Khabari za wakosefu. Ni nini kilicho kupelekeni Motoni? Waseme: Hatukuwa miongoni mwa walio kuwa wakisali.” [Mudathir 74 : 41-43].

Ama kwa wale wenye tabia ya kuswali baadhi  ya vipindi na kuacha baadhi wajue kuwa hawajasalimika na adhabu za Allah, kwani Anasema: “Basi, ole wao wanao Sali. Ambao wanapuuza Sala zao.” [Al-Mauun 107 : 4-5].

Pia kuna baadhi ya ndugu zetu wanapofikishiwa ujumbe wa kutakiwa kuswali husema: “Nitaswali vipi hali ya kuwa mifuko yangu mitupu?” au “Nitaswali vipi na tonge haijaenda kinywani” kwa kumaanisha kuwa hawatoswali mpaka wapate mahitaji yao. Watu wa aina hii wajijue kuwa ni katika waliokhasirika khasara iliyokubwa kama anavyosema Allah: “Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.” [Hajj 22 : 11].

Tunamuomba Allah atujaalie tuweze kuisimamisha ibada hii na nyenginezo na atukubalie ibada zetu zote na atuwezeshe kuingia katika pepo yake kwa Rehma Zake. Amin.

2 comments:

  1. Mungu awalipe kila laherry kutukumbusha kilasiku mwenye masikiyo amesikiya

    ReplyDelete