Saturday 14 June 2014

NI UPI MOTO WA ALLAH-SEHEMU YA PILI

Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

AINA ZA ADHABU NDANI YA MOTO

Baada ya kutoka hukmu ya kila mmoja, watu wa motoni wataingizwa sehemu zao na kila mtu na namna yake ya kuingizwa. Allah ameeleza vipi wataingizwa watu wa motoni katika makaazi yao hayo. Wako watakaofungwa na minyororo na kutupwa jahannam, kama anavyosema katika suratul-Haaqah 30-32“Mkamateni na mfungeni. Kisha mtupeni motoni. Tena katika mnyororo wenye urefu wa dhiraa sabiini”. Na wako watakaokokotwa kifudifudi mpaka Jahannam,kama anavyosema Allah katika suratul-Qamar aya ya 48 “Siku watakayokokotwa kifudifudi (huku wakiambiwa)onjeni mguso wa jahannam”

.Na wako watakaochukuliwa kwa nywele za utosi na nyayo zao kama anavosema Allah katika suratul-Rahman aya ya 41 “Watajulikana waovu kwa alama zao,basi watakamatwa kwa nywele zao za utosi na nyayo zao (watumbukizwe jahannam)”.

Na humo ndani ya jahannam watakutana na adhabu mbalimbali, ikiwemo kupigwa marungu ya chuma ya moto amesema Allah “Na kwa ajili yao (yatakuwepo)marungu ya chuma”(Hajj: 21). Pia wapo watakaobabuliwa nyuso zao na moto, kama anavyosema Allah katika suratul-muuminuun aya ya 104 na Maarij 16. Na Allah anasema kua kila zinapoungua ngozi zao tutawabadilishia ngozi nyengine badala ya zile ili wapate kuwonja adhabu.(Nisai : 56). Pia ndani ya jahannam kuna nyoka ambae akimgonga mtu basi machungu yake hayamalizki muda wa miaka 40.(hadith hasan imepokelewa na Imam Ahmad).

Adhabu za jahannam ni nyingi, na ni adhabu juu ya adhabu, kiasi kwamba watu wake watatamani kufa, na watanadi kumwambia mshika funguo za Moto Maalik “Ewe Maalik na atufishe Mola wako (tumalizane na hii adhabu).watajibiwa bila shaka mtaka humohumo” (Zukhruf 77).

Na katika aya nyengine wataambiwa nyamazeni na wala msizungumze nami . Na katika hadith sahihi inayosimuliwa na Abdullah bin Qays kua “Watalia watu wa jahannam mpaka machozi yao yataisha, na baadae ianze kutoka damu kiasi kwamba lau kama italetwa jahazi basi itatembea juu ya damu hiyo.” Subhanallah hakuna anaeweza kustahmili adhabu za jahannam ata kwa sekunde moja.Mtu mwenye adhabu ya chini katika jahannam ,kama hadith ilokuwemo katika Riyadhu-Swalihin walowafikiana bukhari na Muslim kua adhabu yake ni kua ataekewa vijiwe vya moto chini ya viatu vyake na utatokota ubongo kutokana na joto la moto wa chini ya viatu” basi ni vipi kwa adhabu ya juu? Na ni vipi kwa wale wanafik watakaokua katika daraja ya chini ya moto? (Allah atuhifadhi) .

CHAKULA CHA WATU WA MOTONI

Vyakula vyao vimetajwa kua ni:
1-Dhari’i: Hii ni miba ichomayo koo na imetajwa katika Suratul Ghaashiyah aya ya 6.

2-Ghisliin: Amesema Allah kuhusiana na Ghisliin “ Hawatokua na chakula humo ila Usaha”. Suratu Haaqah aya ya 36. Hivyo ghisliin ni usaha ambao utawatoka wenyewe watu wa motoni kutokana na adhabu kali na kisha watakula usaha wao huo.

3-Zaquum: Ni mti mchungu huu ambao unaota katika jahannam, umoto wake umefananishwa na shaba iloyayushwa ambayo itachemkia tumboni. Matunda yake yanatisha kama vichwa vya mashetani. Umetajwa katika suratu-Dukhaan aya ya 43-45 na Suratu Swaaffaat aya 62-66 na suratul_waaqiah 52-53.

4-Ghuswah: Ni aina nyengine ya chakula cha watu wa motoni. Allah amekitaja katika suratul-Muzammil “Na chakula kikwamacho na adhabu iumizayo” 13.

D :VINYWAJI VYA WATU WA MOTONI

Kabla ya kutaja vinywaji vya watu wa motoni, tukumbuke kua baada ya watu wa motoni kuingizwa jahannam watashikwa na kiu kali kutokana na joto la jahannam, hivyo watawapigia kelele watu wa peponi na kuwaambia kama anavyotusimulia Allah “Watu wa motoni watawanadia watu wa peponi: Tumiminieni maji au kile alichokuruzukuni Allah watasema (watu wa peponi kuwajibu):Hakika Allah ameviharamisha kwa kwa makafiri. Ambao waliifanya dini yao kua ni upuuzi na mchezo,na yakawadanganya maisha ya dunia. Basi leo tutawasahau (na kuwaacha humohumo motoni)kama walivyosahau mkutano wa siku hii” (Aaraf). Baada ya joto la jahannam kuzidi wataoneshwa maji yachemkayo, kisha watayaendea lakini hawatoweza kunywa kwa umoto wake, watataka kurudi tena mahali walipokua na wakirudi, watazidiwa na kiu watataka kwenda kwenye yale maji na huo ndo utakua mzunguko wao. Amesema Allah katika suratu Rahman 44 “Watakua wakizunguka baina ya (Jahannam)na baina ya maji ya moto yachemkayo”. Amesema Allah kuhusiana na maji hayo katika suratu-Muhammad 15“……na kunyweshwa maji yachemkayo yatakayokata chango zao” 15 na wapo ambao maji hayo yatatoa ngozi zao na yalokuwemo kwenye matumbo yao kama anavyosema Allah katika suratul-hajj.
Ama vinywaji vyengine ni:

1- Maji ya usaha. Amesema Allah katika suratu –Ibrahiim aya ya 16-17“ Na atanyeshwa humo maji ya usaha. Awe anayagugumiza na asiweze kuyameza. Na mauti yatamjia kutoka kila mahali na hatokufa”. 16-17.

2- Maji ya shaba. Amesema Allah kuhusiana na maji haya katka suratul-Kahfi “ Na watakapoomba msaada (kutokana na kiu kali)watapewa maji kama ya shaba iliyoyayushwa itakayounguza nyuso zao, kinywaji kibaya kilioje hicho”

Ama kwa upande wa hadithi: Inasimuliwa kua watu wa jahannam wakiyasogelea maji kwa ajili ya kuyanywa basi itatoka ngozi ya uso na kuingia katika chombo chenye maji yale kutokana na shida ya vuke la moto.

MAVAZI YA WATU WA MOTONI

Motoni watu watavishwa Qatirani, nazo ni nguo za Lami. Amesema Allah katka Suratu-Ibrahiim aya ya 50 “Nguo zao zitakua ni lami,na moto utazijia nyuso zao (uzibabue)”. Na maana nyengine ya Qatirani ni shaba iloyounguzwa mpaka ikapiga wekundu.

ADHABU NYENGINEZO ZA WATU WA MOTONI

1- Kutomuona Allah: Watu wa motoni hawatomuoni muumba wao, Kwani Allah ni nuru na nuru yake haionekani na waovu. Amesema Allah katika suratu-Mutaffin “Sivyo hivyo,siku hiyo kwa Mola wao watazuiwa (kumuona). Kama ilivyokua watu wema moja ya starehe zao ni Kumuona Allah basi na watu wa motoni moja ya adhabu yao ni kutomuona Allah.

2- Kuishi Milele: Kama tulivyoona katika makala kuhusu pepo ya Allah, kua baada ya watu kuingia sehemu zao stahiki, yataletwa mauti kwa sura ya kondoo na kuchinjwa kuonesha kua hakuna kufa katika jahannam,na inatosha adhabu kua adhabu kwa kitendo chake kua ni milele. Amesema Allah “Kisha hatokufa humo wala kuwa hai” A’laa 13. Basi itakua ni majuto kwa watu wa jahannam kwani wajua hawatoki tena.

UTANABAHISHO

Ili Mja aweze kuepukana na jahannam, ni lazima mezani yake ya mema izidi ya maovu. Kila binaadamu ni mkosa, lakini mbora wa wakosaji ni yule anaetubia. Ni muhimu kuzidisha kuleta istighfaar hasa katika mwezi wa Ramadhan, ili tukienda kwa Allah iwe tumesamehewa. Allah anasamehe makosa yote madamu yataletewa toba yake ya kweli kabla ya roho kufika shingoni na jua kuchomoza magharibi, na kuna makosa baada ya kufa Allah hayatoyasamehe na adhabu yake ni kali. Pia makosa ambayo Mtume ameyataja kua ni yenye kuporomosha amali haya ni makosa yaloandaliwa adhabu kali na moja wapo ni Kumshirikisha Allah. Amesema Allah katika suratul Maidah 72 “…hakika atakaemshirikisha Allah basi Allah amemharamishia pepo, na makaazi yake ni motoni..”

Jengine ni Kuua, amesema Allah katika suratu Nisai 93 “Na mwenye kumuua muislamu kwa kukusudia, basi malipo yake ni jahannam,atakaa humo milele,na Allah amemghadhibikia na amemlaani na amaemwandalia adhabu kali”

Jengine ni Kula mali ya yatima, Amesema Allah “Hakika wale wanaokula mali ya mayatima kwa dhulma bila shaka wanakula moto matumboni mwao na wataingia katika moto uwakao”.

Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasalam mambo yatakayowaingiza watu kwa wingi jahannam ni ulimi na utupu na katika hadith nyengine akasema atakaenidhamini kinyama kilochokuwepo baina ya taya zake mbili (yani ulimi)na kinyama kilichoko baina ya mapaja yake mawili (yani utupu)basi nami namdhamnini Jannah (Hadith sahih). Hivyo ili mtu aepukane na jahannam basi na achunge matamanio ya ulimi wake na utupu wake.

Ama madhambi mengine amesema Mtume wa Allah “ Makundi mawili sikuyaonapo,nayo ni makundi ya motoni,akayataja kua ni wanawake wanaotembea uchi,na vichwa vyao vimekaa kama nundu za ngamia. Akimaanisha wanawake wanaojisuka wakanyanyua nywele zao na wakatia wanayoyatia ili ifanyike nundu, hili ni kundi la motoni na tunaomba madada zetu na mama zetu wa kiislamu wakifanya haya. Je hawaijui hii hadithi au ni kumuendekeza sheitwaan na nafsi zao?
Na pia Mtume swalla Allahu alayhi wasalam amesema”Ameoneshwa moto na akawakuta wengi wao walokuwemo humo ni wanawake..”hivyo akawataka wazidishe kutoa sadaka.

Ili mtu aepukane na jahaanam ni muhimu kuzidisha amali zifuatazo:
Kuzidisha kutoa sadaka kwani amesema Mtume wa Allah “Sadaka huondoa makosa kama moto unavokula kuni.(Hadith sahih).
Kuzidisha Kufunga funga za Sunnah : Amesema Mtume wa Allah katka hadith “Atakaefunga siku moja kwa ajili ya Allah basi Allah atamueka mbali na jahannam umbali wa mwendo wa miaka 70.(Bukhari).

Kulia kwa ajili ya Allah kwani amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake “Jicho lenye kulia kwa ajili ya Allah halitogusa jahannam mpaka maziwa yarudi kwenye chuchu yake.(Hadith Sahih).

Allah atuepushe na Jahannam na atuwafikishe kufanya matendo ili tupate pepo yake. Innahu waliyyu dhaalika walqqadir alayhi.

MAKALA IMEANDALIWA NA RAUDHWAH ISLAMIC GROUP

No comments:

Post a Comment