Saturday 14 June 2014

NI UPI MOTO WA ALLAH -SEHEMU YA KWANZA


Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Kua na khofu ni katika jambo la kimaumbile kwa wanaadamu. Na hakuna mwanadamu asiekua na khofu , kwani kila mtu anacho kinachomkhofisha kwa mfano tajiri atakhofu kufilisika au kiongozi kuadhirika na khofu nyenginezo, lakini muislamu wa kweli hakuna kitu ambacho anakikhofu zaidi ya kukhofu adhabu za Allah (subhanahu wataala). Anajua kua Allah ameandaa adhabu kali kwa atakaemuasi. Muumini wa kweli anajua lengo lake ni kuepukana na adhabu hiyo ya jahannam, na hayo ndio mafanikio ya kweli ,kama anavyosema Allah (subhanahu wataala) “ Atakaevushwa na moto na akaingizwa peponi basi huyo amefuzu” (3:185). Allah (subhanahu wataala), ameeleza kua yeye ni mkali wa kuadhibu, na adhabu zake hakuna kiumbe aliewahi kumuadhibu kiumbe mwenzake, na kifungo chake ndani ya jahananam hakuna aliwahi kumfunga mwenziwe hapa duniani.

Amesema“Basi siku hiyo hatoadhibu yoyote namna ya adhabu yake.(25) Na wala hatafunga yoyote mfano wa kifungo chake.(26)” (Suratul Fajri). Jee aya hizi tumezizingatia? Maana tunaona adhabu mbalimbali wanazoadhibiwa watu duniani, iwe waislamu na wasiokua waislamu,hadi wengine kufikia kujiua kwa uchungu wa adhabu, lakini yote hayo hayafui dafu mbele ya Adhabu za Allah. Allah ameuleza moto kiasi kwamba, amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) yake kua ,hatolala mwenye kuukimbia,akimaanisha kua mtu atakaesikia habari zake, basi atafanya juhudi aepukane na jahannam. Hii kuonesha kua adhabu zake ni kali mno. Tumekatazwa kuadhibiana kwa moto duniani kwani adhabu ya moto ni adhabu yenye kufedhehesha na ni ya Allah pekee. Allah ameandaa malipo mabaya kwa watakaofanya ubaya.

Ameyakariri hayo Allah (subhanahu wataala) takriban katika kila sura ndani ya Qur-an, ili kuwatisha watu na Moto. Kila anapotaja pepo hutaja na moto, ili watu wapate kutafakari. Lakini jee tumeyazingatia haya? Allah ameuumba moto na tayari upo,na uko karibu na mmoja wetu kuliko nyuzi za viatu vyake (Hadith), na unazidi kukolea siku hadi siku kwa ajili ya kuwachoma watu watakaoingia humo. Mara Moja moto ulishtaki kwa Allah (subhanahu wataala), kua unaanza kujila wenyewe kwa wenyewe kutokana na makali yake. Allah akauruhusu kupumua mara mbili kwa mwaka, katika kipindi cha joto na kipindi cha baridi. Inasimuliwa katika hadithi kua Allah alivyouumba moto aliukoleza miaka 1000 ukawa mwekundu kuliko chochote, akaukoleza tena miaka 1000 mengine, ukawa mweupe kuliko chochote, na akaukoleza tena miaka 1000 ukawa mweusi, na sasa ni mweusi kama weusi wa shimo lenye kina kirefu. Amesema Rasuul (swalla Allahu alaihi wa sallam) kua Moto wa duniani ni moja kati ya sehemu 70 za Jahannam(Bukhari na Muslim). Tukumbuke kua kuni za moto huo ni watu na mawe, kama anavyosema Allah “Enyi mloamini jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, kutokana na moto kuni zake ni watu na mawe” (Tahrym : 6).

Na watu hao wataengezwa maumbile yao yawe makubwa, ili adhabu iwafaidi, kama anavyosema Rasuul (swalla Allahu alaihi wa sallam) katika hadith iliyopokelewa na Abi-Hurayra kua “Baina ya mabega mawili ya makafiri ni mwendo wa siku tatu, kwa aliepanda mnyama anaekwenda mbio” (Bukhari) .Na katika hadith sahihi kua jua litaingizwa ndani ya jahannam siku ya qiyamah,basi vipi litakua joto lake ikiwa hivi sasa liko mbali kilomita na ma kilomita vipi likiwa limo ndani ya tanuri la jahannam na watu wamo ndani yake? Habari za jahannam ni nzito ambazo hazielezeki kwa maneno wala hazifirikiki kwa akili, kwani ni adhabu juu ya adhabu. (Allah atuhifadhi).

Moto umetajwa kua una milango saba (suratul-Hijri), na umetajwa takriban mara 66 ndani ya Qur-an, na na kumetajwa majina yake,sifa ya watu watakaoingia humo, aina za adhabu zao,chakula chao,vinywaji vyao,mavazi yao na adhabu nyenginezo. Moto una darakaat yani daraja za kwenda chini, na kila daraka ya chini ndio yenye adhabu kali kuliko ya juu yake,na daraka ya chini kabisa ni ya wanafik kama anavyosema Allah katika suratu-Nisai “Hakika wanaafiki watakuwa katika t'abaka ya chini kabisa Motoni,…”(4:145). (Allah atuhifadhi).

A : MAJINA YA MOTO

Moto umetajwa kwa majina takriban tisa ndani ya Qur-an nayo ni:

1- JAHANNAM: Huu ndio moto mkubwa na uwakao vikali, wameandaliwa makafiri. Umetajwa mara nyingi katika Qur-an. Amesema Allah katika suratu-Qaaf kuonesha ukali wa moto huu “Siku tukapoiambia jahannam : Jee umejaa? Itasema Jee kuna nyongeza?”.

2- Saqar: Huu ni moto ambao wataingia ndani yake watu wasioswali,na wengineo.Amesema Allah kuhadithia watu wa peponi watakapowauliza watu wa motoni “Nini kilichokuingizeni katika SAQAR, watasema tulikua si wenye kusali.”(Mudathir 42-43). Akasema tena kuelezea moto huu “Na ni nini kitakachokujuulisha huo (saqar)?,(27) Haubakishi wala hauwachi,(28) unababua ngozi maramoja,(29)Juu yake kuna walinzi 19.(30)” Suratu Mudathir.

3- Ladhaaa: Amesema Allah katka Suratul-Maarij kuhusiana na moto huu: “Kwa hakika huo ni moto uwakao barabara,(15) unaobabua maramoja ngozi ya mwili (16)”

4- Hutwamah: Huu ni moto watakaoingia ndani yake wasengenyaji,na wenye kurundika mali bila ya kutumia katika kheri. Allah ameutaja katika suratul-Humazah. “Bila shaka atavurumishwa katika moto wa Hutwamah(4)”.

5- Sairaa: Umetajwa katika sehemu nyingi ndani ya Qur-an kama katika suratul-mulk na nyenginezo

6- Jahiim: Ni moto uwakao vikali na umetajwa katika sehemu nyingi ndani ya Qur-an kama katika Suratu Shuraa ya ya 91 na nyenginezo

7- Haawiyah: umetajwa katika Suratul-Qariah aya 9-11

8- Daarul-Bawaar: Umetajwa katika suratu-ibrahiim aya ya 28.

9- Nnaar : Pia umetajwa sehemu nyingi ukiambatanishwa na majina mengine au kutajwa pekee yake.Mfano ndani ya Suratul Baqara aya ya 275.

Usikose muendelezo wa mada hii nzito yenye kumtia khofu muislamu kuogopa adhabu za Allah. Allah atukinge na adhabu ya moto. Aaamin.

MAKALA IMEANDALIWA NA RAUDHWAH ISLAMIC GROUP

No comments:

Post a Comment