Saturday 7 June 2014

BAADHI YA SALA ZA SUNNA NA FADHILA ZAKE


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Allah subhanahu wataala ametufaradhishia sala tano kila siku. Sala ambazo ni wajibu wa kila muislamu kuzisali. Pia Allah subhanahu wataala akatuwekea sala za sunna. Sala za sunna  ni muhimu sana kuzisali kwani hujaza mapengo ya sala za faradhi ikiwa zina mapungufu siku ya Qiyama. Kwa ujumla sala ni lazima mwanadamu azisali na tuzisali kwa unyenyekevu kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah. Umuhimu wa sala za fardhi na faida ya sala za sunna imeelezwa na Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi ifuatayo : Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) anatuelezea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi  wasallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika amali za mja wa Allaah siku ya Qiyaamah ni Swalah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalah zake za fardhi Allaah Azza wa Jalla Atasema: Angalia ikiwa mja Wangu ana Swalah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad].

Hivyo ndugu zanguni tujihimizeni kusali sala za faradhi na pia tuzikimbilie sala za sunna kwani zitakuja kujaza mapengo katika sala zetu.  Leo katika makala yangu hii nitazungumzia baadhi tu ya sala za sunna  na faida zake kwa uchache. Miongoni mwa hizo ni :

1- Rakaa 12 za sunna
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
3- Sala ya dhuha.
4- Sala ya witri.

Ama upande wa sala  ya tahajjud na fadhila zake hiyo tutaiwekea makala maalum na utaweza kuisoma.

1-Fadhila ya rakaa 12 za sunna

Imesimuliwa na Bibi Ummu habibah Ramla bint Abi Sufyan(Radhia Allahu anha) amesema amemsikia Mtume wa Allah(swalla Allahu alayhi wasallam) akisema " Hakuna mja yoyote muislamu atakaeswali kwa aijli ya Allah rakaa 12 kila siku kwa kujipendekeza na si za Fardhi ila Allah atamjengea nyumba peponi” Imepokelewa na Imam Muslim.

Mwenye kudumu na kusali rakaa hizi 12 kwa ajili ya Allah na kwa ajili ya kujipendekeza kwa mola wake basi Allah subhanahu wataala atamjengea mja huyo nyumba katika pepo yake. Ni nani asiyetaka pepo ya Allah ? Tuko wapi Umma wa kiislamu kuzikimbilia kheri kama hizi. Wako wapi wenye kushindana kwa ajili ya kupata nyumba katika pepo ya Allah ? Suala litakuja je ni zipi hizo rakaa 12 ? Jibu la suala hilo linapatikana katika hadithi ifuatayo : Bibi Aisha(Radhia Allahu anha)  anasema " Amesema Mtume wa Allah rehma na amani ziwe juu yake " Yoyote atakaedumu na rakaa 12 usiku na mchana ataingia peponi: rakaa 4 kabla ya adhuhuri na 2 baada yake. Rakaa 2 baada ya sala ya maghrib, Rakaa 2 baada ya sala ya ishaa na rakaa 2 kabla ya sala ya alfajiri"(Imepokelewa na tirmidhy,nasai na ibn majah).

2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.

Rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri imetajwa ndani ya rakaa 12 za kila siku ambazo mwenye kuzisali Allah humjengea mtu nyumba katika pepo. Ila nimeamua kwa uchache kuielezea sunna hii kwani wengi wa watu wamekuwa wakiipuza. Pia Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akiwahimiza zaidi watu kusali rakaa hizi mbili. Inasimuliwa na Bibi Aisha kuwa” Hakuna swala yoyote ya Sunna ambayo Mtume alikua akiitilia mkazo zaidi kama rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri”Imepokelewa na Bukhari na Muslim. Rakaa 2 hizi husaliwa kabla ya sala ya alfajiri. Na imethibiti kwamba Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akisoma sura ndogo ndani ya rakaa mbili hizi.

Zama hizi watu wamekuwa wakiamka bado kwa dakika chache kusaliwa sala ya alfajiri ndio mtu nae hukimbilia kusali. Au wengine husali alfajiri hali ya kuwa sala tayari imeshatoka. Rakaa mbili hizi Mtume swalla Allahu alayhi wasallam anapiga mfano wa ubora wake kuliko dunia na vilivyomo ndani yake. Dunia ina mazuri mangapi? Ina  vitu vya thamani vingapi ? Lakini vyote hivyo haviwezi kuzidi thamani ya rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri. Imesimuliwa na Bibi Aisha (radhwiya Allahu anha) amesema Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam)" Rakaa mbili za sunna kabla ya sala ya alfajiri ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani yake" Imepokelewa na Imam Muslim na Tirmidhi.

Wito kwa wenye kusali sala ya alfajiri na kutojihimu na rakaa mbili hizi tusiache kukimbilia kheri kama hizi. Na wito wangu kwa wenye kulala wakati wa sala ya alfajiri unampita jua kwamba utaenda kuulizwa kwa Allah juu ya kila sala iliyokupita na pia unakosa nafasi za kheri kama hizi kwa kufuata matamanio ya nafsi yako pamoja na shetani.

3- Sala ya dhuha.

Sala ya dhuha ni sala ambayo husaliwa robo saa baada ya kuchomoza kwa jua na mwisho wake ni kabla ya kuingia kwa adhuhuri. Sala hii ni miongoni mwa wasia wa Mtume Muhammad swalla Allahu alayhi wasallam kwa sahaba wake Abuu Hurayra na wengine katika masahaba. Ila ni wasia ambao na sisi unatufaa kuufuata na kuufanyia kazi. Imesimuliwa na Abu-Hurayra -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema:"Ameniusia Kipenzi changu(swalla Allahu alayhi wasallam) mambo matatu: Kufunga siku tatu kila mwezi,Rakaa mbili za Dhuha na kusali witri kabla ya kulala" Imepokelewa na Bukhari na Muslim na pia Mtume swalla Allahu alayhi wassalam alimuusia hayo hayo swahaba wake mwengine Abuu-Dardai radhia Allahu anhu katika hadityhi ilopokelewa na Imam Muslim na Abu-Daud.

Sala husaliwa rakaa mbili mbili hadi kufikia nane. Na imethibiti zaidi kuwa Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akisali rakaa nne. Hii ni sunna ambayo wengi wa watu wameisahau labda kwa sababu ya maisha au kughurika na dunia na starehe zake. Je ni yapi malipo kwa mwenye kusali dhuha? Atakaeswali Dhuha kachukuliwa dhamana na Allah ya kusimamiwa mambo yake kwa siku ile kama anavyosema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi ilopokelewa na Uqba bin Amir radhia Allahu anhu kua "Amesema Allah kumwambia mwanadamu:Ewe mwanadamu nitosheleze mwanzo wa mchana kwa rakaa nne nami nitakutosheleza mwisho wa mchana" Imepokelewa na Imam Ahmad .

4- Sala ya witri

Imesimuliwa na Jabir radhiallahu anhu amesema:” Amesema Mtume sallahu alayhu wasslam “Atakaekhofu kutosimama mwisho wa usiku, basi aswali witri mwanzo wa usiku, na anaetarajia kua atasimama mwisho wa usiku basi na aswali witri mwisho wake, kwan witri mwisho wa usiku ni yenye kushuhudiwa na inayohudhuriwa (na malaika) na hiyo ndo bora” Imepokelewa na Imam Muslim, Tirmidhi na wengineo.
Sala ya witri ina faaida kubwa sana na malipo makubwa. Yatosha fadhila yake kuwa sala ya witri inashuhudiwa na malaika. Pia ni katika wasia alousia Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) kama tulivyoeleza katika hadithi iliyopita. Witri ni 1,3,5,7,11. Mtu anasali rakaa 2. Halafu anamalizia 1. Au anasali rakaa 2 halafu tena 2 halafu anamalizia moja.

Kwa ujumla sala zote zina faida kwetu waislamu. Ni wajibu wote tujihimu na kuacha uvivu katika kuzisali sala hizi. Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale watakaosali na kukubaliwa sala zao. Na wale wenye kukumbushwa kheri na kuzikimbilia kheri hizo. Aaamin.

Allah ni mjuzi zaidi.

13 comments:

  1. jazzakallah allah akujaze khery zake na akulipe kwa hili in sha allah

    ReplyDelete
  2. ALLAH akupe nguvu kwani nimepata elimu kubwa sana juu swali langu

    ReplyDelete
  3. Alhamdulillah mungu akupe kheri ktk kheri

    ReplyDelete
  4. Shukrani Allah akupe nguvu,uzima na moyo wa imani wa kutukumbusha zaidi. Amen.

    ReplyDelete
  5. Allah akulipe kwa kazi nzuri hii In shaa Allah

    ReplyDelete
  6. Allah s.w atulipe pepo yake inshaalah

    ReplyDelete
  7. Allah s.w atulipe pepo yake inshaalah

    ReplyDelete
  8. Allah s.w atulipe pepo yake inshaalah

    ReplyDelete
  9. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
  10. Allah atuongoze katika kheri amiin.

    ReplyDelete