Sunday 1 June 2014

UMUHIMU WA KUCHUNGA WAKATI


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Makala yetu itazungumzia suala zima la kuuchunga wakati. Tukizungumzia kuchunga wakati maana yake ni kuutumia wakati wetu kuyafanya yalio ya kheri katika kila sekunde na bila ya kuupoteza katika mambo ya shari au yasio na faida na sisi hapa duniani mpaka kesho akhera.

Wakati ni kitu ambacho kitukufu na kina thamani kubwa na umuhimu mkubwa kwa mwanadamu. Tosheka kwa kujua utukufu wake kwa kuapiwa na Allah ndani ya Quraan katika aya tofauti. Wanazuoni wa tafsiri wanasema kuwa Allah haapi kwa kitu ila kitu hicho huwa ni kitukufu na anataka wanaadamu waweze kukizingatia zaidi.  Miongoni mwa sehemu ambazo Allah ameapa ni “Naapa kwa Zama!” (103:1)” Naapa kwa mchana!” (93:1).

Ewe mwanaadamu unatambua ya kuwa maumbile yako ni sawa na muda wako wa kuishi hapa duniani? Nikimaanisha Kila unavyoutumia muda wako ndio unapopunguza sehemu ya maisha yako. Nasema hivi ili kuonesha umuhimu wa wakati tulionao. Maana yake kila mtu ana wakati maalum aliopangiwa na Allah Subhanahu wataala kuishi katika ulimwengu huu. Kama anavyotuambia Allah “Na hakuna chochote ila asili yake inatokana na Sisi; wala hatukiteremshi ila kwa kipimo maalumu” (15:21)

Na utakapoisha tu wakati wake basi hana kitakachomsubirisha tena kama anavyotueleza Allah “Na kila umma una muda wake. Utakapo fika muda wao basi hawatakawia hata saa moja, wala hawatatangulia.” (7:34) Hivyo basi, Ewe ndugu yangu inatubidi mimi na wewe kuutumia vyema uhai wetu kwani hakika tutaenda kuulizwa kulingana na uhai wetu tuliutumiaje. Allah Subhanahu Wataala anatuambia “ Ati anadhani binaadamu kuwa ataachwa bure? “(75:36) Hapa Allah subhanahu wataala anatuuliza suali ya kuwa tunatarajia tutaachwa bure bila ya kuulizwa neema alizotupa tukiwa hapa duniani? Bila shaka hapana na katika kusisitiza hilo akasema tena Allah aliyetukuka “ [[Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.]] “ (102: 8). Na tambua kuwa wakati ni moja wapo kati ya neema za Allah alizotupa.

Pia Ametusimulia Mtume Swalla Allahu Alayhi wasallam kwamba :(( Hautoondoka mguu wa mja siku ya Qiyama mpaka aulizwe kuhusu mambo manne,Umri wake aliumalizaje, Na elimu yake aliitumiaje, Na mali yake aliichumaje na akaitumiaje, na Mwili wake aliutia mtihani gani?)) Tabraniy.

  Hima hima ewe ndugu yangu tujitahidi kadri tunavyoweza katika kuutumia muda kufanya mambo ya kheri yalio katika uwezo wetu, kwani kheri zipo nyingi za kimaneno na kimatendo. Na kamwe tusidharau jema hata liwe dogo vipi na vile vile baya hata liwe na udogo kiasi gani kwani hakika yote hayo tutaenda kuona malipo yake. Kama Allah anavyosema: [[Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona!..*Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!]]( 99:7-8). Bila ya shaka mbora wetu ni yule atakaezinduka mapema na kuutumia umri wake katika yalio ya kheri na kinyume chake hua ni muovu. Allah asitujaalie kuwa miongoni mwa hao.

Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam anatuambia,((..Na Mbora wenu ni mwenye kurefuka umri wake na yakawa mema matendo yake na Muovu  wenu ni mwenye kurefuka umri wake na yakawa maovu matendo yake.)) Ahmad.

Kwa kutambua jambo hili inabidi kila tunapopata fursa ya kufanya kheri tuikimbilie kwani Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam Ametuambia, ((Faidika na Matano kabla ya Matano, Ujana wako kabla Uzee wako, Afya(Uzima) wako kabla ya Ugonjwa wako, Utajiri wako kabla ya Ufakiri wako, Uhai wako kabla ya Kifo chako na Faragha yako kabla ya Shughuli zako.)) Rawahul Al hakim.

Hadithi hii ya Mtume inatuhamasisha kuutumia muda wetu ipasavyo kabla hatujawa ni wenye kujuta pale yanapotujia mauti na tukaona tunakoelekea. Allah anatupa khabari  [[..Mpaka yanapo mfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu Mlezi! Nirudishe.(99) Ili nitende mema sasa badala ya yale niliyo yaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kipo kizuizi mpaka siku watapo fufuliwa.(100)]] ( Suratul Muuminun)

Hayo ndio majuto ya wale ambao waliotumia vibaya wakati wao hapa duniani. Na siku ya Qiyama kwa mfadhaiko watakao upata pindi watakapoonyeshwa madaftari yao na watakanusha kabisa muda mrefu waliopewa kuishi hapa duniani, wataona waliishi siku chache tu..kama anavyotuelezea Allah [[Na Siku atakapo wakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa ila saa moja tu ya mchana! Watatambuana. Hakika wamekhasirika walio kanusha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuwa wenye kuongoka.]] (10: 45) Na watakapoulizwa haya ndio yatakua majibu yao [[Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa hisabu ya miaka?(112) Watasema: Tulikaa siku moja au sehemu ya siku. Basi waulize wanao weka hisabu (113)Atasema: Nyinyi hamkukaa huko duniani ila kidogo, laiti ingeli kuwa mnajua.(114)Je! Mlidhani ya kwamba tulikuumbeni bure na ya kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa? (115)]] (Suratul Muuminun)

Hivi ndugu yangu baada ya yote haya bado utabakia kuutumia mda wako vibaya? Ni majuto ya aina gani unapoharibu kitu halafu iwe hamna nafasi ya pili ya kukirudia tena ili ukifanye vizuri?  Basi anza sasa, usingoje baadae wala kesho kwani hakika hujui kama utafika hio baadae au kesho. Weka nia  halafu ujitahidi kadri ya uwezo wako na Allah atakufanyia wepesi. Kwani ametuahidi. [[Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.]] (29:69)
Mwisho kabisa napenda kumalizia kwa aya za Allah zisemazo : [[Na anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'amali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa. ]]   (17: 19)
[[Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa bora ya waliyo kuwa wakiyatenda.]](16: 97)   

ALLAH ATUJAALIE TUWE NI WENYE KUUTUMIA UMRI WETU KATIKA KHERI NA ATURUZUKU MWISHO MWEMA SISI NA WAISLAM WOTE KWA UJUMLA..

NA ALLAH NDIE MJUZI ZAIDI

No comments:

Post a Comment