Tuesday 17 June 2014

FUNGA NA AINA ZAKE


Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

                Sifa zote njema zinamstahikia Allah Subhaanahu Wa Taala muumba mbingu na ardhi bila ya vizuizi, Swala na Salaamu zimshukie kipenzi cha Umma huu ulio bora Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi Wa Sallam, pamoja na ahli zake na Swahaba zake na wote waliowema hadi siku ya malipo.

                Ndugu yangu katika Imani leo napenda kukuletea makala hii muhimu kwa waislamu, kwani sote tunatambua ya kwamba tumekabiliwa na mwezi mtukufu mno na wenye fadhila nyingi kwa waislamu katika maisha ya duniani na kesho Akhera. Kwa maana hiyo tumeonelea tukumbushane yaliyo bora zaidi mbele ya Allah ili tupate kuwa waja wema na anaowapenda Allah Subhaanahu Wa Taala, Kwani Allah mwenyewe ametuhimiza tuyakimbilie mambo mazuri katika kuyatenda ili tupate kuingizwa katika fungu la WachaMungu. Anasema Allah Subhaanahu Wa Taala Katika kuyatilia Mkazo hayo : “Na yaendeeni upesi upesi maghfira ya mola wenu na Pepo yake ambayo upana wake tu ni sawa na mbingu na ardhi, Pepo iliyowekewa kwa wamchao Allah.”   (AL-IMRAN : 133).

                Ndugu yangu katika Imani, Mada tutakayoizungumzia leo ni kuhusu Funga.

MAANA YA FUNGA

               Funga Kilugha ni kile kitendo cha kujizuilia na kitu chochote. Kwa maana hiyo tunapata mafunzo kwamba unaweza ukajizuilia na kitendo chochote kile kama kusema au kuzungumza au kula kwa muda wowote uliojiwekea na ukasema nimefunga. Allah Subhaanahu wa Taala anatupa mfano wa hayo katika Qur-an Tukufu pale alipomzungumzia Bibi Maryam wakati alipomzaa Nabii Issa Alayhi Salaam, alipoulizwa na jamaa zake kuhusu mtoto yule amempata wapi ? Bibi Maryam akajibu kwa kuashiria : “Hakika mimi nimeweka nadhiri ya kufunga kwa Allah mwingi wa Rehma, basi sitozungumza na mtu yeyote kwa siku ya leo.”  (MARYAM : 26).  Kwa hiyo inawezekana ukanuia kufunga kwa kutofanya kitendo chochote kile ulichodhamiria. Kama hapa bibi Maryam amesema kufunga kwa maana ya kujizuia na kuzungumza. 
          
              Funga Kisheria ni kujizuilia kula, kunywa na mambo yote yenye kufunguza mchana kutwa, kuanzia alfajiri ya kweli mpaka kuzama kwa jua. Kwa uthibitisho wa hayo ni pale Allah Subhaanahu Wa Taala aliposema katika Qur-an yake Tukufu : “Na kuleni na kunyweni mpaka kubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku, Kisha timizeni saumu mpaka usiku.”  (BAQARA : 187).

              Maneno hayo matukufu yanabainisha nyakati za kujizuia huko ni kuanzia alfajiri ya kweli hadi kuzama kwa jua yaani kuanza kuingia kwa usiku.

HIKMA YA FUNGA

             Miongoni mwa hikma za Funga ni kama ambavyo wanazuoni walivotufahamisha, ni kuizoesha nafsi kuwa na subra kwani jambo la kufunga linahitaji subira ya kweli kweli. Hikma nyengine ni kujua thamani ya neema za Allah Subhaanahu Wa Taala, Huwezi  kujua neema ya chakula, kinywaji, au kukutana na mke wako mpaka zitakapokuondokea neema hizo au kuzuiliwa. Mfano asiyejua njaa basi atajua njaa inakuwaje kwa kufunga, na atajua thamani ya vyakula hivyo. Hikma nyengine ni kumpiga    Shetani na kumbana kwani binaadamu anaposhiba na vyakula vikajenga mwili wake, ndipo anapokaribia katika mwili wake na kumfanya ayaendee maasi mbali mbali. Pia Funga humfanya mwanadamu kuwa na afya iliyo njema, Kwa maneno ya Mtume Swalla Allahu Alayhi Wa Sallam aliposema :”Fungeni mupate afya njema.”

AINA ZA FUNGA

                Funga zipo za aina mbili nazo ni Funga za Fardhi (Lazima) na Funga za Sunna (zisizo za Lazima).
1)FUNGA ZA SUNNAH

                Funga za Sunna ni zile Funga zote zisizokuwa na ulazima kwa muislamu kuzitekeleza. Kwa maana hiyo muislamu yeyote atakae zitekeleza atapata ujira wake maalumu uliowekwa na Allah Subhaanahu wa Taala, na vile vile muislamu yeyote asipozitekeleza hatopata ujira wala dhambi. Mfano wa Funga hizo za Sunna ni kama Funga za Jumatatu na Alhamisi ambazo Mtume wetu Muhammad Swalla Allahu Alayhi Wa Sallam alikuwa akizitekeleza.  Mfano mwengine ni Funga ya Arafa, Funga ya Ashuraa, Funga za masiku meupe na kadhalika.

2)FUNGA ZA FARDHI.

Funga za Fardhi ni funga zote zilizokuwa za lazima kwa muislamu kuzitekeleza. Kwa maana hii muislamu yeyote atakae zitekeleza atapata ujira uliowekwa na Allah Subhaanahu Wa Taala, kinyume chake kwa muislamu yeyote atakaeziwacha asizitekeleze na hali ya kuwa zinamuwajibikia atapata dhambi na khasara kubwa mbele ya Allah Subhaanahu Wa Taala.

                  Funga za Fardhi zimegawika sehemu tatu, nazo ni :-

a)Funga ya Ramadhani.
b)Funga ya Kafara.
c)Funga ya Nadhiri.

               Ramadhani ni mwezi miongoni mwa miezi kumi na mbili katika mwaka wa Hijriya, ndani ya mwezi huu kuna funga za lazima kwa kila muislam aliyewajibikiwa kufunga kwa takribani siku ishirini na tisa kwa muandamo wa mwezi, ama siku thalathini kwa kukamilisha. Kwa uthibitisho wa hayo ni pale Allah Subhaanahu Wa Taala aliposema : “Enyi mlioamini, mumefaradhishiwa kufunga kama walivyo faradhishiwa waliopita kabla yenu.”  “Ni masiku machache tu ya kuhesabika ………..” (BAQRA :   ).

Kwa hivyo kila muislamu aliyebaleghe, mwenye akili timamu, mwenye afya njema na mkaazi (mwenyeji katika mji ) ni lazima kwake kufunga katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

               Yaani Funga haisihi kwa kafiri, na sio lazima kwa mtoto mdogo aliyekuwa hajafikia baleghe, na sio lazima kwa asiyejiweza au mgonjwa na vile vile sio lazima kwa msafiri wakati wa safari yake ya halali iliyofikia masafa ya kupunguza sala (Marhalatain).

               Tumuombe Allah Subhaanahu Wa Taala atufikishe katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na atuwafikishe kuitekeleza ibada hiyo kwa salama na afya njema, na atujaaliye tuwe miongoni mwa watakaofikia lengo la funga.

               Waswalla Allahu alaa sayyidna Muhammad wa Alaa Aalihi Waswahbihi Wasallam, Walhamdulillahi Rabbil Aalamiin.

1 comment: