Tuesday, 20 October 2015

Fadhila Za Mwezi Wa Muharram

Imeandikwa na Alhidaaya

AlhamduliLLaah, Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kutufikisha tena katika mwaka mwengine mpya wa Kiislamu. Katika mwezi  wa Muharram, kuna fadhila zake maalumu juu ya kwamba ni sawa na miezi mitukufu mingineyo. Fadhila nyingi Muislamu anaweza kuzipata atakapotekeleza maamrisho ili aweze kujichumia thawabu nyingi. Mojawapo ni funga ya tarehe 9 na 10 Muharram zinazojulikana kamaTaasu'aa na 'Aashuraa. Hivyo ndugu Waislamu tusiache kufunga siku hizi mbili kwani thawabu zake ni kama ilivyotajwa katika mapokezi yafuatayo:

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله)) رواه مسلم

Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka uliotangulia)) [Muslim]

(soma maelezo chini kujua kwanini tufunge pia na tarehe 9 Muharram)

 

Jumla ya miezi mitukufu ni minne na mwezi huu wa Muharram ndio mwezi wa kwanza unaoanza kuhesabika kama ni mwaka mpya.

 

((إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللّهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللّهِ يَوْمَ خَلَقالسَّمَاوَات وَالأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلاَ تَظْلِمُواْ فِيهِنَّأَنفُسَكُمْ))

 

((Idadi ya miezi (ya mwaka mmoja) mbele ya Allaah ni miezi kumi na mbili katika ilimu ya Allaah (Mwenyewe tangu) siku Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo imo minne iliyo mitukufu kabisa (nayo ni Rajab, Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram) (kufanya) hivi ndiyo dini iliyo sawa. Basi msijidhulumu nafsi zenu (kwa kufanya maasi) katika (miezi) hiyo)) [At-Tawbah 9:36]

 

Na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hadiyth iliyotoka kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu 'anhu):   

 

 (السنة اثنا عشر شهرا، منها أربعة حرم: ثلاث متواليات، ذو القعدة، وذو الحجة، والمحرم، ورجب مضر الذي بين جمادى وشعبان)) رواه البخاري، ومسلم

 

((Mwaka una miezi kumi na mbili, minne miongoni ya hiyo ni mitukufu, mitatu inafuatana pamoja; Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab ambao uko baina ya (mwezi wa) Jumaada na Sha'abaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Ni neema kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   Kutujuaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au masiku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine.

 

Kuhesabika Kwa Mwaka Mpya Wa Hijriyah 
 

Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya kuhama (Hijrah) kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba kutoka Makkah kuhamia Madiynah. Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji ambao wataanza kutumia Sharia'h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana kamaMuharram. Na pia inasemekana kuwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipata barua kutoka kwa mabalozi wake wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislam, na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe. Akawashauri Maswahaba wenzake kuwa kuwe na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohamia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah.

 

Na mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama A.H au H kwa kirefu yenye maana 'After Hijrah'au Hijriyah, tarehe 1 Muharram A.H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622M. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka mwezi wa Dhul-Hijjah unapomalizika na mwezi wa Muharram utakapoingia hivi karibuni

 

Fadhila Za Mwezi Huu Khaswa

 

Ingawa miezi minne yote iliyotajwa katika Aayah ya juu ni mitukufu lakini mwezi huu wa Muharram umefadhilishwa zaidi ya miezi mingine kama ilivyo katika Hadiyth zifuatazo:

 

 عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ((أَفْضَلُ الصِّيَامِ بَعْدَ رَمَضَانَ شَهْرُ اللَّهِ الْمُحَرَّمُ )) رواه مسلم

 

Imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kasema; Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Funga bora kabisa baada ya Ramadhaan ni funga ya mwezi wa Allaah wa Muharram)) [Muslim]

 

 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ : "مَا رَأَيْتُ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَتَحَرَّى صِيَامَ يَوْمٍ فَضَّلَهُ عَلَى غَيْرِهِ إِلّا هَذَا الْيَوْمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَهَذَا الشَّهْرَ يَعْنِي شَهْرَ رَمَضَنِان " رواه البخاري

 

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) ambaye amesema: "Sijapata kumuona Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisubiri kufunga siku yoyotekama siku hii ya siku ya 'Aashuraa na mwezi huu yaani mwezi wa Ramadhaan" [Al-Bukhaariy]  

 

Swawm ya 'Ashuraa imependezeshwa hata kwa watoto kuifunga kamawalivyokuwa wakifanya Maswahaba katika siku hiyo.

 

عن الرُّبيّع بنت معوذ رضي الله عنها قالت: "أرسل رسول الله صلى الله عليه وسلم غداة عاشوراء إلى قرى الأنصار  "من أصبح مفطرا فليتم بقية يومه ومن أصبح صائما فليصم" ، قالت : فكنا نصومه بعد ونصوّمه صبياننا ...  رواه البخاري ومسلم  

 

Kutoka kwa Ar-Rubay'i  bint Mu'awwadh (Radhiya Allaahu 'anhaa) amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituma ujumbe Alfajiri ya siku ya 'Ashuraa katika vijiji vya Answaar "Aliyeamka akiwa amefuturu amalize siku yake (kwa kutokula) na aliyeamka amefunga afunge" Akasema (Ar-Rubay'i: 'Tulikuwa tukifunga baada yake na tukiwafungisha watoto wetu...'[Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Sababu Ya Kufunga Siku Ya 'Aashuraa  
 

 عَنْ ابْنِ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: " قَدِمَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ الْمَدِينَةَ فَرَأَى الْيَهُودَ تَصُومُ يَوْمَ عَاشُورَاءَ فَقَالَ: ((مَا هَذَا)) قَالُوا هَذَا يَوْمٌ صَالِحٌ هَذَا يَوْمٌ نَجَّى اللَّهُ بَنِي إِسْرَائِيلَ مِنْ عَدُوِّهِمْ فَصَامَهُ مُوسَى، قَالَ: (( فَأَنَا أَحَقُّ بِمُوسَى مِنْكُمْ)) فَصَامَهُ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ"   رواه البخاري

 

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alielekea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah akawaona Mayahudi wanafunga siku ya 'Aashuraa, akasema: ((Nini hii?)) (yaani kwa nini mnafunga?) Wakasema hii ni siku njema, hii ni siku Allaah Aliyowaokoa Wana wa Israili kutokana na adui wao, na Muusa alifunga siku hii. Akasema (Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Mimi nina haki zaidi juu ya Muusa kuliko nyinyi)). Akafunga siku hiyo na akaamrisha ifungwe" [Al-Bukhaariy]    

 

Lakini Mtume wetu (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa tukhitilafiane na Mayahudi kufunga siku hiyo kwa kuongeza siku moja kabla.    

 

روى عَبْدَ اللَّهِ بْنَ عَبَّاسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قال : "حِينَ صَامَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَوْمَ عَاشُورَاءَ وَأَمَرَ بِصِيَامِهِ قَالُوا يَا رَسُولَ اللَّهِ إِنَّهُ يَوْمٌ تُعَظِّمُهُ الْيَهُودُ وَالنَّصَارَى فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((فَإِذَا كَانَ الْعَامُ الْمُقْبِلُ إِنْ شَاءَ اللَّهُ صُمْنَا الْيَوْمَ التَّاسِعَ)) قَالَ فَلَمْ يَأْتِ الْعَامُ الْمُقْبِلُ حَتَّى تُوُفِّيَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّىاللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ". رواه مسلم 

 

Imepokelewa na Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhuma) kasema "Alipofunga Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya 'Aashuraa na akaamrisha ifungwe wakasema: Ewe Mtume wa Allaah, hii ni siku wanayoitukuza Mayahudi na Manaswara.  Akasema Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Ikifika mwakani In shaa Allaah tutafunga siku ya tisa pia)). Akasema (Ibn 'Abbaas) haukufika mwaka uliofuata ila alifariki Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)[Muslim]

 

Kwa hiyo ni bora kufunga siku ya tisa na kumi Muharram, na kama mtu hakujaaliwa kufunga siku ya tisa na kumi, basi afunge siku ya kumi peke yake ili asikose kupata fadhila ya siku hiyo. 

 

Kwa vile siku hii ni siku Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyomnusuru Muusa ('Alayhis-Salaam) na Wana wa Israaiyli, na sisi pia tutakaofunga tuwe na tegemeo kuwa nasi Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atatunusuru pia kutokana maadui wetu na mabaya kamaAlivyotuahidi In shaa Allaah     

 

 ((إِنَّا لَنَنصُرُ رُسُلَنَا وَالَّذِينَ آمَنُوا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَيَوْمَ يَقُومُ الْأَشْهَادُ))

 

((Bila ya shaka Sisi Tunawanasuru Mitume Yetu na wale walioamini katika maisha ya dunia ya siku watakaposimama mashahidi (kushuhudia amali za viumbe)) [Ghaafir 40: 51]

 

Juu ya kwamba fadhila ya kufunga Swawm ni ibada Aipendayo kabisa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kamailivyo katika Hadiyth mbali mbali, vilevile funga hii itatusafisha na madhambi ya mwaka mzima,       

 

 قال النبي صلى الله عليه وسلم : (( صيام يوم عاشوراء ، إني أحتسب على الله أن يكفر السنة التي قبله))رواه مسلم

 

Kasema Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): ((Funga ya siku ya 'Aashuraa, nataraji kutoka kwa Allaah Ayafute madhambi ya mwaka wa nyuma)) [Muslim]

 

Ndugu Waislam, hii ni fursa kubwa ya kujisafisha na dhambi na kuzidisha taqwa (ucha Mungu) ili kujibebea zawadi nyingi twende nazo Akhera kwa vile  hatujui  amali njema zipi zitakazokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na hatujijui kama tutakuwa na umri wa  kuchuma zaidi.

 

Bid'ah Katika Siku Ya 'Aashuraa   
 

Katika mwezi huu wa Muharram, tarehe kumi ambayo ni siku ya 'Ashuraa, tunawaona baadhi ya watu wakifanya maandamano na kuvaa nguo nyeusi wakidai ni nguo za msiba, na huku wakijipiga vifua kwa ngumi na wengine kujikata kwa visu, kujipiga kwa minyororo na damu kuwamwagika, wakidai wanaomboleza kifo cha mjukuu wa Mtume, Al-Husayn (Allaah Amrehemu). Matendo hayo ni mambo ambayo hayakubaliki kisheria na wanachuoni wote wa Kiislam wanapinga na kulaani anayefanya hivyo kwani ni kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).   

 

Amesema Ibn Taymiyyah (Allaah Amrehemu):

"Bid'ah zinazofanyika katika siku hii ni kuwa baadhi ya watu wameitenga na kuifanya kuwa ni siku ya huzuni kwa kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) na kujipiga, kulia  wakati Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliharamisha kamailivyo katika Hadiyth hii  sahihi:

 

 عن عبد الله بن مسعود رضي الله عنه قال : قال النبي صلى الله عليه وسلم: ((ليس منا من لطم الخدود وشق الجيوب ودعا بدعوى الجاهلية)) البخاري .

 

Imetoka kwa Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema ((Sio miongoni mwetu atakayejipiga mashavuni na kuchanachana nguo na kupiga mayowe ya kijahiliya)) [Al-Bukhaariy]

 

Na haitoshi hayo wayafanyao, bali wanatukana na kuwalaani Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika siku hiyo."

 

Ibn Rajab amesema:

"Wanayoyafanya Ma-Rafidhah (Mashia) katika siku hii kuwa ni siku ya huzuni kwa ajili ya kuuliwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu) ni amali ambazo anazopoteza mtu katika uhai wake akadhani kuwa wanafanya amali njema, wala hakuamrisha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kufanya siku za misiba na vifo vya Mitume kuwa ni siku za huzuni, sasa vipi iwe siku ya huzuni kwa wasio Mitume?"

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atujaalie katika wale ambao husikiliza kauli wakafuata zile zilizo njema.  Aamiyn.

Monday, 7 September 2015

Adhkaar za Jioni

Audhubillahi mina shaitani rajim

اللَّهُ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ ۚ وَسِعَ كُرْسِيُّهُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ ۖ وَلَا يَئُودُهُ حِفْظُهُمَا وَهُوَ الْعَلِيُّ الْعَظِيمُ

Mwenyezi Mungu - hapana mungu ila Yeye Aliye hai, Msimamia mambo yote milele. Hashikwi na usingizi wala kulala. Ni vyake pekee vyote viliomo mbinguni na duniani. Ni nani huyo awezaye kuombea mbele yake bila ya idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao; wala wao hawajui chochote katika vilio katika ujuzi wake, ila kwa atakalo mwenyewe. Enzi yake imetanda mbinguni na duniani; na wala haemewi na kuvilinda hivyo. Na Yeye ndiye aliye juu, na ndiye Mkuu.

Mwenye kusoma (Ayatul-Kursiy) pindi anapoamka atalindwa  kutokana na majini mpaka jioni, na atakaeisoma jioni atalindwa nayo mpaka asubuhi.

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehema Mwenye Kurehemu

قل هو الله أحد* الله الصمد* لم يلد ولم يولد* ولم يكن له كفوا أحد

Sema: Yeye Mwenyezi Mungu ni wa pekee.
Mwenyezi Mungu Mkusudiwa.
Hakuzaa wala hakuzaliwa.
Wala hana anaye fanana naye hata mmoja.

بسم الله الرحمن الرحيم


Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehema Mwenye Kurehemu

قل أعوذ برب الفلق* من شر ما خلق* ومن شر غاسق إذا وقب* ومن شر النفاثات في العقد* ومن شر حاسد إذا حسد

Sema: Najikinga kwa Mola Mlezi wa mapambazuko,
Na shari ya alivyo viumba,
Na shari ya giza la usiku liingiapo,
Na shari ya wanao pulizia mafundoni,
Na shari ya hasidi anapo husudu.

بسم الله الرحمن الرحيم

Kwa Jina La Mwenyezi Mungu Mwingi Wa Rehema Mwenye Kurehemu

 قل أعوذ برب الناس* ملك الناس* إله الناس* من شر الوسواس الخناس* الذي يوسوس في صدور الناس* من الجنة و الناس

Sema: Ninajikinga kwa Mola Mlezi wa wanaadamu,
Mfalme wa wanaadamu,
Mungu wa wanaadamu,
Na shari ya wasiwasi wa Shetani, Khannas,
Anaye tia wasiwasi katika vifua vya watu,
Kutokana na majini na wanaadamu.
(Mara tatu tatu)

(Mwenye kusisoma (sura hizi) mara tatu asubuhi na jioni zinamtosheleza na kila kitu.

أَمْسَيْـنا وَأَمْسـى المـلكُ لله وَالحَمدُ لله ، لا إلهَ إلاّ اللّهُ وَحدَهُ لا شَريكَ لهُ، لهُ المُـلكُ ولهُ الحَمْـد، وهُوَ على كلّ شَيءٍ قدير ، رَبِّ أسْـأَلُـكَ خَـيرَ ما في هـذهِ اللَّـيْلَةِ وَخَـيرَ ما بَعْـدَهـا ، وَأَعـوذُ بِكَ مِنْ شَـرِّ هـذهِ اللَّـيْلةِ وَشَرِّ ما بَعْـدَهـا ، رَبِّ أَعـوذُبِكَ مِنَ الْكَسَـلِ وَسـوءِ الْكِـبَر ،
رَبِّ أَعـوذُبِكَ مِنْ عَـذابٍ في النّـارِ وَعَـذابٍ في القَـبْر

“Tumeingia jioni na imefika jioni na Ufalme ni wa Mwenyezi Mungu , na sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu , hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki, ila Mwenyezi Mungu , hali yakuwa peke yake, hana mshirika. Niwake Ufalme, na nizake sifa njema, na yeye juu ya kila kitu ni muweza, Ewe mola, nakuomba kheri ya usiku wa leo, na kheri ya baada ya usiku wa leo, na ninajilinda Kwako kutokana na shari ya usiku wa leo na shari ya baada ya usiku huu. Ewe Mola, najilinda Kwako, kutokana na uvivu, na ubaya wa uzee (uzee ubaya) Ewe mola najilinda Kwako kutokana na adhabu
ya moto na adhabu ya kaburi”

اللّهُـمَّ بِكَ أَمْسَـينا، وَبِكَ أَصْـبَحْنا، وَبِكَ نَحْـيا، وَبِكَ نَمـوتُ وَإِلَـيْكَ المَصـير

“Ewe Mwenyezi Mungu kwa ajili yako tumefika jioni, na kwa ajili yako tumefika asubuhi, na kwa
ajili yako tuko hai na kwa ajili yako tutakufa na ni kwako tu marejeo.

اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك ، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت ، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت ، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ

“Ewe Mwenyezi Mungu Wewe ni Mola wangu, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, umeniumba mimi na mimi ni mja wako, nami niko juu ya ahadi yako, na agano lako, kiasi cha uwezo wangu, najilinda kwako kutokana na shari ya nilicho kifanya, nakiri kwako kwa kunineemesha, na
nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unisamehe kwani hasamehe madhambi ila Wewe”

اللّهُـمَّ إِنِّـي أَمسيتْ أَُشْـهِدُك ، وَأُشْـهِدُ حَمَلَـةَ عَـرْشِـك ، وَمَلائِكَتِك ، وَجَمـيعَ خَلْـقِك ، أَنَّـكَ أَنْـتَ اللهُ لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ وَحْـدَكَ لا شَريكَ لَـك ، وَأَنَّ ُ مُحَمّـداً عَبْـدُكَ وَرَسـولُـك

“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nimefika jioni nakushuhudia na nina washuhudia wabeba wa
arshi yako na malaika wako, na viumbe vyako vyote kwamba Wewe ndiye Mwenyezi Mungu hapana apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, hali ya kuwa peke yako huna mshirika, na kwamba Muhammad ni mja wako na ni Mtume wako”

(Utasema hivi mara nne)

Atakaye yasema haya asubuhi au jioni mara nne Mwenyezi Mungu سبحانه وتعالى atamuepusha na moto.

اللّهُـمَّ ما أَمسي بي مِـنْ نِعْـمَةٍ أَو بِأَحَـدٍ مِـنْ خَلْـقِك ، فَمِـنْكَ وَحْـدَكَ لا شريكَ لَـك ، فَلَـكَ الْحَمْـدُ وَلَـكَ الشُّكْـر

“Ewe Mwenyezi Mungu sikufika jioni na neema yoyote au kati ya kiumbe chako chochote, na neema ila inatoka kwako hali ya kuwa peke yako huna mshirika wako, ni zako sifa njema na nizako shukurani”
Atakae yasema haya kila asubuhi basi atakuwa ametekeleza shukurani ya siku nzima, na atakae yasema jioni atakuwa ametekeleza shukurani ya usiku mzima
اللّهُـمَّ عافِـني في بَدَنـي ، اللّهُـمَّ عافِـني في سَمْـعي ، اللّهُـمَّ عافِـني في بَصَـري ، لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ
اللّهُـمَّ إِنّـي أَعـوذُبِكَ مِنَ الْكُـفر ، وَالفَـقْر ، وَأَعـوذُبِكَ مِنْ عَذابِ القَـبْر ، لا إلهَ إلاّ أَنْـتَ 
“Ewe Mwenyezi Mungu nipe afya ya mwili wangu, Ewe Mwenyezi Mungu nipe afya ya usikizi wangu, Ewe Mwenyezi Mungu nipe afya ya uwoni wangu,hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe”
“Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi najilinda kwako kutokana na ukafiri, na ufakiri, na najilinda kwako kutokana na adhabu ya kaburi, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe” (mara tatu )
حَسْبِـيَ اللّهُ لا إلهَ إلاّ هُوَ عَلَـيهِ تَوَكَّـلتُ وَهُوَ رَبُّ العَرْشِ العَظـيم
“Mwenyezi Mungu ananitosha, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Yeye, kwake Yeye nimetegemea, na Yeye ni Mola wa Arshi Tukufu”
(mara saba)
اللّهُـمَّ إِنِّـي أسْـأَلُـكَ العَـفْوَ وَالعـافِـيةَ في الدُّنْـيا وَالآخِـرَة ، اللّهُـمَّ إِنِّـي أسْـأَلُـكَ العَـفْوَ وَالعـافِـيةَ في ديني وَدُنْـيايَ وَأهْـلي وَمالـي ، اللّهُـمَّ اسْتُـرْ عـوْراتي وَآمِـنْ رَوْعاتـي ، اللّهُـمَّ احْفَظْـني مِن بَـينِ يَدَيَّ وَمِن خَلْفـي وَعَن يَمـيني وَعَن شِمـالي ، وَمِن فَوْقـي ، وَأَعـوذُ بِعَظَمَـتِكَ أَن أُغْـتالَ مِن تَحْتـي
“Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba msamaha na afya duniani na akhera. Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba msamaha na afya katika dini yangu na dunia yangu na jamaa zangu, na mali yangu, Ewe Mwenyezi Mungu nisitiri uchi wangu, na unitulize khofu yangu, Ewe Mwenyezi Mungu nihifadhi mbele yangu, na nyuma yangu, na kulia kwangu, na kushoto kwangu, najuu yangu, na najilinda kwa utukufu wako kwakutekwa chini yangu”
اللّهُـمَّ عالِـمَ الغَـيْبِ وَالشّـهادَةِ فاطِـرَ السّماواتِ وَالأرْضِ رَبَّ كـلِّ شَـيءٍ وَمَليـكَه ، أَشْهَـدُ أَنْ لا إِلـهَ إِلاّ أَنْت ، أَعـوذُ بِكَ مِن شَـرِّ نَفْسـي وَمِن شَـرِّ الشَّيْـطانِ وَشِـرْكِه ، وَأَنْ أَقْتَـرِفَ عَلـى نَفْسـي سوءاً أَوْ أَجُـرَّهُ إِلـى مُسْـلِم
“Ewe Mwenyezi Mungu , Mjuzi wa yaliyofichika na yaliyowazi, muumba wa mbingu na ardhi, Mola wa kila kitu, na Mfalme wake, nakiri kwamba hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, najilinda kwako kutokana na shari ya nafsi yangu na shari ya shetani na shirki yake na kujichumia uovu kwa nafsi yangu au kumletea Muislamu”
بِسـمِ اللهِ الذي لا يَضُـرُّ مَعَ اسمِـهِ شَيءٌ في الأرْضِ وَلا في السّمـاءِ وَهـوَ السّمـيعُ العَلـيم
“Kwa jina la Mwenyezi Mungu ambae hakidhuru kwa jina lake kitu chochote kile kilicho ardhini, wala mbinguni, nae ni Msikivu na ni Mjuzi"
(mara tatu )
رَضيـتُ بِاللهِ رَبَّـاً وَبِالإسْلامِ ديـناً وَبِمُحَـمَّدٍ صََلى الله عليه وسلم نَبِيّـا
“Nimeridhika kuwa Mwenyezi Mungu ndie Mola wangu, na Uislamu ndio dini yangu, na Muhammad صََلى الله عليه وسلم kuwa ni Mtume wangu”
(mara tatu)
يا حَـيُّ يا قَيّـومُ بِـرَحْمَـتِكِ أَسْتَـغـيث ، أَصْلِـحْ لي شَـأْنـي كُلَّـه ، وَلا تَكِلـني إِلى نَفْـسي طَـرْفَةَ عَـين
“Ewe Uliyehai, Uliyesimama kwa dhati yako, kwa rehema zako ninakuomba uniokoe, nitengenezee mambo yangu yote, wala usiniachie mambo yangu mwenyewe (pasina kunisaidia) hata kwa muda (mdogo kama muda) wa kupepesa jicho”
أَمْسَيْـنا وَأَمْسـى المُـلكُ للهِ رَبِّ العـالَمـين ، اللّهُـمَّ إِنِّـي أسْـأَلُـكَ خَـيْرَ هـذهِ اللَّـيْلَة ، فَتْحَهـا ، وَنَصْـرَهـا ، وَنـورَهـا وَبَـرَكَتَـهـا ، وَهُـداهـا ، وَأَعـوذُ بِـكَ مِـنْ شَـرِّ ما فـيهـاِ وَشَـرِّ ما بَعْـدَهـا
“Tumeingia jioni na imefika jioni na Ufalme ni wa Mwenyezi Mungu, Mola wa viumbe vyote, Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakuomba kheri ya usiku huu, ufunguzi wake na nusura yake, na nuru yake na baraka yake, na uongofu wake, na najilinda kwako kutokana na shari ya kilicho ndani ya usiku huu, na shari ya baada ya usiku huu”
أَمْسَيْنا علـى فِطْـرَةِ الإسْلام ، وَعَلـى كَلِـمَةِ الإخْـلاص ، وَعلـى دينِ نَبِـيِّنا مُحَـمَّدٍ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم وَعَاـى مِلَّـةِ أبينـا إِبْـراهيـمَ حَنيـفاً مُسْلِـماً وَمـا كـانَ مِنَ المُشـرِكيـن
“Tumeingia jioni na maumbile ya kiislamu na neno la ikhlasi na dini ya Mtume wetu Muhammad صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم na mila (dini) ya baba yetu Ibrahim iliyo sawa hali yakuwa musilamu wala hakuwa ni mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu “
سُبْحـانَ اللهِ وَبِحَمْـدِه
“Ametakasika Mwenyezi Mungu na sifa njema zote nizake”
(mara mia moja)
لا إلهَ إلاّ اللّهُ وحْـدَهُ لا شَـريكَ لهُ، لهُ المُـلْكُ ولهُ الحَمْـد، وهُوَ على كُلّ شَيءٍ قَدير
“Hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila ni Mwenyezi Mungu peke yake, hana mshirika wake, niwake Ufalme, na nizake sifa njema zote na Yeye juu ya kila kitu ni Muweza”
(mara kumi, au mara moja ukisikia uvivu)
اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْأَلُـكَ عِلْمـاً نافِعـاً وَرِزْقـاً طَيِّـباً ، وَعَمَـلاً مُتَقَـبَّلاً
“Ewe Mwenyezi Mungu, nakuomba elimu yenye kunufaisha, na riziki iliyo nzuri, na ibada yenye kukubaliwa”
أَسْتَغْفِرُ الَّلهَ وَ أَتُوبُ إِلَيْه
“Namuomba msamaha Mwenyezi Mungu na ninarejea Kwake”
(mara mia kwa siku )
Alikuwa Mtume صلى الله عليه وسلم akisema asubuhi na jioni :
أَعُوْذُ بِكَلِماتِ اللَّهِ التَّامَّتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَق
“Najilinda na maneno ya Mwenyezi Mungu yaliyotimia kutokana na shari aliyoiumba”
(mara tatu)
Mwenye kuisema jioni mara tatu hatodhuriwa na mdudu wa sumu (kama nyoka au kitumbo-nge) usiku huo .
اللّهُـمَّ صَلِّ عَلـى مُحمَّـدٍ وَعَلـى أَزْواجِـهِ وَذُرِّيَّـتِه، كَمـا صَلَّيْـتَ عَلـى آلِ إبْراهـيم . وَبارِكْ عَلـى مُحمَّـدٍ وَعَلـى أَزْواجِـهِ وَذُرِّيَّـتِه، كَمـا بارِكْتَ عَلـى آلِ إبْراهـيم . إِنَّكَ حَمـيدٌ مَجـيد
“Ewe Mwenyezi Mungu mrehemu Muhammad, na wake zake, na kizazi chake, kama ulivyowarehemu jamaa wa Ibrahim. Na mbariki Muhammad, na wake zake, na kizazi chake, kama ulivyowabariki jamaa zake Ibrahim, hakika Wewe Umesifika na Umetukuka”
…."Mwenye kuniombea rehema asubuhi mara kumi na jioni mara kumi, nitamuombea shifaa (msamaha) siku ya kiama "

Saturday, 18 July 2015

Sita Za Shawwaal Na Swawm Nyinginezo Baada Ya Ramadhan


Muhammad Baawazir

  
Ndugu Waislam, baada ya kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhwaan, ambao umejaa fadhila nyingi na kheri zisizopatikana katika miezi kumi na moja iliyobaki, kuna umuhimu mkubwa wa kuendeleza zoezi hili la Funga baada ya mwezi huu mtukufu hususan, na kwa mwaka mzima kwa ujumla In shaa Allaah.

 

Swawm kwa ujumla na Swawm za Sunnah haswa ni jambo kubwa sana la ki-'Ibaadah. Na ni bora sana ieleweke ndugu zangu, kuwa Swawm si 'Ibaadah ifanyikayo katika mwezi wa Ramadhwaan pekee, bali ni jambo ambalo linalofanyika mwaka mzima katika nyakati mbalimbali kama tutakavyoona katika makala haya.

 

Kama ilivyo katika ‘Ibaadah ya Swalah, kuna Swalah za Sunnah au Rawaatib au Nawaafil, ambazo ndizo zitakazokuwa viraka siku ya Qiyaamah wakati zile Swalah za Fardh zitakapopelea katika Mizani. Nazo Swawm za kujitolea au za Sunnah, ndizo zitakazomuongezea mja thawabu na ujira pamoja na ile Swawm yake ya Fardh ambayo ni Ramadhwaan.

 

Hapa chini tutaziorodhesha Swawm za SUNNAH ambazo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kazipendekeza kwetu tuzitekeleze:

 

SWAWM YA SIKU SITA ZA MWEZI WA SHAWWAAL

Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhwaan na siku ya 'Iyd ul Fitr. Na Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

((من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر)) رواه مسلم و الترمذي و ابن ماجه, أبو داود وأحمد

((Atakayefunga mwezi wa Ramadhwaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima)).Imepokewa na ma-Imaam Muslim, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Abu Daawuud na Ahmad.

 

'Ulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhwaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhwaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.

Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu.

 

SWAWM YA SIKU YA 'ARAFAH (Kwa wale wasio katika Hajj)

Hadiyth ifuatayo inaonyesha uzito na muhimu wa Swawm ya siku hiyo:

عنْ أَبي قتَادةَ رضِي اللَّه عَنْهُ ، قالَ:سئِل رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِوسَلَّم: عَنْ صَوْمِ يوْمِ عَرَفَةَ؟ قال:يكفِّرُ السَّنَةَ المَاضِيةَ وَالبَاقِيَةَ  رواه مسلمٌ

Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Swawm ya 'Arafah akasema ((Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka uliopo)) [Imepokewa na Muslim].

 

SWAWM YA SIKU TATU KATIKA KILA MWEZI 'AYAAMUL-BIYDHW'

Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

((من صام ثلاثة أيام من كل شهر فذلك صوم الدهر فأنزل الله عز وجل تصديق ذلك في كتابه {من جاء بالحسنة فله عشر أمثالها} فاليوم بعشرة أيام)) رواه الترمذي قال الشيخ الألباني : صحيح

((Yeyote atakayefunga kila mwezi siku tatu,ni sawa amefunga mwaka mzima, kisha Allaah Akashusha Aayah ithibitishayo maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: {{Atakayetenda jambo zuri basi malipo yake ni mara kumi mfano wake}}. Siku moja kwa malipo ya siku kumi))[Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni Sahihi].

 

Ukiitazama Hadiyth hii, utakuta makusudio yaliyotajwa kuwa malipo ya Funga hiyo ya siku tatu za kila mwezi, ni sawa na ya mwaka mzima, ni kuwa, ukipiga hesabu ya hizo siku tatu za kila mwezi, mara miezi kumi na mbili ya mwaka, ni sawa na siku 36. Na siku hizo 36 mara 10 ambazo ndizo malipo ya kila siku kwa mara kumi, basi utapata jumla ya siku 360 ambazo ni takriban idadi ya mwaka mzima wa Kiislam. Fadhila zilizoje na Ujira mrahisi kiasi gani wa kuuchuma ndugu watukufu.

 

Masiku haya matatu, Masiku Meupe ''Ayaamul-Biydhw'', yametajwa katika Hadiyth ifuatayo:

Abu Dharr Al-Ghifaariy anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:  

((يا أبا ذر إذا صمت من الشهر ثلاثة أيام فصم ثلاث عشرة وأربع عشرة  وخمس عشرة)) رواهالترمذي. قال الشيخ الألباني: حسن صحيح  

((Ee Abu Dharr! Endapo utafunga siku tatu za kila mwezi, basi funga siku ya 13, ya 14, na ya 15)) (Hizi huitwa 'Ayaam ul Biydhw' Masiku Meupe kwa sababu katika masiku hayo kunakuwa kweupe zaidi kwa mwanga wa mbalamwezi). [Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni Sahihi].

 

SWAWM YA JUMATATU NA ALKHAMIYS

عن أبي هريرة  رضي الله عنه قال: كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصوم الإثنين والخميس وعندما سئل قال: (( تُعْرَضُ الْأَعْمَالُ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ وَالْخَمِيسِ فَأُحِبُّ  أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ }))  رواه الترمذي وقال حديث حسن

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga Jumatatu na Alkhamiys. Alipoulizwa sababu ya Swawm katika siku hizo, akajibu: ((Matendo ya Wanaadam huwekwa mbele ya Allaah kila siku ya Jumatatu na Alkhamiys, nami napenda matendo yangu yawekwe mbele ya Allaah nikiwa nimefunga)). [Imepokewa At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan].

 

SWAWM YA SIKU YA TAASU'AANA 'AASHURAA

Hizi ni Swawm za siku ya tisa na ya kumi ya mwezi wa Muharram (Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislam). Hizi ni Swawm kwa kumbukumbu na kumshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) kwa kumuokoa Nabii Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) pamoja na watu wake, kutokana na balaa la Fir’awn na jeshi lake.

 

SWAWM NYINGINEZO

Swawm katika mwezi wa Muharram zina fadhila nyingi kama Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwelezea Abu Hurayrah. pia Swawm katika mwezi wa Sha'abaan, ambapo mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) anasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikithirisha sana kufunga.

 

NIYYAH

Swawm kama amali zingine, ni lazima kuwepo na Niyyah ndani yake. Niyyah pahala pake ni moyoni, na si kutamka, ukishapitisha uamuzi wa kufunga, basi hiyo yatosha na si kukariri maneno au kutafuta mtu akufundishe namna ya kuitamka Niyyah kwa Kiarabu au vinginevyo kama wanavyodhania baadhi ya watu.

 

Wa Allaahu A’lam