Monday 23 December 2013

Sababu Zilizosahaulika Za Kujibiwa Du’aa  


Imeandaliwa Na Kuandikwa Na Swaalih Fallaah Al-Mawraqy

Bismi Allahi alrrahmani alrraheemi

KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

Hakika ya kumuomba Mola aliyetukuka aliye juu ni katika vitendo vitukufu na vilo bora.

Amesema Mola aliyetukuka katika ubora wake:

{{Yalaiti iwajiapo adhabu wangenyenyekea kwa kuomba du’aa lakini zimekua ngumu nyoyo zao hazina imaan; Na wamepambiwa na shaytwaan kwa yale wayafanyao.}} [Al-An’aam: 43]

Na akasema Aliyetukuka:

{{Sema kuwaambia hamukukithirisha; kufanya kwa wingi; wala kuzingatia lau mungenyenyekea na kumuomba Yeye katika shida; hakika mumekanusha; mumekataa; kwanini adhabu isiwe lazima kwenu? Mwastahili kuadhibiwa.}} [Al-Furqaan: 77]

Yaani lau musingejali kwa kuomba na kufanya ‘ibaadah kwa wingi.

Na Hadiyth iliyopokewa na at-Tirmidhiy akiisahihisha Shaykh Al-Albaaniy; amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakuna kitu kitukufu  kuliko du’aa; kuomba du’aa.))

Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kutaka kujibiwa du’aa na Mwenyezi Mungu wakati wa shida na dhiki, na azidi kufanya kwa wingi wakati wa raha zake kuomba.)) [Imepokewa na at-Tirmidhy akasema Shaykh Al-Albaaniy ni Hasan]

Na imepokewa na Daylamiy kutoka kwa Anas bin Maalik amesema: Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hamfungulii Mola mja Wake kuomba kisha akamfungia mlango wa kujibiwa, Mola ni Mtukufu hawezi kufanya hivyo.))

Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Mwenye kushindwa katika watu (yaani mpungufu ama dhaifu) ni yule anayeshindwa katika du’aa (mpungufu ama dhaifu wa kuomba du’aa).)) [Imepokewa na at-Twabraaniy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]

Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakuna kinachorudisha hukumu ya Mola isipokuwa du’aa.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy  na akaipendezesha Shaykh Al-Albaaniy]

Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa Mola Aliyetukuka na Aliye juu, kulingana na thamani ya du’aa ya kinga aliyo hukumu Mola kwa mja Wake.

Kwa hivyo amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Du’aa yanufaisha kwa yaliyoteremka na yasiyoteremka, kutoka kwa Allaah.)) [Imepokewa na al-Haakim kutoka kwa Ibnu ‘Umar]

Na amesema Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuusisitiza Ummah wake katika kuomba kwa kila kitu:

((Hakika ataomba mmoja wenu Mola wake haja zake mpaka uzi wa viatu vyake.)) yaonyesha hatodharau kumuomba hata kwa kitu kidogo mfano gani ataomba. [Imepokewa na at-Tirmidhiy na Ibnu Hibbaan kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu).]

Na kujibiwa kwa du’aa kuna sababu nyingi, mwenye kushikana nazo kwa uwezo wa Mola Aliyetukuka na Aliye juu ni sababu ya kuondolewa mazito yake na kutekelezewa haja zake.

Tutazitaja sehemu katika hizo tukitaraji kwa Mola kukubaliwa na kunufaisha.

1) Du’aa uinukapo usingizini usiku ni sababu katika sababu za kujibiwa du’aa. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) zimfikie: Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema:

((Mwenye kuinuka usiku akasema laa ilaaha illa Allaah wahdahu laa shariyka lahu, lahul mulku wa lahul hamdu wa huwa ‘alaa kulli shay-in qadyr, wala hawla wala quwwata illa biLlaah, kisha  akasema  ee Mola nisamehe, ama aombe atakalo atajibiwa, na akitawadha na kuswali itakubaliwa Swalah yake.))

2) Na katika sababu ya kukubaliwa du’aa ni neno: Hakuna Mola isipokuwa Wewe, umetakasika, hakika mimi nimekuwa katika madhaalimu. Imetoka kwa Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Uombezi wa Dhannuun alipoomba naye yupo tumboni mwa samaki ni:

La ilaaha illa anta subhaanaka inniy kuntu mina dhw dwaalimiyn

Hataomba kwa du’aa hiyo Muislam yeyote kwa neno hilo ila atajibiwa du’aa yake.)) [Imepokewa na Tirmidhiy]

3) Kujiepusha na haraam katika kula kunywa na mavazi. Hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa na kutofanya hilo ni sababu ya kutojibiwa. Kwa kujivisha maasi hiyo ni katika sababu kubwa ya kutojibiwa du’aa.

Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((Hakika Mola ni mzuri na hakubali isipokua mazuri... kisha akamtaja mtu aliyekuwa safarini mwake ndefu aliyejawa na vumbi, akainua mikono yake mbinguni: Ee Mola, Ee Mola, na chakula chake ni cha haraam na kinywaji chake haraam, na mavazi yake haraam na nyama yake ya mwili imekuwa kwa haraam. Vipi Mola Aijibu du’aa yake.)) [Imepokewa na Muslim]

Amemuweka mbali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu huyu kuwa hatojibiwa du’aa hata akiomba vipi. Kule kuwa mbali kwake na kujibiwa du’aa ni kuwa katika haraam.

Ameifasiri Ibn Rajab Hadiyth hii kuwa ni dalili kubwa kuwa haikubaliwi ‘amali yoyote wala haitakaswi isipokuwa kwa kula halali. Na kula haraam huharibu kitendo cha mtu na kukataza kupokelewa du’aa na Allaah Aliyetukuka.

Imepokewa na Ikrimah bin ‘Ammaar kutoka kwa Asfar kuwa amesema: Aliambiwa Sa’ad bin Abi Waqaas: Kwa nini du’aa zako katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni zenye kujibiwa? Akasema: “Sitii mdomoni kwangu tonge isipokuwa niijue imetoka wapi, na imekuja kivipi.”

Kutoka kwa Wahaab bin Manbah amesema:

“Mwenye kutaka kujibiwa du’aa yake na Mwenyezi Mungu, kiwe halali chakula chake.”

Fanya pupa ewe ndugu Muislam kiwe chakula chako, kinywji chako, na mavazi yako yawe halali, ili upate kujibiwa du’aa yako na uepuke na moto.

4) Kuomba kwa (kutawasali) du’aa zako kwa kuziunganisha na vitendo vyema, basi hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa.

Dalili ya hilo ni Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika swahiyh yake: Kutoka kwa Ibnu ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Walikuwa watu watatu wakitembea, ikawanyeshea mvua wakajisitiri katika pango, likafunikika mahali pa kutokea jiwe kubwa katika jabali, wakasema wao kwa wao: Angalieni vitendo vyema mulivyofanya mumuombee navyo Mwenyezi Mungu, huenda Akatufariji. Akasema wa kwanza wao: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na wazazi wawili na mke na watoto wadogo nikiwalea, niwaendeapo na maziwa huwaanzia wazazi wangu nikawanywesha kabla watoto wangu. Nilichelewa siku moja sikuja isipokuwa usiku nikawakuta wamelala nikasimama na maziwa kwa kuchukia kuwaamsha, na kuchukia kuwanywesha watoto kabla yao, nikaendelea kusimama mpaka Alfajiri, ikiwa nililifanya hilo kwa ajili yako tuokoe, likafunguka kiasi kidogo cha kuiona mbingu.

Akasema mwengine: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na mtoto wa ‘ammi yangu nikimpenda sana kama vile mwanamume anavyokuwa na mapenzi kumpenda mwanamke. Nikamtaka akanikataa, mpaka siku alitaka dinaar mia, nikamkusanyia kwa taabu nikamletea, nilipotaka kumuingilia aliniambia: Muogope Mwenyezi Mungu ewe mja wa Mungu usiivae pete isipokuwa kwa haki, nikainuka. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, wakafunguliwa.

Akasema mwengine: Hakika mimi nilimuajiri mtu kwa kiasi cha kilo sita ya mchele malipo yake, alipomaliza kazi yake akasema: Nipe malipo yangu, nikampa malipo yake akayakataa, nikawa naikuza kiuchumi mpaka ikaleta faida ya ngo’mbe, akanijia akaniambia muogope Mola wala usinidhulumu haki yangu! Nikamwambia nenda kwa yule ngo’mbe, akaniambia muogope Mungu usinifanyie istihzai (shere), nikamwambia sikufanyii shere mchukue ngo’mbe. Akamchukua akaenda naye. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, likafunguka lote na wakatoka Akawaokoa Mwenyezi Mungu
Amesema Wahab bin Manbah: Mfano wa yule anayeomba bila ya vitendo vyema ni kama mrushaji arushae chombo bila ya kamba. Akasema pia vitendo vyema huipeleka du’aa mbinguni. Kisha akasoma neno la Mola Aliyetukuka:

{{Kwake yeye yapanda kila maneno mazuri [mfano wa du’aa, tasbiih, adhkaar, usomi wa Qur-aan]; na vitendo vyema anavipokea, na kupata thawabu mtendaji.}} [Faatwir: 10] Amesema Qataadah: Hakubali Mwenyezi Mungu neno ila kwa kitendo.

5) Na katika sababu pia ni kuwafanyia wema na mazuri wazazi wawili. Lajulisha hilo kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiih yake kuwa: ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), alikuwa wamjiapo watu wa Yeman anawauliza je hapo kuna Uways bin ‘Aamir? Mpaka alipojiwa na Uways, akamwambia wewe ni Uways bin ‘Aamir, akasema ndio, unatoka Muraad kisha Qarn? Akasema ndio, akasema ulikuwa na mambalanga ukapoa isipokuwa sehemu kama mfano wa dirham? Akasema ndio, akasema una mama? Akasema ndio, akasema nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:

((Atawajia nyinyi Uways bin ‘Aamir pamoja na watu wa Yeman, kutoka Muraad kisha Qarn, yeye ana mambalanga akapozwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa sehemu kama dirham, ana mama anamfanyia wema, lau atawaombea kwa Mwenyezi Mungu atapokelewa du’aa yake, ukiweza akuombee msamaha lifanye hilo.)) nikataka kuombewa msamaha akaniombea.

Na Hadiyth iliyokuja katika Swahiyh Muslim katika Hadiyth ya watu wa Jabalini waliotajwa zamani, walikuwa kuna katika wao wanaojikaribisha kwa Mwenyezi Mungu kwa wema wao wa wazazi wawili, ikawa ni sababu ya kujibiwa du’aa.

6) Katika sababu za kujibiwa du’aa ni kumuombea mtu ndugu yake kwa siri. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiyh yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Du’aa ya mtu kumuombea ndugu yake kwa siri inajibiwa kupitia kwa Malaaikah aliowakilishwa kuwa kila amuombeapo ndugu yake kwa wema, mazuri, anasema Malaika: “Aamiyn nawe upate mfano wake”.))
Hadityh ni nyengine ni ile iliyopokewa na Abu Daawuud katika Sunan yake: Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Hakika du’aa inayojibiwa kwa wepesi, haraka ni ile inayoombwa kumuombea mtu kwa siri.))

7) Na du’aa katika safari hairudishwi kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Maombi matatu ni yenye kujibiwa, haina shaka ndani yake: Du’aa ya mwenye kudhulumiwa, du’aa ya msafiri na du’aa ya mzazi kwa mtoto wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]

Imekuwa du’aa ya msafiri ni yenye kukubaliwa, kwa kule kupata mashaka safarini, taabu na upungufu wa kila kitu akifanyacho kumfanyia Mola wake Aliye na cheo Mwenye nguvu.

8) Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni katika sababu za kujibiwa du’aa. Hili linathibitishwa kupitia Hadiyth ya Hudhayfah bin al-Yamaan kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Naapa kwa Yule nafsi yangu ipo mikononi mwake, mtaamrishana mema na kukatazana mabaya, ama atawaunganishia kwa kuwapa mfano wake Mwenyezi Mungu na kuwateremshia nyinyi adhabu itokayo Kwake, kisha mumuombe Yeye na asiwajibu du’aa zenu.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]

Imepokewa na Ahmad na al-Bazzaar kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

((Enyi watu, hakika Mola Aliyetukuka Aliye juu Anawaambia nyinyi: Amrishaneni mema, na mukatazane mabaya kabla haijafikia kuniomba na nisiwajibu du’aa zenu, na mutake kwangu nisiwapatie, na mutake nusra kwangu nisiwanusuru.))

 
Amesema Ibnu Rajab katika Jaami’ul ‘Uluum Wal-Hikam “Hakika kufanya vitendo vilivyoharamishwa kwa kuendelea, kunazuia kujibiwa du’aa, na hivyo hivyo kuacha yaliyolazimishwa kama vile Hadiyth ilivyotuelekeza kuacha kuamrisha mema na kukataza mabaya ni sababu ya kuzuia kujibiwa du’aa, na yajulisha kufanya kila liloamrishwa inafanya du’aa kujibiwa.”

9) Na sababu ya kujibiwa du’aa ni kurudia Yaa Rabb, Yaa Rabb. Nalo ni jambo kubwa linalotakiwa katika du’aa. Amesema Yaziyd Ruqashiy kutoka kwa Anas: “Hakuna mja yoyote atakaesema: Yaa Rabb, Yaa Rabb, Yaa Rabb isipokuwa  humwambia Mola wake nakuitikia, nakuitikia, nakuitikia.”

Imepokewa na Abu Dardaa na Ibnu ‘Abbaas kuwa wao wawili walikuwa wakisema: Jina kubwa la Mwenyezi Mungu Rabb, Rabb.

Kutoka kwa Atwaa amesema: “Hatosema mja Yaa Rabb, Yaa Rabb mara tatu, isipokuwa Mola humuangalia yeye, akasema je hamusomi Qur-aan? Kisha akasoma neno lake Mola Aliyetukuka:

{{Wale ambao wanamkumbuka kwa kumtaja Mwenyezi Mungu wakiwa wamesimama, wameketi, wamelala kwa ubavu na wanafikiria uumbaji wa mbingu na ardhi wakasema: Ee Mola wetu hukuumba hizi bure bure umetakasika tukinge na adhabu ya moto.}} Mpaka katika neno lake: {{Akawajibu wao Mola wao: Hakika Yangu Mimi sipotezi kitendo cha mtendaji kati yenu.}} [Al-‘Imraan: 191- 195]
Amesema Ibnu Rajab na mwenye kuzingatia du’aa zilizotajwa katika Qur-aan, atazikuta du’aa nyingi zimeanza kwa jina la Rabb kama neno lake:

{{Na katika wao wanaosema Mola wetu, tupe sisi katika dunia mema na Akhera mema na utukinge na adhabu ya moto.}} [Al-Baqarah: 201]

Na neno Lake:

{{Mola wetu usizigeuze kwa kuzipoteza nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na tupe sisi rahmah itokayo Kwako, hakika Yako Wewe ni mwema kwa kutoa.}} [Al-‘Imraan: 8]

10) Na pia imepokewa na AbU Dunya katika kitabu cha Mujaabiyna Fiy Du’aa kutoka kwa Hasan amesema: “Alikuwa mtu katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Answaar amebandikwa jina la Aba Mu-uliq. Alikuwa mfanyabiashara kwa mali yake na wengine akienda nao safarini alikuwa akiinamisha kichwa kwa uchaji Mungu. Siku moja alitoka akakutana na mwizi aliyebeba silaha, akamwambia: Toa ulicho nacho, nitapigana na wewe, akamwambia kwanini waitaka damu yangu? Unalolitaka ni mali, akasema ama mali ni yangu sitaki ila damu yako, akamwambia ikiwa hilo ni lengo lako niwache niswali rakaa nne, akamwambia swali ikiwa huna budi kufanya hilo, akatawadha akaswali rakaa nne, akasema katika sijdah yake ya mwisho kwa kuomba: “Ee Mwenye mapenzi, Mwenye kiti cha enzi, Mtendaji kwa ulitakalo, nakuomba kwa cheo Chako kisichomalizika, na ufalme Wako usio na dhulma, na mwangaza wako uliojaa nguzo za ‘Arshi Yako, unikinge na shari ya mwizi huyu, ewe Msaidizi nisaidie, ewe Msaidizi nisaidie, akasema mara tatu, akatokea mpanda farasi amebeba silaha za vita ameziweka katika farasi wake, alipomuona mwizi alimuelekea akamchoma (akamdunga) na akamuua.

Kisha akamuendea akamwambia inuka. Akamuuliza wewe ni nani, hakika Ameniokoa Mwenyezi Mungu kwa njia yako leo. Akamwambia mimi ni Malaika wa mbingu ya nne uliomba kwa du’aa yako ikagonga mlango wa mbinguni kwa mshindo wake, kisha ukaomba mara ya pili ikasikika vilio vya watu wa mbinguni, kisha uka omba mara ya tatu, nikaambiwa du’aa ya mwenye dhiki. Nikamuomba Mwenyezi Mungu Anipe mimi uwezo wa kumuua. Amesema Hasan: “Mwenye kutawadha akasali rakaa nne na akaomba kwa du’aa hii atajibiwa du’aa yake, mwenye dhiki ama awe hana dhiki (shida).”

11) Na katika sababu za kujibiwa du’aa ni kuchunguza (kujua) wakati wa kujibiwa, na kuwa mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuulinganisha moyo wako unapoomba du’aa - uwe moyo wako upo hapo.

Amesema Ibnu Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu cha Jawaabul-Kaafiy  “Yatakapoungana mambo mawili  kwa muombaji - kuuhudhurisha moyo wake na kupata wakati wa kujibiwa katika wakati sita nao; - thuluth ya mwisho ya usiku, na wakati kunapoadhiniwa, na baina ya adhaan na iqaamah, na mwisho wa kila Swalah tano za faradhi, na apandapo Imaam katika mimbari siku ya Ijumaa mpaka Swalah imalize kuswaliwa, na saa ya mwisho baada ya alaasiri siku ya Ijumaa, na ikapatikana unyenyekevu moyoni  na kujiweka chini mbele ya Mola wake, na kuwa mnyonge, dhaifu, kujielekeza kwa Mola,  na kuelekea Qiblah, na akawa ametawadha (yuko twahara), na akainua mikono yake kwa Mola wake, na akaanza kumshukuru Mola na kumsifu, kisha akafuatiliza kumswalia Muhammad mja Wake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akazitanguliza haja zake, kwa kutubia na kuomba msamaha, kisha akajilazimisha katika kuomba, kwa kujipendekeza kwa Mola wake, katika du’aa zake kwa kuwa na hima na hicho, kwa kuziunganisha kwa majina ya Mola, na sifa Zake, pamoja na kumpwekesha, na akawa du’aa  zake anazifuatanisha na Swadaqah, hakika du’aa hii haitokuwa ni yenye kurudishwa kabisa.

Na rahmah na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad na aali zake na Maswahaba zake na amani.

Thursday 11 April 2013

Majina ya Allah Mazuri Sana

Imeandikwa na: Sheikh Rashid Ashueli.

Mwenyezi Mungu S.W.T. katuamrisha sisi Waislamu katika Kitabu Chake, Qurani Tukufu, tumuombe kwa kutumia majina Yake. Kama alivyosema katika Suratil Israa aya ya 110,
 قُلْ ادْعُوا اللَّهَ أَوْ ادْعُوا الرَّحْمَانَ أَيًّا مَا تَدْعُوا فَلَهُ الأَسْمَاءُ الْحُسْنَى…

Maana yake, “Sema: “Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri…”
Pia Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil A`araaf aya ya 180,
 وَلِلَّهِ الأَسْمَاءُ الْحُسْنَى فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ…

Maana yake, “Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri mazuri; muombeni kwayo. Na waache wale wanaoharibu utakatifu wa majina Yake…”

Na Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi ilyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na Ahmad, “
‘‘إِنَّ لِلَّهِ تِسْعَةً وَتِسْعِينَ اسْمًا ، مِائَةً إِلاَّ وَاحِدًا مَنْ أَحْصَاهَا دَخَلَ الْجَنَّةَ’’

Maana yake, “Hakika Mwenyezi Mungu ana majina tisini na tisa. Majina mia isipokuwa moja. Atakayeyahifadhi (majina haya na kujua maana yake) ataingia Peponi.”
Pia Mtume S.A.W. kasema katika Hadithi ilyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na iliyotolewa na L-Bukhari, “
‘‘لِلَّهِ تِسْعَةٌ وَتِسْعُونَ اسْمًا ، مِائَةٌ إِلاَّ وَاحِدًا ، لا يَحْفَظُهَا أَحَدٌ إِلاَّ دَخَلَ الْجَنَّةَ’’

Maana yake, “Mwenyezi Mungu ana majina tisini na tisa. Majina mia isipokuwa moja. Hakuna atakayeyahifadhi (majina hayo na kujua maana yake) isipokuwa ataingia Peponi.”

Ingawa Mwenyezi Mungu Mtukufu katuelezea kwamba majina Yake ni tisini na tisa, lakini hata hivyo majina Yake ni zaidi kuliko hivyo. Hakuna mtu yeyote yule hapa duniani anayeyajua majina Yake yote isipokuwa Mwenyewe Muumba wa mbingu na ardhi. Na Majina haya tisini na tisa yanatafsiri sifa Zake nzuri ambazo sifa hizo hazilingani na sifa za viumbe Wake. Ndio maana Mwenyezi Mungu S.W.T. katuamrisha wakati tunapotaka kumuomba basi kwanza kabla ya kuomba dua tumuombe kwa majina hayo, halafu tuombe tunachotaka kuomba. Na wakati wa kumuomba tuwe katika tohara na moyo na kiwiliwili vimnyenyekee Mola Mtukufu, wala tusijishughulishe na mambo mengine.
Ndio maana Mtume S.A.W. kasema,
“Mwenyezi Mungu hapokei dua ya mtu yule moyo wake umeghafilika wakati anapoomba.”
Na majina hayo tisini na tisa yametajwa na Mtume S.A.W. kama yalivyokuja katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Huraira R.A.A. na kutolewa na Ttirmidhi.
Na anayetaka kuomba dua kwanza asome,
“AUDHU BILLAAHI MINA SHAITAANI RRAJIYM. BISMI LLAAHI RRAHMAANI RRAHIYM: ALLAAHUMMA INNIY ATAWAJJAHU ILAIKA BIASMAA-IKAL HUSNAA YAA MAN HUWA, “
‘‘اللَّهُ الَّذِي لا إِلَهَ إِلاَّ هُوَ ، الرَّحْمَنُ ، الرَّحِيمُ ، الْمَلِكُ ، الْقُدُّوسُ ، السَّلامُ الْمُؤْمِنُ ، الْمُهَيْمِنُ ، الْعَزِيزُ ، الْجَبَّارُ ، الْمُتَكَبِّرُ ، الْخَالِقُ ، الْبَارِئُ ، الْمُصَوِّرُ ، الْغَفَّارُ ، الْقَهَّارُ ، الْوَهَّابُ ، الرَّزَّاقُ ، الْفَتَّاحُ ، الْعَلِيمُ ، الْقَابِضُ ، الْبَاسِطُ ، الْخَافِضُ ، الرَّافِعُ ، الْمُعِزُّ ، الْمُذِلُّ ، السَّمِيعُ ، الْبَصِيرُ ، الْحَكَمُ ، الْعَدْلُ ، اللَّطِيفُ ، الْخَبِيرُ ، الْحَلِيمُ ، الْعَظِيمُ ، الْغَفُورُ ، الشَّكُورُ ، الْعَلِيُّ ، الْكَبِيرُ ، الْحَفِيظُ ، الْمُقِيتُ ، الْحَسِيبُ ، الْجَلِيلُ ، الْكَرِيمُ ، الرَّقِيبُ ، الْمُجِيبُ ، الْوَاسِعُ الْحَكِيمُ ، الْوَدُودُ ، الْمَجِيدُ ، الْبَاعِثُ ، الشَّهِيدُ ، الْحَقُّ ، الْوَكِيلُ ، الْقَوِيُّ ، الْمَتِينُ ، الْوَلِيُّ ، الْحَمِيدُ ، الْمُحْصِي ، الْمُبْدِئُ ، الْمُعِيدُ ، الْمُحْيِي ، الْمُمِيتُ ، الْحَيُّ ، الْقَيُّومُ ، الْوَاجِدُ ، الْمَاجِدُ ، الْوَاحِدُ ، الصَّمَدُ ، الْقَادِرُ ، الْمُقْتَدِرُ ، الْمُقَدِّمُ ، الْمُؤَخِّرُ ، الأَوَّلُ ، الآخِرُ ، الظَّاهِرُ ، الْبَاطِنُ ، الْوَالِيَ ، الْمُتَعَالِي ، الْبَرُّ ، التَّوَّابُ ، الْمُنْتَقِمُ ، الْعَفُوُّ ، الرَّءُوفُ ، مَالِكُ الْمُلْكِ ذُو الْجَلالِ وَالإِكْرَامِ ، الْمُقْسِطُ ، الْجَامِعُ ، الْغَنِيُّ ، الْمُغْنِي ، الْمَانِعُ ، الضَّارُّ ، النَّافِعُ ، النُّورُ ، الْهَادِي ، الْبَدِيعُ ، الْبَاقِي ، الْوَارِثُ ، الرَّشِيدُ ، الصَّبُوْرُ’’

ALLAAHU LLADHIY LAA ILAAHA ILLA HUWA (Yeye Ndiye Mwenyezi Mungu Ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu), ARRAHMAANU (Mwingi wa rehema), ARRAHIYMU (Mwenye kurehemu), AL-MALIKU (Mfalme wa milele), AL-QUDDUWSU (Mtakatifu, ametakasika na sifa zote chafu), ASSALAAMU (Mwenye kuleta amani), AL-MU-UMINU (Mtoaji wa amani), AL-MUHAYMINU (Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo Yake), AL-`AZIYZU (Mshindi katika mambo Yake), AL-JABBAARU (Anayefanya analolitaka), AL-MUTAKABBIRU (Mkubwa), AL-KHAALIQU (Muumbaji), AL-BAARI-U (Mtengenezaji), AL-MUSAWWIRU (Mtia sura), AL-GHAFFAARU (Mwenye kusamehe), AL-QAHHAARU (Mwenye nguvu juu ya kila kitu), AL-WAHHAABU (Mpaji mkuu), ARRAZZAAQU (Mwenye kuruzuku), AL-FATTAAHU (Hakimu), AL-`ALIYMU (Mjuzi wa kila kitu), AL-QAABIDHU (Mwenye kunyima au kuzuia), AL-BAASITU (Mwenye kutoa), AL-KHAAFIDHU (Mfedheheshaji waovu), ARRAAFI`U (Mpandisha daraja), AL-MU`IZZU (Mtoa heshima kwa amtakaye), AL-MUDHILLU (Mnyima heshima kwa amtakaye), ASSAMIY`U (Mwenye kusikia), AL-BASIYRU (Mwenye kuona), AL-HAKAMU (Mwenye kuhukumu), AL-`ADLU (Muadilifu), AL-LLATIYFU (Mwenye kujua yaliyofichikana), AL-KHABIYRU (Mwenye kujua yaliyo dhahiri), AL-HALIYMU (Mpole), AL-`ADHIYMU (Aliye Mkuu), AL-GHAFUWRU (Mwingi wa kusamehe), ASHAKUWRU (Mwenye kushukuru), AL-`ALIYYU (Aliye juu), AL-KABIYRU (Aliye mkuu), AL-HAFIYDHU (Mwenye kuhifadhi), AL-MUQIYTU (Mlinzi), AL-HASIYBU (Mwenye kuhesabu), AL-JALIYLU (Wa hali ya juu), AL-KARIYMU (Mkarimu wa hali ya juu), ARRAQIYBU (Mchungaji), AL-MUJIYBU (Mwenye kujibu), AL-WAASI`U (Mwenye wasaa), AL-HAKIYMU (Mwenye hekima), AL-WADUWDU (Mwenye kupenda waja Wake), AL-MAJIYDU (Mwenye utukufu), AL-BAA`ITHU (Mfufuaji), ASHAHIYDU (Mwenye kushuhudia kila kitu), AL-HAQQU (Wa Haki), AL-WAKIYLU (Mtegemewa), AL-QAWIYYU (Mwenye nguvu), AL-MATIYNU (Aliye madhubuti), AL-WALIYYU (Mlinzi na Msaidizi), AL-HAMIYDU (Mwenye kusifika na kila sifa njema), AL-MUHSIYU (Mwenye kuhesabu), AL-MUBDI-U (Mwenye kuanzisha), AL-MU`IYDU (Mwenye kurejeza), AL-MUHYIYU (Mwenye kuhuisha), AL-MUMIYTU (Mwenye kufisha), AL-HAYYU (Mwenye uhai wa milele), AL-QAYYUWMU (Msimamia kila jambo), AL-WAAJIDU (Mtambuzi), AL-MAAJIDU (Wa kuheshimiwa), AL-WAAHIDU (Mmoja tu), ASSAMADU (Mwenye kukusudiwa kwa kuabudiwa), AL-QAADIRU (Mwenye uwezo wa kufanya au kutokufanya), AL-MUQTADIRU (Mwenye uwezo wa pekee juu ya kila kitu), AL-MUQADDIMU (Mwenye kutanguliza), AL-MU-AKHIRU (Mwenye kuakhirisha), AL-AWWALU (Wa Mwanzo), AL-AAKHIRU (Wa Mwisho), ADHAAHIRU (Wa Dhahiri), AL-BAATINU (Wa Siri), AL-WAALIYA (Mpanga mipango ya watu), AL-MUTA`AALI (Mtukufu Aliye juu), AL-BARRU (Mwema), ATTAWWAABU (Mwenye kupokea toba za waja Wake), AL-MUNTAQIMU (Mlipa kisasi kwa waovu), AL-`AFUWWU (Mwenye kusamehe madhambi), ARRAUFU (Mwenye huruma), MAALIKU L-MULKI DHUL JALAALI WAL IKRAAMI (Mfalme wa wafalme Mwenye utukufu na heshima), AL-MUQSITU (Mtoaji haki sawa kwa kila anayestahiki), AL-JAAMI`U (Mkusanyaji viumbe siku ya Mwisho), AL-GHANIYYU (Tajiri), AL-MUGHNIYU (Mwenye kutajirisha), AL-MAANI`U (Mwenye kuzuia viumbe visidhurike), ADHAARRU (Mwenye kudhurisha), ANNAAFI`U (Mwenye kuleta nafuu), ANNUWRU (Mwenye nuru), AL-HAADIY (Mwongozaji wa kheri), AL-BADIY`U (Mzuaji), AL-BAAQIYU (Mwenye kubakia milele), AL-WAARITHU (Mwenye kurithi kila kitu), ARRASHIYDU (Mwenye kuongoa waja kuiendea njia ya kheri), ASSABUWRU (Mwenye kusubiri).”

Wednesday 10 April 2013

Uvutaji Sigara


Uvutaji wa sigara umeenea na kushamiri dunia nzima licha ya kuwa madhara yake yapo wazi.  Baadhi ya Waislamu wametumbukia katika balaa hili na kuziathiri nyumba zao bila ya kujijua. Kuna sababu tosha zenye kuonyesha uharamu wa jambo hili kwa Muislamu.  Sigara ina athari sana katika dini, afya, mazingira, familia, rasilimali na mengineyo.
 
i.              MADHARA KATIKA DINI
 
Sigara inaathiri  ibada ya mja na inapunguza malipo ya ibada hiyo.  Kwa mfano ibada ya sala ambayo ni nguzo muhimu ya Muislamu;   Kutokana na hadithi iliyosimuliwa na wengi; Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi wa Ssalam
 
 “Mwenye kula Kitungu maji au thawm, basi asiukaribie Msikiti wetu na akae nyumbani”
[Bukhari na Muslim]
 
Tunaona makatazo yamekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na vitu hivyo amabayo huwakirihisha watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini).
 
Bila ya shaka mdomo wa mvutaji sigara una harufu mbaya zaidi  kuliko vitunguu, ima huwakera watu na Malaika kwa harufu hiyo au kukosa fadhila za sala ya jamaa msikitini kwa mwanamme.
 
i.              MADHARA KATIKA MWILI
 
Hakuna anaepinga madhara ya sigara katika mwili wa binadam.  Utafiti wa kiafya umeyaona haya na kuyaeleza kwa kina; hata imekuwa ni sheria kuweka wazi  maandishi ya tahadhari kwa kila paketi la sigara angalau watu wazinduke.
 
Ndani ya sigara hupatikana kemikali zenye sumu kama vile nicotine, arsenic, carbon monoxide na vyenginevyo ambavyo mvutaji huathirika kidogo kidogo hadi kuua sehemu muhimu za mwili wake.  Athari za zake ni kubwa na ni nyingi; husababisha cancer, TB, mshituko wa moyo, pumu, ubovu wa meno, na huwa ni  chimbuko la  maradhi mengi mengineyo.
 
Allaah Alietukuka anatuonya tusiwe wenyenye kujidhuru.  Suuratu Nnisaa’:29
 
وَلَا تَقۡتُلُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِكُمۡ رَحِيمً۬ا

Wala msijiue, hakika Allah ni mwenye kukurehemuni

 Pia katika Suuratul Baqarah:195
 
وَلَا تُلۡقُواْ بِأَيۡدِيكُمۡ إِلَى ٱلتَّہۡلُكَةِ

Wala msjiitie kwa mikono yenu katika maangamizo
 
Na Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema katika Hadithi:
 
" لا ضرر ولا ضرار "
 
Kusiwe na kudhuriana wala kulipa dhara.
 
 
ii.    ATHARI KWA AKILI NA MATAMANIO
 
Sigara huathiri akili ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa.  Mvutaji mzoefu  anapoikosa  huwa vigumu kwake kufikiri kitu, kutatua tatizo au kuwa makini katika jambo mpaka aipate.  Badala kuwa mtumwa wa Mola wake, hugeuka na kuwa mateka wa sigara yake na kuifanya dhaifu akili na hisia zake.
 
Allah Subhaanahu wa Ta’ala anatueleza katika Suuratu An-Nisaa’:27
 
وَٱللَّهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيۡڪُمۡ وَيُرِيدُ ٱلَّذِينَ يَتَّبِعُونَ ٱلشَّہَوَٲتِ أَن تَمِيلُواْ مَيۡلاً عَظِيمً۬ا

Allah anataka kukukhafifishieni.  Lakini wanaofuata matamanio yao wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa
 
iii.           MADHARA KATIKA MALI
 
Mvutaji sigara hupoteza pesa nyingi karibu kila siku kununulia sigara isiyomletea tija yeyote bali ni kuwafaidisha hao wanaoendesha bishara hii haramu.  Kumbuka kuwa mali tunayoipata tutakuja kuulizwa kwa njia gani tumeichuma na vipi tumeitumia.
 
Katika Suurat An-nisaa’:5  Allah Subhaanahu Wata’ala anatueleza:
 
وَلَا تُؤۡتُواْ ٱلسُّفَهَآءَ أَمۡوَٲلَكُمُ ٱلَّتِى جَعَلَ ٱللَّهُ لَكُمۡ قِيَـٰمً۬اوَٱرۡزُقُوهُمۡ فِيہَا

Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allah amezijaalia kwa maisha yenu
Pia katika Suuratul Israa:26 – 27
 
وَلَا تُبَذِّرۡ تَبۡذِيرًا  إِنَّ ٱلۡمُبَذِّرِينَ كَانُوٓاْ إِخۡوَٲنَ ٱلشَّيَـٰطِينِ‌ۖ

Wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu.  Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani
 
Na kutoka kwa Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema:
 
" إن الله ينهاكم عن قيل وقال ، وكثرة السؤال  وإضاعة المال

Hakika Allah anakukatazeni na mazungumzo yasiyokuwa na faida (huyu kasema au kimesemwa) na kukithirisha kuuliza masuali na kupoteza mali
.
Licha ya nchi za Magharibi kutoa indhaari tu katika paketi kuonesha madhara ya sigara, Maulamaa wa kiislamu takriban wote wamekubaliana kwamba sigara ni haraam. Angalia Fatwa ifuatayo kutoka katika Fataawa Islaamiyah 442/3
 
Kuvuta sigara ni haraam kwa sababu ya kuleta madhara mengi  wakati Allah Subhaanahu Wata’ala amehalalisha kwa waja wake vyote vilivyo vizuri katika vyakula na vinywa na akaharamisha vibaya vyao. Na aina zote za uvutaji ni miongoni mwa vitu vibaya  kwa sababu ya kuleta madhara na kulewesha.
 
Ni vyema kutanabahi ndugu Muislamu na kuachana na mazoea sugu na potofu ya kuvuta sigara. Mvutaji sigara huwa hajali kuvuta mbele ya wale waliomzunguka ndani ya nyumba yake, kama mkewe/mumewe, watoto na wengineo. Huwasababishia kuvuta moshi wa sumu na wale walio karibu nae. Huleta hali mbaya hasa kwa mazingira ya ndani ya nyumba na ni mfano mbaya kwa kile kinachochungwa (mke na watoto) ndani ya nyumba hiyo.
 
Ndugu yangu Muislamu , kama ni miongoni mwa wenye kuendeleza uovu huu basi rudi kwa Mola wako kwa moyo ulio mwepesi wenye kusikiliza nasaha na kukubali yale yote yanayotoka kwa Mola kwa ajili ya kuinusuru nafsi yako kwanza, kisha dini yako, kisha akili yako, kisha familia yako, kisha mali yako na kadhalika.

Tuesday 9 April 2013

Yenye kuhatarisha nyumba

Imeandikwa na:   Ummu Nassra


BISMILLAHIR-RAHMAANIR-RAHIIM

UTANGULIZI

Hakika shukrani zote ni zake Allaah Subhaanahu Wata’ala, tunaemshukuru, tunaemtegemea, kumtaka msamaha na kutubu kwake. Tunajikinga Kwake Allaah Subhaanahu Wata’ala kutokana na shari za nafsi zetu na makosa ya matendo yake. Mwenye kuongolewa na Allaah hakuna wa kumpotoa, na mwenye kumpotoa hakuna wa kumuongoa.  Rehma na Amani ziwe juu ya kipenzi chetu Muhammad SwallaAllahu ‘Alayhi wa Aalihi wa Sallam.

‘Amma Ba’ad

Nyumba ni neema kubwa ambayo mwanadamu amebarikiwa, [An-Nahl 16:80]

وَٱللَّهُ جَعَلَ لَكُم مِّنۢ بُيُوتِڪُمۡ سَكَنً۬ا

Na MwenyeziMungu amekujaalieni majumba yenu yawe maakaazi (yenu)

Kuweka mazingira sahihi ndani ya majumba ni jukumu la kila muislam mume na mke, na ni lazima mazingira hayo yaoane sambamba na sheria alizotuwekea Allah Subhanahu wa Ta’ala.   Moja kati ya njia ya kuyafikia hayo ni kuepukana na  kila aina ya uovu na uharibifu ndani ya majumba. 

Kuna sababu nyingi kwa mwenye kuamini kuwa makini katika kuijenga na kuilinda nyumba yake katika misingi mema ya kiislam.  Miongoni mwa sababu hizo ni:

1.    Kujilinda yeye pamoja na familia yake kutokana na moto wa jahannam,  na kujiweka mbali na ghadhabu zake. [At-Tahriym 66:6]


يَـٰٓأَيُّہَا ٱلَّذِينَ ءَامَنُواْ قُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ وَأَهۡلِيكُمۡ نَارً۬ا وَقُودُهَا ٱلنَّاسُ وَٱلۡحِجَارَةُ


Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu na moto ambao ambao kuni zake ni watu  na mawe.

2.    Kujua wajibu wake juu ya jukumu la kuchunga nyumba, na kujiweka tayari kujibu kwa kila unachokichunga.  Hadith:

Kutoka kwa Abdullah, Allah amuwie radhi, kwamba  Mtume SwallaAllahu ‘Alayhu wa Aalihi wa Ssallam amesema:

“Nyote ni wachunga na nyote mtaulizwa juu ya mlivyovichunga. Kiongozi anaewaongoza watu ni mchunga na ataulizwa juu wachungwa wake. Mwanamume ni mchunga kwa watu wake wa nyumbani na ataulizwa juu ya wachungwa wake. Na mwanamke ni mchunga kwa nyumba ya mumewe na watoto wake nae ataulizwa juu ya wachungwa wake .Mtumwa ni mchunga katika mali ya bwana wake na anawajibika juu ya mali hiyo. Hakika nyote ni wachunga na na kila mmoja wenu anawajibika juu ya wachungwa wake”   

 

                                                                                             

Imesimuliwa na Bukhari na Muslim

3.    Nyumba ni sehemu ya hifadhi kwa binaadamu, kujiweka mbali na kila aina ya ubaya na uovu ukiwa wa mnyama, binaadamu au majini, na kupata utulivu ndani yake.  Amesema Mtume SwallaAllahu ‘Alayhu wa Ssallam: 

Usalama wa mtu katika wakati wa fitnah ni kubakia nyumbani kwake.

Kilicho muhimu zaidi ni kuzingatia kuwa nyumba ni sehemu nyeti (muhimu) ya kujenga mazingira mazuri ya kiislam, kwani jamii bora hujengeka kuanzia nyumbani.   Kwa masikitiko makubwa majumba yetu mengi yamejiweka mbali na mafundisho sahihi ya kiislam. 

InshaAllaah katika makala hizi tutaweza kugusia na kutanabahisha baadhi ya vitu ambavyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibika mfumo wa kiislam ndani ya majumba na jamii kwa ujumla, na kujaribu kutafuta njia muafaka kurejesha mazingira mazuri ndani ya majumba yetu.

Kuna mambo mengi ya wazi kabisa ambayo sheria yameyakataza katika Uislamu na jamii imeghafilika nayo.  Mambo hayo huchangia  kuharibika na kuhatarisha mfumo  mzima wa kiislam ndani ya majumba.  Miongoni mwa yenye kuhatarisha ni haya yafuatayo:

 

TELEVISHENI (TV) - LUNINGA.

  

Televisheni kama inavyojuilikana (TV) ni chombo ambacho hakikosekani katika kila nyumba.  Kama kitatumika vizuri chombo hicho kwa mambo ya kheri yenye kuzidisha imani, kupeleka dini mbele, kukuweka mbali na maasi na kuhifadhi dini ya mja kinaweza kuleta faida.  Na kama kitatumika vibaya kinaweza kuathiri familia kwa asilimia kubwa kabisa.

Ukweli ni kuwa kuangalia TV kuna madhara mengi na makubwa kuliko faida. Familia za kiislam zinaogelea kwa kasi kubwa bila ya kujali au kuona mabaya ya chombo hicho. 

Tuchukue mfano mdogo tu wa athari za televisheni kwa watoto kama utafiti huu mdogo uliofanyika hapa Uingereza unavyofafanua.

 

Watoto wenye kuangalia televisheni kwa zaidi ya masaa mawili kila siku wanakabiliwa na hatari ya kupatwa na ugonjwa wa athma. Uchunguzi huo umeonyesha kuwa, kuangalia televisheni kwa muda mrefu kunaleta uwezekano wa kupata athma uongezeke mara mbili kwa watoto.

Jinsi mfumo wa kupumua unavyofanya kazi wakati mtoto anapokaa tu bila kufanya chochote, hupelekea kutokea mabadiliko katika mapafu pamoja na magojwa mengine ya kupumua ikiwemo athma.

Unene wa kupita kiasi pamoja na kutokufanya mazoezi kunakosababishwa na kuangalia muda mrefu televisheni hupelekwa kutokea hali hiyo Wataalamu wamesema kuwa, kuishi maisha ya kutokuwa na harakati yoyote katika umri mdogo hupelekea kuongezeka uwezekano wa hatari ya kupata athma ukubwani.

Hivyo wamewashauri wazazi kuwashajiisha watoto wao kufuata maisha ya kawaida ya kuwa na mishughuliko na kupunguza muda wanaoutumia kuangalia TV.

Wataalamu wa Uingereza wametoa taarifa hiyo baada ya kuwafanyia uchunguzi watoto 3,000  kuanzia wale waliozaliwa mpaka walio na miaka 11.

Hasara moja ya kupoteza muda kuangalia TV inaweza kuzaa makosa mengi ndani yake.  Kuona na kusikiliza kunawavutia wengi na kuwafanya watu kutawaliwa na tabia hiyo na kutoweza kuiepuka.  Hakuna shaka kuwa jamii hasa watoto imeathirika sana na jambo hili.  TV inasababisha kwa kiasi kikubwa watoto wa Kiislamu kutumbukia katika tabia zisizo na maadili, ulevi, uzinzi, kukosa heshima, kujinasibisha na uzungu na mengi mengine maovu tunayoyaona katika jamii zetu.  Yote hayo wanayaona na kujifunza moja kwa moja kutoka kwenye TV.

Mtu huhisi kuwa anapoteza wakati tu kujistarehesha na TV, anayakata masaa na dakika kwa ajili ya chombo hicho, ni makosa!!.  TV si chombo cha starehe, bali ni chombo kinachotumika kuchochea hisia, kubadilisha muelekeo na utiifu wa mtu. Na ndiyo hali halisi ndugu yangu Muislamu kama bado hujatanabahi.


Yafaa Waislamu tuzinduke na kuziona faida chache na hasara nyingi za chombo hiki.  Kama tunaona ni neema hakika tutakuja kuulizwa namna tulivyoitumia.  [At-Takaathur 102:8]

ثُمَّ لَتُسۡـَٔلُنَّ يَوۡمَٮِٕذٍ عَنِ ٱلنَّعِيمِ

Kisha mtaulizwa siku hiyo juu ya neema mlizopewa mlizitumiaje.

Na kwa hakika hata  masikio na macho tunayoyatumia kwa chombo hicho pia tutakuwa ni wenye kuulizwa. Hivyo ni juu yetu kuchagua ni kipi cha kutizama. [Al-Israa 17:36]. 

إِنَّ ٱلسَّمۡعَ وَٱلۡبَصَرَ وَٱلۡفُؤَادَ كُلُّ أُوْلَـٰٓٮِٕكَ كَانَ عَنۡهُ مَسۡـُٔولاً

Hakika masikio na macho na moyo, hivyo vyote vitaulizwa

Tv ni kama upanga ukiutumia vizuri unaweza kuleta faida na ukiitumia vibaya unaweza kuleta madhara makubwa.  Kwa mfano mtu akiweza kuidhibiti na kuangalia kwa nadra kwa vipindi vya kheri vyenye kwenda sambamba na dini yetu inaweza kukubalika, bali ni wachache wenye kufanya hivyo.  Wengi wao wameogolea na kuangalia tu bila hata ya kujali faida na hasara zake, na hii ndio iliopelekea madhara kuwa mengi kuliko faida.



 Miongoni mwa madhara ya TV ni:

-      Kunapoteza wakati bure na kupuuza mengi ya wajibu

-      Inaeneza tamaduni za kikafiri kama ni njia moja ya kuigwa katika maisha

-      Inaeneza upotofu na uhuru kwa kupitia katika michezo, nyimbo matangazo yasiyo ya heshima ambayo hupelekea watizamaji kutumbuka na tabia hizo za kijinga.

-      Mazoea ya kuangalia TV yanaharibu akili na kuathiri afya ya mja.


Hivyo kama kuna watu wazuri wenye kumuogopa Allah  Subhaanahu Wata’ala na kuonyesha mazuri yenye faida bila ya kukiuka mipaka ya Allah, basi unaweza kuangalia na ni jambo la kupendeza kwa wengi. Ni vyema kuchunga aina gani ya vipindi tunavyoangalia ndani ya majumba yetu.

Ni wajibu wa kila mtu kueleweka wazi madhara na faida ya kifaa hichi ili tuweze kukitumia vyema ama kujiepusha nacho kabisa ikiwa tutashindwa kuweka vidhibiti katika majumba jinsi chombo hiki kitumike katika kunufaisha, kuelimisha na kuleta faida na si kuharibu, kupoteza muda na kupelekea jamii iliyozugika na hatimaye kupotoka na kupotosha wengine. 

 

 

 

UVUTAJI SIGARA

Uvutaji wa sigara umeenea na kushamiri dunia nzima licha ya kuwa madhara yake yapo wazi.  Baadhi ya Waislamu wametumbukia katika balaa hili na kuziathiri nyumba zao bila ya kujijua. Kuna sababu tosha zenye kuonyesha uharamu wa jambo hili kwa Muislamu.  Sigara ina athari sana katika dini, afya, mazingira, familia, rasilimali na mengineyo.

i.              MADHARA KATIKA DINI

Sigara inaathiri  ibada ya mja na inapunguza malipo ya ibada hiyo.  Kwa mfano ibada ya sala ambayo ni nguzo muhimu ya Muislamu;   Kutokana na hadithi iliyosimuliwa na wengi; Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi wa Ssalam

 “Mwenye kula Kitungu maji au thawm, basi asiukaribie Msikiti wetu na akae nyumbani”

[Bukhari na Muslim]

Tunaona makatazo yamekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na vitu hivyo amabayo huwakirihisha watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini).   

Bila ya shaka mdomo wa mvutaji sigara una harufu mbaya zaidi  kuliko vitunguu, ima huwakera watu na Malaika kwa harufu hiyo au kukosa fadhila za sala ya jamaa msikitini kwa mwanamme.

 

i.              MADHARA KATIKA MWILI

Hakuna anaepinga madhara ya sigara katika mwili wa binadam.  Utafiti wa kiafya umeyaona haya na kuyaeleza kwa kina; hata imekuwa ni sheria kuweka wazi  maandishi ya tahadhari kwa kila paketi la sigara angalau watu wazinduke.

Ndani ya sigara hupatikana kemikali zenye sumu kama vile nicotine, arsenic, carbon monoxide na vyenginevyo ambavyo mvutaji huathirika kidogo kidogo hadi kuua sehemu muhimu za mwili wake.  Athari za zake ni kubwa na ni nyingi; husababisha cancer, TB, mshituko wa moyo, pumu, ubovu wa meno, na huwa ni  chimbuko la  maradhi mengi mengineyo.

Allaah Alietukuka anatuonya tusiwe wenyenye kujidhuru.  Suuratu Nnisaa’:29

وَلَا تَقۡتُلُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِكُمۡ رَحِيمً۬ا

Wala msijiue, hakika Allah ni mwenye kukurehemuni

 Pia katika Suuratul Baqarah:195

وَلَا تُلۡقُواْ بِأَيۡدِيكُمۡ إِلَى ٱلتَّہۡلُكَةِ

Wala msjiitie kwa mikono yenu katika maangamizo

Na Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema katika Hadithi:

" لا ضرر ولا ضرار "

Kusiwe na kudhuriana wala kulipa dhara.

 

ii.            ATHARI KWA AKILI NA MATAMANIO

Sigara huathiri akili ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa.  Mvutaji mzoefu  anapoikosa  huwa vigumu kwake kufikiri kitu, kutatua tatizo au kuwa makini katika jambo mpaka aipate.  Badala kuwa mtumwa wa Mola wake, hugeuka na kuwa mateka wa sigara yake na kuifanya dhaifu akili na hisia zake. 

Allah Subhaanahu wa Ta’ala anatueleza katika Suuratu An-Nisaa’:27

وَٱللَّهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيۡڪُمۡ وَيُرِيدُ ٱلَّذِينَ يَتَّبِعُونَ ٱلشَّہَوَٲتِ أَن تَمِيلُواْ مَيۡلاً عَظِيمً۬ا

Allah anataka kukukhafifishieni.  Lakini wanaofuata matamanio yao wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa

 

iii.           MADHARA KATIKA MALI

Mvutaji sigara hupoteza pesa nyingi karibu kila siku kununulia sigara isiyomletea tija yeyote bali ni kuwafaidisha hao wanaoendesha bishara hii haramu.  Kumbuka kuwa mali tunayoipata tutakuja kuulizwa kwa njia gani tumeichuma na vipi tumeitumia. 

Katika Suurat An-nisaa’:5  Allah Subhaanahu Wata’ala anatueleza:

وَلَا تُؤۡتُواْ ٱلسُّفَهَآءَ أَمۡوَٲلَكُمُ ٱلَّتِى جَعَلَ ٱللَّهُ لَكُمۡ قِيَـٰمً۬ا وَٱرۡزُقُوهُمۡ فِيہَا

Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allah amezijaalia kwa maisha yenu

Pia katika Suuratul Israa:26 – 27

وَلَا تُبَذِّرۡ تَبۡذِيرًا  إِنَّ ٱلۡمُبَذِّرِينَ كَانُوٓاْ إِخۡوَٲنَ ٱلشَّيَـٰطِينِ‌ۖ

Wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu.  Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani

 

Na kutoka kwa Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema:

" إن الله ينهاكم عن قيل وقال ، وكثرة السؤال  وإضاعة المال

Hakika Allah anakukatazeni na mazungumzo yasiyokuwa na faida (huyu kasema au kimesemwa) na kukithirisha kuuliza masuali na kupoteza mali.

Licha ya nchi za Magharibi kutoa indhaari tu katika paketi kuonesha madhara ya sigara, Maulamaa wa kiislamu takriban wote wamekubaliana kwamba sigara ni haraam. Angalia Fatwa ifuatayo kutoka katika Fataawa Islaamiyah 442/3

Kuvuta sigara ni haraam kwa sababu ya kuleta madhara mengi  wakati Allah Subhaanahu Wata’ala amehalalisha kwa waja wake vyote vilivyo vizuri katika vyakula na vinywa na akaharamisha vibaya vyao. Na aina zote za uvutaji ni miongoni mwa vitu vibaya  kwa sababu ya kuleta madhara na kulewesha.

 

Ni vyema kutanabahi ndugu Muislamu na kuachana na mazoea sugu na potofu ya kuvuta sigara. Mvutaji sigara huwa hajali kuvuta mbele ya wale waliomzunguka ndani ya nyumba yake, kama mkewe/mumewe, watoto na wengineo. Huwasababishia kuvuta moshi wa sumu na wale walio karibu nae. Huleta hali mbaya hasa kwa mazingira ya ndani ya nyumba na ni mfano mbaya kwa kile kinachochungwa (mke na watoto) ndani ya nyumba hiyo.

Ndugu yangu Muislamu , kama ni miongoni mwa wenye kuendeleza uovu huu basi rudi kwa Mola wako kwa moyo ulio mwepesi wenye kusikiliza nasaha na kukubali yale yote yanayotoka kwa Mola kwa ajili ya kuinusuru nafsi yako kwanza, kisha dini yako, kisha akili yako, kisha familia yako, kisha mali yako na kadhalika.

 

MUZIKI NA NYIMBO


Miongoni mwa yenye kuzoeleka katika majumba yetu ni mziki. Kwa kweli mziki umeenea kila pembe ya dunia kiasi ambacho unawaumiza Waislamu wengi kimwili na kiakili bila ya kujijua. Kila mtu amekabiliana na hali ambayo humuingiza kusikiliza muziki ama kwa hiari au kwa lazima. Kuongezeka umaarufu wa muziki kunahatarisha sana majumba ya Waislamu na hatimae kutumbukia katika balaa hilo usiku na mchana

Ukweli ni kuwa muziki unaathiri sana mioyo ya Waislamu na kuishughulisha akili kwa mambo ya kipuuzi. Tunatumia muda na pesa nyingi katika kununulia CD za majimbo yasiyo na faida, zana za miziki, na hata kuwatumbukiza watoto wetu kwa vifaa (toys) mbali mbali vilivyojaa miziki; Tunajitia makosani na kuuporomoa itikadi sahihi ya Muislamu. Kuna dalili tosha katika Quraan na Sunnah zenye kuonyesha uharamu wa muziki. Katika Suurat Luqmaan aya ya 6 Allaah Subhaanahu wa Ta'ala anatueleza:

((وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا أُولَئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ))


Na miongoni mwa watu wapo wanaonunua maneno ya upuuzi, ili wawapoteze watu na njia ya Mwenyezi Mungu pasipo kujua, na wanaichukulia ni maskhara. Hao watapata adhabu ya kuwafedhehesha Maulamaa pamoja na wafasiri wengi wa Quraan wameeleza kuwa neno "Lahwal-hadith" katika aya hii inakusudiwa nyimbo na zana za miziki.

Mfano Ibn Mas'uud Radhiya Allahu 'anhu amesema kuhusu Aya hii "Naapa kwa Allah hii inamaanisha ni nyimbo" Pia miongoni mwa hadithi zenye kuonyesha uharamu wa ngoma na kila aina ya muziki ni hadithi mashuhuri ya Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam:
"Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Bukhari
Ni vyema tuelewe kuwa hakuna chochote alichokikataza Allah Subhaanahu wa Taala isipokuwa kina madhara ndani yake katika ustawi wa jamii. Jua kuwa miziki tunayoichezesha majumbani yanaweza kuchochea hisia za mja, jazba pamoja na muengezeko wa mapigo ya moyo na kushughulisha akili.

Ujumbe unaopatikana katika miziki na nyimbo nyingi hasa wakati huu tulionao huenda kinyume kabisa na maadili ya Kiislamu, huamsha hisia za mapenzi, uzinzi na uhuru wa kufanya lolote bila ya kuzingatia wajibu wa mja. Umefika wakati kwa Waislamu kutanabahi na kujaribu kwa kadiri ya uwezo wetu kuepukana na balaa hili na kurejesha mandhari nzuri ndani ya majumba yetu. Tusiziuwe nyumba zetu kwa sauti za shetani (nyimbo na miziki) na kuwawekea makaazi, Ni lazima tuziuhishe nyumba zetu kuwa ni sehemu ya kumkumbukwa Allah Subhaanahu wa Taala (dhikr) kwa kila hali; kwa sala, kusoma Quraan, na vitabu vyengine vya dini pamoja na masuala mbali mbali yanayowahusu Waislamu. Hii itatupelekea kuzungukwa na Malaika, kulindwa na kupata ridhaa ya Allah Subhaanahu wa Taala.

 MCHANGANYIKO WA WANAUME NA WANAWAKE

Moja katika jambo linaloonekana ni la kawaida hasa katika majumba yetu ni michanganyiko ya wanaume na wanawake (Ikhtilaatw). Ni wajibu wa kila Muislamu kuelewa hukumu ya kisheria juu ya jambo hili. Ikhtilaatw ni kuchanganyika kwa wanawake na wanaume waliokuwa sio maharim ima kwa wingi au uchache katika sehemu moja. Hali hii imezoeleka sana majumbani mwetu, katika shughuli zetu zikiwa ni za furaha au misiba au hata siku za kawaida.

Tuelewe kuwa mijumuiko ya aina hii na kudhihirika mapambo ni kitu kilichokatazwa katika sheria kwa sababu huwa ni mzizi wa fitina na ni kichochezi cha maasia mengine kwani shaytwan huwa pamoja nao. Katika hadithi iliyosimuliwa na 'Umar, Radhiya Llahu 'Anhu inatueleza:
Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Hachanganyiki mwanamume na mwanamke ila shaytwaan huwa ni watatu wao. [At-Tirmidhiy]


Dini yetu imetuwekea adabu maalum; na kama kuna ulazima wa kuchanganyika majumbani, basi ni vyema kuwe na sehemu tofauti kati ya wanaume na wanawake pindi wakikujia kwao. Tunatakiwa tuwe na hadhari tunapotembelewa na mgeni, hata kama ni ndugu wa mume au mke. Mtume Swalla Llahu 'Alayhi wa Ssalaam aliwaeleza maswahaba zake na Waislamu wote kuwa: Tahadharini kuingilia majumbani mwao wanawake; Wakasema: Ewe Mjumbe wa Allaah, je, vipi kuhusu shemeji? Akasema: Shemeji ni mauti Al-Bukhaariy na Muslim]

Pia Allaah Subhanahu wa Taala anatueleza katika Suuratul Al-Ahzaab: 53
Nanyi mnapowauliza (wakeze) waulizeni nyuma ya pazia. Kufanya hivyo kunasafisha nyoyo zenu za zao. Ni jukumu letu kama ni wazazi kuzielewa sheria hizi na kuzidi kuzipamba nyumba zetu katika mandhari nzuri ya kiislam. Hii itasaidia hata na vizazi vyetu kuinukia kwa maadili na tabia njema na kujua mipaka yao. Na kama itatokea kwa mwanamme au mwanamke kutembea au kutembelewa na kukutana na mwenyeji wa jinsia tofauti basi na tumuogope Allaah na kujihifadhi kwa kadiri ya uwezo wetu, bila ya kurefusha mazungumzo.

Allaah Alietukuka Anatufahamisha katika Suuratu Nnuur:30-31

Wambie waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa) na wazilinde tupu zao hili ni takaso kwao; bila ya shaka Allaah anazo habari za wanayoyafanya. Na wambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika.


 MAMBO YA KUZINGATIA HASA KWA KINA MAMA

Miongoni mwa mambo yenye kuporomoa Uislamu katika majumba ya Waislamu ni udhaifu wa baadhi ya kinamama kuupuuza au kutoyatambua mafunzo muhimu yanayowahusu ambayo dini yetu yameyaweka wazi. Miongoni mwa hayo ni haya yafuatayo:

i.              Kudhihirisha kwa Mapambo:

Kawaida, wanawake huwa na mvuto wa kimaumbile. Hivyo Uislamu umeweka sheria maalum juu ya kuhifadhi maumbile hayo, heshima, staha pamoja na hadhi zao. Suurat Al-Ahzab: 59 Allaah Subhaanahu Wata’ala Anatueleza:


يَـٰٓأَيُّہَا ٱلنَّبِىُّ قُل لِّأَزۡوَٲجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَآءِ ٱلۡمُؤۡمِنِينَ يُدۡنِينَ عَلَيۡہِنَّ مِن جَلَـٰبِيبِهِنَّۚ ذَٲلِكَ أَدۡنَىٰٓ أَن يُعۡرَفۡنَ فَلَا يُؤۡذَيۡنَۗ

Ewe Mtume! Waambie wake zako na binti zako na wanawake wa Kiislamu wajiteremshie uzuri shungi zao, kufanya hivyo kutapelekea wepesi wajuulikane (kuwa ni watu wa heshima) ili wasiudhiwe

.

Ni mazoea ya wanawake wengi wanapotaka kutoka au kupata wageni majumbani mwao hudhihirisha mapambo yao yakiwemo maumbile yao kwa nguo za wazi au za kubana, manukato pamoja na mapambo mengine.  Hali hii inaweza kusababisha vishawishi vingi, fitina na mtafaruku katika familia.  Ni lazima tuwe waangalifu ni nani waliotuzunguka hasa wale wasiotakikana kuona mapambo hayo (wasiokuwa mahrim).  Suuratu Nnuur: 31 Allaah Subhaanahu Wata’ala Anatuhimiza.

 

وَقُل لِّلۡمُؤۡمِنَـٰتِ يَغۡضُضۡنَ مِنۡ أَبۡصَـٰرِهِنَّ وَيَحۡفَظۡنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبۡدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنۡهَا‌ۖ

Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe  viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika.

Kujistiri kwa hijabu ya ki shari’ah kunapelekea kupata ridhaa ya Allaah Subhaanahu Wata’ala na kutii amri Yake, kujitakasa pamoja na kuheshimika na wengine.

 

i.              Kutoka toka bila ya sababu maalum

Wanawake wa Kiislamu hawajakatazwa kutoka nje ima kwa, kufanya kazi, kutembelea wazee, marafiki au katika shughuli za kijamii, ikiwa hakuna kipingamizi chochote cha shari’ah kitachowazuia. Muhimu ni kuchunga na kuielewa mipaka iliyowekwa katika dini.  Hata hivyo kutulia majumbani ni bora zaidi kwao na kutawaepusha na mambo mengi. 

Ulimwengu tulionao, kina mama wengi imekuwa ni adimu kutulia majumbani mwao, hii hupelekea familia kukosa utulivu, kizazi kukosa malezi na maadili mema kutokana na wazazi huwa hawana muda wa kutosha na watoto wao. Allaah Subhaanahu Wata’ala Anatufahamisha katika Suuratul Ahzaab: 33

وقَرۡنَ فِى بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجۡنَ تَبَرُّجَ ٱلۡجَـٰهِلِيَّةِ ٱلۡأُولَىٰۖ

Na kaeni majumbani mwenu, wala msionyeshe mapambo yenu kama walivyokuwa wakionyesha wanawake wa zama za ujahili (ujinga)

 

Hivyo ni lazima kwa kinamama kuzingatia ni sababu gani zitakazowatoa ndani ya majumba yao, kuwe na mtizamo na upeo wa hali ya juu kabla ya kuamua kutoka. Na ikibidi kutoka basi azingatie mipaka ya Allaah Subhaanahu Wata’ala, kusiwe na aina yoyote ya mapambo kama vipodozi, manukato, udi na mengineyo. Awe amejihifadhi vizuri kwa mujibu wa shari’ah. Kufanya hivyo kutahifadhi utu wao, dini yao pamoja na kizazi chao kwa ujumla.

 

HITIMISHO

Ni wajibu wa Waislamu kudumisha mafunzo mazuri tuliyoekewa wazi katika dini yetu. Jamii bora huanza majumbani. Ni vyema kwa wasimamizi wa majumba kusaidiana na kushirikiana pamoja katika kulinda na kuhifadhi mazingira mazuri kwa kumuogopa Allaah Subhaanahu Wata’al. Ni juu yetu kuwa waangalifu wa kile tunachokikuza - watoto, kwani wao husoma kutoka kwetu. 

Ni jukumu la kila mmoja wetu kusoma na kujifunza kitu gani Allaah Subhaanahu Wata’ala Anapendezeshwa nacho na kipi Amekikataza hasa ndani ya majumba yetu ili tuishi hali ya kuwa Allaah Subhaanahu Wata’ala Ameturidhia. Tuzipambe nyumba zetu kwa misingi ya Kiislamu ili zitofautike na zile zisizo za Kiislamu. Huu ni ukumbusho kwa wenye kukumbuka.

Tumuombe Allaah Atuongoze katika haki na kuifuata, tuijuwe batili na kuiacha, Atupe tawfiyq, Atulinde na Kutuweka katika msimamo ulio sawa. Aamiyn

 

 








Wednesday 3 April 2013

Swalatul-Istikhara

(Swala ya kuomba ushauri kutoka kwa Allah)



Dua ya Swalatul-Istikhara

Amesema Jaabir Bin Abdillah رضى الله عنه “alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu akitufundisha Swala ya Istikhara kama vile anavyotufunza sura ya Qur’an. Anasema
رضى الله عنه

 ‘Akikusudia mmoja wenu kufanya jambo, aswali rakaa mbili zisizo za faradhi, kisha aseme:


اللّهُـمَّ إِنِّـي أَسْتَخيـرُكَ بِعِاْـمِك، وَأسْتَقْـدِرُك
َ بِقُـدْرَتِـك، وَأَسْـألُـكَ مِنْ فَضْـلِكَ العَظـيم، فَإِنَّـكَ تَقْـدِرُ وَلا أَقْـدِر، وَتَـعْلَـمُ وَلا أَعْلَـم، وَأَنْـتَ عَلاّمُ الغُـيوب، اللّهُـمَّ إِنْ كُنْـتَ تَعْـلَمُ أَنَّ هـذا الأمْـرَ (وَيُسَـمِّي حاجته) خَـيْرٌ لي في دينـي وَمَعـاشي وَعاقِـبَةِ أَمْـري، ( عَاجِلِهِ و آجِلِه) فَاقْـدُرْهُ لي وَيَسِّـرْهُ لي ثـمَّ بارِكْ لي فيـه، وَإِنْ كُنْـتَ تَعْـلَمُ أَنَّ هـذا الأمْـرَ شَـرٌ لي في دينـي وَمَعـاشي وَعاقِـبَةِ أَمْـري، ( عَاجِلِهِ و آجِلِه) فَاصْرِفْـهُ عَنّيِ وَاصْرِفْني عَنْـهُ وَاقْـدُرْ ليَ الخَـيْرَ حَيْـثُ كانَ ثُـمَّ أَرْضِـني بِِـه .



Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi nakutaka ushauri (muelekezo) kwa ujuzi Wako, na nakuomba uniwezeshe kwa uwezo Wako, na nakuomba fadhila Zako kubwa, hakika Wewe unaweza, nami siwezi, nawe unajua nami sijui, nawe nimjuzi wa yale yaliyofichikana. Ewe Mwenyezi Mungu iwapo jambo hili kutokana na ujuzi wako (utalitaja jambo lako) lina kheri na mimi katika dini yangu na maisha yangu na mwisho wa jambo langu (karibu na mbali ) basi nakuomba uniwezeshe nilipate, na unifanyie wepesi, kisha unibariki, na iwapo unajua kwamba jambo hili ni shari kangu katika dini yangu namaisha yangu na mwisho wa jambo langu (karibu na mbali) basi liepushe na mimi naminiepushe nalo, na nipangie jambo jengine lenye kheri nami popote lilipo, kisha niridhishe kwalo”

Sunday 31 March 2013

MAJINA YA MALAIKA NA KAZI ZAO

Mwenyezi Mungu S.W.T. kajaalia kila kitu alichokiumba kina jina lake maalum ili iwe ni alama yake ya kutambulikana kwake. Na kama vile kila mwanaadamu analo jina lake basi ni hivyo hivyo kwa Malaika, kila Malaika ana jina lake, lafudhi ya majina yao hayafanani na lafudhi ya majina ya kibinaadamu, yaani wao hawana majina kama Athmani, au Ramadhani na Mariam kadhalika na hii inawezekana pengine ni kwa sababu wao wameumbwa si waume wala wake. Mwenyezi Mungu S.W.T. na Mtume wake S.A.W. wametufunulia ndani ya Qur-ani na Hadithi majina ya Malaika 12 pamoja na shughuli zao, kama ifuatavyo:-

1.JIBRIL.


Jibril ni mkubwa wa Malaika na ametajwa katika aya zaidi ya moja ndani ya Qur-ani. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Baqarah aya ya 97, “


قُلْ مَنْ كَانَ عَدُوًّا لِجِبْرِيلَ فَإِنَّهُ نَزَّلَهُ عَلَى قَلْبِكَ بِإِذْنِ اللَّهِ مُصَدِّقًا لِمَا بَيْنَ يَدَيْهِ وَهُدًى وَبُشْرَى لِلْمُؤْمِنِينَ


Maana yake, “Sema: “Aliyekuwa ni adui wa Jibril, (kwa kuwa ndiye aliemletea Utume Nabii Muhammad asiwapelekee Mayahudi ni bure hana kosa Jibril); hakika yeye ameiteremsha Qur-ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu (sio kafanya kwa kupendelea kwake); (Qur-ani) inayosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake, na ni uwongozi na khabari njema kwa wanaoamini.”


Jibril A.S. ni Malaika mwenye nguvu sana, na Mwenyezi Mungu S.W.T. amemsifu katika Surat Najm aya ya 5 kwa nguvu zake, kasema,


"Amemfundisha (Malaika) Mwenye nguvu sana."


Na baadhi ya Wanavyuoni wamesema kwamba,

“Jibril A.S. kwa ushujaa na nguvu zake aliweza kuiinua miji ya watu wa Luut pamoja na kila kitu kilichomo ndani yake pamoja na watu wake ambao idadi yao inasemekana kuwa ni watu mia nne elfu, aliwainua mpaka mbinguni kwa kutumia bawa lake moja kati ya mabawa yake mia sita. Mbwa na majogoo walisikika sauti zao na Malaika wengine wakati wakilia; na kwa amri ya Mola wake aliiangamiza miji ile na kila kilichokuwemo humo kwa kuigeuza juu chini.”

Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Huud aya ya 82, “

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِنْ سِجِّيلٍ مَنْضُودٍ

Maana yake, “Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza nchi juu chini, na tukawateremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu uliokamatana wa Motoni.”


Moja ya kazi ya Malaika huyu mwaminifu ni kupeleka wahyi kwa Mitume na Manabii wote waliotangulia. Na alimwijia mara nyingi zaidi Mtume wetu S.A.W. kuliko Mitume wengine wote, kwa ajili ya kumshushia wahyi au kumfundisha baadhi ya mambo kutoka kwa Mola wake kama vile kusali na kusoma Qur-ani. Jibril ameitwa kwa majina tofauti ndani ya Qur-ani. Na majina yenyewe ni haya yafuatayo:-

1.1.ROHO (RUUH).


Naye ndiye "Roho ambae alitumwa kwa Bibi Maryam mama wa Nabii Issa A.S."

Kama alivyomuita Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Maryam aya ya 17, “

فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا

Maana yake, “Tukampeleka Roho Yetu (Jibril A.S.) akajifananisha kwake (kwa sura ya) binaadamu alie kamili.”

1.2.ROHO MWAMINIFU (RUUHUL AMIIN).


Na katika Qur-ani anajulikana pia kama "Roho mwaminifu" Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Ash-Shu`araa aya ya 193 na ya 194, “


نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الأمِينُ * عَلَى قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنْ الْمُنذِرِينَ

Maana yake, “Ameuteremsha haya Roho mwaminifu (Jibril). Juu ya moyo wako, ili uwe miongoni mwa Waonyaji.”

1.3.ROHO TAKATIFU (RUUHUL QUDUS).


Naye kaitwa na Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa jina la "Roho takatifu" katika Suratil Nahal aya 102, “


قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِنْ رَبِّكَ بِالْحَقِّ… 

Maana yake, “Sema: “Roho takatifu (yaani Jibril) ameiteremsha hii (Qur-ani) kutoka kwa Mola wako kwa haki…”

1.4.NAMUUS.


Na ameitwa "Namuus" kama alivyosema Waraqa bin Noufal kumwambia Mtume S.A.W. wakati wa mwanzo kabisa Jibril alipomteremshia wahyi Mtume S.A.W.. Kasema Noufal, “


"لقد جاءك النَّامُوسُ الَّذِي أَنْزَلَ اللَّهُ عَلَى مُوسَى".

Maana yake, “Amekuijia Namuus (yaani Jibril) ambaye alimteremsha Mwenyezi Mungu kwa (Nabii) Musa (A.S.).”


Naye ni Malaika mwenye heshima na cheo kikubwa sana mbele ya Mola wa walimwengu wote. Mwenyezi Mungu S.W.T. kamsifu kwa sifa za nguvu zake na cheo chake katika Surat Takwyr aya ya 20, “


ذِي قُوَّةٍ عِنْدَ ذِي الْعَرْشِ مَكِينٍ

Maana yake, “Mwenye nguvu, mwenye cheo cha heshima kwa Mwenyezi Mungu.”

2.MIKAIIL.


Mikaiil ni Malaika mwingine mwenye daraja ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu S.W.T. kama alivyomtaja katika Suratil Baqarah aya ya 98, “


مَنْ كَانَ عَدُوًّا لِلَّهِ وَمَلائِكَتِهِ وَرُسُلِهِ وَجِبْرِيلَ وَمِيكَالَ فَإِنَّ اللَّهَ عَدُوٌّ لِلْكَافِرِينَ

Maana yake, “Aliyekuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na Mitume Wake na Jibril na Mikaiil (basi mtu huyo anatafuta kuangamia) kwani Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.”

Naye amewakilishwa kwa ajili ya mvua na mimea kwa amri ya Mola wake. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil A`araaf aya ya 57, “

وَهُوَ الَّذِي يُرْسِلُ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ حَتَّى إِذَا أَقَلَّتْ سَحَابًا ثِقَالا سُقْنَاهُ لِبَلَدٍ مَيِّتٍ فَأَنزَلْنَا بِهِ الْمَاءَ فَأَخْرَجْنَا بِهِ مِنْ كُلِّ الثَّمَرَاتِ كَذَلِكَ نُخْرِجُ الْمَوْتَى لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ


Maana yake, “Na Yeye Ndiye anayepeleka pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara (khabari njema) kabla ya kufika Rehema Yake (mvua). Hata hizo pepo zinapobeba mawingu mazito tunayachunga mpaka kwenye nchi iliyo kufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, ndio kama hivyo tukatolesha kila aina ya matunda. Basi hali kadhalika tunavyo wafufua wafu, ili mpate kukumbuka.

3.ISRAFIIL.


Israfiil ni jina la Malaika ambaye atakayepuliza baragumu siku ya Kiyama. Naye ni mmoja wa Malaika ambaye aliyekuwa akitajwa sana na Mtume wetu S.A.W. katika dua yake kila anapoamka usiku kuabudu. Alikuwa Mtume S.A.W. anamtaja yeye pamoja na Jibril na Mikaiil, kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Aisha R.A.A.H. na iliyotolewa na Abu Daud, “

"اللَّهُمَّ رَبَّ جِبْرِيلَ وَمِيكَائِيلَ وَإِسْرَافِيلَ أَنْتَ تَحْكُمُ بَيْنَ عِبَادِكَ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ، اهْدِنِي لِمَا اخْتُلِفَ فِيهِ مِنَ الْحَقِّ بِإِذْنِكَ إِنَّكَ تَهْدِي مَنْ تَشَاءُ إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ".

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu! Mola wa Jibril na Mikaiil na Israfiil Wewe Ndiye unayehukumu baina ya waja Wako katika yale waliokuwa wakikhitilafiana, niongoze kwendea haki katika yale waliokhitilafiana kwa idhini Yako, unamuongoza umtakae kwendea njia iliyonyooka.”

4.MAALIK.


Maalik ni jina la Malaika mkubwa wa Malaika walio walinzi wa Motoni. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Surat Zzukhruf aya ya 77, “

وَنَادَوْا يَا مَالِكُ لِيَقْضِ عَلَيْنَا رَبُّكَ قَالَ إِنَّكُمْ مَاكِثُونَ

Maana yake, “Nao watapiga kelele (kumwambia yule Malaika anayewaadhibu waseme) “Ee Maalik! Naatufishe Mola wako!” (Maalik) aseme “Bila shaka mtakaa humu humu (Motoni).”

5.RIDHWAAN.


Ridhwaan ni jina la Malaika ambae kazi yake ni mlinzi wa Peponi. Mwanachuoni Ibn Kathiir kasema, “

"وخازن الجنة ملك يقال له رضوان ، جاء مصرحا به في بعض الأحاديث".

Maana yake, “Na mlinzi wa Peponi ni Malaika anaeitwa Ridhwaan, ameitwa (kwa jina) Musarrihan katika baadhi ya Hadithi.”

6.MUNKAR NA NAKIIR.


Munkar na Nakiir ni Malaika wawili ambao amewataja Mtume S.A.W. katika Hadithi sahihi kuwa ni Malaika waliowakilishwa kuuliza watu maswali kaburini. Nao wana umbo la kutisha na sauti kali sana. Mwenyezi Mungu S.W.T. atuepushe na adhabu ya kaburi. Kila mmoja wetu baada ya kufa kwake anapozikwa kaburini mwake humwijia Malaika hawa wawili na kumuuliza maswali kama vile. "Nani Mungu wako? Nani Mtume wako? Na nini dini yako?" Ikiwa mtu huyo hapa duniani alikuwa mtiifu kwa Mwenyezi Mungu S.W.T. na Mtume Wake S.A.W. ataweza kujibu maswali hayo kwa urahisi lakini ikiwa ni kinyume ya hivyo maswali hayo yatakuwa magumu kwake, hivyo inatupasa tujitayarishe kwa maswali hayo ya kaburini. Na urahisi wa kujibu kwake inategemea na jinsi mtu alivyoishi katika maisha yake hapa duniani. Yaani mtu mwema au muovu?

7.HARUUT NA MARUUT.


Nayo haya ni majina ya Malaika wawili aliowatuma Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa watu wa Baabil (Babylon hivi sasa ni nchi ya Iraq) ili wawafanyie mtihani wa kuwafundisha uchawi. Na walikuwa hawamfundishi mtu yeyote yule ila baada ya kumuonya kwao kwamba ukitaka tukufunze basi utakufuru. Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Baqarah aya ya 102, “


وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ وَلَكِنَّ الشَّيَاطِينَ كَفَرُوا يُعَلِّمُونَ النَّاسَ السِّحْرَ وَمَا أُنزِلَ عَلَى الْمَلَكَيْنِ بِبَابِلَ هَارُوتَ وَمَارُوتَ وَمَا يُعَلِّمَانِ مِنْ أَحَدٍ حَتَّى يَقُولا إِنَّمَا نَحْنُ فِتْنَةٌ فَلا تَكْفُرْ… 


Maana yake, “Na (Nabii) Suleiman hakukufuru, bali Mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi (waliokuwa wakiujua wenyewe tangu zamani) na (uchawi) ulioteremshwa kwa Malaika wawili, Haruut na Maruut, katika mji wa Baabil. Na wala (Malaika hao) hawakumfundisha mtu yeyote mpaka wamwambie: “Hakika sisi ni mtihani, basi usikufuru…”

8.IZRAIL.


Na hili ndilo jina alilopewa Malaika wa mauti, jina hili halikutajwa ndani ya Qur-ani wala halikutajwa katika Hadithi sahihi, lakini hii ni kauli ya Wanavyuoni kwa jina hili.

9.RAQIIB NA ATIID.


Hayo ni majina ya Malaika wawili, ambao wamewakilishwa na Mwenyezi Mungu S.W.T. kwa ajili ya kuandika kauli na vitendo vya watu. Na maana ya majina haya Raqiib na Atiid ni kuwa wamehudhuria, mashahidi kwa vile daima hawaachani wako pamoja na watu ila kwa baadhi ya mambo fulani, kama vile mtu akiwa na janaba au akiwa uchi au akiingia msalani (chooni). Mwenyezi Mungu S.W.T. kasema katika Suratil Qaaf aya ya 17 na ya 18, “


إِذْ يَتَلَقَّى الْمُتَلَقِّيَانِ عَنْ الْيَمِينِ وَعَنْ الشِّمَالِ قَعِيدٌ * مَا يَلْفِظُ مِنْ قَوْلٍ إِلا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ

Maana yake, “Wanapopokea wapokeaji wawili, anaekaa kuliani na (anaekaa) kushotoni, (Malaika). Hatoi kauli yoyote isipokuwa karibu nae yuko mngojeaji (mwangalizi) tayari (kuandika).”