Tuesday 10 June 2014

NI IPI PEPO YA ALLAH (SUBHANAHU WATAALA)


Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Allah subhanahu wataala ameumba dunia na akaumba ndani yake starehe ambazo ndio kitakua kipimo cha mwanaadamu ima mafanikio yake au hasara yake ya milele. Allah amewapambia wanadamu starehe mbali mbali kama anavyosema “ Wamepambiwa watu kupenda wanawake,na watoto,na mrundikano wa wa fedha na dhahabu….”( Aal-Imraan : 14). Lakini kila anapotaja dunia na starehe zake, humalizia kwa kusema kuwa ni starehe za kipuuzi ,zenye kudanganya na ni zenye kupita, hivyo tusihadaike nazo. Amesema Allah subhanahu wataala katika Suratu Faatir aya ya 5: “Yasikundanganyeni maisha ya dunia,na asikudanganyeni mdanganyifu mkubwa”. Ni Kweli yasitudanganye maisha ya dunia, kwani kila starehe ya duniani ni starehe bandia, starehe ya kula ipo kwenye sentimita chache za ulimi, na chakula kinapovuka tu ulimi hakina tena ladha,halikadhalika starehe nyenginezo zimo katika sentimita chache tu za viungo vyake husika.

Starehe za dunia zina kiwango chake, na kinapovuka kiwango hicho hua adhabu badala ya starehe, mlaji anapozidisha kula na akavimbiwa,basi mwisho wake ni kuumwa na tumbo na madhara mengineyo. Maisha ya dunia hayakosi misukosuko mara kuumwa,kuchoka, alimuradi starehe za dunia ni zenye kudanganya.

Allah badala yake ameweka starehe za kudumu na zilizo bora kwa waja wake wema. Amesema Allah katika Suratul ‘Aala aya ya 17 “Na Akhera ni bora na ni yenye kubaki”. Amejaalia maisha ya dunia kua ni yenye mapungufu, ili watu wakimbilie maisha ya Akhera.Amesema katika suratu Aal Imraan aya ya 133 “Na kimbilieni msamaha wa Mola wenu na pepo (yake), ambayo upana wake ni sawa na mbingu na ardhi. Imewekwa kwa wacha-Mungu” na akayarejea hayo hayo tena katika (Suratul-Hadyd : 21).

Allah ameeleza kua malipo ya watu wema kua ni ujira usiokwisha. Kitendo cha starehe za Akhera kubaki milele, yatosha kua ni starehe, kwani starehe yoyote isiyodumu basi hiyo si starehe ya kweli, kwani kila unapokumbuka kua itakwisha basi furaha yote huondoka, halikadhalika adhabu ambayo ina mwisho, si adhabu ya kweli kwani iko siku itamalizika na kusahaulika. Allah ameandaa malipo mazuri kwa watakaotenda mema, na mabaya kwa watakaofanya ubaya, na hakuna malipo ya tatu.

Ima Pepo au Moto. Na amaeyakariri hayo takriban katika kila sura ndani ya Qur-an, ili kuwatia hamu watu kuikimbilia pepo na kuepukana na Moto. Kila anapotaja Pepo hutaja na Moto ili watu wapate kutafakari. Lakini je nani anayazingatia haya? Pepo imetajwa takriban mara 126 ndani ya Qur-an na kumetajwa majina yake,sifa ya watu watakaoingia humo,chakula chao,vinywaji vyao,mavazi yao, makasri na vyumba vyao na starehe nyenginezo.

Inshaa Allah tutaanza kuangalia kipengele kimoja baada ya chengine, lakini ufupi wa neema hizo anasimulia Mtume rehma na amani ziwe juu yake, katika hadith Qudsy ilopokelewa na Tirmidhy kua amesema Allah(subahanahu wataala) “Nimewaandalia waja wangu wema (malipo ambayo)macho hayajawahi kuona,wala masikio kusikia, wala haijawahi kumpitikia mtu kwenye akili yake.” Mtu wa chini katika pepo basi atapewa ufalme wa dunia mara 10 yake seuze wa daraja ya juu. Pepo ina daraja 100 kama anavyosema Rasuul na watu wa daraja ya chini watawaona wa juu yao kama wanavyoona nyota na baina ya daraja moja na nyengine ni umbali baina ya mbingu na ardhi.(Hadith imepokelewa na Bukhari). Nyuso za watu wa peponi zitang’ara na wataishi humo kama wafalme, kama anavyosema Allah kufupisha starehe hizo “Na utakapoyaona yalioko huko utaona ni neema na ufalme mkubwa”

MAJINA YA PEPO

Pepo inatajwa kua na milango minane kama iliyvopokelewa katika hadithi mbalimbali na haikuja aya kuonesha milango ya pepo bali aya zimekuja kutaja majina ya pepo. Miongoni mwa milango hiyo ya pepo uko mlango wa kulia ambao wataingia wale watu sabini elfu bila ya hesabu wala adhabu,kuna mlango wa wafungaji unaoitwa Rayyan,kuna mlango wa wenye kukithirisha sala,kuna mlango wa wenye kukithirisha kutoa sadaka,kuna mlango maalum kwa mashahidi (waliokufa wakipigania dini ya Allah) na kuna mlango maalum kwa wenye kuzuia ghadhabu zao. Hii milango imekuja katika Hadith mbalimbali za Rasuul (swalla Allah alayhi wasallam) na mengine miwili ilobaki ni Qiyas ya wanavyuoni. Wallah A’alam.
Ama majina ya pepo yaliyotajwa katika Qur-an ni:

1-Firdaus :Nayo ni pepo ya daraja ya juu kwa lugha ya kimombo ni “First Class”. Sakafu yake ya juu ni Arshi Ya Allah, na mito yote peponi huanzia katika pepo hii. Waloandaliwa pepo hii wametajwa sifa zao mwanzo wa suratul-muuminuun aya ya 10-11 na akamalizia kwa kusema “Hao ndio warithi. (10)Ambao watarihi Firdaus milele(11)”. Na imepokelewa kua watakaoingia kupitia mlango wa kulia wa pepo basi mafikio yao ni katika pepo hii.

2-Jannaatu Adnin : Inasimuliwa kua pepo zote Allah ameziumba kwa kusema kua na zikawa, lakini pepo hii ameiumba kwa mikono yake. Ni pepo iliyotajwa mara nyingi katika Qur-an. Ama majina mengine ni: Jannaatul-khuld, Jannatul-Aaliyah, Jannaatu-Nnaim, Daarul-Akhirah, Daaru-Salaam, Daarul-Qaraar, Daarul-Mutaqin,na Daarul-Muqamah.

WAKE WA WATU WA PEPONI

Tuanzie na wanawake wa jannah, kwani kama alivyotanguliza Allah kua kawapambia watu kupenda wanawake kama tulivyoona hapo kabla. Amesema Allah(subhanahu wataal) katika Suratul-Waaqiah aya ya 22-23 “(Watapewa humo) wanawake wenye macho mzuri na makubwa.(22)(wanapendeza) kama kwamba lulu zilofichwa (ndo kwanza zinapasuliwa)(23)”. Wanawake wa jannah wamepewa jina la “Huurul-Ayn” kutokana na macho yao kua makubwa, ambayo yamekooza weusi wa mboni zao katika weupe wa macho yao.

Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi sahih ilowafikiwa na Bukhari na Muslim “…na kila mtu atakua na wake wawili,wanaonekana uboko wa miguu yao,nyuma ya nyama zao,na hakutakua na mjane peponi” Akimaanisha kua ngozi zao zitaonesha mpaka kilicho ndani mfano wa kioo.

Vilevile Mtume amewasifu wanawake wa jannah kua lau kama mmoja wao ataletwa duniani basi harufu yake itaenea dunia nzima, na nuru yake itaangaza dunia nzima.(Hadith sahih Bukhari na Muslim).

Amesema Allah katika Suratu-Rahman aya ya 56-58 “Watakuwemo humo wanawake watulizao macho yao,(56)hawajaguswa na binaadamu yoyote wala jini kabla ya hapo,(57) kama kwamba ni yakuuti na marijani (58)” na Akasema tena katika Suratu-Swaffaat aya ya 48-49 “Pamoja nao watakua wanawake wenye macho mazuri na makubwa. (48) Wanawake hao kama mayai yalohifadhiwa(49)”. Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ”….Hakika mmoja wenu atapewa nguvu za watu 100 katika kula,kunywa na kuingiliana na mkewe.”(Ahmad).Pamoja na uzuri wao lakini mwanamke mwema atakaeingia jannah atawazidi mahurul-ayn.

Usikose kusoma sehemu ya pili ya Makala hii hapo kesho in shaa Allah.

Makala imetolewa na Raudhwah Islamic Group

No comments:

Post a Comment