Saturday 19 July 2014

ISTIGHFAAR

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group


Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wa ta‘ala) Muumba wa kila kilichomo katika ulimwengu huu. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Nini maana ya Istighfaar.?

Sayyidina Ally (radhi za Allah ziwe juu yake) alimsikia mtu mmoja akisema: Astaghfirullah. Akamuuliza unajua maana ya Istighfaar? Naye akamuuliza nini maana yake ewe Amirul muuminiin? Akajibu Sayyidina Ally: “Istighfaar ni daraja la juu la uchamungu (ililyiin) nalo ni jina lenye maana ya vitu sita: Kwanza kujuta kwa yale makosa uliyoyafanya, Kuazimia kutorejea makosa uliyoyafanya, Kuwapa watu haki zao mpaka ukutane na Allah bila ya kubaki na deni hata moja, Kutekeleza fardhi zote kwa ukamilfu, usile haramu,Uonje  na utamu wa kutenda  mema kama ulivyoonja utamu wa maasi, ukishakuyatekeleza hayo ndipo useme: ASTAGHFIRULLAH hali ya kuwa unajua maana yake”.

Sayyidina Ally (radhi za Allah ziwe juu yake) ameelezea kwa undani ni nini maana ya mtu kusema Astaghfirullah. Wengi wetu tumekuwa tukitamka tu katika midomo yetu bila ya kujua maana yake.
Ni wajibu wetu waislamu kudumu na kufanya istighfaar daima na iwe kila siku. Kwani Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ambae alisamehewa na Allah (subhanahu wataala) madhambi yake yaliyopita na yatakayokuja ila bado alikuwa akileta istighfaar kila siku. Je vipi sisi ambao daima ni wenye kumuasi Allah (subhanu wataala) usiku na mchana?  Imetoka kwa Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) alimsikia Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) akisema: "Wallaahi mimi naomba maghfirah kwa Allaah na kutubu Kwake zaidi ya mara sabiini kwa siku" Bukhaariy

Sisi tunamuasi Allah (subhanahu wataala) na tunajisahau kuwa tutaondoka hapa duniani na ndio maana hatuandai mazingira ya kukutana na mola wetu. Daima tuwe ni wenye kudumu na istighfaar. Na iwe ni istighfaar kutoka ndani ya nyoyo zetu itakayothibitishwa na vitendo vyetu vyema. Istighfaar ndio jahazi la kumuokoa muumini katika dunia hii kutokana na maasi anayomuasi Allah (subhanahu wataala) asubuhi na usiku. Na ndio maana Mtume wetu (swalla Allahu alayhi wasallam) ambae ndio kigezo chetu akawa ni mwenye kudumu na istighfaar.

Anasema Sufyan “ Ajabu kwa mwenye kuzama na pamoja yake jahazi la kumuokoa.” Wakauliza walio pamoja nae “Na ni lipi hilo jahazi la uokovu? Akajibu ISTIGHFAAR”

MANENO YA KUMPA FARAJA MWENYE KUASI

Anasema Allah (subhanahu wataala) “ Sijapata kumghadhabia mtu kama ninavyomghadhabia mtu ambae anaona dhambi yake ni kubwa kuliko msamaha wa Allah”

Maneno haya yanatupa picha halisi kuwa Allah (subhanahu wataala) anataka aombwe msamaha na wala mtu asione kafanya kubwa ambalo hawezi kusamehewa na Allah. Juu ya lolote ambalo mtu amelifanya basi alete istighfaar kwa Allah (subhanahu wataala) nae atamsamehe kwani hakika ya Allah ni mwingi wa kusamehe. "Na hakika Mimi ni Mwingi wa Kusamehe kwa anayetubia, na akaamini, na akatenda mema, tena akaongoka" (Twaaha:82)

Imetoka kwa Anas (Radhiya Allahu anhu) ambaye amesema: Nimemsikia Mtume (Swalla Allahu alayhi waaalihi wasallam) akisema: "Amesema Allahِ: Ewe Mwanadam! Hakika ukiniomba na ukanitaraji (kwa malipo) Nitakusamehe yale yote uliyonayo na wala Sijali, Ewe Mwanadam! Lau zingefikia dhambi zako ukubwa wa mbingu, kisha ukaniomba msamaha, Ningekughufuria bila ya kujali (kiasi cha madhambi uliyoyafanya). Ewe Mwanadam, Hakika ungenijia na madhambi yakaribiayo ukubwa wa ardhi, kisha ukakutana nami na hali hukunishirikisha chochote, basi Nami Nitakujia na msamaha unaolingana nao"Imepokelewa na At-Tirmidh

Hivyo ndugu zangu wakiislamu daima tuwe ni wenye kuomba msamaha kikweli kwa Allah (subhanahu wataala) ili turudi kwa Allah akiwa yupo radhi na sisi na tusiwe wenye kukata tamaa na rehma za Allah (subhanahu wataala).

BAADHI YA ISTIGHFAAR MUHIMU
Bwana wa Istighfaar
Imetoka kwa Shaddaad Bin Aws (radhi za Allah ziwe juu yake) kwamba Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) kasema: Bwana wa Istighfaar  ni kusema: "Allaahumma Anta Rabbiy laa ilaaha illa Anta, Khalaqtaniy wa-ana ‘Abduka, wa-ana ‘alaa ‘Ahdika wa-Wa’dika mas-tatwa’tu. A’uudhu Bika min sharri maa swana’tu, abuu Laka Bini’matika ‘alayya wa abuu bidhambi, Faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh-dhunuuba illa Anta" 
Maana yake ni :
"Ee Allaah,  Wewe ni Mola wangu, hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Wewe, Umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano lako, kiasi cha uwezo wangu, najilinda Kwako kutokana  na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba unisamehe kwani hasamehi madhambi ila Wewe"Bukhaariy.

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema " Yeyote atakaesema "ASTAGHFRIULLAHA LLADHY LAA ILAHA ILLA HUWAL HAYYUL QAYYUM WA-ATUBU ILAYHI"
“Namuomba msamaha Allah ambaye hapana mola apasae kuabudiwa kwa haki ila yeye, aliye hai aliyesimama kwa dhati yake, na ninatubia kwake”………Allah atamsamehe hata kama ana makosa ya kukimbia vitani’

DUA YA NABII YUNUS
Dua ya Nabii Yuunus (alayhis-salaam) alipokuwa tumboni mwa  samaki alisema maneno yafuatayo "Laa ilaaha illa Anta Subhaanaka inniy kuntu minadh-dhwaalimiyn"
“Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhaanaka Uliyetakasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu"  (Suratul Anbiyaa: 87).

NI ZIPI FAIDA ZA ISTIGHFAAR?

Kutoka kwa Abdillah bin Abbas radhi za Allah ziwe juu yao amesema, amesema Mtume (swallalahu alayhi wasallam): “ Mwenye kuleta Istighfaar/akaomba msamaha, Allah humjaalia mtu huyo katika kila zito na tatizo apate ufunguzi, na kila tatizo atapata faraja, na atamruzuku bila ya yeye kutegemea.”
Hadithi hii inatuonesha kwa namna gani mtu anapoleta istighfaar na kuomba msamaha Allah humpa kheri tofauti tofauti.

Faida nyengine ya istighfaar tutaipata kutoka ndani ya Quraan kupitia kisa cha Hassan Al Basri.
Mtu wa kwanza alimuendea Hassan Al Basri akamuambia kuwa nina tatizo la mtoto Hassan Al basri akamjibu lete istighfaar.Mtu wa pili akamuendea Hassan Al Basri  akamwambia nina ugumu wa maisha na hali yangu ni maskini.Nini nifanye nipate wepesi? Akamwambia lete istighfaar.Mtu wa tatu akamuendea Hassan Al Basri akamwambia mazao yangu yanakauka na mvua hakuna.Nini nifanye?akamwambia lete istighfaar.Watu waliokuwa wakisikia yale majibu wakamwambia vipi leo mbona kila anaekuja na jambo lake unamwambia lete istighfaar.au hujui nini wafanye? Hassan Al Basri akawajibu hivi mumesahau katika Suratu Nuuh aya 9-12 ya ALLAH aliwaambia waja wake walete istighfaar ili wapate watoto,wapate mali na wapate mvua kwa ajili ya mazao yao.” Nikasema: Ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi; hakika Yeye ni Mwingi wa kusamehe(10) Atakuleteeni mvua inyeshe mfululizo.(11) Na atakupeni mali na wana, na atakupeni mabustani na atakufanyieni mito.(12).

Hii yote inaonyesha jinsi gani madhambi ndio yanayoleta balaa na mitihani duniani, kama ni bakora na adhabu kwa watu kama Allah alivoeleza kisa cha watu wa bustani na visa vya kaumu zilizopita, baada ya kukufuru na kutenda dhambi Allah aliwapa njaa na kiu pamoja ukame. Ila njia pekee ni kurudi kwa Allah (subhanahu wataala) na kuleta istighfaar.

Usiende kwa mganga kumshirikisha Allah ewe mwanadamu una matatizo, mambo yako hayakai vizuri basi kimbilia kuleta istighfaar ya kweli kutoka ndani ya moyo basi Allah (subhanahu wataala) atakusamehe dhambi zako na atakuneemesha neema mbali mbali kama alivyosema katika Quraan.

Hizi fadhila na faida kubwa katika istighfaar pale mja anapoomba msamaha kwa mola wake subhaanahuu wataala. Je ni wangapi ambao huleta istighfaar na wakapata kheri na neema hizi alizoahidi Allah (subhaanahuu wataala). Daima tudumu na kuleta ISTIGHFAAR.

Allah ni mjuzi zaidi.

2 comments:

  1. mashaallah allah akulinde na Shari za dunia hii inshaallah🤲

    ReplyDelete