Monday 7 July 2014

RAMADHANI NA QUR-AN


                  Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

             Sifa zote njema zinamstahikia Allah Subhaanahu Wataala Muumba mbingu na ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, Sala na salamu zimuendee kipenzi cha umma bora Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi Wa Sallam pamoja na Ahli zake na Swahaba zake na walio wema hadi siku ya malipo.

            Ndugu yangu katika Imani hatuna budi kumshukuru Allah Subhaanahu Wa Taala kwa kutujaalia kuwemo miongoni mwa waja wake aliowachagua kuudiriki mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Tunamuomba Allah Subhaanahu wa Taala atuwezeshe kuzitekeleza Ibada zote kwa wingi na atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake watakaofikia lengo la kufunga mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani na siku ya malipo ikifika atujaalie kwa Rehma zake kuingia katika Pepo yake kwa daraja za juu bila ya hisabu.

            Ndugu yangu katika Imani, katika makala yetu tutajaribu kuzungumzia kuhusu kufungamana kwa Ramadhani na Qur-an.

             Ibada baada ya Sala na Zakka iliyofaradhishwa kwetu na Allah Subhaanahu wa Taala ni Funga ya Ramadhani. Ibada hii ya kufunga imefaradhishwa katika sheria za Mitume wote tangu mwanzo. Umma zote zilizopita zilikuwa zikifunga kama Umma huu wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi wasallam unavyofanya.  Lakini kuhusu masharti ya kufunga na idadi ya siku za kufunga vilikuwa vikitafautiana kwa kila sheria ya kila umma. Historia hii fupi ya Funga imethibitishwa ndani ya Qur-an katika Suratul BAQARA  aya ya 183, pale Allah Subhaanahu wa Taala aliposema :- “Enyi mlioamini! Mumefaradhishiwa kufunga kama walivyofaradhishiwa waliopita kabla yenu ili mupate kuwa Wacha-Mungu.”

               Kutokana na aya hii inaonesha wazi kwamba katika kila sheria aliyoleta Allah Subhaanahu Wa Taala kwa kila Umma basi haikukosekana Ibada ya Funga.

             Ndani ya mwezi wa Ramadhan muislamu anatakiwa ajibidiishe katika kufanya yaliyo ya kheri kuanzia ya faradhi na yale ya sunna. Pia muislamu anatakiwa ajitahidi  aisome sana Quraan ndani ya mwezi wa Ramadhan. Na usomaji wenyewe uwe tofauti na usomaji mwengine. Uwe ni usomaji wenye mazingatio. Ili muislamu atumie chuo cha Ramdhani katika kuiweka sawa imani yake na kuzingatia ujumbe kutoka kwa mola wake. Ndani ya mwezi wa Ramadhani ndipo ilipoteremshwa Qur-an Tukufu kwa namna tofauti.

Amesema Allah Subhaanahu wa Taala katika Sura ya pili (2) (AL-BAQARA), Aya ya 185 :- “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa Qur-an ili iwe uongofu kwa watu, na hoja zilizowazi za uongofu na upambanuzi (wa baina ya haki na batili)………”

                   Aya hii inatuthibitishia wazi kuwa Qur-an iliteremshwa katika mwezi wa Ramadhani, kwa hiyo inaonekana wazi kwamba mwezi huu wa Ramadhani haukuchaguliwa kuwa mwezi wa kufunga bure bure tuu bila ya sababu, isipokuwa mwezi huu umechaguliwa kwa sababu ndio mwezi ambao ndani yake iliteremshwa Qur-an kwa namna tofauti na nyakati tofauti. Na Quraan ndio nuru kwa umma.

QUR-AN
                    Qur-an Tukufu ni kitabu cha Allah Subhaanahu wa Taala kilichoteremshwa kwa Mtume Swalla Allahu Alayhi wa Sallam ili iwe uongofu kwa watu wote (viumbe vyote).

                  Qur-an ni kitabu kilichokusanya mambo yote ya maisha ya kidunia  na Akhera  ya mwanzo na ya mwisho, Pia ni kipambanuzi cha haki na batili. Pia ni yenye kuwaonya waumini na  kwa maana hizo tunaona wazi kwamba Allah Subhaanahu wa Taala ameiteremsha Qur-an ili tupate kujua namna ya kuishi maisha bora ya utii hapa duniani ili kupata Rehma za Allah Subhaanahu wa Taala katika maisha ya duniani na akhera.

Anasema Allah (subhanahu wataala) :
“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi.”(Baqara :185).
“……Hizi ni Aya za Kitabu na Qur'ani inayo bainisha.”(Hijri :1).

“Ametukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote” (Furqaan :1).
                  Qur-an Tukufu ilikuwa imehifadhiwa katika Ubao unaoitwa “LAUHI-MAHFOODH”. Anasema Allah (subhanahu wataala) katika Suratul Buruj “Bali hii ni Qur'ani tukufu(21)Katika Ubao Ulio Hifadhiwa. (22)
Na baada ya hapo iliteremshwa hadi katika wingu wa kwanza wa dunia kwa ujumla wake, wakati huo ilikuwa katika mwezi wa Ramadhani. Na baadae ilianza kuteremshwa kwa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi wa Sallam kidogo kidogo, Mara ya kwanza kuanza kuteremshwa kwa Mtume Swalla Allahu Alayhi wa Sallam ilikuwa katika mwezi wa Ramadhani katika kumi la mwanzo, na aya za mwanzo kuteremshwa ni aya tano za mwanzo za Suratul-Alaq. Na ilikuwa ikiteremshwa na Malaika mtukufu JIBRIL Alayhi Salaam ambaye alikuwa akiwashukia Mitume wote kwa ajili ya kuwapelekea Wahyi kutoka kwa Mola wao.

                  Kutokana na Historia hiyo fupi tunaona wazi kwamba Qur-an imefungamana na mwezi wa Ramadhani kwa sababu ndio mwezi ulioteremshwa Qur-an kwa namna tofauti na nyakati Tofauti.

                       Ndugu yangu katika Imani, hakika ya Funga pamoja na kusoma Qur-an ni Ibada zilizokuwa kubwa zaidi na zenye malipo makubwa. Lakini kuisoma Qur-an kusiwe juu juu tuu na sauti zilizokuwa nzuri zenye kuvutia. Isipokuwa kuisoma Qur-an kunatakiwa umakini mkubwa pamoja na kuizingatia vizuri tafsiri yake na kuifanyia kazi katika maisha. Allah (subhanahu wataala) anasema “Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?”( Suratu Muhammad :24). Hivyo basi na sisi tuisome Quraan kwa mazingatio makubwa kwa sababu kwenye Qur-an ndipo tunapopata kila kitu juu ya maisha tunayotakiwa tuishi. Kwa hivyo tunapofunga katika mwezi huu wa Ramadhani tujitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu wote kuisoma Qur-an kwa wingi na kwa mazingatio pamoja kuifanyia kazi mafundisho yake ili tupate kuongoka. Tunapofanya hivyo ndipo tunapofikia yale malengo ya kufunga mwezi wa Ramadhani nayo ni kufikia daraja za Ucha-Mungu.

Fadhila za kusoma Quraan hatutozielezea kwani tayari tumezieleza katika darsa zetu nyengine.

                     Tumuombe Allah Subhaanahu wa Taala atuwafikishe kuifunga Funga hii ya Ramadhani na atuwezeshe kuisoma Qur-an kwa mazingatio na atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake watakaofikia daraja ya Ucha-Mungu, na Siku ya malipo ikifika atuingize Peponi kwa Rehma zake. Aaamin.

No comments:

Post a Comment