Saturday 19 July 2014

VIPI UTAIPA NGUVU IMANI YAKO

Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Imani ya mja huwa inapanda na kushuka. Na hii ni miongoni mwa tabia za muislamu. Kuna wakati muislamu imani yake humjaa na huwa anajitahidi katika Ibada. Sala tano hazimpiti tena kwa jamaa. Funga za sunna huwa ndio vazi lake. Adhkaar na sala za usiku ndio mapambo yake. Lakini baada ya muda haya mambo yote huwa hayafanyi tena. Na huanza uvivu wa kutekeleza mambo hayo.

Wengine wao huwa na imani kubwa sana na hamu ya kutenda matendo mema na nia hasa pale wanapokumbushwa. Ila baada ya muda hamu ile ya kufanya ibada inapotea. Lakini hawa wote tujiulize ni kipi kinachowafanya wawe hivyo? Tatizo lao ni udhaifu wa imani au kushuka kwa imani. Imani inapokuwa juu basi ndipo kheri zote huzikimbilia au ndipo hamu ya kufanya ibada humjaa mtu. Lakini imani inaposhuka basi huyu mtu huwa hana tena hamu ya mambo hayo na huwa na uvivu. Sasa nini afanye ili aipe nguvu imani yake? Leo katika makala hii tutajaribu kuelezea baadhi ya njia ambazo muislamu anaweza kuzifanya ili aweze kuipa nguvu imani yake. Njia zenyewe ni kama zifuatazo :

1-Kusoma Quraan kwa mazingatio
Endapo muislamu anapohisi imani yake imeshuka au inatetereka basi akimbilie kusoma sana Quraan. Ila aisome Quraan kwa mazingatio kwa kujua ni kipi ambacho Allah (subhanahu wataala) anakielezea ndani ya Quraan. Na ikiwa mtu hajui tafsiri ya Quraan basi asome kwa kutumia msahafu wa tafsiri.

Hakuna yeyote ambae amesoma Quraan kwa mazingatio isipokuwa umelainika moyo wake. Na hapo ndipo sifa ya muum,ni inapopatika. Na endapo ukaona kuwa unasoma Quraan na moyo wako hauathiriki na chochote basi jua wewe ni  maiti inayotembea duniani. Allah (subhanahu wataala) anasema “Hakika Waumini ni wale ambao anapo tajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa khofu, na wanapo somewa Aya zake huwazidisha Imani, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.” (8:2). Aya hii inaonesha wazi kuwa yeyote yule anaesoma Quraan kwa ufahamu na mazingatio basi kwa hakika imani yake itapanda.

Pia Allah (subhanahu wataala) anasema ndani ya Suratu Muhammad aya ya 24 “Je! Hawaizingatii hii Qur'ani? Au kwenye nyoyo (zao) zipo kufuli?” Je sisi waumini hatuna mazingatio na aya za Allah? Au nyoyo zetu zimefungwa? Ndipo Allah akauliza au zina kufuli? Kwa maana zimefungika hakuna ndani yake kinachoingia. Tujitahidini tulainishe nyoyo zetu ili Quraan iwe ni ukumbusho kwetu.

Vipi watu wema walikuwa wakiathirika kwa kusoma Quraan kwa mazingatio ? Tuangalie mifano ifuatayo halafu tujiulize na sisi nafsi zetu zipo sehemu gani?

Siku moja Sayyidina Omar (radhiya Allahu anhu) alikuwa akiisoma aya katika aya za Quraan. Alipozisoma akaanza kulia na kulia. Mpaka akawa anashindwa kutoka nje ya nyumba yake kwa sababu ya kilio alichokuwa nacho. Je alilia tu bure bure? Hapana alilia kwa sababu aliyafahamu maneno ya Allah kwa upeo wa juu na akawa anajiuliza vipi yeye hali yake itakuwa. Aya yenyewe aliyoisoma ni  “Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea.(7) Hapana wa kuizuia.(8). Machozi yake yalishindwa kujizuia akikaa akijiuliza vipi adhabu za Allah (subhanahu wataala) zitakuwa. Vipi mimi na wewe tunapozisoma aya kama hizi? Je nyoyo zetu hazipaswi kunyenyekea na kuwa na mazingatio?

Tumuangalie nae Omar Ibn Abdul Aziz. Siku moja Omar Ibn Abdul Aziz alisikilikana analia kwa sauti na kushindwa kujizuia.Jirani yake akaenda kumuuliza “Je ni kipi kimekusibu hadi unalia?”Omar Ibn Abdul Aziz akamwambia ”Hakuna kinachoniliza isipokuwa aya hii ndani ya Quraan,Allah(subhanahu wataala)anasema “…Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi, na kundi jengine Motoni”(42:7).Najiuliza ndani ya nafsi yangu je nitakuwa katika kundi lipi kati ya haya mawili?.

Hebu tuangalie vipi wenzetu wamekuwa wakiathirika na kusoma Quraan. Vipi mimi na wewe? Je hatuzipiti aya hizi? Je tunaisoma Quraan kwa mazingatio? Hawa ni wachache tu ambao wanaathirika kwa kusoma Quraan. Mifano ipo mingi ndugu zangu wakiislamu. Tujitahidini sana kuisoma Quraan kwa mazingatio ili tuweze kuzikuza imani zetu.

2- KUKITHIRISHA KUKUMBUKA MAUTI

Mauti ni safari ya lazima kwa kila mwanadamu. Nayo ni safari ya kutoka katika dunia katika maisha ya mpito na kuelekea katika maisha ya akhera. Mwanadamu yanapomkuta mauti basi muda wa mtihani wake ndio unakuwa umekwisha na kinachobaki ni kwenda kukutana na hesabu. Je ulishwahi kujiuliza ni vipi roho yako itatolewa? Itatolewa kwa ajili ya kwenda jannah au itatolewa kwa ajili ya kwenda motoni? Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa hali yake pale utakapokuwa umebebwa kwenye jeneza? Je ulishawahi kukaa na kujiuliza vipi utaikuta hesabu yako? Je umeshawahi kujiuliza nini utamjibu Allah pale utakaposimamishwa mbele yake? Mauti ni mazingatio tosha kwa muislamu na kumkumbusha ili aweze kukaa katika njia ya Allah (subhanahu wataala).

Mtihani mkubwa zaidi ni watu kuyachukia mauti. Na wapokuwa wakikumbushwa kuhusu mauti huwa wanachukia na kuona Sheikh hakuwa na mawaidha ila ya kuwatisha. Kumbe wanasahau kukumbushwa mauti ni kumfanya mtu aizidishe imani yake na kujiandaa na siku ya kutoka roho. 

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema katika hadithi “ Kithirisheni katika kukumbuka chenye kukata ladha “ Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ameyaita mauti kama ni kikata ladha. Ndiyo mauti ni yenye kukata ladha ya starehe za uongo za dunia. Mwnadamu anapokumbuka mauti basi awe anajiuliza masuala ya msingi ambayo atakutana nayo. Na endapo muislamu ataona kuwa hata akikukumbuka mauti moyo wake hauthiriki basi pi ana yeye ataingia katika kundi la wale maiti wanaotembea katika dunia hii.
Anasema Allah (subhanahu wataala) ““Kila nafsi itaonja mauti. Na bila shaka mtapewa ujira wenu kamili Siku ya Qiyaama.”(3:185).

Tujiandaeni mauti na tujitahidini katika kukithirisha kukumbuka mauti kila wakati hili litamsaidia muumini na kumuasi Allah (subhanahu wataala).

3-KUTEMBELEA MAKABURI

Makaburi nayo yana siri nzito ndani yake. Tayari tumeshamuhifadhi ndugu yetu katika kuelekea katika maisha yake ya milele. Nini kinachojiri ndani ya mauti. Mwanadamu atakapokaa na kuliwaza kaburi, giza lake na juu yake kufukiwa na michanga. Vipi atakaa ndani ya shimo hilo?  Je ulishawahi kujiuliza vipi itakuwa usiku wa kwanza ndani ya kaburi lako?Je wakati watu watakapokuwa washamzika ataweza kujibu maswali ya Munkar na Nakir? Je kaburi lake litakuwa ni bustani katika bustani ya peponi au mashimo katika mashimo ya motoni?

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ametuusia kutembelea makaburi pale aliposema “Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) amesema, “Nilikuwa nimewakataza kwanza kuzuru makaburi lakini kuanzia sasa yatembeleeni.” (Muslim) katika riwaya nyingine , “Kwani huko kuzuru makaburu hukukumbusheni na akhera.” (Ahmad) .Kutembelea huku sio ule wakati wa kwenda kuzika. Mtu awe anapanga siku maalum kwenda kuyatembelea makaburi kwa lengo iwe ni mazingatio kwake yeye. Kwa lengo na yeye ajiulize vipi itakuwa hali yake pale atakapowekwa ndani ya kaburi.

Sayyidina Othman Ibn Affan (radhiya Allahu anhu) alikuwa akitajiwa kuhusu moto na adhabu za Allah analia. Lakini anapotembelea makaburi huwa analia zaidi mpaka ndevu zake zikarowa machozi. Maswahaba wakamuuliza ni kipi kinachomfanya hivyo ? Sayyidina Othman akajibu kaburi ndio nyumba ya kwanza ya maisha ya akhera. Ikitengenea hali ndani ya kaburi ndio yametengenea mengine na hali ikiwa mbaya basi ndio mwanadamu amekhasirika. Sasa najiuliza vipi kaburi langu litakuwa?

Mmoja ya watu wema alikuwa akiingia sehemu ya makaburi basi huuziba uso wake kwa kilemba chake. Kwa nini huuzibaa? Ili asionekane akilia kwani alikuwa anashindwa kujizuia asilie akikaa akiliwaza kaburi lake. Litakuwa na hali gani.

Hawa ndio ambao wakikumbuka vitu kama hivi huvikumbuka kwa mazingatio makubwa ndani yake. Je vipi mimi na wewe? Sio wale ambao tunaenda kwenye makaburi na simu zetu za kuchat mkononi? Sio sisi tunaenda kwenye makaburi na mazungumzo ya kusema watu yapo kwenye midomo yetu?
Tembelea makaburi ili uizidshe imani na uwe ni mwenye kujiandaa daima na kukaa katika kaburi lako.

4- KUKAA NA MARAFIKI WEMA NA KUSHIRIKI VIKAO VYA KHERI

Rafiki huchangia kwa kiwango kikubwa maisha ya binaadamu. Na hili linathibitishwa na Mtume Muhammad(swalla Allahu alayhi wasallam) kwa kauli yake pale aliposema “ Mtu hufuata mwenendo wa rafiki yake,basi aangalie mmoja wenu ni nani anaemfanya kuwa ni rafiki” Attirmidhy.

Jitahidi sana na kuwaepuka marafiki waovu kwani hawawezi kukusaidia katika kuikuza imani yako. Kaa na rafiki mwema rafiki ambae daima atakuwa ni mwenye kukuhimiza katika kufanya yalo mema na yaliyo mazuri. Tumeona mifano ya wengi ambao wamepotoka kwa sababu tu ya marafiki.

Na Allah (subhanahu wataala) anatuambia ndani ya Quraan “Wala usimt'ii tuliye mghafilisha moyo wake asitukumbuke, na akafuata matamanio yake yakawa yamepita mpaka.”(18:28). Aya hii ni ukumbusho kwa muumini awe mbali na wale ambao hawako katika kumtii Allah (subhanahu wataala) nao hufuata matamanio ya nafsi zao.

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema "Mfano wa rafiki mwema na rafiki mbaya ni kama ule wa muuzaji wa misk na mhunzi. Basi kwa muuzaji wa misk, imma atakunusisha, au utanunua kwake ama angalau utafurahia harufu nzuri kwake. Na kwa yule mhunzi, imma atakuchomea nguo au utapata harufu mbaya kutoka kwake.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

Katika tafsiri ya Hadiyth hii, Imam An-Nawawiy alisema: Mtume ((Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)) alilinganisha rafiki mzuri na muuzaji misk kwasababu, kwa rafiki mzuri mwenye tabia ya upole, na elimu, utapata faida kwake. Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitukataza kukaa na wale wenye kufanya maovu.

Hivyo ndugu yangu muislamu tafuta rafiki mwema ambae daima mazungumzo yenu yatakuwa ni ya kheri na ni yenye kuhimizana kufanya mema na kukumbushana pale mtu anapokosea.

Pia kushiriki katika vikao vya kheri katika misikiti,kwenda katika mihadhara kwani katika vikao hivyo hukumbushwa yaliyo mema na kukatazwa yaliyo mabaya ambayo mtu yatamfaa katika maisha yake ya dunia na kesho akhera. Na tusichoke kuhudhuria kwa wingi na kwa wakati mwingi kama vile tunavyotumia wakati mwingi katika kuangalia michezo,mipira au kupoteza wakati kwa kuchat na ndani ya facebook.
Mwisho kabisa ndugu yangu wa kiislamu nakuusia mambo mawili. Jambo la kwanza kithirisha sana katika kumuomba dua Allah (subhanahu wataala) katika kuifanya imani yako isiwe yenye kutetereka na aijaalie imani yako iwe ni yenye kuzidi pale unapokutana na misukosuko. Pia kuwa ni mwenye kuihesabu nafsi yako daima kabla ya kulala hii itasaidia katika kukuzindua ni kwa kiasi gani uko mbali na Allah. Na hesabu hiyo uwe unaifanya ni sababu ya wewe kujiepusha na maasi yale ambayo umeyatenda.

Namuomba Allah atujaalie imani zetu ziwe thabiti na aturidhie pale tutapoondoka hapa duniani. Aaamin.

No comments:

Post a Comment