Saturday 19 July 2014

TAQWA NA VIPI TUTAIPATA TAQWA NDANI YA RAMADHANI

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Allah (subhanahu wataala) ametufaradhishia juu yetu kufunga. Na pale alipotufaradhishia akatuambia kuwa lengo kuu la kutufaradhishia funga ni kupata uchamungu(Taqwa). Pale aliposema “Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.”(2:183). Suali linaweza kuja nini maana ya uchamungu. Na vipi mtu anaweza kuupata uchamungu ndani ya Ramadhan? Kwa uwezo wa Allah kwa uchache majibu ya masuala hayo yatapatikana ndani ya makala hii.

TAQWA

Taqwa ni vazi ambalo anatakiwa avae kila muislamu. Vazi ambalo limekusanya yale yote aliyoamrisha Allah (subhanahu wataala) ambayo yanatakiwa yatekelezwe na yale yote yaliyoharamishwa ambayo yanatakiwa kuachwa. Msingi mkuu wa taqwa ni kufuata Quraan na Sunna za Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam). Na vazi hili la uchamungu ndio vazi bora kuliko vazi jengine lolote. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo. Na nguo za uchamungu ndio bora…”(7:26).

Taqwa ni amri kutoka kwa Allah. Allah ametuamrisha tumche yeye pekee hapa ulimwenguni. Na akatuambia tuchukue zawadi ya uchamungu kwani ndio zawadi iliyokuwa bora kabisa na ndio itakayomfaa mwanadamu siku ya kukutana na mola wake. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Na jitengezeeni zawadi. Na hakika bora ya zawadi ni uchamngu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili! (2:197).

Pia Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amelisisitiza hilo kwa kututaka tuwe wenye kumcha Allah (subhanahu watala)popote tulipo iwe peke yake mtu au mbele za watu. Kutoka kwa Abu Dharr Jundub Ibn Junaada na Abu Abdur Rahmaan Muadh Ibn Jabal (radhi za Allah ziwe juu yao) kutoka kwa   Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: "Mche Allah popote pale ulipo, na fuatisha kitendo kibaya kwa kitendo kizuri kitafuta kitendo kibaya, na kaa na watu kwa uzuri"  At-Tirmidhiy.

Sayyidina Ali Ibn Abi Taalib (radhiya Allahu anhu) aliulizwa nini maana ya uchamungu? Akajibu “ Kumuogopa Allah, Kufanyia kazi yaliyoteremshwa (Quraan na Sunna), na kuridhia kwa kidogo (alichoruzukiwa mtu na Allah), na kujiandaa na siku ya kuondoka(kifo).

Pia Sayyidina Umar Ibn Khattwaab (radhiya Allahu anhu) aliulizwa kuhusu uchamungu. Akamuuliza yule muulizaji nini utafanya ikiwa unatembea katika njia yenye miba? Yule mtu akajibu nitatembea kwa tahadhari ili isinichome miba. Sayyidina Umar akamwambia basi huo ndio uchamungu wakati unapoishi katika ulimwengu huu. Kwa maana yale yote ya haramu mtu anatakiwa achukue tahadhari nayo ili yasije kumuingiza katika moto. Na yale ya halali ndio sehemu ya mtu kuweka mguu wake.

Kwa ujumla kabisa Taqwa ni mtu kumuogopa Allah (subhanahu wataala) na kufanya yale yote aliyoamrishwa na kuwa mbali  na yale aliyokatazwa na Allah (subhanahu wataala).

NI YAPI MALIPO YA MWENYE KUMCHA ALLAH (SUBHANAHU WATAALA)

1- Kupata wepesi wa mambo yake kutoka kwa Allah (subhanahu wataal). Anasema Allah (subhanahu wataala)“Na anaye mcha Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu humfanyia mambo yake kuwa mepesi.” (65:4).
2- Kusamehewa dhambi zake na Allah (subhanahu wataala). Anasema Allah (subhanahu wataala) “Na anaye mcha Mwenyezi Mungu atamfutia maovu yake, na atampa ujira mkubwa.”(65:5).
3- Kupata njia ya kutokea katika mambo yake na kuruzukiwa bila ya kutarajiwa. Anasema Allah (subhanahu wataala) katika Suratu Twalaaq “na anaye mcha Mwenyezi Mungu humtengezea njia ya kutokea.(2) Na humruzuku kwa jiha asiyo tazamia…(3).
4- Kupata pepo ya Allah subhanahu wataala. Tujue kuwa ndani ya pepo ya Allah hatoingia ila yule ambae ni mchamungu. Anasema Allah (subhanahu wataala) :
“Na yakimbilieni maghfira ya Mola wenu Mlezi, na Pepo ambayo upana wake ni mbingu na ardhi, iliyo wekwa tayari kwa wachamngu,”(3:133).

“Hiyo ndiyo Pepo tutayo warithisha katika waja wetu walio kuwa wachamngu.”(19:63).

Na kwa upande wa hadithi kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) Amesema: Na aliulizwa Mtume (swalla Allahu ayahi wasallam ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi? Akasema: "Kumcha Mwenyeezi Mungu na tabia njema" Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema "kinywa (mdomo) na utupu." Imepokelewa na At-Tirmidhiy.

VIPI TUTAIPATA TAQWA NDANI YA RAMADHANI

Muislamu anaweza kuupata uchamungu kutoka kwenye Ramadhan kwanza kwa kufunga saumu yake kwa imani na kutarajai malipo kutoka kwa Allah. Unapofunga kwa imani unaamini kuwa hiyo ni amri ya Allah ambayo inatakiwa kutekelezwa kwa vile ambavyo Allah (subhanahu wataala) ameamrisha itekelezwe.

Mwenye kufunga kwa imani daima atakuwa ni mwenye kukaa mbali na kufanya na maasi. Pia kwa kutaraji malipo. Mwanadamu akiahidiwa pesa nzuri au mshahara mzuri kutokana na kazi yake atakayoifanya basi bila ya shaka atakuwa na jitihada kufanya kazi ile kwa uzuri wa hali ya juu kabisa. Je vipi ikiwa malipo yenyewe yanatoka kwa Allah? Bila ya shaka utakuwa ni mwenye jitihada za hali ya juu kabisa kwa sababu unajua unaemfanyia jambo hilo yeye hafaidiki na kitu ila wewe ndio unafaidika na pia wewe ndio unafaidika na malipo anakupa yeye. Tuangalieni uzito wa jambo hili.

Pili kuwa na Ikhlaas katika ibada zetu zote. Ikhlaas ni kufanya jambo kwa ajili ya Allah (subhanahu wataala) pekee. Na lazima mtu awe mbali kabisa na ajiepushe na masuala ya kujionesha. Sio mtu afunge ili watu wamuone. Au afanye jambo lolote la kheri kwa sababu tu watu wapate kumuona au kumsifia. Hayo ni makosa na muislamu hatakiwi kufanya hayo.

Tatu kujibidiisha katika kuswali sala za faradhi kwa uzuri na kwa khushui. Na pia kusali sala za Sunna. Mwenye kusali sala kwa khushui na kwa ajili ya Allah (subhanahu wataala) basi kwa hakika atakuwa mbali na maasi na ndipo atakapoweza kuupata uchamungu. Allah (subhanahu wataala) anasema “Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu.”(29:45).

Kujibidiisha kufanya ya kheri ikiwemo kusoma quraan kutoa sadaka,kufanya umra na mengineyo.

Muislamu ajitahidi kufanya mambo kama haya ya kheri. Na mwisho abakie kumuomba Allah (subhanahu wataala) amjaalie awe miongoni mwa wacha mungu. Kwani bila ya tawfiq ya Allah hatuwezi kufika katika darja kama hizo.

Pia muislamu anatakiwa awe mbali kabisa na kujitukuza na kujiona kuwa yeye ni mchamungu kwa sababu tu anajitahidi kufanya ibada na anakuwa mbali na mambo ya haramu. Hakuna anaeweza kujijua kuwa yeye ni mchamungu isipokuwa Allah (subhanahu wataala) ndie anaetujua sisi. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Basi msijisifu usafi. Yeye anamjua sana mwenye kujikinga na maovu “(53:32). Tuwe na tahadhari nalo sana. Muhimu ni kuwa na bidii na mwisho ni kumuomba dua Allah atuwafikishe katika hayo.

Allah atujaalie tuwe miongoni mwa wachamungu. Aaamin.

No comments:

Post a Comment