Friday 4 July 2014

REHMA ZA ALLAH (SUBHANAHU WATA‘ALA) KWA WAJA WAKE


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Ndugu zangu wa kiislamu Mtume (swalla Allahu alayhi wasalam) anatuambia kuwa Ramadhan imegawika katika makumi matatu. Kumi la kwanza ni REHMA, la pili ni MAGHFIRA na la tatu ni KUACHWA HURU NA MOTO. Kwa hakika sasa hivi tuko katika kumi la Rehma. Rehma za Allah kwa waja wake ni nyingi na hatuwezi kuzielezea au kuzizungumza na tukaweza kuzimaliza. Hivyo basi tutazungumza kwa uchache kuhusu Rehma za Allah kwa waje. Muislamu atakapoyafahamu vizuri haya ndipo atakapojua umuhimu wa yeye daima kuomba Rehma za Allah (subhanahu wata‘ala).

Awali kabisa katika mada hii napenda nielezee maneno haya mawili nayo ni ARRAHMAAN NA ARRAHYM. Maana ya maneno haya ni kuwa Allah ni mwingi wa Rehma na mwenye kurehemu. Maneno haya ni majina miongoni mwa majina ya ALLAH kwani ALLAH (subhanahu wata‘ala) ana majina mengi. Na kwa kuangalia maana ya majina haya kwa haraka kabisa utaona kuwa yana maana moja kwa sababu yanatokana na neno Rehma (huruma). Ila maana zake kiundani ni kuwa, ARRAHMAAN maana yake ni rehma za ALLAH kwa waja wake wote hapa ulimwenguni. Kila kiumbe chake Allah basi anapata rehma kutoka kwa muumba wake. Anasema Allah (subhanahu wata‘ala): “Na rehema yangu imeenea kila kitu.” (7:156). Na neno ARRAHYM hizi ni rehma maalum kwa waja wake walioamini pekee katika siku ya malipo pale Allah aliposema katika suratul Ahzaab mwisho wa aya ya 43: “Naye ni Mwenye kuwarehemu Waumini.”

Rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwa waje wake ni nyingi mno. Na huruma za Allah kwa viumbe vyake ni kubwa sana. Hebu tuangalie kwa uchache baadhi ya mifano ya rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwetu.

Hebu angalia rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwa mtoto mchanga ndani ya tumbo la mama yake. Mbali ya kuwa mtoto yumo ndani ya tumbo na hana anaemuona wala kumshughulikia, Allah (subhanahu wata‘ala) anajaalia mtoto yule anakuwa vizuri na anapata rizki zake akiwa yumo mule mule ndani ya tumbo la mama yake.

Mtoto amezaliwa tayari wako baadhi yao wamezaliwa wakiwa na upungufu wa viungo na wengine wakiwa na viungo kamili. Wote hawa kuzaliwa na hali yoyote ile basi huwa ni rehma kwao. Leo binaadamu hajakaa kumuomba Allah (subhanahu wata‘ala) ampe macho, masikio, miguu wala akili ila Allah (subhanahu wata‘ala) amemjaalia kiumbe yule amezaliwa akiwa na viungo vyote hivyo na hajaviomba. Jee hatuoni kuwa hii ni rehma katika rehma zake Allah (subhanahu wata‘ala) kwetu?

Wengine wamezaliwa hawaoni, hawasikii au hawatembei vipi tutasema kwao wao ni rehma? Ndio ni rehma kwani tayari wameshapewa takhfif ya mtihani huko akhera. Mtihani ambao kila aliyepewa neema hizo lazima akazielezee vipi amezitumia. Mwenye macho ataulizwa vipi ameyatumia macho yake, jee ameyatumia katika halali au haramu? Ila yule aliyekosa macho basi hatokuwa na mtihani huo kwani jicho lake halikuwahi kudiriki kuona. Hivyo tuwe waangalifu na ambayo tunayafanya.

Rehma nyengine ya Allah kwetu sisi ni kuwa tumezaliwa katika neema kubwa ya Uislamu. Si kwa ubabe wetu wala uhodari wetu bali ni kwa rehma zake Allah (subhanahu wata‘ala) kwetu sisi. Kwani wako wengine wanazaliwa hali ya kuwa si Waislamu. Suala litakuja je hawa wamekosa rehma za Allah? Hapana hawakukosa rehma za Allah. Zipo rehma za Allah kwake na ndio maana akampa akili na baadae kumpelekea mjumbe wa kumlingania katika haki. Allah (subhanahu wata‘ala) hataki hata mja wake mmoja afe hali ya kuwa anamuasi. Ila sisi wenyewe ndio tunaojiingiza katika maangamizo.

Pia ni katika Rehma za Allah kwetu sisi kutujaalia tumezaliwa tukiwa tumo katika Umma bora, umma wenye kitabu bora pamoja na kuletewa Mtume bora. Je hatujui sisi kuwa katika wakati huu pekee ni rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwetu sisi. Nabii Mussa alayhi salaam alitamani awe mfuasi tu ndani ya Ummat Muhammad. Jee mimi na wewe tunathamini hilo? Jee tunajua kuwa ni rehma zake Allah (subhanahu wata‘ala) kutujaalia sisi kuwa katika Umma huu?

Ndugu zangu wa kiislamu rehma za Allah kwetu sisi ni kubwa mno. Hatuwezi kumaliza mifano kwa kuiandika wala kuzungumza.

Tutosheke na mifano hiyo michache ambayo iwe ni mazingatio kwetu sisi.

KIMBILIA KATIKA KUZIPATA REHMA ZA ALLAH NA USIKATE TAMAA KUTOKANA NA REHMA ZAKE

Mifano tuloitaja juu ni mifano ya rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwetu sisi. Mifano ambayo hatukukaa kuiomba bali mwenyewe Allah ametujaalia. Muislamu hatakiwi kukaa tu akasema rehma za Allah zipo tu kwangu na zitakuja. Lazima Muislamu wa kweli ajibidiishe katika kuzitafuta rehma za Allah. Hakika kila mmoja wetu ni muhitaji wa rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) kwa kila jambo. Hakuna mtu anaeweza kusema kuwa ametosheka na rehma za Allah.

Jee Muislamu ili azipate rehma za Allah afanye nini? Jambo la kwanza Muislamu anatakiwa awe ni mwingi wa kufanya mazuri na kujiepusha na haramu. Kufanya hivyo kutamfanya aweze kupata rehma za Allah kwa ushahidi wa Quraan: “Hakika rehma za Allah zipo karibu kwa wenye kufanya mazuri(muhsinin).” (7:57).
Aya hapo juu inaonyesha wazi kabisa rehma za Allah ziko na wenye kufanya mazuri. Hivyo Muislamu azitafute rehma za Allah kwa kukimbilia kufanya mazuri na kujiepusha na kufanya madhambi.
Jambo la pili ni kwa Muislamu kuzidisha dua kumuomba Allah (subhanahu wata‘ala) aweze kumpa rehma zake. Msingi wa ibada ni dua. Wakati watu wanakimbilia kuomba majumba, fedha na utajiri ndugu yangu Muislamu wewe kimbilia katika kuomba rehma za Allah (subhanahu wata‘ala).

Latatu Muislamu akithirishe katika kumtaka msamaha Allah (subhanahu wata‘ala) kwa wingi itamfanya aweze kupata rehma za Allah. Ukiangalia katika Quraan sehemu nyingi ambazo Allah anataja kuhusu msamaha au yeye Allah ni mwingi wa kusamehe basi hutaja mbele yake neno RAHIIM. Hii ni kuonyesha wazi kwetu sisi tunapotaka rehma za Allah basi tukimbilie katika kuomba msamaha wa kweli kwa Allah ili tuzipate rehma zake.

Mfano wa aya hizo ni:
1. “Waambie waja wangu ya kwamba Mimi ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (15:49).
2. “Na ALLAH ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu.” (2:218).
3. “ Ni vyeo hivyo vinavyo toka kwake, na maghfira na rehema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira na Mwenye kurehemu.” (4:96).

Lamuhimu kuambizana ni kuwa tuombe msamaha wa kweli kwa Allah basi atatusamehe kwa rehma zake na tutazipata rehma za mambo mengine. Miongoni mwa rehma anazozipata mwenye kuomba msamaha ni kule kujaaliwa dhambi zake kuwa ni thawabu. “Isipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (25:70). Lakini haya hayapatikani isipokuwa mtu kuomba msamaha wa kweli kwa Allah (subhanahu wata‘ala).

Mwisho kabisa natoa nasaha kwa Waislamu wote kuwa mtu asikate tamaa na rehma za Allah (subhanahu wata‘ala). Kadri utakavyokuwa umemuasi Allah basi utakapoamua kurudi kwake kikweli basi Allah atakupokea na atakusamehe dhambi zako. Muhimu ni mtu kuamua kurudi kikweli kwa Allah (subhanahu wata‘ala). Pia hata yule asiyekuwa Muislamu basi atasamehewa dhambi zake na kuwa kama mtoto mchanga pale anapozaliwa wakati atakapoingia katika Uislamu.

Na angalia rehma za Allah kwa waje wake. Mja juu ya kumuasi Allah bado Allah anamwita mja huyo kwa jina la Mja ( abdu). Mwanadamu akikerwa kidogo tu basi yule aliyemkera humwita kila aina ya majina kuonyesha hasira zake. Ila Allah (subhanahu wata‘ala) juu ya mja kumuasi bado humuita kwa jina la abdu. Na anamwambia arudi kwake na asikate tamaa. Vipi rehma za Allah zilivyokubwa kwetu sisi. Allah (subhanahu wata‘ala) anasema: “Sema: Enyi waja wangu walio jidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (39:53).

Tusikate tamaa na rehma za Allah (subhanahu wata‘ala) na tujitahidini kuzitafuta rehma zake kwa kuyafanya yale aliyotuamrisha. Allah atuwafikishe. Aaamin.

1 comment:

  1. Betway Group - 머니 토토토토토토토 카지노 카지노 starvegad starvegad 593PGA TOUR TOUR 2021 | Online Gambling in Malaysia - Virtual

    ReplyDelete