Monday 7 July 2014

MILANGO YA KHERI NDANI YA RAMADHAN


   Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

MILANGO YA KHERI NDANI YA RAMADHANI

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Milango ya kheri ndani ya Ramadhani hii ni milango ambayo muislamu ajitahidi aifungue na aingie ndani yake kwa ajili ya kupata radhi za Allah (subhanahu wataala) pia kwa ajili ya kupata matunda ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Milango ya kheri ndani ya Ramadhani ni mingi mno. Ila tutaielezea baadhi ambayo muislamu ajitahidi aifanyie kazi.

1-KUFUNGA KWA IMANI NA KUTARAJI MALIPO

Jambo la kwanza kabisa ambao muislamu anatakiwa alifanye ni kufunga Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo. Mwenye kufunga kwa imani na kutaraji malipo basi husamehewa dhambi zake zote zilizopita. Kwa ushahidi amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)katika hadith sahihi, iliyopokelewa na Bukhari,Muslim na Nasai Rahimahumullah na kusimuliwa na Abu-Hurayra radhiallahu anhu :“Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”.
Hili ni jambo la kwanza muhimu kabisa mtu alifanye ili aweze kusamehewa dhambi zake.

2-KUSALI SALA ZA USIKU
Muislamu ajitahidi sana kusali tarawehe,sala za usiku (tahajjud). Mtume (Swalla Allaahu alayhi waaalihi wasallaam) amesema:  "Atakayesimama (kwa Swalah ya usiku) kwa imani na kutaraji malipo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia" Bukhaariy na Muslim

Sala ya tahajjud hii ni sala inayosaliwa wakati wa usiku katika thuluthi ya tatu ya usiku, kuanzia saa saba mpaka saa kumi na sunna zaidi mtu alale aamke.

Na sala hii husaliwa rakaa nane na kumalizia rakaa za witri 1,3,5 kwa rakaa mbili mbili na kumaliza na rakka moja ya witri, au tatu au tano.

Kwa ushahidi wa hadithi aliyopokea Ibnu Abbas radhi za Allah ziwe juu yake anasema, “Nilienda kumtembelea Mtume Swallalahu alayhi wasallam tukalala usiku wake akaamka akatia udhu wa kuswali, akasimama kisimamo cha rakaa mbili, akaatoa salamu, akasali tena rakaa mbili refu zaidi kuliko za mwanzo, akafanya hivo mpaka rakaa nane, ndipo akasimama kuswali rakaa moja, riwaya nyengine akasali rakaa tatu mfululizo  bila ya kutoa  salamu.

Sala hizi zote mtu akisali humuweka karibu mja na Allah subhaanahuu wataala na kupanda darja katika imani na uchamungu.

3-KUMFTARISHA YULE ALIYEFUNGA

Amesema mtume swallalahu alyhi wasallam “Atakayemfutarisha aliyefunga , atapata ujira sawa na Yule aliyefunga bila ya kupungua chochote katika ujira wa Yule aliyefunga” ıimepokelewa na Imam Ahmad na Annasaiy).

Wengi wa watu wanajisahau hapa. Watu huwaftarisha wale wenye uwezo na kusahau maskini. Ili mtu apate ujira zaidi basi awe ni mwenye kuwaftarisha wale wahitaji zaidi. Kwani ndani ya jamii zetu kuna watu wanafunga lakini ftari zao hawajui n inini kwa sababu ya umaskini.

4-KUKAA ITIKAFU KATIKA MSIKITI

Kutoka kwa bibi A’aisha radhi za Allah ziwe juu yake amesema: “Alikuwa Mtume swallalahu alyhi wassalam  akikaa itikaafu katika kumi la mwisho wa mwezi wa Ramadhani, na mwaka ambao aliondoka duniani alikaa siku ishiriini” (Imepokelewa na Imam Bukhary)

Hadithi inaonesha fadhila za iitikafu nayo ni kukaa kikao katika msikiti kwa kuleta adhkaar, kusoma qur-an, kusikiliza mawaidha, kusoma darsa za dini nk.

Kufanya hivi mtu huandikiwa thawabu kwa muda wote aliokaa katika masjid mpaka atakapoondoka.
5- USIKU WENYE CHEO (LAYLATUL QADRI)

Laylatul Qadri ni usiku mmoja ndani ya mwezi wa Ramadhan. Usiku huu ni usiku bora kwa zaidi ya miezi elfu moja (miaka 83) kwa usiku wa kawaida. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatil-Qadr (usiku wa cheo). Na nini kitakachokujulisha ni nini huo (usiku wa) Laylatul-Qadr? (Usiku wa) Laylatul-Qadr ni (usiku) mbora kuliko miezi elfu Wanateremka humo Malaika na Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri (jambo). (Usiku huo ni) Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. (Al-Qadr: 97).

Yeyote utakaomdiriki usiku huu anafanya ibada basi Allah (subhanahu wataala) anamuandikia ibada zake sawa na ibada ya miaka 83. Imehisabiwa mtu atakapofanya ibada katika usiku huo mmoja ni kama amefanya ibada sawa na miaka 83 na hii ni katika fadhila kubwa kabisa. Na katika kitabu Muwatwaa, Imamu Maalik  amesema. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) ameona umri wa umma za mwanzo ni mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi akapewa usiku wa Laylatul-Qadr uwe ni bora kuliko miezi elfu.

Usiku huu haujulikani lini ila kauli yenye nguvu zaidi ni kumi la mwisho ndani ya ramadhani. Ili muislamu aweze kuupata usiku huu basi awe ni mwenye kufanya ibada kwa wingi nyakati za usiku. Na azidishe zaidi katika kumi la mwisho wa Ramadhani.

6- KUKITHIRISHA KUSOMA QURAAN

Muislamu ajitahidi sana kusoma Quraan tena aisome kwa mazingatio. Mwezi wa Ramadhan ndio mwezi ambao imeteremshwa Quraan. Anasema Allah (subhanahu wataala)” Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe Hidaaya kwa watu na hoja bayana za Hidaaya na Al-Furqaan (Upambanuzi). (Al-Baqarah: 185).

7- AKITHIRISHE KUTOA SADAKA
Mtume (Swalla Allaahu alayhi waaalihi wasallaam) amesema: "Sadaka iliyo bora  ni ile inayotolewa katika mwezi wa Ramadhaan" At-Tirmidhiy.

8- KUKITHIRISHA KULETA ISTIGHFAAR

Muislamu aitumie vizuri fursa ya Ramadhan kumuomba msamaha Allah (subhanahu wataala) kutoka na makosa yake. Hivyo basi akithirishe kuleta istighfaar. Ili asije akaingia katika wale wanaokula khasara. Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) aliitikia Aamin kutokana na dua iliyoombwa na Jibril kuwa amekula khasara yeyote yule ambae ameidiriki ramadhani na hakusamehewa dhambi zake.

Na nyakati nzuri zam tu kuleta istighfaar ni katika thuluthi ya mwisho ya usiku. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira (Adh-Dhaariyaat: 18).

Tujitahidini katika kuyafanyia kazi haya tunayoambizana. Na tuitumie fursa ya ramadhani kwa ajili ya kupata rehma za Allah (subhanahu wataala) na kusamehewa dhambi zetu. Allah atuwafikishe katika hayo. Aaamin.

No comments:

Post a Comment