Tuesday 1 July 2014

KOMBE LA DUNIA (WORLD CUP) NA RAMADHAN

Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group 

“IMEWAKARIBIA WATU HESABU YAO, NA WAO WAMEGHAFILIKA NA KUPUUZA.

HAYAWAJII MAWAIDHA MAPYA KUTOKA KWA MOLA WAO, ILA HUYASIKILIZA HALI YAKUA WANACHEZA. ZIMEGHAFILIKA NYOYO ZAO………..” (AL-ANBIYAA 1-3)

Ni suali wanalojiuliza walimwengu wote, kuhusu nani atakaekua bingwa wa soka mwaka huu? Ni kike kwa kiume, wakubwa na wadogo, WAISLAMU na wasiokua waislamu,hukusanyika chini ya vioo vya televishen ifikapo usiku, na kupoteza dakika 90 au zaidi, kuangalia michuano ya soka la kombe la dunia.
Tumejisahau kama tuko ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Tumesahau kua wakati huo wa usiku, Allah hushuka katika wingu wa dunia, na kuuliza nani anaeniomba nimjibu? Nani anaeniuliza nimpe? Na nani anaenitaka msamaha nimsamehe,?(Imesimuliwa na Abu-Hurayra na kupokewa na Muslim na Tirmidhy).

Je sisi tuko katika kundi gani, tunalomuomba ili atupe au kumtaka msamaha atusamehe? Ni kweli imekaribia hesabu ya watu, lakini wenye kuhesabiwa WAMEGHAFILIKA juu ya hilo. Hivi hatuoni kua ni kumfanyia istihzai Allah (subhanahu wataala), kua anashuka kwa ajili yetu na sisi tumeshughulika tukishangiria kandanda? Mara moja alipita Hassanulbasry rahimahullah ,akamkuta mtu anacheka kupindukia, akamuuliza: Je umeweza kuvuka katika Swiraat? Akamjibu: Laa, akamuuliza Je umevuka kutokana na Jahannam? Akamjib: Laa, akamuliza basi hicho kicheko ni cha nini?. Basi nasi tujiulize hivi vicheko vya nini? Au jibu ni kua timu yangu imeshinda?

Tunajiuliza kuhusu nani atashinda mechi ya leo, na nani atanyakua ubingwa, huku tukisahau kujiuliza nini tufanye ili tuifaidi Ramadhan? Je tukifa wakati huu, tunacho cha kumjibu Allah (subhanahu wataala? Tumejiandaa vipi kwa mauti na sakarati yake,kaburi na giza lake,ufufuo na zahma zake,hesabu na undani wake,na mwishowe Jahannam na joto lake?

Mara moja alipita Sayyidina Aliy kwenye kaburi akaliuliza: Je nikupe habari za duniani, ili na mimi unipe za uko ulipo? Akamwambia ama za duniani: Wake zenu wameshaolewa,majumba yashakaliwa na mali zenu zishagaiwa, na kama ungeliweza kunambia habari za uko ulipo, nadhani ungenambia kua :“Chukueni masurufu, kwani safari ya Akhera ni ndefu.”

Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam katika hadithi inayosimuliwa na Abi-Ya’ala: “Mwenye akili ni yule anaejipima nafsi yake, na akafanya yatakayomsaidia baada ya mauti.Na mjinga ni yule anaendekeza matamanio ya nafsi yake, na akatarajia mazuri kutoka kwa Mola wake” (Tirmidhy). Je sisi tuko katika kundi gani? La Wenye akili ama wajinga kutokana na hadithi hii.

Si kama haijulikani kama mwezi huu ni mwezi wa ibada, lakini makafiri hawatoacha kufanya kila aina ya hila, ili waislamu waghafilike, na kwa hilo wamefanikiwa. Amesema ALLAH subhanah“Na hawatoacha kukupigeni vita (makafiri),mpaka wakurejesheni kwenye dini yao ikiwa wataweza”.(Baqarah :217). Umma wa kiislamu umekua ukijua habari za ulimwengu wa mipira, kuliko habari zinazoendelea katika ulimwengu wa sasa wa kiislamu, seuze habari za wema walotangulia, ambapo habari zao wameachiwa wenyewe.

umesahau kua, waislamu wenzetu wanafunga lakini hawajui watakula nini. Na wengine wanafunga, huku wakiwa hawana uhakika kama wataimalizia funga ile palepale nyumbani au hospitalini, baada ya kujeruhiwa na risasi au wataimalizia kaburini. Hii ndio hali ya waislamu nchini Syria, Palestina, Iraq, Myenmaar (Burma), Kashmiir, Afganistan, Chechenia, Somalia,Afrika ya kati na kwengineko. Lakini tuliobaki tumejishau kua tuko katika neema, na ndio tunaitumia neema hiyo, ya uhai ,uzima na amani katika michuano ya kombe la dunia. Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam)“Asiejali mambo ya waislamu basi si katika sisi.”

Yamehifadhiwa majina ya wachezaji ,mwaka alozaliwa, mwaka alojiunga na klabu, pesa ilonunuliwa mkataba wake, mwaka gani atastaafu, anachezea mguu gani ,anapenda nini na hata nani atakaemuoa.Imesahauliwa historia ya Rasuul na nasaba yake,na yule alokua anadai kua anajitahid katika mambo ya dini, basi atamjua mpaka babu yake Abdul-Muttalib. Masahaba 10 walobashiriwa pepo hawajulikani. Majina ya Wake za Mtume na baba zao hayajulikani. Vita vya badri havijulikani vimepiganwa mwaka gani,na idadi ya waislamu walopigana,wala idadi ya mashahidi, Lakini ratiba za mechi na saa zilochezwa fainali zote, tokea mtu apate akili zake anazijua.

Tumeanza kuwapenda wachezaji, mpaka kusahau imani zetu kua sisi ni waislamu na wao ni makafiri, na hatuna uhusiano nao. Tumesahau kua sahaba alimuua baba yake katika vita vya Badri, kwa sababu anaipinga dini ya Allah, na Allah akateremsha aya kumsifia kwa kitendo hicho cha ki-imani na kishujaa, lakini sisi ndio kwanza tunawakumbatia na kujinasibisha nao. Amesema Allah subhanah“Hutowakuta watu wanaomuamini Allah na siku ya mwisho, wakawa wanawapenda wale wanaompinga Allah na Mtume wake, hata wakiwa baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao.” (Mujadalah: 22).

Akasema tena katika suratu-Tawbah 23: “Enyi mloamini,msiwafanye baba zenu na ndugu zenu,kua ni vipenzi vyenu,ikiwa watapenda kufru badala ya Imani” Ikiwa hali ndo hiyo ata kwa jamaa wa karibu, madamu kafiri basi hutakiwi kumpenda, seuze wachezaji mipira ambao hata hajui kama kuna watu wanalia anapouumizwa.

Tumeanza kuwapenda na baadae tukawaiga mikato yao, mienendo yao,na hatimae hadi majina yetu tukaengeza viambishi ili kufanana na yao. Mchezaji kamaliziwa na “vin” basi na mimi jina langu litakua ni “Saidivin”. Tumesahau kua jina la Said lina maana ya kua ni mtu mwema, sasa sijui kua likiengezewa na “vin” litaleta maana gani. Tumesahau kua Said ni jina la sahaba alobashiriwa pepo na mtu analikataa, na badala yake anaeka jina la kafiri. Na mfano wa majina kama hayo yapo mengi. Amesema Allah subhanah“Hawatoridhika mayahudi wala manasara mpaka uwafate mila zao” (Baqarah 120), na ndo izo tunazifuata na kuziiga.

Tumekatazwa kufanya urafiki na makafiri na kuwakumbatia ikawa ndio vipenzi vyetu. Amesema Allah(subhanahu wataala) “Enyi mloamini msiwafanye mayahudi na manasara, kua ni vipenzi vyenu.” (Maidah :51). Je tumeizingatia aya hii au ndio tunalia kwa kifo cha kafiri, na kusahau kua yeye alimkana Mola ambae wewe unadai kua ni Mola wako? Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi iliyopokelewa na Ibnu-Hibbaan na kusimuliwa na Ibnu-Umar,“Atakaejifananiza na kaumu basi nae ni miongoni mwao” Tunawapenda watu ambao Allah amewalaani.

Wangapi kati ya wachezaji huvaa herini? Jee hayo si katika mapambo ya wanawake? Tumesahau kua wanaojifananisha na wanawake Allah amewalaani? Wangapi katika wachezaji hukata mikato ya ki fir-aun? Bado tu tunaendelea kuwapenda,? na hao ambao watasemwa kua ni waislamu, basi matendo yao hayatofautiani na makafiri kwani hutia herini kama wanavyotia wachezaji wenzake,hufanya mengineo kama wanavyofanya wenzake. Basi ni lipi la kuwatofautisha?

Tunasahau kua wanawafanya waungu watatu kua ndo wanaondesha ulimwengu huu kama familia,kuna baba, mwana na roho mtakatifu.Imekuja sura nzima kuwazungumzia mayahudi na manasara kua wamekufuru, na sisi waislamu hatutakiwi kua na mapenzi nao, badala yake tuwe na juhudi ya kuwalingania, na sio kufurahia matendo yao na kuyaiga. Amesema Allah (subhanahu wataala) katika Suratul-Maidah aya ya 73“Hakika wamekufuru wale wailosema Allah ndie Masih Issa bin Maryam, na akasema katika aya inayofata “. Hakika wamekufuru wale walosema kua Allah ni mmoja kati ya waungu watatu. Hakuna Mola wa haki zaidi ya Allah” Basi ni nani hao zaidi ya hao hao makafiri tunaowashabikia, na kufikia kujiua pindi timu zao zinapofungwa?

Kwa kua ndio ilikua desturi yetu kabla ya ramadhan kuwacha yalo muhimu, na kupoteza dakika 90 chini ya kioo, basi shetani ameendelea kututeka akili zetu mpaka ndani ya Ramadhan, tunaendeleza yale yale badala ya kurudi kwa Mola wetu, na kumlilia atusamehe madhambi yetu.

Swala zimekosa Khushui kwani kila unaposali mtu hukumbuka mechi ya jana, na ya leo sijui itakuaje. Kazi ya ukocha hufanywa ndani ya swala, na kupangwa namba za wachezaji ndani yake, na kama si takbira za imamu basi maamuma hatojua ameswali rakaa ngapi. Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadith inayosimuliwa na Ibni Abbaas radhia Allahu anhuma “ Faidika na mambo matano kabla ya matano: Uhai wako kabla ya kifo, Uzima wako kabla ya maradhi yako, Ujana wako kabla ya uzee wako, Faragha yako kabla ya mashughuliko yako,na utajiri wako kabla ya ufakiri wako.” [Al-Haakim].

Je sisi kwa muda wa dakika 90, tunafaidika na kipi kabla ya kipi? Amesema Allah subhanah“Waachie wale, na wastarehe na yawadanganye matarajio,karibuni ivi watajua” ( Suratul Hijri :3). Tusisahau kua Qur-an imeteremshwa ndani ya mwezi huu, na Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alimshtakia Mola wake kua umma wake umeihama Qur-an. Wakati wa mchana kila mtu yuko mbioni kutafuta dunia yake, na usiku hufungwa kazi zote na watu hujiandaaa vizuri si kwa jengine, zaidi ya kuangalia kandandanda dakika 90. Je tungesoma Qur-an ingekua tushafika juzuu ya ngapi? Tukumbuke kua pamoja na kua milango ya pepo iko wazi,na ya moto kufungwa ndani ya Ramadhani, si kwamba atakaekufa na mwisho mbaya hatoingia motoni. Laa hasha wakalla. Badala yake atakaekufa akishuhudia upuuzi basi atafufuliwa hali yakua anashuhudia upuuzi, kutokana na hadithi ya Mtume wa Allah“Atafufuliwa mtu kutokana na kile alichofia.”(Muslim).
Na akasema katika hadithi nyengine “Watafufuliwa watu na wale wanaowapenda” (Ahmad).Basi na sisi nani tunaowapenda kina Abubakar na Umar ama wachezaji mipira na waimbaji.

"ALLAH TUJAALIE WALE WENYE KUAMBIWA MAZURI NA KUYAFANYIA KAZI NA KUKATAZWA MABAYA NA KUYAWACHA"Aaamin.

No comments:

Post a Comment