Wednesday 10 April 2013

Uvutaji Sigara


Uvutaji wa sigara umeenea na kushamiri dunia nzima licha ya kuwa madhara yake yapo wazi.  Baadhi ya Waislamu wametumbukia katika balaa hili na kuziathiri nyumba zao bila ya kujijua. Kuna sababu tosha zenye kuonyesha uharamu wa jambo hili kwa Muislamu.  Sigara ina athari sana katika dini, afya, mazingira, familia, rasilimali na mengineyo.
 
i.              MADHARA KATIKA DINI
 
Sigara inaathiri  ibada ya mja na inapunguza malipo ya ibada hiyo.  Kwa mfano ibada ya sala ambayo ni nguzo muhimu ya Muislamu;   Kutokana na hadithi iliyosimuliwa na wengi; Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi wa Ssalam
 
 “Mwenye kula Kitungu maji au thawm, basi asiukaribie Msikiti wetu na akae nyumbani”
[Bukhari na Muslim]
 
Tunaona makatazo yamekuja kutokana na harufu mbaya inayotokana na vitu hivyo amabayo huwakirihisha watu pamoja na Malaika katika nyumba za Allaah (Misikitini).
 
Bila ya shaka mdomo wa mvutaji sigara una harufu mbaya zaidi  kuliko vitunguu, ima huwakera watu na Malaika kwa harufu hiyo au kukosa fadhila za sala ya jamaa msikitini kwa mwanamme.
 
i.              MADHARA KATIKA MWILI
 
Hakuna anaepinga madhara ya sigara katika mwili wa binadam.  Utafiti wa kiafya umeyaona haya na kuyaeleza kwa kina; hata imekuwa ni sheria kuweka wazi  maandishi ya tahadhari kwa kila paketi la sigara angalau watu wazinduke.
 
Ndani ya sigara hupatikana kemikali zenye sumu kama vile nicotine, arsenic, carbon monoxide na vyenginevyo ambavyo mvutaji huathirika kidogo kidogo hadi kuua sehemu muhimu za mwili wake.  Athari za zake ni kubwa na ni nyingi; husababisha cancer, TB, mshituko wa moyo, pumu, ubovu wa meno, na huwa ni  chimbuko la  maradhi mengi mengineyo.
 
Allaah Alietukuka anatuonya tusiwe wenyenye kujidhuru.  Suuratu Nnisaa’:29
 
وَلَا تَقۡتُلُوٓاْ أَنفُسَكُمۡ‌ۚ إِنَّ ٱللَّهَ كَانَ بِكُمۡ رَحِيمً۬ا

Wala msijiue, hakika Allah ni mwenye kukurehemuni

 Pia katika Suuratul Baqarah:195
 
وَلَا تُلۡقُواْ بِأَيۡدِيكُمۡ إِلَى ٱلتَّہۡلُكَةِ

Wala msjiitie kwa mikono yenu katika maangamizo
 
Na Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema katika Hadithi:
 
" لا ضرر ولا ضرار "
 
Kusiwe na kudhuriana wala kulipa dhara.
 
 
ii.    ATHARI KWA AKILI NA MATAMANIO
 
Sigara huathiri akili ya mwanadamu kwa kiasi kikubwa.  Mvutaji mzoefu  anapoikosa  huwa vigumu kwake kufikiri kitu, kutatua tatizo au kuwa makini katika jambo mpaka aipate.  Badala kuwa mtumwa wa Mola wake, hugeuka na kuwa mateka wa sigara yake na kuifanya dhaifu akili na hisia zake.
 
Allah Subhaanahu wa Ta’ala anatueleza katika Suuratu An-Nisaa’:27
 
وَٱللَّهُ يُرِيدُ أَن يَتُوبَ عَلَيۡڪُمۡ وَيُرِيدُ ٱلَّذِينَ يَتَّبِعُونَ ٱلشَّہَوَٲتِ أَن تَمِيلُواْ مَيۡلاً عَظِيمً۬ا

Allah anataka kukukhafifishieni.  Lakini wanaofuata matamanio yao wanataka mkengeuke mkengeuko mkubwa
 
iii.           MADHARA KATIKA MALI
 
Mvutaji sigara hupoteza pesa nyingi karibu kila siku kununulia sigara isiyomletea tija yeyote bali ni kuwafaidisha hao wanaoendesha bishara hii haramu.  Kumbuka kuwa mali tunayoipata tutakuja kuulizwa kwa njia gani tumeichuma na vipi tumeitumia.
 
Katika Suurat An-nisaa’:5  Allah Subhaanahu Wata’ala anatueleza:
 
وَلَا تُؤۡتُواْ ٱلسُّفَهَآءَ أَمۡوَٲلَكُمُ ٱلَّتِى جَعَلَ ٱللَّهُ لَكُمۡ قِيَـٰمً۬اوَٱرۡزُقُوهُمۡ فِيہَا

Wala msiwape wapumbavu mali zenu ambazo Allah amezijaalia kwa maisha yenu
Pia katika Suuratul Israa:26 – 27
 
وَلَا تُبَذِّرۡ تَبۡذِيرًا  إِنَّ ٱلۡمُبَذِّرِينَ كَانُوٓاْ إِخۡوَٲنَ ٱلشَّيَـٰطِينِ‌ۖ

Wala usitawanye (mali yako) kwa ubadhirifu.  Hakika watumiao kwa ubadhirifu ni ndugu wa mashetani
 
Na kutoka kwa Mtume Swalla Allahu ‘Alayhi Wasallam anasema:
 
" إن الله ينهاكم عن قيل وقال ، وكثرة السؤال  وإضاعة المال

Hakika Allah anakukatazeni na mazungumzo yasiyokuwa na faida (huyu kasema au kimesemwa) na kukithirisha kuuliza masuali na kupoteza mali
.
Licha ya nchi za Magharibi kutoa indhaari tu katika paketi kuonesha madhara ya sigara, Maulamaa wa kiislamu takriban wote wamekubaliana kwamba sigara ni haraam. Angalia Fatwa ifuatayo kutoka katika Fataawa Islaamiyah 442/3
 
Kuvuta sigara ni haraam kwa sababu ya kuleta madhara mengi  wakati Allah Subhaanahu Wata’ala amehalalisha kwa waja wake vyote vilivyo vizuri katika vyakula na vinywa na akaharamisha vibaya vyao. Na aina zote za uvutaji ni miongoni mwa vitu vibaya  kwa sababu ya kuleta madhara na kulewesha.
 
Ni vyema kutanabahi ndugu Muislamu na kuachana na mazoea sugu na potofu ya kuvuta sigara. Mvutaji sigara huwa hajali kuvuta mbele ya wale waliomzunguka ndani ya nyumba yake, kama mkewe/mumewe, watoto na wengineo. Huwasababishia kuvuta moshi wa sumu na wale walio karibu nae. Huleta hali mbaya hasa kwa mazingira ya ndani ya nyumba na ni mfano mbaya kwa kile kinachochungwa (mke na watoto) ndani ya nyumba hiyo.
 
Ndugu yangu Muislamu , kama ni miongoni mwa wenye kuendeleza uovu huu basi rudi kwa Mola wako kwa moyo ulio mwepesi wenye kusikiliza nasaha na kukubali yale yote yanayotoka kwa Mola kwa ajili ya kuinusuru nafsi yako kwanza, kisha dini yako, kisha akili yako, kisha familia yako, kisha mali yako na kadhalika.

No comments:

Post a Comment