Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group
Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wata‘ala) Mola wa viumbe vyote vyenye kuonekanwa na visivyoonekanwa. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba zake.
Ndugu wa Kiislamu, kama ilivyo katika ibada ya swala kuwa kuna baadhi ya matendo ya sunnah hufanywa ndani yake ili kuengeza fadhila na daraja ya swala hiyo, kadhalika katika ibada ya swaum (funga) kuna matendo ya sunnah amabayo mfungaji akiyafanya hupata fadhila zaidi katika funga yake na kupata ujira maradufu.
Katika makala hii in sha Allah, tutazungumzia baadhi ya mambo yaliyo sunnah kwa mwenye kufunga kuyafanya. Miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo.
Kula daku
Daku ni chakula kinacholiwa mwishoni mwa usiku kwa ajili ya kutekeleza sunnah ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) na pia kumfanya mfungaji awe mchangamfu na mwenye nguvu hali itakayompelekea kutokushindwa kufanya harakati zake za maisha kama ilivyo kawaida yake katika siku za kula mchana. Imethibiti hadithi kutoka kwa Anas bin Malik (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Kuleni daku kwani katika daku kuna baraka.” Bukhary na Muslim.
Kuchelewesha kula daku
Pia imesuniwa kuchelewesha kula daku hadi karibu na swala ya asubuhi kama ilivyopokewa hadithi na Anas kutoka kwa Zayd bin Harith (radhi za Allah ziwe juu yake) ambae amesema: “Tulikula daku na Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) kisha tukainuka tukaswali.” Nikasema: “Kulikuwa na muda gani baina ya adhana na daku?” Akasema: “Ni muda wa kusoma aya hamsini (50).” Bukhary
Kuharakisha kufutari (kufunguwa)
Vile vile ni sunnah kuharakisha kufunguwa mara tu baada ya jua kuzama kama alivyokuwa Akifanya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam), tofauti kabisa na wafanyavyo baadhi ya ndugu zetu ambao husubiri mpaka wamalize kuwali magharibi pamoja na sunnah yake ya baadiyah. Kufanya hivi sio sahihi kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume wetu. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Watu wataendelea kuwa katika hali nzuri maadam wanaharakisha kufunguwa (funga zao).” Bukhary na Muslim.
Kufunguwa kwa kula tende
Ni sunnah kwa mwenye kufunga kufutari kwa kula tende mbichi, ikiwa atakosa basi kwa tende kavu na ikiwa atakosa basi na afungue kwa kunywa mafunda ya maji. Kama ilivyopokewa kutoka kwa Anas (radhi za Allah ziwe juu yake) ambae amesema: “Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) alikuwa akifunguwa kwa tende mbichi kabla ya kuswali, ikiwa hamna tende mbichi basi kwa kavu na ikiwa hamna basi hunywa mafunda machache ya maji.” Abu Daud na Tirmidhy.
Kuomba dua kwa wingi
Vile vile inahimizwa kuomba dua kwa wingi wakati mtu akiwa amefunga na kabla ya kufutari kwani mtu aliyefunga ni katika watu ambao hukubaliwa dua zao, kama ilivyokuja hadithi ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) isemayo: “Dua za watu watatu hazirejeshwi (hazikataliwi), dua ya baba (kwa mwanawe), dua ya mtu aliyefunga, na dua ya msafiri.” Imepokewa na Al-Bayhaky kutoka kwa Anas (radhi za Allah ziwe juu yake).
Kujitenga na mabishano na majibizano
Mtu aliyefunga hatakiwi kuanzisha mabishano na malumbano, na kama mtu atakuja kwa ajili ya kugombana naye au kutaka kupigana naye basi ni wajibu wake kujizuia na kusema kuwa “mimi nimefunga” ili kuepukana na kuiharibu funga yake na kupunguza fadhila za funga yake.
Amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Funga ni Pepo hivyo kusiwe na mazungumzo machafu na tabia chafu. Ikiwa mtu atampiga au kumtukana (aliyefunga) na aseme, “Mimi nimefunga” mara mbili. Naapa kwa yule ambaye roho yangu iko Mikononi Mwake, harufu itokayo kinywani mwa mtu aliyefunga ni bora mbele ya Allah kuliko harufu ya miski. (Allah anasema:) “Ameacha chakula chake, kinywaji na matamanio yake kwa ajili Yangu. Funga ni kwa ajili Yangu Nami nitailipa, na matendo mema hupata malipo mara kumi yake.” Bukhary na Muslim.
Ndugu wa Kiislamu, ni muhimu pia juu yetu kuzidisha kufanya ‘amali nyingi tukiwa tumefunga kama vile kutoa sadaka, kuwasaidia wahitaji na kutumia muda wetu mwingi kuisoma Quran na kuhudhuria madarsa ili kujifunza maana yake, kwani bila ya kujifunza maana yake hatutoweza kuishi kwa mujibu wa Quran na kupelekea kuishi maisha ambayo Allah haridhiki nayo na hatimae kuingia katika adhabu za Allah.
Ni muhimu pia kuendeleza yale yote ya kheri tunayoyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan katika miezi myengine khassa kuhudhuria madarsa na kujifunza dini yetu. Kwani bila ya elimu hakuna litakalofanywa kwa usahihi wake.
Tunamuomba Allah atuwezeshe kuyafanya haya na mengine ya kheri hadi mwisho wa maisha yetu na Atuweze kupata Rehma zake na Kutuingiza katika Pepo yake. Amin.
No comments:
Post a Comment