Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Nini Israafu?
Israafu ina maana nyingi miongoni mwa hizo ni:
1. Israafu ni kule kutumia kitu zaidi ya kile unachohitaji, kwa maana ya kwamba israfu inaendana na matumizi ya mtu anayohitaji ambayo anaweza kuweka kiwango cha kufanya yanapozidi basi ni israafu.
2. Israafu pia ina maana ya kutumia jambo au kitu chochote usichokihitaji, kwa maana kumiliki au kuwa na kitu chochote ambacho si cha lazima na si muhimu kwako.
3. Vilevile Israafu haina maana kuwan ni matumizi mabaya ya fedha lakini inajumuisha matumizi mabaya ya rasilimali yoyote ile, ikiwa matumizi ya maji wakati mtu anapotumia, au kuwacha chakula katika sahani baada ya kujaza kisichokuwa saizi yake, au hata kula zaidi ya kiwango chake au baada ya kushiba.
Baadhi ya dalili katika Qur-an na Sunna zinazozungumzia na kukemea Israafu
“Naye ndiye Aliyeziumba bustani zilizoegemezwa na zisizoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbalimbali, na mizaituni na mikomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake ipambapo, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake, wala msitumie kwa fujo (israafu), hakikaYeye hawapendi watumiao kwa fujo.” (Qur-an: 6:141)
“Na umpe ndugu haki yake, na maskini na msafiri, wala usitumie (mali yako) kwa ubadhiri. Hakika watumiao kwa ubadhiri ni ndugu za mashetani; na Shetani ndiye asiyemshukuru Mola wake” (17:26-27)
“Bila shaka ninyi mnaniita kwa yule ambaye hana wito duniani wala Akhera, na marudio yetu ni kwa Mwenyezi Mungu, na wapitao kiasi hao ndio watu wa Motoni.” (Qur-an:40:43)
Kwa mujibu wa Tafsiri ya Majmaul Bayaan, Bakhti Shoa alikuwa na daktari maalum wa Haroun Rashyd, na alikuwa mkristo. Siku moja alimuuliza Waqidi “Je katika kitabu chenu (Qur-an) kuna elimu ya tiba?” Waqidi akamjibu, Allah mtukufu amekusanya tiba yote katika aya moja tu “….Kuleni na kunyweni wala msifanye israfu”
Yule tabibu akauliza je Mtume wenu ametaja chochote katika elimu hii ya tiba?
Waqidi akamjibu ndiyo, Mtume ameelezea na kuchambua elimu ya tiba katika sentensi fupi. Mtume (swallalahu alayhi wassalam) anasema: “ Tumbo ni nyumba ya maradhi na kutovimbiwa na chakula ni dawa kubwa, kila mtu anatakiwa ale kwa kiasi kinachomtosha na asivimbiwe” Pale aliposikia maneno yale tabibu akakiri na kusema “kitabu chenu na Mtume wenu hakijaacha kitu katika elimu ya tiba na wataalamu wa kigiriki, sina chochote cha kusema.
Kutoka kwa Ibnu Jurayj radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Imepokelewa hadithi kuwa Thabit Ibnu Qays bin Shamaas, anbae alivuna tende katika shamba lake, akasema ndani ya nafsi yake “Siku ya leo Mtu yeyote atakaekuja kwangu basi nitamlisha tende hii, akalisha watu kutwa nzima mpaka ikafika jioni, kuangalia akawa hana alichobakisha katika tende zile.
Ndipo Allah akateremsha aya hii: “Enyi wanadamu, shikeni mapambo yenu wakati wa kila Sala; na kuleni na kunyweni wala msipite kiasi; hakika Yeye Hawapendi wapitao kiasi” (Qur-an: 7:31).
Baada ya kuona makemeo ya Israafu na uharamu wake, Je ni kipi kifanyike kujiepusha na Israafu:
1. Kwanza ni kumuomba Allah akulinde na akuepushe na Israafu, maana binaadamu hatuna ujanja wa kuzizuia nafsi zetu tusifanye israafu.
2. Usiwe mwenye kutamani vitu visivyo vya lazima, kwa kuwa kufanya hivyo kutakupelekea kufanya matumizi yasiyo ya lazima.
3. Jitahidi kutafuta bidhaa au matumizi yako kwa thamani ya chini zaidi, ili uweze kujipunguzia matumizi zaidi ya kile unachohitaji.
4. Kupunguza ufakhari na kutaka mambo makubwa. Hili khasa kwa upande wa mama na dada zetu,
Mtu anasema naenda na fashion au uptodate, kwa maana nguo au kiatu au kitu chochote kikitoka sokoni basi yeye huwa na pupa ya kutafuta kila njia apate kitu hicho.
Wanajaza makabati kwa nguo walizozivaa kwa siku moja au mbili, kila harusi mtu avae nguo mpya, hii ni israafu.
5. Kwa wale wenye familia usijaze friza lako kwa vyakula vingi, kuliko uwezo na matumizi yako. Watu huwacha mpaka vitu vinaharibika na wakati jirani yako analala na njaa. Weka matumizi yako kwa kujua kile unachohitaji, sawasawa na unapoweka chakula chako basi unatakiwa uweke kulingana na uwezo wako kuepusha kukimwaga huko ndiko kufanya israafu.
6. Kwa vijana wa leo, hatusemi haramu ila tupunguze na kuvaa kila kitu kwa nembo/kampuni/brand.
Kwa mfano shati, suruali, nguo za ndani mpaka viatu mtu anavaa vya nembo maalum. Huku ni kufanya matumizi yasiyo ya lazima.
7. Mwisho ni kuweka nia kwa ikhlaas, kumuomba Allah atusamehe na atulinde kufanya israafu, pamoja na kutuweka mbali na israafu.
EWE ALLAH MUUMBA TULINDE NA UWALINDE WAISLAMU NA DHAMBI HII YA ISRAFU EWE MWINGI WA KUREHEMU.
No comments:
Post a Comment