Makala kutoka Raudhwah Islamic Group
Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Makala yetu itazungumzia Historia ya Funga,aina za funga na tofauti ya nia za funga za faradhi na funga za sunna.
Kwanza kabisa tukiangalia neno Funga lina maana kilugha ni kujizuilia na chochote. Kujizuilia huku inawezana ikawa kujizuilia na kupigana, kutozungumza au kutofanya kitu chengine chochote. Ama kisheria ni kujizuilia na vyenye kufunguza kuanzia kuchomoza kwa alfajiri ya kweli hadi kuzama kwa jua kwa nia maalum.
Funga imefaradhishwa katika mwaka wa pili wa hijra yaani tokea kuhama kwa Mtume Swalla Allahu Alayhi wa Sallam Makka kuelekea madina, wakati walipokuwepo huko Madina ndipo ilipofaradhiswa funga,na wakati huo ilikuwa katika mwezi wa shaaban. Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa tisa katika miezi ya hijriyyah na ndio mwezi uliobora kulilko miezi mengine yote kwa sababu mwezi huu umekusanya kila aina ya kheri na neema za Allah Subhaanahu Wataala na ndio maana Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi Wa Sallam akasema katika kusisitiza ibada katika mwezi huu : “ameangamia yule ambae ataudiriki mwezi wa Ramadhani wote na asisamehewe madhambi yake.” Maneno hayo ya Mtume Swala Allahu Alayhi Wa Sallam yanaonesha wazi kuwa mwezi huu ni mwezi mtukufu kuliko miezi mengine.
Umeitwa mwezi wa Ramadhani kwa sababu kuna kauli inasema, “zama walipokuwa wanawake waarabu katika siku za joto kali, wakauita mwezi huu jina hilo la Ramadhani kwa kauli yao mina RAMDHWAI yaani ni joto kali. Vile vile kuna kauli nyengine inasema umeitwa Ramadhani kwa sababu unaunguza madhambi, (maneno haya utayapata katika kitabu cha Takriratu-ssadidah fii masailil-Mufiidah, Ukurasa wa 433).
Asili ya Funga tunaipata pale Allah Subhaanahu Wataala Aliposema katika kitabu chake kitukufu : “Enyi mlioamini, Mmefaradhishiwa kufunga kama walivofaradhishiwa waliopita kabla yenu, Ili mupate kumcha Mungu.” (Baqara : 183). Maneno haya matukufu yanatuonesha wazi kuwa Funga ni Ibada ambayo ilikuwepo katika nyumati nyingi zilizopita kabla yetu, kwa maana ummati huu wa Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayhi wa Sallam hatujaletewa jambo geni katika dini yetu ya uislamu isipokuwa mitume iliyopita pamoja na watu wao walifaradhishiwa pia kufunga na wakatekeleza. Kwa mfano historia inatwambia pale ambapo Nabii Mussa na watu wake walipookolewa na Allah kutokana na Firauni alolaaniwa, alitoka Nabii Mussa Alayhi Salaam kwenda kwenye jabali kuzungumza na mola wake na huko Nabii Mussa Alayhi Salaam alifunga siku Arubaini (40). Kwa hiyo asili ya Funga inatoka katika nyumati zilizopita kabla ya Ummati wetu huu.
Funga imegawika katika Makundi mawili makuu, nayo ni :-
1)WAJIBU : Yaani ni lazima kuzifunga, na hapa zipo aina sita, nazo ni :-
a)Funga ya Ramadhani.
b)Funga ya kulipa.
c)Funga ya Nadhiri.
d)Funga ya Hajji na Umra badala ya kuchinja.
e)Funga ya kuomba mvua anapoamrisha kadhi.
f)Funga ya kafara.
2)SUNNAH : Yaani ni hiyari kuitekeleza, Na hii imegawika sehemu tatu, nazo ni :-
a)Zinazokuja kwa kila mwaka.
b)Zinazokuja kwa kila mwezi.
c)Zinazokuja kwa kila wiki.
3)MAKRUH : Yaani kuchukiza, na hii ipo sehemu moja nayo ni kufunga siku ya ijumaa peke yake.
4)HARAMU : yaani ni makosa kuitekeleza, Na hii imegawika sehemu mbili, nazo ni :-
a)Haramu pamoja na kusihi Funga hiyo.
b)Haramu pamoja na kutokusihi funga hiyo.
Sehemu ya pili katika haramu inagawika sehemu tano, nazo ni :-
1)Kufunga siku ya Eid-el-Fitri.
2)Kufunga siku ya Eid-el-Hajj au Eid-el-Adhha.
3)Kufunga siku ya kushiriki yaani (Ayyamu Tashrik).
4)Kufunga nusu ya pili katika mwezi wa Shaabaan.
5)Kufunga siku ya shakka yaani (yaumu shakka).
Tumalizie makala yetu hii kwa kuangalia tafauti za nia za Faradhi na nia za Sunnah, kwa sababu amali yoyote ni lazima kuwe na nia ndani yake, kama alivosema Mtume Swalla Allahu Alayhi wa Sallam : “Hakika kila amali ina nia yake, na hakika kila mtu na anavyonuia,………” (BUKHARY NA MUSLIM). Kwa hiyo na funga nayo ina nia zake kama amali nyengine zote.
TOFAUTI ZA NIA ZA FUNGA ZA FARADHI NA FUNGA ZA SUNNAH
1- NIA YA FUNGA YA FARADHI :Unaingia wakati wake tokea kuzama kwa jua mpaka kchomoza kwa alfajiri, inalazimika uitie usiku. NIA YA FUNGA YA SUNNA Unaingia wakati wake tokea kuzama kwa jua mpaka kupindukia kwa jua (yaani kuingia kwa wakati wa Adhuhuri), na sio lazima uitie usiku.
2. NIA YA FUNGA YA FARADHI : Ni lazima uibainishe kama ni ya Ramadhani au ya Nadhiri n.k. NIA YA FUNGA YA SUNNA Sio lazima kuibainisha isipokuwa Funga yenye wakati maalumu kama Arafa kwa makubaliano ya wanavyuoni.
3. NIA YA FUNGA YA FARADHI Haifai kuzikusanya Faradhi mbili kwa pamoja katika siku moja au kwa nia moja. NIA YA FUNGA YA SUNNA Inafaa kukusanya Sunna mbili na zaidi katika siku moja au kwa nia moja.
Haya yote utayapata katika kitabu cha (TAKRIRATU SSADIDAH FII MASAILIL MUFIIDAH) Ukurasa wa 440.
Bila shaka mambo ya kuyazungumza katika mwezi huu wa Ramadhani ni mengi sana na wala hatutayamaliza, ila kwa haya machache na mengine utakayoyapata katika makala nyengine tumuombe Allah Subhaanahu wa Taala atuwafikishe kuyatekeleza ili tufikie ujira wa wamchao Allah.
Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group
No comments:
Post a Comment