Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Makala yetu itazungumzia suala zima la kuunga udugu katika uislam. Tambua ewe ndugu yangu muislam ya kuwa udugu upo wa namna mbili. Nao ni :
1-Udugu wa Kiimani
2-Udugu wa damu.
Udugu wa kiimani ni ule ambao unatukutanisha pale tunapokiri ya kuwa hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah.Allah subhanahu wataala amesema “..Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.”( 49:10)
Ama udugu wa pili ni udugu wa damu ambao ndio niliopenda kuuzungumzia leo kwa Tawfiq ya Allah Subhanahu Wataala.
Uislam ni dini ambayo imetuwekea mfumo wa kiibada kuanzia kuzaliwa kwetu mpaka kufa kwetu na hili ni kwa kutambua kuwa lengo letu kuu hapa duniani ni kumuabudu Allah na si vinginevyo.Kwa kutambua hilo, Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam ametufundisha ibada kimatendo na kimaneno katika kila kipengele cha maisha yetu ili tupate kuutumia vizuri uhai wetu na tusiwe katika watakao juta siku utakapo katika uhai huu. Na katika ibada hizo miongoni mwao ni hii ya kuunga udugu.
Kuunga udugu ni ibada iliyojengeka kimaneno na kivitendo. Ni miongoni mwa ibada ambayo imetiliwa mkazo kwa malipo mengi kwa mwenye kuifanya na vilevile kuahidiwa kwa adhabu kali kwa mwenye kuiacha. Kwa masikitiko makubwa wengi wetu tumekua tukiipuuza ima kwa kujua au kutojua. Allah Subhanahu Wataala anasema “ Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri” (4:36).
Aya hii imeanza kwa kutaja Tawhiid kisha kufuatanishwa na suala la kuunga udugu nako ni kuwafanyia wema wazazi na ndugu wa karibu. Hii ni kuonyesha nafasi kubwa ya ibada hii na ikaonyesha pia kuwa mwenye kulipinga jambo hili Allah anamchukia kwani hua ana kibri na ni mwenye kujifakharisha.
Umuhimu wa Kuunga Udugu
Kwanza ni alama ya kuwa na Imaan. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam : ((..Na mwenye kumuamini Allah na Siku ya mwisho basi na aunge udugu wake..)) Bukhari na Muslim.
Pili kuunga Udugu ni miongoni mwa matendo anayoyapenda Allah Subhanahu Wataala. Aliulizwa Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam, Ni amali gani bora mbele ya Allah? Akajibu ((Swala kwa Wakati wake)) akaulizwa tena kisha ipi? Akajib ((Kuwafanyia wema wazazi)) kisha ipi?? Akasema ni Jihaad katika njia ya Allah)) Bukhariy na Muslim.
Tatu ni sababu ya kuongezewa Rizki na Umri. Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam: ((Mwenye kupenda kukunjuliwa katika rizki yake na kuongzewa Umri wake, basi na aunganishe udugu wake)) Bukhary na Muslim.
Nne ni sababu ya kuingizwa peponi.Kuna Mtu alimfata Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam akamwambia, Ewe Mtume wa Allah nijulishe jambo ambalo litaniingiza peponi,akasema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam : (( Muabudu Allah Usimshirikishe na chochote, Simamisha Swala, Toa zaka na Unga Udugu)) Bukhari na Muslim.
Je Vipi tutauunga udugu ?
Zipo njia nyingi za kuunga udugu ila nitazungumzia kwa ujumla tu kama kwa kuwatembelea wakiwa wazima au wagonjwa, kuwasaidia wanapopatwa na shida, kuwaheshimu, kuwafurahisha kwa kila njia kwa maneno na vitendo kama kuwapa maneno mazuri na pia kuwapa zawadi na mengine mengi yanayopendwa na familia yako pendelea kuwafanyia kwa kadri ya uwezo wako.
UBAYA WA KUVUNJA UDUGU
1..Hulaaniwa na Allah. Amesema Allah Subhanahu Wataala “ Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na muwatupe jamaa zenu? Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatia uziwi, na akawapofoa macho yao.” ( 47 :22-23).
2..Haingii peponi mwenye kukata ukoo. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam. ((Haingii peponi mwenye kukata udugu) Bukhary na Muslim.
Tunapoongelea kuunga udugu wazazi tusiwasahau kuwa wao ndio wenye nafasi ya kwanza..kama anavyosema Mtume Swalla ALlahu Alayhi Wasallam: ((Ameangamia mtu, Ameangamia mtu,
Ameangamia mtu...Mwenye kuwakuta wazazi wake wapo hai, mmoja wao au wote wawili na hakuingia peponi.)). Hadithi hii inaonyesha ni namna gani uislam unavyohizima kuwafanyia wema wazazi wetu kiasi ya kwamba Mtume Swalla Allahu alayhi wasallam amesisitiza maangamizo yake mara tatu. Na pia katika sUala la kuunga udugu tunatakiwa tuunge udugu hata bila ya kuangalia kama wazazi au ndugu zetu ni waislam au laa... ni wema au waovu..kama anavyotusimulia Bibi Asmaa bint Abubakar radhi za Allah ziwe juu yao. Anasema "Alinijia mama yangu hali ya kuwa ni mshirikina katika enzi za Mtume, Nikamtaka ushauri Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam; Amenijia Mama yangu nae ni mwenye shida, Je nimuunganishe ? Akasema (( Muunge Mama yako)) Bukhari na Muslim. Na maana ya kumuunga yani nimtendee wema..
Baada ya kuona faida za kuunga udugu na ubaya wa kuacha kufanya hivyo. Nitapenda kumalizia mada hii kwa kuwakumbusha na kuwatanabahisha mambo ambayo huvunja udugu ili tupate kuepukana nayo. Miongoni mwa hayo ni :
a- Kutojua fadhila za kuunga udugu na adhabu za kuvunja udugu.
b-Kibri
c-Choyo na Ubakhili
d-Husda
e-Talaka
f-Kuoa au kuolewa na mume au mke muovu ambae atakuzuia kuwa karibu na ndugu zako.
g- Mali.
h-Kazi.
i-Masafa baina yako na familia yako.
Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayosababisha watu kuvunja udugu Allah atujaalie tuwe ni wenye kuunga udugu wetu ili tupate malipo hapa duniani na kesho akhera. Na wale ambao wamehasimiana basi waondoshe tofauti zao na tujue kuwa kuunga ukoo ni amri kutoka kwa Allah. Takriban kila familia siku hizi za kiislamu watu huhasimiana na wanasahau kuwa kuunga udugu ni katika amri zake Allah subhanahu wataala.
Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale wanaoambiwa mema na kuyafanyia kazi na kukatazwa maovu na kuywacha. Aaamin.
*Msitusahau kwenye dua zenu**
NA ALLAH NDIE MJUZI ZAIDI.
USISAHAU KUSAMBAZA UJUMBE HUU
No comments:
Post a Comment