Wednesday, 18 June 2014

WANAOWAJIBIKA KUFUNGA, WALIORUHUSIWA WASIFUNGE NA WENYE KURUHUSIWA KULA NA KUFIDIYA


Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba.

MAKALA HIZI ZIMEKUSANYA HUKUMU ZILIZOKUWA LAZIMA KUZIJUA KWA KILA MFUNGAJI WA MWEZI WA RAMADHANI, ILI MFUNGAJI AWE NA UJUZI KAMILI KATIKA KUTEKELEZA IBADA HII TUKUFU YA SWAUMU YA MWEZI WA RAMADHANI. KWA HIVYO NDUGU MUISLAMU, TUJIITAHIDI SANA KUZISOMA MAKALA HIZI KWA MAKINI SANA NA UYAELEWE YALIYOMO. NAOMBA MWENYEZI MUNGU ATUFANYIE WEPESI KATIKA KUZIJUA HUKUMU ZA KUFUNGA NA FADHILA ZA RAMADHAN.

Baada ya utangulizi huo,

Ndugu Waislam, Ni katika baraka zake Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kwa Muislamu Kumuwezesha kufunga mwezi wa Ramadhani na kuutumia wakati wake wa usiku kwa Swalah. Ni mwezi ambao ndani yake amali njema huzidishwa malipo na watu hupandishwa daraja (vyeo). Ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) huwaachia huru baadhi ya watu kutokana na Moto. Kwa hivyo Muislamu ni lazima ajitahidi sana kufanya mambo mema katika mwezi huu; ni lazima afanye hima katika kuutumia wakati wa uhai wake kwenye ibada. Kuna watu wangapi ambao wamenyimika katika mwezi huu kutokana na maradhi, mauti au kukosa maelekezo mema.
Ndugu waislamu, Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) ametufaradhishia kufunga swaum ya Ramadhan kama iliyokuja katika qur-an tukufu "Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu”. (Al Baqara : 183).

Pia Allah (Subhaanahu wa Ta’ala) anaendelea kusema "..... Basi ataye kuwa mjini katika mwezi huu naafunge.....”(Al Baqara : 185).
Wakati tunapojiandaa na kuianza Ramadhani, tunapaswa kujua kwamba, amri ya kufunga ni yake Mwenyezi Mungu. Na wala amri hii haikuwa ya yeyote yule kati ya viumbe,hivyo basi ni vyema kujua masharti ambayo ukiyakamilisha itakua ni wajibu kwako kufunga
Na masharti yafuatayo ukiwa umeyakamilisha utalazimika kuanza Saumu, na wala hutokuwa na udhuru wowote ukuzuiao kufunga.

I. AL-ISLAM: Uislamu ni shuruti moja katika shuruti za kukubaliwa Saumu na ibada zote. Ijapokuwa juu ya kafiri pia ni wajibu kufunga na kufanya ibada zote, lakini kwa vile yeye si Mwislamu basi haitasihi na kukubaliwa ibada zake.

II. BALEGHE: Mtu huhesabika kuwa amebaleghe kwa kutimiza miaka kumi na mitano, au akiwa mwanamke aliyewahi kutokwa na damu ya mwezi. Pia ikiwa amewahi kuota kama anatangamana na mke (akiwa mume) au na mume (akiwa mke) na kutokwa na manii kwa ndoto hiyo, basi atalazimika kuanza kufunga.

III. AKILI: Funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani haiwajibiki kwa mtu asiyekuwa na akili mfano Kichaa,kama zilivyo ibada nyingine.

Pia katika vitabu vyengine wameeleza sharti nyengine ikiwemo kuepukana na hedhi, kuwa mkaazi (msafiri anaruhusiwa kutokufunga kama tutakavyoieleza hapo baadae) na pia kuweza kufunga. (Kuna watu wana maradhi sugu hawawezi kufunga au uzee hawa kwao haiwajibikii kufunga. Ila tutaeleza nini wakifanye watu hawa.

Kama tulivyosema awali,kila muislamu aliye baleghe na mwenywe akili timamu lazima afunge Ramadhani.Wanaosameheka ni watu wa namna hii
a) Wanawake wenye hedhi au nifas
b) Wagonjwa na wasafir

WANAWAKE WENYE HEDHI AU NIFAS

• Wanawake wanapokuwa katika siku zao za miezi au katika damu ya uzazi ni haramu kwao kufunga.

• Ramadhani ikianza na yeye yumo katika hedhi au nifasi hatofunga mpaka atakapomaliza na kuoga na kuwa tohara.

• Damu ikitoka katika swaumu hapo,mwanamke lazima avunje swaumu,hata kama bado muda mchache wa kuzama kwa jua.

• Damu ikimalizika usiku,anaweza kutia nia ya kufuga bila ya kupoteza wakati kwa kujitoharisha lakini iwe kabla ya kuchomoza alfajiri ya kweli.

• Mwanamke mwenye damu humbidi azifunge siku alizowacha .Bi Aisha radhi za Allah ziwe juu yake amesema” Katika kipindi cha Mtume tuliamrishwa kuzilipa siku tulizowacha kwa sababu ya kutokwa na damu wala hatukuamrishwa tuzilipe sala tano”

• Mwanamke mjamzito au mwenye kunyonyesha wameruhusiwa kutofunga kwa kuja kuzilipa. Anas bin Malik (radhi za Allah ziwe juu yake) anasimulia hadithi kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)

"إن الله وضع عن المسافر شطر الصلاة ووضع عن المسافر والحبلي والمرضع الصوم أو الصيام"
“Mwenyezi Mungu kampunguzia msafiri sala na kampunguzia msafiri na mwenye mimba pamoja na mwanamke mnyonyeshaji saumu” (muslim)

TANBIH
Mwanamke mjamzito au anayenyonyesha ambae atakuwa anaikhofia nafsi yake huyu atalipa tuu hatatoa fidia,lau ikiwa anakhofia nafsi yake pamoja na kiumbe kilichokuwa tumboni atalipa na kutoa fidia

MGONJWA NA MSAFIRI

• Kwa huruma zake mola,mgonjwa na msafiri wameamrishwa wasifunge ila waje kuzilipa funga zilizowapita “………..Na aliyekuwa mgonjwa au msafiri basi atomize hesabu siku nyengine…..”(Baqarah:184)

• Qur-an haikutaja ugonjwa maalumu wala kuelezea namna ya ugonjwa,ila baadhi ya wanzuoni wamesema ugonjwa utakaomkalifisha asiweze kufunga.

• Safari iliyoruhusiwa kufungua ni ilie safari ambayo inaruhusa ya kufupisha sala na kusali safari.

Mtu anaweza kufuturu au kuendelea kufunga anapokua katika safari kwa kauli ya Anas bin Malik (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema” Tulikuwa tunasfiri pamoja na Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ,Hakupata kuwalaumu hata mara moja wale waliokua wakifunga au wale ambao hawakufunga”

Vile vile bwana Hamza Al-Aslami alimwambia Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) “Yaa Rasulla allah mimi najiona ninazo nguvu za kufunga huku nimo safarini Je! Kuna ubaya wowote” Mtume alimjibu << Hii ni ruhusa kutoka kwa Mwenyezi Mungu atakayeitumia ni bora ,Ama yule apendaye kufunga hana ubaya wowote ule>> “ (Muslim)

• Na safari, sharti iwe ya halali, isiwe kazi yake kama kondakta, dreva nahodha n.k. asiwe atakaa huko zaidi ya siku 10 akiwa atakaa zaidi ya siku 10 atafunga hata huko huko safarini.

WENYE KURUHUSIWA KULA NA KUFIDIYA

Uislamu ni Dini ipendayo kusahilisha mambo kwa wale wasioweza kuyatenda,kwa hiyo watu wafuatao wamepewa ruhusaya kula na kutoa fidia kwa kulisha kila siku chakula {kibaba (sawa na kilo kasorobo) kwa kila siku. Kibaba hiki kiwe ni cha chakula kitumiwacho sana na watu wa sehemu hiyo }cha wastani cha mtu futari,hapa inategemea hali ya huyo mlishaji ikiwa yeye mwenye hana uwezo huwa amesamehewa..Watu wenyewe ni
a) Mzee mtu mzima sana hawezi kufunga ila kwa shida sana
b) Mgonjwa asiyekuwa na tamaa ya kupona maradhi yake
c) Mwanamke mwenye kunyonyesha au mja mzito mwenye kuogopea kile kizazi

HITIMISHO

NDUGU ZANGU KATIKA IMAN,FUNGA YA RAMADHANI NI FARADHI NA NI LAZIMA KWETU KUFUNGA,INASIKITISHA KUWAONA BAADHI YA WAISLAMU KUWA HAWAFUNGI,ABU HURAIRA (RADHI ZA ALLAH ZIWE JUU YAKE) AMEPOKEA KWA MTUME (SWALLA ALLAHU ALAYHI WASALLAM) “ MWENYE KUFUNGUA SIKU MOJA KATIKA RAMADHANI BILA YA UDHURU WENYE KUKUBALIWA KISHERIA,MTU HUYO HATAWEZA KUIFIDA KWA KITU HATA KAMA ATAFUNGA MILELE”(BUKHARIY)

PIA WAMEKUBALIANA WANAZUONI KUWA MTU ASIYEFUNGIA RAMADHANI NA AKAACHA KUIFUNGA BILA YA SABABU HUWA MBAYA ZAIDI KULIKO MZINZI NA MLEVI.

HIVYO SHIME WAISLAMU TUFUNGE MWEZI WA RAMADHANI KWA AJILI YA ALLAH ILI TUWEZE KUPATA UJIRA MKUBWA. ALLAHU A’ALAM.

No comments:

Post a Comment