Sunday, 29 June 2014

SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA - SEHEMU YA KWANZA


Makala imeandaliwa na Raudhwah islamic Group

Ili swaum isihi kuna sharti zake zitimizwe ndipo funga hiyo itasihi. Na sharti hizi zisipokamilika basi funga haitosihi au funga itabatilika na itamlazimu mwenye kufunga aje kuilipa funga hiyo. Hivyo hatutokuja kueleza yanayofunguza. Bali makala hii in shaa Allah itamtosheleza msomaji kujua sharti za kusihi kwa funga na kubatilika kwa funga. Pia katika baadhi ya vitabu wametumia neno NGUZO ZA FUNGA zote hizo ni sawa na wanakusudia kukieleza kitu hicho hicho.

1-KUTIA NIA KILA SIKU
Ni lazima kwa mwenye kufunga atie nia kwa kila siku anayofunga. Iwe funga hiyo ya sunna au faradhi kama Ramadhan. Na hatokuwa na funga yule atakaekuwa hajatia nia. Kwani katika hadithi kutoka kwa Sayyidina Omar (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “ Nimemsikia Mjumbe wa Allah akisema: “ Hakika kila jambo huambatana na nia na kila mtu atalipwa kutokana na kile alichokinuwia … .” Bukhari na Muslim.

Na inamuwajibikia mwenye kufunga Ramadhan atie nia kabla ya kuanza kwa alfajiri ya kweli. Na endapo mwenye kutaka kufunga hatotia nia kabla ya wakati huo basi hatokuwa na funga. Na itamuwajibikia kwake yeye kuja kuilipa funga hiyo. Kwa ushahidi wa Hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam): “Yeyote ambae hatoweka nia ya kufunga kabla ya alfajiri hatokuwa na funga.” Imepokewa na Imam Ahmad na An-Nasai. Hivyo inamlazimu atie nia kwa kuzingatia kabla ya kuanza kwa funga na nia hiyo iwe kwa kila siku atakayoifunga. Ama mwenye kufunga sunna anaweza kutia nia kabla ya kupambazukwa kwa jua kama ilivyoelezwa katika mada zilizopita.

Kwa nini mtu atie nia kila siku ndani ya Ramadhani? Swala humalizika kwa mtu kutoa salam. Na anapotaka kuingia katika swala nyengine basi analazimika kutia nia ya swala nyengine. Hivyo hivyo kwa mwenye kufunga, swaumu humalizika kwa kuzama kwa jua hivyo basi anaetaka kufunga siku ya pili lazima atie nia nyengine. Kwani anakuwa ameanza swaumu nyengine. Na hii ndio kauli yenye nguvu.

Je kutia nia ni kwa kutamka au moyoni tu inatosha?
Kwanza ni jambo lisilokuwa na shaka kuwa nia mahali pake ni moyoni. Ama suala la kutamka kwa kauli za maulamaa wengi ni jambo ambalo halikuthibiti katika dini. Hivyo basi mwenye kufunga atatia nia moyoni mwake kwani Allah anajua yale yote yaliyomo ndani ya nafsi zetu na hakifichiki kwake kitu chochote.
Ama ziko kauli katika madhehebu ya Imam Shafi kuwa kutamka nia ni sunna. Rejea katika kitabu cha MUQADDIMATUL HADHARAMIYYAH katika Mlango wa funga.

Ama mimi muandishi wa makala hii naunga mkono zaidi rai ya kuwa kutamka nia sio lazima. Muhimu mtu atie nia ndani ya moyo wake.

2- KUJIZUIA KULA NA KUNYWA

Ni lazima kwa mtu mwenye kufunga ajizuie kula na kunywa kuanzia kuingia kwa alfajiri ya kweli hadi kuzama kwa jua. Kwa kauli ya Allah (subhanahu wata‘ala): “Na kuleni na kunyweni mpaka kubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku, Kisha timizeni saumu mpaka usiku.”  (Suratul Baqara : 187).

Nini hukmu ya kula kwa kusahau

Yule ambae atakula kwa kusahau iwe kidogo au sana basi haitobatilika funga yake kwa ushahidi wa hadithi ya Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema : Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam): “Mwenye kusahau nae amefunga, basi akala au akanywa na aikamilishe funga yake.” Al Bukhariy na Muslim. Na katika riwaya nyengine “Kwani hakika Allah amemlisha na amemnywisha.” Ila Muislamu azingatie asije kujiigiza kuwa amesahau kwani ataweza kuwadanganya watu lakini Allah hawezi kumdanganya hata kidogo.

Je kupiga mswaki ndani ya Ramadhan kwa kutumia dawa inasihi?

Kupiga mswaki ndani ya funga hilo linasihi kwani Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akipigwa mswaki nae amefunga. Ama suala linakuja kwenye kupiga mswaki kutumia dawa.  Dawa ya mswaki haibatilishi swaum ikiwa wakati anasafisha meno atatema na wala hamezi. Ama ikiwa atakusudia kumeza, swaumu yake itabatilika.  Na yule ambae anakhofia anaweza kumeza basi bora asitumie dawa. Na kilichopendekezwa zaidi na maulamaa mtu apige mswaki kwa kutumia dawa kabla ya kuanza kwa saumu na itakapoingia saumu apige mswaki bila ya kutumia dawa ili asije kutumia dawa na kuimeza.

Je kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi?

Kuonja chakula wakati mtu amefunga inasihi kwa sharti ahakikishe kuwa hamezi kile alichokiweka kwenye ulimi kwa ajili ya kuonja.

Je kukoga katika mchana wa Ramadhan inasihi?

Kukoga au kukosha uso ikiwa mtu yumo kwenye funga inasihi. Ila ahakikishe maji hayaingii katika matundu ya mwili. Ama yakiingia bila ya kukusudia hilo halina tatizo. Na yakiingia kwa kusudia basi atakuwa amefungua.

Ni ipi hukmu ya mwenye kufunga kutia dawa kwenye macho?
Anaruhusika kutumia na haitobatilika funga yake.

Nini hukmu ya kuchoma sindano  wakati mtu amefunga?

Ikiwa sindano  ni ya dawa tu basi haifunguzi. Ila sindano ikiwa imewekewa kitu chochote ambacho ndani yake kitampa mwenye kufunga nguvu kama glucose basi hapo itakuwa amefungua. Allah ni mjuzi zaidi.

3-KUJIZUIA NA KUJITAPISHA KWA MAKUSUDI

Pia ni wajibu kwa mwenye kufunga kujizuia na kujitapisha kwa makusudi. Ama akitapika bila ya kukusudia basi ataendelea na funga yake kama kawaida. Na akijitapisha kwa makusudi ni lazima ailipe funga hiyo. Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhiya Allahu anhu) amesema: Amesema Mtume (Swalla Allahu alayhi wa sallam): "... na mwenye kujitapisha basi inamuwajibikia kulipa." Bukhari na Muslim.

4-KUWA MUISLAMU
Ikiwa mtu sio Muislamu basi kwake yeye haimuwajibikii kufunga. Na akija kusilimu basi hatolipa kwa zile siku ambazo hakufunga kwani alipokuwa sio Muislamu haikumuwajibikia kufunga.
Ama Muislamu ambae ataritadi wakati amefunga basi moja kwa moja funga yake itabatilika na akija kutubu na kuamua kurudi kwenye Uislamu basi inamuwajibikia kuzilipa siku zote ambazo aliziwacha wakati ametoka kwenye Uislamu.

5-KUWA NA AKILI KATIKA MCHANA MZIMA WA RAMADHAN
Pia ili swaumu isihi lazima mwenye kufunga awe na akili na ikiwa atarukwa na akili basi funga yake itabatilika. Na hakuna tatizo kwa mtu kuzimia kwa muda mchache katika mchana wa mwezi wa Ramadhan.

Usikose kusoma sehemu ya pili ya makala hii.

No comments:

Post a Comment