Monday, 9 June 2014

Sadaka na fadhila zake

Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Ewe ndugu yangu kila siku unasikia kama kuna jambo la sadaka, je unafahamu maana yake na faida za ibada hii na thawabu za mwenye kulifanya jambo hili ?

Basi leo ndio nimependa kulizungumzia jambo hili kwa Tawfiq ya Allah SubhanaLlah Wataala.
Maana ya SADAKA

Ni kile kinachotolewa ili kujikurubisha kwa Allah na hali ya kutarajia malipo kutoka kwake. Sadaka zipo za aina nyingi kwa mfano kimaneno na kimatendo. Miongoni mwa mifano ya sadaka ni kama mali, nguo, chakula,tabia njema, nasaha, kulea mayatima, kujenga msikiti, n.k

Baada ya kwisha jua maana na aina za sadaka hebu sasa tuangalie faida za kutoa sadaka . Zifuatazo ni Faida au Fadhila za Kutoa Sadaka :

1-Itakua ni kuvuli kwa mwenye kuitoa siku ya Qiyamah siku ambayo haitokua na kivuli ila kivuli ambacho Allah atawafunika waja wake maalumu. Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi wasallam
(( Kila mtu atakua chini ya kivuli cha sadaka yake mpaka watakapo hukumiwa watu-siku ya kiama-)) imepokelewa na Ahmad.

2-Huondosha Hasira za Allah.
Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hakika ya sadaka huzima hasira za Allah))Tirmidhiy.

3-Huunganisha udugu

Nalo ni jambo ambalo limesisitizwa sana katika dini kuuchunga na kuunga udugu kwani amezawadiwa pepo kila mwenye kuunga udugu na amelaaniwa mwenye kuukata. Na kwa ajili hio sadaka kwa ndugu wa karibu huandikwa ujira mara mbili wa kutoa sadaka kuunga udugu. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam ((Sadaka kwa maskini huhesabika kama ni sadaka, nayo kwa ndugu wa karibu huhesabika mara mbili, sadaka na kuunga udugu)) Ahmad na tirmidhiy.

4-Huepushwa mbali mwenye kuitoa na vitimbi vya shetani..

Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hatoi mmoja wenu chochote katika sadaka isipokuwa huwekwa mbali nae kwa sadaka ile mashetani sabini)) Imepokelewa na Ahmad na ameisahihisha Albaniy.
5-Inamtwaharisha mwenye kuitoa na kumtakasa.

Amesema Allah subhanahu wataala [[Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.]] 9:103.

6-Malipo yake huendelea hata baada ya kufa kwako.

Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam.((Atakapo kufa mwanaadamu hukatika matendo yake ILA katika matatu;sadaka yenye kuendelea au elimu yenye kunufaisha au mtoto mwema mwenye kumuombea mzazi wake.)) Muslim. Miongoni mwa sadaka yenye kuendelea ni kujenga au kushiriki katika kujenga kisima, msikiti au kupanda mti ambao viumbe vitanufaika nao n.k.

7-Malipo yake huongezwa mara dufu na Allah Subhanahu Wataala.

Kama anavyotuelezea [[Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.]] 2:261.

Pia amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hili ((Mwenye kutoa sadaka kiasi cha tende kutoka kwenye chumo jema na wala Hakubali Allah ila kilicho chema, basi Allah anaipokea kwa mkono wa kulia kisha huilea kwa ajili ya alieitoa kama anavyomlea mmoja wenu farasi wake mpaka iwe kama jabali.)) Bukhari na Muslim.

8-Sadaka ni Sababu ya Kuponywa Maradhi.
Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Jiponesheni maradhi yenu kwa kutoa sadaka))Albaniy.

9-Sadaka hufuta madhambi madogo.
Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi Wasallam : ((..Na sadaka huzima madhambi madogo kama yanavyozima maji moto.)) Tirmidhiy.

10-Humuepusha mwenye kuitoa na kifo kibaya..Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam, ((...Na pia Sadaka humuepusha na Kifo kibaya.)) Tirmidhiy.

Mambo Ya Kujizingatia Katika Kutoa Sadaka

a-Jiepushe kuwaudhi watu na kuwasimanga baada ya kuwapa sadaka. Amesema Allah Subhanahu Wataala.
[[Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. ]]2 :262
b)Jiepushe na Ria, Toa kwajili ya Allah.

Allah subhanahu wataala anasema : [[Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.]]2:264

c) Jitahidi kujificha wakati unapotoa sadaka yako kadri uwezavyo.
Hili linakuepusha na ria na dhana mbaya kutoka kwa watu. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam.. ((Watu saba watafunikwa na kivuli cha Allah siku ambayo haina kivuli ila kivuli chake…) na miongoni mwao akatajwa ni ( Na mtu alietoa sadaka akaificha mpaka mkono wake wa kushoto usijue kilichotolewa na mkono wa kulia)) Bukhari na Muslim.

d) Tambua kuwa Sadaka bora ni ile unayompa mtu wa karibu yako.
Yaani wazazi,mkeo, wanao na ndugu zako. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam : ((Dinar unayoitoa katika njia ya Allah, na dinar unayoitoa katika mtumwa na Dinar unayoitoa kwa maskini na Dinar unayoitoa kwa watu wako, iliyobora kwa malipo ni ile ulioitoa kwa watu wako)). Imepokelewa na Imam Muslim. na watu wako maana yake ni ndugu zako wa karibu. Kama tulivyo wataja hapo juu.

e) Toa kitu kizuri katika unavyovipenda na sio usichokipenda au ambacho hukitaki. Amesema Allah Subhanahu Wataala : [[KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.]] 3:92.

f) Pendelea kuwapa sadaka yako watu wema. Hili litakusaidia kupata dua zao pia utakua na uhakika kama wataitumia katika njia nzuri kwani endapo utampa mtu muovu kama mlevi n.k utakua umemsaidia katia kuyafanya maasi.

g) Tambua ya kwamba Sadaka haipunguzi mali bali huiongeza. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi wasallam. ((Haipungui mali kutokana na kutoa sadaka)) Muslim.

Tujihimize katika kutoa sadaka ili tuweze kupata ujira uliotajwa hapo juu. Muhimu zaidi tuyazingatie yote tuliyoelezwa ili tuweze kupata ujira kamili kutoka kwa Allah. ALLAH ATUTAKABALIE SADAKA ZETU.AMIIIN.

No comments:

Post a Comment