Makala kutoka Raudhwah Islamic Group
CHAKULA CHA WATU WA PEPONI
Anasema Allah subhanah katika suratu swaffat aya ya 41-42 “Hao ndio watakaopewa rizki maalum.(41) Matunda (ya kila namna) na wataheshimiwa(42)”. Na kasema katika suratul waaqiah aya ya 21 “ Na ndege kama watakavotamani wenyewe” . Vitu hivyo vitawajia palepale walipo kama anavyosema Allah “Na vivuli vyake vitakua karibu yao na mashada ya matunda yake yataning’inia mpaka chini (walipo)”. Inasimuliwa kua peponi kutakua na mti ambao kivuli chake atatembea mpandaji mnyama kwa muda wa miaka 100 ,na hajakimaliza.Na katika Hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) iliyokua sahihi ilopokelewa na Imam Muslim na Abu-Daud anaeleza kua watu wa peponi watakula, na hawatoenda chooni si kufanya haja ndogo wala kubwa,na jasho lao litakua ni miski.
Allah mara nyingi akitaja chakula cha jannah hutaja matunda aina kwa aina kama alivyotaja katika Suratu Rahman kua kutakua na makomamanaga na mengineo, hii ni kutokana na kua wanaadamu wengi wanafadhilisha nyama na matunda kuliko aina nyengine za vyakula ,lakini tukumbuke kua kuna neema ambazo macho hazijawahi kuona wala akili kuwahi kuzifikiri hivyo yawezekana kuna aina nyengine nyingi za vyakula ambazo wahusika watakutana nazo (Allah atujaalie miongoni mwao).
VINYWAJI VYA WATU WA PEPONI
Anasema Allah(subhanahu wataala) kuelezea vinywaji vya watu wa peponi kwa mjumuiko katika Suratu-Muhammad aya ya 15, “Mfano wa pepo waloahidiwa wacha-Mungu, imo mito ya maji isiyovunda,na mito ya maziwa isiyoharibika ladha yake,na mito ya ulevi wenye ladha kwa wanywaji,na mito ya asali ilosafishwa...”. Mito yote hiyo asili yake inaanzia katika pepo ya juu ya Firdaus na baadae kushuka katika pepo nyenginezo za chini . Pia kutakua na kinywaji cha Tasneem kimetajwa katika Suratul-Mutaffin kinywaji ambacho watapata watu wa Firdaus waliokua karibu zaidi na Allah ambacho hakijachanganywa na chochote ama waliobaki watapata ambacho kimechanganyika na kitu chengine.
Vinywaji hivyo vitasambazwa na vijana ambao wanang’ara kama anavyosema Allah “Na humo watanyweshwa kinywaji kilochanganyika na tangawizi. Huo ni mto ulokuwemo humo unaitwa Salsabil.Na watawazungukia(kuwatumikia) vijana wasiochakaa,ukiwaona utafkiri lulu zilotawanywa” (Dahri 17-19). Na vyombo vyao kama anavyosema Allah”Na watapitishiwa vyombo vya fedha na vikombe vya vigae. Vigae vya fedha kujazwe humo kwa kipimo”(Suratu Dahr :15-16)
MAVAZI YA WATU WA PEPONI: Watu wa peponi watavishwa nguo za Hariri ambazo zina thamani ya hali ya juu,na Allah ameharamisha kuvaliwa duniani ili akawape waja wake wema Peponi. Amesema Allah “Juu yao wana nguo za Hariri laini, za kijani kibichi na za Hariri nzito. Na watavishwa vikukuu vya fedha..” (Dahri 21). Na katika hadith ilopokelwa na Imam Muslim ua nguo hizo hazitochakaa.
NYUMBA ZA WATU WA PEPONI
Makaazi ya watu wa peponi kama anavosema Rasuul kua matofali ya nyumba zao itakua ni dhahabu na fedha na saruji yake ni Miski,na mchanga wake ni zafarani na changarawe zake ni lulu na yaaquut (Imepokelewa na Tirmidhy na Ahmad).
Humo wataishi katika maghorofa kama anavosema Allah katika suratu Furqaan 75. Pia kutakua na mahema ambayo Rasuul amaeyasifu kua yanatokana na lulu ilo kavu na urefu wake ni maili 60…(Mutaafaqun alayhi). Ndani ya majumba hayo kutakua na mapambo mbalimbali kama anavosema Allah katika suratul-Ghaashiyah 13-16 “Humo kuna viti vya fahari vilivyonyanyuka juu. Na gilasi zilizopangwa.
Na mito ilopangwa safu kwa safu. Na mazulia yalotandikwa”. Na katika suratu Dahr amesema “Na wataegemea humo viti vya enzi hawataona humo jua wala baridi”. Na akasema tena katika suratu-Rahman 76 “wataegemea katika mito ya kijani kibichi, na wakae juu ya mazulia mazuri”
STAREHE NYENGINEZO ZA WATU WA PEPONI
Ukiachilia mbali vyakula,vinywaji,mavazi na wanawake wa jannah, pia peponi kutakua na vipando kama anavyosimulia swahaba Abdul- Rahman bin Saidah kua: Nilikua napenda farasi nikamuuliza Mjumbe wa Allah: Je peponi kutakua na farasi? Akajibu “Ikiwa Allah atakuingiza peponi ewe Abdul-Rahman utakua na Farasi wako anaetokana na yaaqut na atakua na mbawa mbili anaruka utakako” Imepokelewa na Twabraniy.
Pia peponi kutakua na soko kama anavyosimulia Anas radhia Allahu anhu “Hakika peponi kutakua na soko, wataliendea watu kila siku ya ijumaa,utavuma upepo kutoka kaskazini, na utawapata katika nyuso zao na nguo zao, na utawazidisha uzuri ,watarejea kwa wake zao hali ya kua wamezidi uzuri. Watu wao watawaambia:”Tunaapa kwa jina la Allah hakika mumetuzidi uzuri na wao watawajibu na sisi tunaapa hakika nyinyi ndio mlotuzidi uzuri”Imepokelewa na Imam Muslim
Ama neema nyengine ambazo ndio neema Muhimu watakazopewa watu wa peponi ni:
Kumuona Allah(subhanahu wataala): Anasema Allah katika Suratul-Qiyaamah “Nyuso siku hiyo zitang’aa. Zitamtazama Mola wao”. Akasema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi inayosimuliwa na Abu-hurayra (Radhi za Allah ziwe juu yake) ,na kuwafikiwa na Bukhari na Muslim kua watu walimuuliza Rasuul. Je tutamuona Mola wetu? Rasuul akawajibu mtamuona kama mnavyouna mbaa mwezi”
Radhi za Allah(subhanahu wataala): Anasimulia Mtume wa Allah(swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi iliyopokelewa na Bukhari na Muslim na kusimuliwa na Abu-Said Khudry kua watu wa peponi baada ya kuingia, Allah atawauliza jee mumeridhika? Watasema: Kwa nini tusiridhike na umetupa ulichokua hujampa yoyote? .. Allah atwaambia:” Nimekuhalalishieni radhi zangu na sitokukasirikieni milele”. Ni furaha ilioje kwa watu wa peponi kwani waliokua wakimkimblia awaridhie amewahakikishia radhi zake milele na milele.
Kuishi Milele: Anasema Allah(subhanahu wataala) katika Suratul-kahfi “Hakika waloamini wakafanya matendo mema makaazi yao yatakua ni pepo za Firdaus. Watakaa humo milele hawatotaka kuondoka” 107-108. Yatosha kukaa milele ni starehe kwani hakuna kuwaza kua neema iko siku itaondoka kama zitakavyoondoka neema za duniani.
Sifa za watakaoingia humo kama anavyosema Rasuul (swalla Allahu alayhi wasallam) kua ucha-Mungu na kua na tabia njema ndio vitakavyowaingiza watu wengi peponi.
HITIMISHO
Mara moja walikaa watu watatu muislamu,mkirsto na yahudi,na kila mmoja akawa anajisifia kua pepo ni yake na imeandaliwa kwa ajili yake. Mkirsto akajisifia kua Mtume wake Issa ni Ruhu-llah na kwamba atakuja duniani kueneza haki,ama yahudi akajisifia kua amaeletewa Mitume wengi na wengi ni mitume mitukufu hivyo pepo ni yake,na muislamu nae akajisifia kua mtume Muhammad(swalla Allahu alayhi wasallam) ndie kipenzi cha Allah na ndio Mtume wa mwisho hivyo pepo ni yake.
Allah akateremsha aya isemayo: “(hiyo pepo) Si kwa matamanio yenu (waislamu) wala si kwa matamanio ya watu wa kitabu (mayahudi na manasara),Atakaefanya uovu basi atalipwa….” Wanavyuon wa Qur-an na baadhi ya masahaba akiwemo sayyidna Ally(radhi za Allah ziwe juu yao) wanasema hii ndio aya yenye kutisha zaidi ndani ya Qur-an,kwani yaonesha wazi iko tofauti na fikra za waislamu wa zama zetu.
Tunadhani kua tukiwa na majina ya kina Muhammad na Ahmad na Khalid basi tutaingia peponi kisa ni waislamu,na hatutoadhibiwa kwa makosa yetu.Tutambue kua pepo haikuwekwa kwa kila anaejiita muislamu, lakini pepo imewekwa kwa walioamni kikweli, na wakafanya matendo mema. Hakuna hata sehemu moja katika Qur-an iliyotaja kua kila atakaeitwa muislamu ataingia peponi tu bila ya kuadhibiwa kwa makosa yake kwanza, lakini sehemu zote Allah(subhanahu wataala) anasema Wale watakaoamini na wakatenda yalo Mema. Amesema Allah(subhanahu wataala) katika Suratu Sabai 37 “Na si mali zenu wala watoto wenu watakaokukurubisheni kwetu katika daraja za (peponi) ila alieamini na akafanya matendo mema,basi hao watapata ujira mkubwa na wa ziada kwa yale waliyoyatenda..”.
Kufanya matendo mema kunakusudiwa mengi,lakini kubwa lao ni kuepukana kuedekeza matamanio ya nafsi, kwani pepo imezungushiwa yale yanayochukiwa na nafsi. Muislamu anahitajika kufanya aliyoamrishwa na Allah, kuanzia nguzo za kiislamu na mengineo ambayo tumetakiwa kuyafanya kama vile sadaka,kupigania dini ya Allah na mengine mengi, kama alivyousiwa swahaba Muadh katika Hadithi ndefu ya Rasuul, na akahitimishiwa kwa kuwaambia, ili uweze kumiliki kufanya yote hayo ni lazima aweze kuumiliki ulimi wake, kwani Ulimi na utupu ndo vitakavowakosesha watu Pepo kulingana na Hadith Sahih ya Rasuul .
Hivyo basi milango ya pepo huachwa wazi ramadhan kwa kila anaetaka kuingia, na ya moto hufungwa.Tufanye juhudi ya kuipata pepo kwani Allah kila akimaliza kutaja neema za peponi husema :Kutokana na hayo washindane na wenye kushindana” na mahali pengine akasema ;Kutokana na hayo(yani starehe za peponi) na wafanye wenye kufanya. Amesema Mtume wa Allah “Hakika bidhaa ya Allah ni ghali, Hakika bidhaa ya Allah ni pepo” basi na tuikimbilie hiyo bidhaa kabla ya kudoda kwani ikidoda hainunuliki tena na ndio itakua ni siku ya majuto.
Allah atuwafikishe katika kheri na ataruzuku pepo na vyenye kutukurubisha kwenye pepo Innahu waliyyu dhaalika wal-Qaadir alayhi.
Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group
Ameena Allah awajaalie kwa maelezo mazuri
ReplyDeleteAmeena Allah awajaalie kwa maelezo mazuri
ReplyDelete