Friday 26 September 2014

Uzushi Wa Unoadaiwa Ni Fadhila Za Siku Kumi Za Dhul-Hijjah


SWALI: 
 
Nimepokea e-mail iliyotumwa yenye kutaja fadhila za siku kumi kila siku kuwa ni jambo fulani limetokea na kadha kama inavyoeleza hapa chini. Je hii ipo dalili au ni katika uzushi?
 
Siku Kumi Bora

Mwenye-ezi mungu subhanahu wataala ameapa kwa masiku bora katika quraan takatifu sura 89 aya 1-2 isemayo : Mtume Muhammad ( S.A.W.) ametusimulia vilivyotendeka na umuhimu wa siku hizi kumi bora za mfungo tatu (DhulHijja); Rasula-llah atueleza sisi ummati wake  kuwa, mwenye kufunga siku hizo hupata fadhla kubwa mno,kwani kila   siku ina fadhila na kheri zake:

 SIKU YA KWANZA YA MFUNGO TATU Mtume (S.A.W.) asema kuwa - "Ni siku  ambayo Mwenye-ezi Mungu alimsamehe Nabii Adam (A.S.) kwa makosa  yake".Mwenye kufunga siku hiyo, Mwenye-ezi Mungu humsamehe madhambi  yake.   
 
 SIKU YA PILI YA MFUNGO TATUMtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku  ambayo  Mwenye-ezi Mungu alikubali maombi ya Nabii Yunus (A.S.)  ya kumtoa  katika matumbo ya samaki".Mwenye kufunga siku hiyo,  ni kama  aliyefanya ibada ya mwaka mzima pasi na kufanya makosa.

   
 SIKU YA TATA MFUNGO TATU Mtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku ambayo  Mwenye-ezi Mungu aliitikia Dua ya Nabii Zakariya (A.S.) yakumpata  mtoto".Mwenye kufunga siku hiyo, Mwenye-ezi Mungu huitikia dua  yake.

 
 SIKU YA NNE YA MFUNGO TATUMtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku ambayo  alizaliwa Nabii Issa(A.S.)".Mwenye kufunga siku hiyo, Mwenye-ezi  Mungu humuondolea matatizo na umasikini.

 SIKU YA TANO MFUNGO TATU Mtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku   alizaliwa  Nabii Musa(A.S) "Mwenye kufunga siku hiyo, Mwenye-ezi Mungu  humtakasa na unafiki na humuondolea adhabu za kabori.

 SIKU YA SITA MFUNGO TATU Mtume (S.A.W.)asema kuwa:-Ni siku ambayo  Mwenye-ezi Mungu alimfungulia Mtume wake (Muhammed (S.A.W.)  )kheri".Mwenye kufunga siko hiyo, Mwenye-ezi Mungu humuangalia kwa  jicho la huruma wala hapati adhabu siku ya kiyama.

 
 SIKU YA SABA YA MFUNGO TATU Mtume asema kuwa:-"Ni siku ambayo  Milango ya Jahannam(Moto)hufungwa na hayafunguliwi hadi masiku kumi  yatimie".Mwenye kufunga Mwenye-ezi Mungu humfungia Milango  thelathini ya mambo mazito na humfungulia Milango thelathini ya  mambo mepesi.

 SIKU YA NANE YA MFUNGO TATUMtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku  iitwayo  Tar-wiya".Mwenye kufunga hupewa malipo ambayo hakuna ayajuwaye  isipokuwa Allah SWT.

 SIKU YA TISA YA MFUNGO TATUMtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku  iitwayo  Arafat".Mwenye kufunga siku hiyo, hufutiwa makosa ya mwaka  uliopita, na utakao kuja.

 SIKU YA KUMI YA MFUNGO TATU:- Mtume(S.A.W.)asema kuwa:-"Ni siku ya  kuchinja Mnyama(itakuwa Iddi Kubwa), tone la kwanza la damu  litakapo tona Mwenye-ezi Mungu humsamehe dhambi zake na za jamaa  zake. Na mwenye kumpa chakula Masikini au akatowa sadaka siku hiyo,  Myenye-ezi Mungu atamfufua siku ya Kiyama kwa amali na mizani ya  uzito, thawabu zake zitashinda uzito wa Mlima Uhud".

  
PLEASE DO NOT FORGET TO ENLIGHTEN OTHER MUSLIMS BY FORWARDING THIS  MAIL

   
 
 
JIBU Kutoka alhidayah
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa  aalihi wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunasikitika kwamba siku hizi fitna za kusambaza uzushi zimezidi kutokana na wepesi wa mawasiliano kupitia barua pepe (e-mail), simu za mkononi n.k. Jambo linaloshangaza ni kwamba Hadiyth zilizo Sahihi zimejaa tele lakini hizo hazisambazwi kama zinavyosambazwa za uzushi. Ni dhahiri kwamba wanaofanya hivyo ima hawajui tofauti ya mafunzo sahihi na yale potofu ima kwa uchache wa elimu, au kwa pupa tu za kutafuta thawabu kwa njia za mkato ndiko kunakowasababisha wao kueneza haya mambo yasiyo na dalili wala asili. Lakini wanaghafilika ndugu hao kutambua madhara yanayopatikana kutokana na hayo wanayoyaeneza kila mara.

Moja ya madhara makuu ni kupoteza mafundisho sahihi ya Dini yetu, na kueneza ya uongo na hivyo kutawala upotofu katika jamii ya Kiislam, Kwani kama wanavyosema wema waliotangulia, kuwa, bid’ah inavyoenea, ndio Sunnah hupotea.

Tumepekuwa vitabu mbalimbali vya Hadiyth vikubwa na mashuhuri na hakuna hata sehemu moja tuliyokuta kuna Hadiyth inayotaja Fadhila za masiku kumi ya Dhul-Hijjah kwa mtindo huo na kwa maelezo hayo! Vilevile Maulamaa waliowahi kukumbana na maelezo hayo, wamesema kuwa ni ‘Mawdhuw’ – yaani ya kutungwa na si ya kweli.

Kuna hatari vilevile ya watu kutumbukia katika maonyo na makemeo aliyoyatoa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

((من كذب علي متعمدا فليتبوأ مقعده من النار)) متفق عليه

((Atakayeniongopea makusudi basi ajitayarishie makazi yake motoni))  [Al-Bukhaariy Na Muslim]

Ukiwa umeeneza mambo hayo na hali unajua kuwa si sahihi, basi tambua kuwa ushaingia katika walioelezwa ndani ya Hadiyth hiyo.

 

Na ikiwa una mazoea ya kueneza au kutuma kila unachopata ukidhani utapata thawabu kwa kufanya hivyo na hali huna uhakika nacho, au huna elimu ya jambo hilo kama ni sahihi au la, basi utakuwa pia una majukumu kwa kuwa Uislam umesisitiza sana elimu na umuhimu wa kuitafuta; hivyo kwanini ubakie katika ujinga na kutokufahamu unayotuma? Pia ikiwa hujui, ushaelezwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) uulize wenye elimu na upambuzi, je, ulijaribu kufanya hayo kabla hujasambaza mambo hayo ya kutunga yenye kupotezea Waislam muda, juhudi, na hata ‘amali zao kwa kufanya yasiyo sahihi na yasiyo katika mafundisho ya Dini?

 

Na madhara mengine ni kwamba dhambi za mwenye kueneza uzushi huzidi kila uzushi unapozidi kusambaa na mwenye kuanza kueneza uzushi hubeba dhambi za kila mtu anayepokea na kujifunza uzushi huo:

 عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وسلم أنه قال : ( من دعا إلى هدى كان له من الأجر من أجور من تبعه لا ينقص من أجورهم شيئاً ومن دعا إلى ضلالة كان عليه من الإثم مثل آثام من تبعه لا ينقص ذلك من آثامهم شيئاً)   رواه مسلم  

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: ((Atakayelingania kwenye uongofu atapata thawabu (ujira) wa yule atakayemfuata bila ya kupungukiwa chochote katika thawabu zao. Na atakayeelekeza katika upotofu atapata dhambi mfano wa dhambi za yule atakayefuata bila ya kupungukiwa chochote katika dhambi zao)) [Muslim]

Tumefanya utafiti mkubwa kutafuta kauli kama hizo kuhakikisha kama ipo kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inayotaja fadhila za siku hizo kama zilivyotajwa humu lakini hatukupata. Mojawapo ya matokeo ya utafiti ni kupata fatwa kutoka kwa Maulamaa kutoka Markaz ya Fataawa walioulizwa kuhusu ujumbe huo nao pia wamehakikisha kuwa ni uzushi usio na dalili yoyote [Markaz al-Fataawa 24 Dhul-Hijjah 1424/16-02-2004].

Tunawanasihi ndugu zetu Waislamu wasome mada muhimu katika kiungo kifuatacho ili watambue hatari ya kueneza uzushi:

 
Hatari Ya Kueneza Hadiyth Dhaifu Na Visa Vya Uongo

Vilevile mtu anatakiwa asome mada hii hapa chini yenye kuhusu uzushi wenye kufanana na huo:

 

Uzushi Unaodaiwa Kuhusu Mambo Yaliyotokea Siku Ya Ashuraa Tarehe 10

 

Jambo jingine muhimu tunalopenda kuwatanabahisha ni kuhusu jinsi hayo majina ya miezi ya Kiislam yanavyoitwa au yalivyozoeleka kuitwa kama tulivyoona kwenye huo ujumbe wa kutungwa kwa jina la mfungo mosi, mfungo pili, mfungo tatu n.k., hakika ni majina yaliyozoeleka lakini si sahihi kwani yanapoteza ufahamu wa majina sahihi na mpangilio wa hiyo miezi ya Kiislam. 

Miezi ya Kiislam hujulikana mwezi wa kwanza kama ni Muharram lakini wao huo mwezi wa kwanza umeitwa ni mfungo nne, na mwezi wa Dhul-Hijjah ambao ni mwezi wa kumi na mbili, wao wanauita mfungo tatu! Hivyo Waislam wengi hudhani kuwa huu mwezi wa 12 wa Dhul-Hijjah tulionao sasa kuwa ni mwezi wa 3 badala ya 12. Kutoka katika mpango uliowekwa na Uislam na kufuata mipango na taratibu za kimila na kitamaduni, kunasababisha mafunzo ya Dini kutofahamika kamwe, au kusahaulika kabisa. Leo hii, Waislamu wengi Waswahili hawajui miezi ya Kiislam kwa majina yake ingawa wengi wanaijua hiyo ‘mifungo’. Huo ni ukweli wenye kusikitisha. Na wengi huita kalenda na tarehe za Kiislam kuwa ni tarehe za Kiarabu badala ya Kiislam; ilihali kuna tofauti kubwa kati ya Uislamu na Uarabu. Miezi ya Kiislam ni hiyo tuliyozungumzia hapo juu na tutaweka chini kabisa mpangilio wake wa majina ya miezi yote ya mwaka mzima. Kalenda au tarehe za kiarabu ni tofauti na za Kiislam na mtu akitaka kujua atazame magazeti ya Kiarabu ataona tofauti. Hivyo, Waislam wajizoeshe kuita tarehe za Kiislam au miezi ya Kiislam na si ya Kiarabu, maana kuna Wakristo Waarabu nao hawafuati kalenda yetu ya Kiislam.

Miezi Ya Kiislam (Kila Muislam Ajitahidi Kuijua Na Kuihifadhi)

1- Muharram محرّم

2- Swafar صفر

3- Rabiy’u al-Awwal ربيع الأول

4- Rabiy’u ath-Thaaniy au Rabiy’u al-Aakhirربيع الآخر  أو ربيع الثاني

5- Jumaada al-Uwlaa جمادى الأول

6- Jumaada ath-Thaaniy au Jumaada al-Aakhir جمادى الآخر  أو جمادى الثاني

7- Rajab رجب

8- Sha’abaan شعبان

9- Ramadhaan رمضان

10- Shawwaal شوّال  

11- Dhul-Qa’adah ذوالقعدة

12- Dhul-Hijjah ذوالحجة

Inasikitisha sana kuona Muislam

 kahifadhi miezi yote ya kikafiri, lakini hawezi kutaja hata miezi sita ya Kiislam. Sana sana utakuta Muislam anajua ile miezi ya karibu na Ramadhaan kama Rajab, Sha’abaan na pia labda mwezi huu wa Dhul-Hijjah na wengine huujua Rabiy’ul al-Awwal kwa sababu ya kusherekea tu Mawlid na huenda asijue kuwa ni Rabiy’u al-Awwal, bali atakuwa anaujua kwa jina la kijamii ‘Mfungo sita’! Huu ndio msiba tulionao Waislam, inatubidi tuamke hivi sasa na tuzindukane na usingizi wa miaka na miaka. Na silaha pekee ya kuzindukana na hayo, ni ELIMU SAHIHI ya Dini.

Pia tunawaomba ndugu zetu kwamba wanapopata jambo lenye shaka kwanza wawe wanahakikisha kabla ya kutuma kwa wenzao kwani tutambue kuwa Muislamu inapomfikia kauli inayodaiwa kuwa ni ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi imeshakuwa ni waajib kwake kuhakikisha. Akipata dalili ya usahihi wake atume kwa wenziwe kama tunavyoamrishwa kufikisha kwa wengine japo Aayah moja na kuamrishana mema na kukatazana maovu. Lakini ikiwa hakupata dalili yake ni bora kuacha kutuma kuliko kuleta madhara ya uzushi na kuzidisha ufisadi katika dini na jamii kwa ujumla kwa kupoteza mafunzo sahihi na kueneza mafunzo ya uzushi.

Kidokezo Cha Kuweza Kutambua Hadiyth Zisizo Sahihi Au Ujumbe Wa Uongo:

Ndugu Muislam, ukitaka kugundua haraka ujumbe ulioupata kwenye barua pepe (e-mail) au ujumbe kwenye simu za mkono, kwanza kitakachokujulisha kuwa ujumbe huo una utata na sio sahihi, ni kuwa, mara nyingi maelezo yaliyomo ndani ya ujumbe huo zikiwemo zinazosemwa ni Hadiyth, utakuta hazitajwi zilipotolewa, kama ni Hadiyth utaona haisemwi nani kasimulia, nani kapokea, kitabu gani, hakuna hata Imaam wa Hadiyth (Muhaddith) aliyetajwa kwenye Hadiyth hiyo n.k. Hayo yote yanatosha kumtia mashaka mtu kuhusiana na alichokipokea. Hivyo, endapo utapokea ujumbe au Hadiyth ambayo imekuja tu na kudaiwa kasema Mtume, bila kutajwa zaidi ya hivyo… basi mrudishie aliyekutumia na muombe akueleze Hadiyth hiyo iko kwenye kitabu kipi, na nani kaisimulia na kama ni sahihi au dhaifu. Usiwe na pupa ya kueneza au kusambaza kwa wengine hadi kwanza upate uhakika 100%. Vilevile unaweza kutuandikia maswali@alhidaaya.comkuulizia masuala kama hayo na inshaAllaah tutakusaidia haraka katika masuala hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

No comments:

Post a Comment