Tuesday, 10 June 2014

NI IPI PEPO YA ALLAH (SUBHANAHU WATAALA)


Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Allah subhanahu wataala ameumba dunia na akaumba ndani yake starehe ambazo ndio kitakua kipimo cha mwanaadamu ima mafanikio yake au hasara yake ya milele. Allah amewapambia wanadamu starehe mbali mbali kama anavyosema “ Wamepambiwa watu kupenda wanawake,na watoto,na mrundikano wa wa fedha na dhahabu….”( Aal-Imraan : 14). Lakini kila anapotaja dunia na starehe zake, humalizia kwa kusema kuwa ni starehe za kipuuzi ,zenye kudanganya na ni zenye kupita, hivyo tusihadaike nazo. Amesema Allah subhanahu wataala katika Suratu Faatir aya ya 5: “Yasikundanganyeni maisha ya dunia,na asikudanganyeni mdanganyifu mkubwa”. Ni Kweli yasitudanganye maisha ya dunia, kwani kila starehe ya duniani ni starehe bandia, starehe ya kula ipo kwenye sentimita chache za ulimi, na chakula kinapovuka tu ulimi hakina tena ladha,halikadhalika starehe nyenginezo zimo katika sentimita chache tu za viungo vyake husika.

Starehe za dunia zina kiwango chake, na kinapovuka kiwango hicho hua adhabu badala ya starehe, mlaji anapozidisha kula na akavimbiwa,basi mwisho wake ni kuumwa na tumbo na madhara mengineyo. Maisha ya dunia hayakosi misukosuko mara kuumwa,kuchoka, alimuradi starehe za dunia ni zenye kudanganya.

Allah badala yake ameweka starehe za kudumu na zilizo bora kwa waja wake wema. Amesema Allah katika Suratul ‘Aala aya ya 17 “Na Akhera ni bora na ni yenye kubaki”. Amejaalia maisha ya dunia kua ni yenye mapungufu, ili watu wakimbilie maisha ya Akhera.Amesema katika suratu Aal Imraan aya ya 133 “Na kimbilieni msamaha wa Mola wenu na pepo (yake), ambayo upana wake ni sawa na mbingu na ardhi. Imewekwa kwa wacha-Mungu” na akayarejea hayo hayo tena katika (Suratul-Hadyd : 21).

Allah ameeleza kua malipo ya watu wema kua ni ujira usiokwisha. Kitendo cha starehe za Akhera kubaki milele, yatosha kua ni starehe, kwani starehe yoyote isiyodumu basi hiyo si starehe ya kweli, kwani kila unapokumbuka kua itakwisha basi furaha yote huondoka, halikadhalika adhabu ambayo ina mwisho, si adhabu ya kweli kwani iko siku itamalizika na kusahaulika. Allah ameandaa malipo mazuri kwa watakaotenda mema, na mabaya kwa watakaofanya ubaya, na hakuna malipo ya tatu.

Ima Pepo au Moto. Na amaeyakariri hayo takriban katika kila sura ndani ya Qur-an, ili kuwatia hamu watu kuikimbilia pepo na kuepukana na Moto. Kila anapotaja Pepo hutaja na Moto ili watu wapate kutafakari. Lakini je nani anayazingatia haya? Pepo imetajwa takriban mara 126 ndani ya Qur-an na kumetajwa majina yake,sifa ya watu watakaoingia humo,chakula chao,vinywaji vyao,mavazi yao, makasri na vyumba vyao na starehe nyenginezo.

Inshaa Allah tutaanza kuangalia kipengele kimoja baada ya chengine, lakini ufupi wa neema hizo anasimulia Mtume rehma na amani ziwe juu yake, katika hadith Qudsy ilopokelewa na Tirmidhy kua amesema Allah(subahanahu wataala) “Nimewaandalia waja wangu wema (malipo ambayo)macho hayajawahi kuona,wala masikio kusikia, wala haijawahi kumpitikia mtu kwenye akili yake.” Mtu wa chini katika pepo basi atapewa ufalme wa dunia mara 10 yake seuze wa daraja ya juu. Pepo ina daraja 100 kama anavyosema Rasuul na watu wa daraja ya chini watawaona wa juu yao kama wanavyoona nyota na baina ya daraja moja na nyengine ni umbali baina ya mbingu na ardhi.(Hadith imepokelewa na Bukhari). Nyuso za watu wa peponi zitang’ara na wataishi humo kama wafalme, kama anavyosema Allah kufupisha starehe hizo “Na utakapoyaona yalioko huko utaona ni neema na ufalme mkubwa”

MAJINA YA PEPO

Pepo inatajwa kua na milango minane kama iliyvopokelewa katika hadithi mbalimbali na haikuja aya kuonesha milango ya pepo bali aya zimekuja kutaja majina ya pepo. Miongoni mwa milango hiyo ya pepo uko mlango wa kulia ambao wataingia wale watu sabini elfu bila ya hesabu wala adhabu,kuna mlango wa wafungaji unaoitwa Rayyan,kuna mlango wa wenye kukithirisha sala,kuna mlango wa wenye kukithirisha kutoa sadaka,kuna mlango maalum kwa mashahidi (waliokufa wakipigania dini ya Allah) na kuna mlango maalum kwa wenye kuzuia ghadhabu zao. Hii milango imekuja katika Hadith mbalimbali za Rasuul (swalla Allah alayhi wasallam) na mengine miwili ilobaki ni Qiyas ya wanavyuoni. Wallah A’alam.
Ama majina ya pepo yaliyotajwa katika Qur-an ni:

1-Firdaus :Nayo ni pepo ya daraja ya juu kwa lugha ya kimombo ni “First Class”. Sakafu yake ya juu ni Arshi Ya Allah, na mito yote peponi huanzia katika pepo hii. Waloandaliwa pepo hii wametajwa sifa zao mwanzo wa suratul-muuminuun aya ya 10-11 na akamalizia kwa kusema “Hao ndio warithi. (10)Ambao watarihi Firdaus milele(11)”. Na imepokelewa kua watakaoingia kupitia mlango wa kulia wa pepo basi mafikio yao ni katika pepo hii.

2-Jannaatu Adnin : Inasimuliwa kua pepo zote Allah ameziumba kwa kusema kua na zikawa, lakini pepo hii ameiumba kwa mikono yake. Ni pepo iliyotajwa mara nyingi katika Qur-an. Ama majina mengine ni: Jannaatul-khuld, Jannatul-Aaliyah, Jannaatu-Nnaim, Daarul-Akhirah, Daaru-Salaam, Daarul-Qaraar, Daarul-Mutaqin,na Daarul-Muqamah.

WAKE WA WATU WA PEPONI

Tuanzie na wanawake wa jannah, kwani kama alivyotanguliza Allah kua kawapambia watu kupenda wanawake kama tulivyoona hapo kabla. Amesema Allah(subhanahu wataal) katika Suratul-Waaqiah aya ya 22-23 “(Watapewa humo) wanawake wenye macho mzuri na makubwa.(22)(wanapendeza) kama kwamba lulu zilofichwa (ndo kwanza zinapasuliwa)(23)”. Wanawake wa jannah wamepewa jina la “Huurul-Ayn” kutokana na macho yao kua makubwa, ambayo yamekooza weusi wa mboni zao katika weupe wa macho yao.

Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi sahih ilowafikiwa na Bukhari na Muslim “…na kila mtu atakua na wake wawili,wanaonekana uboko wa miguu yao,nyuma ya nyama zao,na hakutakua na mjane peponi” Akimaanisha kua ngozi zao zitaonesha mpaka kilicho ndani mfano wa kioo.

Vilevile Mtume amewasifu wanawake wa jannah kua lau kama mmoja wao ataletwa duniani basi harufu yake itaenea dunia nzima, na nuru yake itaangaza dunia nzima.(Hadith sahih Bukhari na Muslim).

Amesema Allah katika Suratu-Rahman aya ya 56-58 “Watakuwemo humo wanawake watulizao macho yao,(56)hawajaguswa na binaadamu yoyote wala jini kabla ya hapo,(57) kama kwamba ni yakuuti na marijani (58)” na Akasema tena katika Suratu-Swaffaat aya ya 48-49 “Pamoja nao watakua wanawake wenye macho mazuri na makubwa. (48) Wanawake hao kama mayai yalohifadhiwa(49)”. Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ”….Hakika mmoja wenu atapewa nguvu za watu 100 katika kula,kunywa na kuingiliana na mkewe.”(Ahmad).Pamoja na uzuri wao lakini mwanamke mwema atakaeingia jannah atawazidi mahurul-ayn.

Usikose kusoma sehemu ya pili ya Makala hii hapo kesho in shaa Allah.

Makala imetolewa na Raudhwah Islamic Group

Monday, 9 June 2014

Sadaka na fadhila zake

Makala kutoka Raudhwah Islamic Group

Ewe ndugu yangu kila siku unasikia kama kuna jambo la sadaka, je unafahamu maana yake na faida za ibada hii na thawabu za mwenye kulifanya jambo hili ?

Basi leo ndio nimependa kulizungumzia jambo hili kwa Tawfiq ya Allah SubhanaLlah Wataala.
Maana ya SADAKA

Ni kile kinachotolewa ili kujikurubisha kwa Allah na hali ya kutarajia malipo kutoka kwake. Sadaka zipo za aina nyingi kwa mfano kimaneno na kimatendo. Miongoni mwa mifano ya sadaka ni kama mali, nguo, chakula,tabia njema, nasaha, kulea mayatima, kujenga msikiti, n.k

Baada ya kwisha jua maana na aina za sadaka hebu sasa tuangalie faida za kutoa sadaka . Zifuatazo ni Faida au Fadhila za Kutoa Sadaka :

1-Itakua ni kuvuli kwa mwenye kuitoa siku ya Qiyamah siku ambayo haitokua na kivuli ila kivuli ambacho Allah atawafunika waja wake maalumu. Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi wasallam
(( Kila mtu atakua chini ya kivuli cha sadaka yake mpaka watakapo hukumiwa watu-siku ya kiama-)) imepokelewa na Ahmad.

2-Huondosha Hasira za Allah.
Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hakika ya sadaka huzima hasira za Allah))Tirmidhiy.

3-Huunganisha udugu

Nalo ni jambo ambalo limesisitizwa sana katika dini kuuchunga na kuunga udugu kwani amezawadiwa pepo kila mwenye kuunga udugu na amelaaniwa mwenye kuukata. Na kwa ajili hio sadaka kwa ndugu wa karibu huandikwa ujira mara mbili wa kutoa sadaka kuunga udugu. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam ((Sadaka kwa maskini huhesabika kama ni sadaka, nayo kwa ndugu wa karibu huhesabika mara mbili, sadaka na kuunga udugu)) Ahmad na tirmidhiy.

4-Huepushwa mbali mwenye kuitoa na vitimbi vya shetani..

Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Hatoi mmoja wenu chochote katika sadaka isipokuwa huwekwa mbali nae kwa sadaka ile mashetani sabini)) Imepokelewa na Ahmad na ameisahihisha Albaniy.
5-Inamtwaharisha mwenye kuitoa na kumtakasa.

Amesema Allah subhanahu wataala [[Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwazo, na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.]] 9:103.

6-Malipo yake huendelea hata baada ya kufa kwako.

Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam.((Atakapo kufa mwanaadamu hukatika matendo yake ILA katika matatu;sadaka yenye kuendelea au elimu yenye kunufaisha au mtoto mwema mwenye kumuombea mzazi wake.)) Muslim. Miongoni mwa sadaka yenye kuendelea ni kujenga au kushiriki katika kujenga kisima, msikiti au kupanda mti ambao viumbe vitanufaika nao n.k.

7-Malipo yake huongezwa mara dufu na Allah Subhanahu Wataala.

Kama anavyotuelezea [[Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua.]] 2:261.

Pia amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hili ((Mwenye kutoa sadaka kiasi cha tende kutoka kwenye chumo jema na wala Hakubali Allah ila kilicho chema, basi Allah anaipokea kwa mkono wa kulia kisha huilea kwa ajili ya alieitoa kama anavyomlea mmoja wenu farasi wake mpaka iwe kama jabali.)) Bukhari na Muslim.

8-Sadaka ni Sababu ya Kuponywa Maradhi.
Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam ((Jiponesheni maradhi yenu kwa kutoa sadaka))Albaniy.

9-Sadaka hufuta madhambi madogo.
Amesema Mtume Swalla llahu Alayhi Wasallam : ((..Na sadaka huzima madhambi madogo kama yanavyozima maji moto.)) Tirmidhiy.

10-Humuepusha mwenye kuitoa na kifo kibaya..Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam, ((...Na pia Sadaka humuepusha na Kifo kibaya.)) Tirmidhiy.

Mambo Ya Kujizingatia Katika Kutoa Sadaka

a-Jiepushe kuwaudhi watu na kuwasimanga baada ya kuwapa sadaka. Amesema Allah Subhanahu Wataala.
[[Wanao toa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishii masimbulizi wala udhia kwa walicho toa, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa khofu juu yao wala hawatahuzunika. ]]2 :262
b)Jiepushe na Ria, Toa kwajili ya Allah.

Allah subhanahu wataala anasema : [[Enyi mlio amini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi, kama anaye toa mali yake kwa kuwaonyesha watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake pana udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa walivyo chuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.]]2:264

c) Jitahidi kujificha wakati unapotoa sadaka yako kadri uwezavyo.
Hili linakuepusha na ria na dhana mbaya kutoka kwa watu. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam.. ((Watu saba watafunikwa na kivuli cha Allah siku ambayo haina kivuli ila kivuli chake…) na miongoni mwao akatajwa ni ( Na mtu alietoa sadaka akaificha mpaka mkono wake wa kushoto usijue kilichotolewa na mkono wa kulia)) Bukhari na Muslim.

d) Tambua kuwa Sadaka bora ni ile unayompa mtu wa karibu yako.
Yaani wazazi,mkeo, wanao na ndugu zako. Amesema Mtume swalla Allahu alayhi wasallam : ((Dinar unayoitoa katika njia ya Allah, na dinar unayoitoa katika mtumwa na Dinar unayoitoa kwa maskini na Dinar unayoitoa kwa watu wako, iliyobora kwa malipo ni ile ulioitoa kwa watu wako)). Imepokelewa na Imam Muslim. na watu wako maana yake ni ndugu zako wa karibu. Kama tulivyo wataja hapo juu.

e) Toa kitu kizuri katika unavyovipenda na sio usichokipenda au ambacho hukitaki. Amesema Allah Subhanahu Wataala : [[KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua.]] 3:92.

f) Pendelea kuwapa sadaka yako watu wema. Hili litakusaidia kupata dua zao pia utakua na uhakika kama wataitumia katika njia nzuri kwani endapo utampa mtu muovu kama mlevi n.k utakua umemsaidia katia kuyafanya maasi.

g) Tambua ya kwamba Sadaka haipunguzi mali bali huiongeza. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi wasallam. ((Haipungui mali kutokana na kutoa sadaka)) Muslim.

Tujihimize katika kutoa sadaka ili tuweze kupata ujira uliotajwa hapo juu. Muhimu zaidi tuyazingatie yote tuliyoelezwa ili tuweze kupata ujira kamili kutoka kwa Allah. ALLAH ATUTAKABALIE SADAKA ZETU.AMIIIN.

Sunday, 8 June 2014

ISRAAFU


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Nini Israafu?

Israafu ina maana nyingi miongoni mwa hizo ni:
1. Israafu ni kule kutumia kitu zaidi ya kile unachohitaji, kwa maana ya kwamba israfu inaendana na matumizi ya mtu anayohitaji ambayo anaweza kuweka kiwango cha kufanya yanapozidi basi ni israafu.

2. Israafu pia ina maana ya kutumia jambo au kitu chochote usichokihitaji, kwa maana kumiliki au kuwa na kitu chochote ambacho si cha lazima na si muhimu kwako.

3. Vilevile Israafu haina maana kuwan ni matumizi mabaya ya fedha lakini inajumuisha matumizi mabaya ya rasilimali yoyote ile, ikiwa matumizi ya maji wakati mtu anapotumia, au kuwacha chakula katika sahani baada ya kujaza kisichokuwa saizi yake, au hata kula zaidi ya kiwango chake au baada ya kushiba.

Baadhi ya dalili katika Qur-an na Sunna zinazozungumzia na kukemea Israafu

“Naye ndiye Aliyeziumba bustani zilizoegemezwa na zisizoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbalimbali, na mizaituni na mikomamanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni matunda yake ipambapo, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake, wala msitumie kwa fujo (israafu), hakikaYeye hawapendi watumiao kwa fujo.” (Qur-an: 6:141)

“Na umpe ndugu haki yake, na maskini na msafiri, wala usitumie (mali yako) kwa ubadhiri. Hakika watumiao kwa ubadhiri ni ndugu za mashetani; na Shetani ndiye asiyemshukuru Mola wake” (17:26-27)

“Bila shaka ninyi mnaniita kwa yule ambaye hana wito duniani wala Akhera, na marudio yetu ni kwa Mwenyezi Mungu, na wapitao kiasi hao ndio watu wa Motoni.” (Qur-an:40:43)

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Majmaul Bayaan, Bakhti Shoa alikuwa na daktari maalum wa Haroun Rashyd, na alikuwa mkristo. Siku moja alimuuliza Waqidi “Je katika kitabu chenu (Qur-an) kuna elimu ya tiba?” Waqidi akamjibu, Allah mtukufu amekusanya tiba yote katika aya moja tu “….Kuleni na kunyweni wala msifanye israfu”

Yule tabibu akauliza je Mtume wenu ametaja chochote katika elimu hii ya tiba?
Waqidi akamjibu ndiyo, Mtume ameelezea na kuchambua elimu ya tiba katika sentensi fupi. Mtume (swallalahu alayhi wassalam) anasema: “ Tumbo ni nyumba ya maradhi na kutovimbiwa na chakula ni dawa kubwa, kila mtu anatakiwa ale kwa kiasi kinachomtosha na asivimbiwe” Pale aliposikia maneno yale tabibu akakiri na kusema “kitabu chenu na Mtume wenu hakijaacha kitu katika elimu ya tiba na wataalamu wa kigiriki, sina chochote cha kusema.

Kutoka kwa Ibnu Jurayj radhi za Allah ziwe juu yake amesema: Imepokelewa hadithi kuwa Thabit Ibnu Qays bin Shamaas, anbae alivuna tende katika shamba lake, akasema ndani ya nafsi yake “Siku ya leo Mtu yeyote atakaekuja kwangu basi nitamlisha tende hii, akalisha watu kutwa nzima mpaka ikafika jioni, kuangalia akawa hana alichobakisha katika tende zile.

Ndipo Allah akateremsha aya hii: “Enyi wanadamu, shikeni mapambo yenu wakati wa kila Sala; na kuleni na kunyweni wala msipite kiasi; hakika Yeye Hawapendi wapitao kiasi” (Qur-an: 7:31).

Baada ya kuona makemeo ya Israafu na uharamu wake, Je ni kipi kifanyike kujiepusha na Israafu:

1. Kwanza ni kumuomba Allah akulinde na akuepushe na Israafu, maana binaadamu hatuna ujanja wa kuzizuia nafsi zetu tusifanye israafu.

2. Usiwe mwenye kutamani vitu visivyo vya lazima, kwa kuwa kufanya hivyo kutakupelekea kufanya matumizi yasiyo ya lazima.

3. Jitahidi kutafuta bidhaa au matumizi yako kwa thamani ya chini zaidi, ili uweze kujipunguzia matumizi zaidi ya kile unachohitaji.

4. Kupunguza ufakhari na kutaka mambo makubwa. Hili khasa kwa upande wa mama na dada zetu,
Mtu anasema naenda na fashion au uptodate, kwa maana nguo au kiatu au kitu chochote kikitoka sokoni basi yeye huwa na pupa ya kutafuta kila njia apate kitu hicho.

Wanajaza makabati kwa nguo walizozivaa kwa siku moja au mbili, kila harusi mtu avae nguo mpya, hii ni israafu.

5. Kwa wale wenye familia usijaze friza lako kwa vyakula vingi, kuliko uwezo na matumizi yako. Watu huwacha mpaka vitu vinaharibika na wakati jirani yako analala na njaa. Weka matumizi yako kwa kujua kile unachohitaji, sawasawa na unapoweka chakula chako basi unatakiwa uweke kulingana na uwezo wako kuepusha kukimwaga huko ndiko kufanya israafu.

6. Kwa vijana wa leo, hatusemi haramu ila tupunguze na kuvaa kila kitu kwa nembo/kampuni/brand.

Kwa mfano shati, suruali, nguo za ndani mpaka viatu mtu anavaa vya nembo maalum. Huku ni kufanya matumizi yasiyo ya lazima.

7. Mwisho ni kuweka nia kwa ikhlaas, kumuomba Allah atusamehe na atulinde kufanya israafu, pamoja na kutuweka mbali na israafu.

EWE ALLAH MUUMBA TULINDE NA UWALINDE WAISLAMU NA DHAMBI HII YA ISRAFU EWE MWINGI WA KUREHEMU.

Saturday, 7 June 2014

BAADHI YA SALA ZA SUNNA NA FADHILA ZAKE


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Allah subhanahu wataala ametufaradhishia sala tano kila siku. Sala ambazo ni wajibu wa kila muislamu kuzisali. Pia Allah subhanahu wataala akatuwekea sala za sunna. Sala za sunna  ni muhimu sana kuzisali kwani hujaza mapengo ya sala za faradhi ikiwa zina mapungufu siku ya Qiyama. Kwa ujumla sala ni lazima mwanadamu azisali na tuzisali kwa unyenyekevu kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah. Umuhimu wa sala za fardhi na faida ya sala za sunna imeelezwa na Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) katika hadithi ifuatayo : Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu anhu) anatuelezea kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi  wasallam) amesema: ((Kitu cha kwanza kinachohesabiwa katika amali za mja wa Allaah siku ya Qiyaamah ni Swalah zake. Zikiwa zimetimia, hapo tena atakuwa kaneemeka na kafuzu, na zikiwa zina kasoro atakuwa kaanguka na kala khasara. Ikiwa pana upungufu katika Swalah zake za fardhi Allaah Azza wa Jalla Atasema: Angalia ikiwa mja Wangu ana Swalah zozote za Sunnah ambazo zinaweza kufidia zile zilizopungua, hapo tena amali yake iliyobaki itaangaliwa hivyo hivyo)) [At-Tirmidhiy, Abu Daawuud, An-Nasaaiy, Ibn Maajah na Ahmad].

Hivyo ndugu zanguni tujihimizeni kusali sala za faradhi na pia tuzikimbilie sala za sunna kwani zitakuja kujaza mapengo katika sala zetu.  Leo katika makala yangu hii nitazungumzia baadhi tu ya sala za sunna  na faida zake kwa uchache. Miongoni mwa hizo ni :

1- Rakaa 12 za sunna
2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.
3- Sala ya dhuha.
4- Sala ya witri.

Ama upande wa sala  ya tahajjud na fadhila zake hiyo tutaiwekea makala maalum na utaweza kuisoma.

1-Fadhila ya rakaa 12 za sunna

Imesimuliwa na Bibi Ummu habibah Ramla bint Abi Sufyan(Radhia Allahu anha) amesema amemsikia Mtume wa Allah(swalla Allahu alayhi wasallam) akisema " Hakuna mja yoyote muislamu atakaeswali kwa aijli ya Allah rakaa 12 kila siku kwa kujipendekeza na si za Fardhi ila Allah atamjengea nyumba peponi” Imepokelewa na Imam Muslim.

Mwenye kudumu na kusali rakaa hizi 12 kwa ajili ya Allah na kwa ajili ya kujipendekeza kwa mola wake basi Allah subhanahu wataala atamjengea mja huyo nyumba katika pepo yake. Ni nani asiyetaka pepo ya Allah ? Tuko wapi Umma wa kiislamu kuzikimbilia kheri kama hizi. Wako wapi wenye kushindana kwa ajili ya kupata nyumba katika pepo ya Allah ? Suala litakuja je ni zipi hizo rakaa 12 ? Jibu la suala hilo linapatikana katika hadithi ifuatayo : Bibi Aisha(Radhia Allahu anha)  anasema " Amesema Mtume wa Allah rehma na amani ziwe juu yake " Yoyote atakaedumu na rakaa 12 usiku na mchana ataingia peponi: rakaa 4 kabla ya adhuhuri na 2 baada yake. Rakaa 2 baada ya sala ya maghrib, Rakaa 2 baada ya sala ya ishaa na rakaa 2 kabla ya sala ya alfajiri"(Imepokelewa na tirmidhy,nasai na ibn majah).

2-Raka mbili kabla ya sala ya alfajiri.

Rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri imetajwa ndani ya rakaa 12 za kila siku ambazo mwenye kuzisali Allah humjengea mtu nyumba katika pepo. Ila nimeamua kwa uchache kuielezea sunna hii kwani wengi wa watu wamekuwa wakiipuza. Pia Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akiwahimiza zaidi watu kusali rakaa hizi mbili. Inasimuliwa na Bibi Aisha kuwa” Hakuna swala yoyote ya Sunna ambayo Mtume alikua akiitilia mkazo zaidi kama rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri”Imepokelewa na Bukhari na Muslim. Rakaa 2 hizi husaliwa kabla ya sala ya alfajiri. Na imethibiti kwamba Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akisoma sura ndogo ndani ya rakaa mbili hizi.

Zama hizi watu wamekuwa wakiamka bado kwa dakika chache kusaliwa sala ya alfajiri ndio mtu nae hukimbilia kusali. Au wengine husali alfajiri hali ya kuwa sala tayari imeshatoka. Rakaa mbili hizi Mtume swalla Allahu alayhi wasallam anapiga mfano wa ubora wake kuliko dunia na vilivyomo ndani yake. Dunia ina mazuri mangapi? Ina  vitu vya thamani vingapi ? Lakini vyote hivyo haviwezi kuzidi thamani ya rakaa mbili kabla ya sala ya alfajiri. Imesimuliwa na Bibi Aisha (radhwiya Allahu anha) amesema Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam)" Rakaa mbili za sunna kabla ya sala ya alfajiri ni bora kuliko dunia na vilivyomo ndani yake" Imepokelewa na Imam Muslim na Tirmidhi.

Wito kwa wenye kusali sala ya alfajiri na kutojihimu na rakaa mbili hizi tusiache kukimbilia kheri kama hizi. Na wito wangu kwa wenye kulala wakati wa sala ya alfajiri unampita jua kwamba utaenda kuulizwa kwa Allah juu ya kila sala iliyokupita na pia unakosa nafasi za kheri kama hizi kwa kufuata matamanio ya nafsi yako pamoja na shetani.

3- Sala ya dhuha.

Sala ya dhuha ni sala ambayo husaliwa robo saa baada ya kuchomoza kwa jua na mwisho wake ni kabla ya kuingia kwa adhuhuri. Sala hii ni miongoni mwa wasia wa Mtume Muhammad swalla Allahu alayhi wasallam kwa sahaba wake Abuu Hurayra na wengine katika masahaba. Ila ni wasia ambao na sisi unatufaa kuufuata na kuufanyia kazi. Imesimuliwa na Abu-Hurayra -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema:"Ameniusia Kipenzi changu(swalla Allahu alayhi wasallam) mambo matatu: Kufunga siku tatu kila mwezi,Rakaa mbili za Dhuha na kusali witri kabla ya kulala" Imepokelewa na Bukhari na Muslim na pia Mtume swalla Allahu alayhi wassalam alimuusia hayo hayo swahaba wake mwengine Abuu-Dardai radhia Allahu anhu katika hadityhi ilopokelewa na Imam Muslim na Abu-Daud.

Sala husaliwa rakaa mbili mbili hadi kufikia nane. Na imethibiti zaidi kuwa Mtume swalla Allahu alayhi wasallam alikuwa akisali rakaa nne. Hii ni sunna ambayo wengi wa watu wameisahau labda kwa sababu ya maisha au kughurika na dunia na starehe zake. Je ni yapi malipo kwa mwenye kusali dhuha? Atakaeswali Dhuha kachukuliwa dhamana na Allah ya kusimamiwa mambo yake kwa siku ile kama anavyosema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi ilopokelewa na Uqba bin Amir radhia Allahu anhu kua "Amesema Allah kumwambia mwanadamu:Ewe mwanadamu nitosheleze mwanzo wa mchana kwa rakaa nne nami nitakutosheleza mwisho wa mchana" Imepokelewa na Imam Ahmad .

4- Sala ya witri

Imesimuliwa na Jabir radhiallahu anhu amesema:” Amesema Mtume sallahu alayhu wasslam “Atakaekhofu kutosimama mwisho wa usiku, basi aswali witri mwanzo wa usiku, na anaetarajia kua atasimama mwisho wa usiku basi na aswali witri mwisho wake, kwan witri mwisho wa usiku ni yenye kushuhudiwa na inayohudhuriwa (na malaika) na hiyo ndo bora” Imepokelewa na Imam Muslim, Tirmidhi na wengineo.
Sala ya witri ina faaida kubwa sana na malipo makubwa. Yatosha fadhila yake kuwa sala ya witri inashuhudiwa na malaika. Pia ni katika wasia alousia Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) kama tulivyoeleza katika hadithi iliyopita. Witri ni 1,3,5,7,11. Mtu anasali rakaa 2. Halafu anamalizia 1. Au anasali rakaa 2 halafu tena 2 halafu anamalizia moja.

Kwa ujumla sala zote zina faida kwetu waislamu. Ni wajibu wote tujihimu na kuacha uvivu katika kuzisali sala hizi. Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale watakaosali na kukubaliwa sala zao. Na wale wenye kukumbushwa kheri na kuzikimbilia kheri hizo. Aaamin.

Allah ni mjuzi zaidi.

Thursday, 5 June 2014

UMUHIMU WA SWALA


Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wata‘ala), Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake. Swala na salamu zimuendee kipenzi cha ummah Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Ndugu wa kiislamu, kama tunavyofahamu kuwa swala ndio nguzo ya pili katika Uislamu na ni ibada iliyotiliwa mkazo na ni yenye umuhimu mkubwa kwetu sisi Waislamu, kwani ni ibada pekee ambayo Allah (subhanahu wata‘ala) hakuifaradhisha kwa kumletea wahyi tu Mtume wetu Muhammad kupitia Jibril (alayhi salam) bali alimuandalia safari maalum ya kiroho na kimwili ili kuweza kumkabidhi jukumu la ibada hii kama tunasoma katika kisa cha Israa na Miraj.

Ndugu wa kiislamu, maana ya swala kilugha ni dua kama ilivyokuja katika Quran pale Allah (subhanahu wata‘ala) aliposema:

“... na uwaombee rehema. Hakika maombi yako ni utulivu kwao ...” [At-Tawbah 9 : 103].
Ama kisheria ni vitendo na kauli maalum zinazoanzwa kwa Takbir na kumaliza kwa salam.

Swala ni katika aina za ibada ambazo walifaradhishiwa Mitume yote iliyopita kwani ni ibada ambayo humkurubisha mja kwa Mola wake na humpa fursa ya kuzungumza na kueleza shida zake kwa Mola wake. Allah alimfaradhishia swala Nabii Mussa (alayhi salam) pale aliposema: “Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu. Hapana mungu ila Mimi tu. Basi niabudu Mimi, na ushike Sala kwa ajili ya kunikumbuka Mimi.” [Twaha 20 : 14].

Swala inayoswaliwa ndani ya wakati wake ndiyo ‘amali bora kuliko ‘amali zote kama alivyosema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) katika hadith iliyosimuliwa na Ibn Masoud (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nilimuuliza Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) ni ipi ‘amali iliyobora? Akasema: “Swala katika wakati wake” Nikasema kisha ipi? Akasema: “Kuwafanyia wema wazazi wawili” Nikasema kisha ipi? Akasema “Jihadi katika njia ya Allah”. Bukhary na Muslim.

Allah (subhanahu wata‘ala) humuwepesishia rizki zake mwenye kuswali, kwani yeye si muhitaji wa swala bali sisi ndio wahitaji. Na kwa kupitia swala Allah ameahidi kumruzuku kwa was‘a yule mwenye kuswali kama Anavyosema: “Na waamrishe watu wako kusali, na uendelee mwenyewe kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mchaMungu.” [Taha 20 : 132].

Pia imethibiti katika hadithil Qudsi kuwa Allah (subhanahu wata‘ala) Amesema: “Ewe Mwanaadamu, kuwa tayari kutekeleza ibada zangu, nami nitajaza katika moyo wako utajiri, na nitauziba mlango wa ufakiri kwako, na kama hutafanya hivyo nitajaza shughuli katika moyo wako, na mlango wa ufakiri sitoufunga kwako.” Ahmad na Tirmidhy.

Ndugu wa kiislamu, Allah (subhanahu wata‘ala) akazidi kuonyesha umuhimu wa swala kwa kututaka sisi waja wake tushikamane nayo na tuihifadhi zaidi pale Aliposema: “Zilindeni Sala, na khasa Sala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti (kunyenyekea).” [Al-Baqara 2 : 238].

Swala tano na Ijumaa mpaka Ijumaa hufuta dhambi ndogo zilizomo baina yao. Imesimuliwa na Ibn Masoud kuwa mtu mmoja alimbusu mwanamke na akaja kwa Mtume kumpa khabari hiyo (kwa kutaka kujua hukmu yake). Basi Allah (subhanahu wata‘ala) akateremsha “Na shika Sala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu” Akasema yule mtu: ni kwa ajili yangu mimi tu hili? Akasema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Ni kwa ajili ya ummah wangu wote.” Bukhary na Muslim.

Pia Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nimemsikia Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) Akisema: “Mnaonaje ikiwa mto (wa maji) upo chini ya mlango wa mmoja wenu naye akawa anakoga humo mara tano kwa siku jee utabakia uchafu katika mwili wake?” Wakasema (maswahaba): “Hautabakia uchafu katika mwili wake.” Akasema: “Huo ndio mfano wa swala tano, Allah hufuta madhambi yalipo baina yake.” Bukhary na Muslim.

Vile vile swala inayoswaliwa vilivyo humkataza mtu na mambo maovu na machafu na kumkurubisha katika rehma za Allah kama Anavyosema Allah katika Quran: “... na ushike Sala. Hakika Sala inazuilia mambo machafu na maovu. ...” [Al-Ankabut 29 : 45].

Ndugu wa kiislamu hayo ni katika baadhi tu ya fadhila za swala kwetu. Hivyo tujihimu katika kuitekeleza na kuisimamisha kisawa sawa kwani khasara iliyoje kwa mwenye kuacha swala! Swala ndiyo ‘amali ya kwanza mja atakayohesabiwa na kutengenea kwake ndiko kutakopelekea kutizamwa ‘amali zake nyengine la sivyo atakuwa mja huyo ni katika waliyohiliki ndani ya mashimo ya moto wa Jahannam (Allah atuhifadhi).

Pia kuacha swala kunampelekea mtu kuingia katika ukafiri kama ilivyothibiti hadithi kutoka kwa Buraydah (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Ahadi iliyopo baina yetu na baina yao (makafiri na wanafiq) ni swala, mwenye kuiacha hakika amekufuru.” Tirmidhy.

Na katika hadithi nyengine Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Hakika baina ya mtu na shirki na ukafiri ni kuacha swala.” Muslim.

Hivyo ndugu wa kiislamu khassa wale waliokuwa hawatekelezi ibada ya swala, turudini haraka kwa Mola wetu  ili tuwe miongoni mwa waislamu na tuepukane na ukafiri na adhabu kali inayotusubiri siku ya Qiyama, kama Allah anavyotukhabarisha : “Khabari za wakosefu. Ni nini kilicho kupelekeni Motoni? Waseme: Hatukuwa miongoni mwa walio kuwa wakisali.” [Mudathir 74 : 41-43].

Ama kwa wale wenye tabia ya kuswali baadhi  ya vipindi na kuacha baadhi wajue kuwa hawajasalimika na adhabu za Allah, kwani Anasema: “Basi, ole wao wanao Sali. Ambao wanapuuza Sala zao.” [Al-Mauun 107 : 4-5].

Pia kuna baadhi ya ndugu zetu wanapofikishiwa ujumbe wa kutakiwa kuswali husema: “Nitaswali vipi hali ya kuwa mifuko yangu mitupu?” au “Nitaswali vipi na tonge haijaenda kinywani” kwa kumaanisha kuwa hawatoswali mpaka wapate mahitaji yao. Watu wa aina hii wajijue kuwa ni katika waliokhasirika khasara iliyokubwa kama anavyosema Allah: “Na katika watu wapo wanao muabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo khasara iliyo wazi.” [Hajj 22 : 11].

Tunamuomba Allah atujaalie tuweze kuisimamisha ibada hii na nyenginezo na atukubalie ibada zetu zote na atuwezeshe kuingia katika pepo yake kwa Rehma Zake. Amin.

Wednesday, 4 June 2014

KUSAMEHEANA NA FAIDA ZAKE


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Kwa hakika mwanadamu ni kiumbe dhaifu sana. Na udhaifu wake huanza kuonesha kwa mola wake kwa kumuasi. Hakuna kiumbe yeyote yule anaeweza kuishi katika ulimwengu huu bila ya kumuasi Allah (subhanahu wataala). Ila Allah (subhanahu wataala) akatuwekea milango ya tawba wazi ili wale wenye kumkosea Allah waweze kurudi kwake na waombe msamaha. Vile vile udhaifu wa binaadamu anauonesha tena baina yake na binaadamu wenzake. Hakuna mwanaadamu  anaeweza kukaa na mwanadamu mwenzake bila ya kumkosea. Sote tunakoseana. Ila suala linakuja je baada ya kukosana tuache tu ? Hapana. Lazima baada ya kukosana tuombane msamaha na tusameheane ili tuyaondoshe yale yaliyomo ndani ya nyoyo zetu. Kufanya hivyo kutatufanya sisi tuweze kuishi kwa uzuri. Jambo la kusameheana baina ya watu limezungumziwa na Allah (subhanahu wataala) pale aliposema ndani ya Quraan “na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema”(3:134). Kuzuia ghadhabu zako na kumsamehe yule aliyekukosea ni katika wema na mwenye kufanya wema basi hupendwa na Allah (subhanahu wataala). Je kweli hatutaki kupendwa na Allah ? Na usipopendwa na Allah vipi utaishi katika ulimwengu huu? Vipi utaikabili akhera yako? Pia katika aya nyengine Allah (subhanahu wataala)anasema “Shikamana na kusamehe, na amrisha mema, na jitenge na majahili (wajinga)” (Al-Araaf 7: 199) .

Ugomvi uko kila sehemu na takriban kwa watu wengi sana ila tukimbilie kusameheana ili turejeshe mapenzi baina yetu. Kusamehe kuko kwa namna tatu kuu, namna ya kwanza ni kumsamehe ndugu yako yule aliyekuomba msamaha kutokana na lile alilolifanya. Pili ni kumsamehe ndugu yako hata kama hajakuomba msamaha. Na tatu ambako kuliko kuwa bora zaidi ni kumuomba wewe msamaha ndugu yako aliyekukosea wewe baada ya kuona hajui kosa lake au kwa kujua na akashindwa kukuomba msamaha.

Ndugu yangu muislamu unapomkosea ndugu yako basi kimbilia kumuomba radhi kutokana na lile ulolifanya. Kumuomba radhi muislamu mwenzako hakukushushi cheo wala hadhi. Bali hukupandisha darja zaidi na kuonesha utu na uungwana uliokuwa nao kutokana na kuufahamu vizuri uislamu wako. Pia anapokuja ndugu yako kukuomba msamaha usimrudishe bila ya kumsamehe kwa sababu sisi tunamuasi mangapi Allah tunajua kama haya ni makosa na tunamuasi ila tukirudi kwake anatusamehe. Hivyo basi na sisi tusimpe sheytwan nafasi katika kutufarakanisha.  Na wala usiwe mwenye kujinadi kwa watu kuwa wewe ni bora na ndio maana unaombwa radhi. Yote hayo tuyafanye kwa ajili Allah (subhanahu wataala). Ukiyafanya kwa ajili ya Allah hutokuwa na kiburi,wala majivuno ndani na nje ya nafsi yako.

Je ni zipi faida za waislamu kusameheana baina yetu?

1-Kupendwa na Allah (subhanahu wataala)

Allah (subhanahu wataala) anasema ndani ya Quraan “na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema”(3:134). Kuzuia ghadhabu zako na kumsamehe yule aliyekukosea ni katika wema na mwenye kufanya wema basi hupendwa na Allah (subhanahu wataala).  Na bila ya shaka muumini ndani ya ulimwengu huu huhitaji mapenzi na radhi za Allah. Hivyo katika njia ya kuzipata radhi za Allah ni kusameheana baina yetu.

2- Kujenga mapenzi ,umoja baina ya familia na kuunga udugu.

Katika matatizo makubwa yanayokumbuka familia zetu sasa hivi ni kukithiri kwa ugomvi ndani ya familia. Na bahati mbaya zaidi watu wengi hawatafuti njia za kusuluhisha bali huzidisha zaidi na kuchochea ugomvi ule. Ugomvi husababishwa aidha kwa mali,wake, watoto n.k. Ndugu zangu wa kiislamu panapotokea ugomvi baina ya familia basi pasuluhishwe ugomvi huo. Ili ugomvi huo uondoshwe. Kuweko kwa ugomvi ndani ya familia kutapelekea kukosa mapenzi baina yao, kukosa kuhurumiana baina yao na mwisho kutapelekea kukatika kwa familia ile. Na je tunajua ni ipi adhabu ya mwenye kukata ukoo ? Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema “Haingii peponi mwenye kukata udugu”  Bukhary na Muslim. Kwa hakika tunaitaka pepo ya Allah hivyo basi tuwe wepesi kuombana msamahan na tusameheane. Na ikiwa moja kati yenu hajaomba msamaha kwa kukhofia kutoipata pepo ya Allah basi muumini wa kweli anatakiwa akamfuate ndugu yake waombane msamahana wasameheane ili waweze kuondosha tofauti baina yao.

3- Kujenga na kurejesha mapenzi baina ya wanandoa.

Ndoa nazo zina dhoruba ya ugomvi wa kila mara. Panapotokezea ugomvi baina ya  wanandoa kitu muhimu zaidi ni subra. Baada ya kuwepo subra basi waombane radhi baina ya mke na mume. Kwa hakika mke au mume anapoombwa radhi na mwenzake huwa na furaha na hulainika moyo wake. Kulainika kwa moyo wake kunapelekea kutuliza ugomvi ule na kurejesha tena mapenzi baina yao. Nasaha zangu kwa wanandoa kusiwe na hata mmoja kati yao ambae atakuwa anaona tabu kumuomba samahani mwenzake. Na wala mume asijione kuwa yeye tu ndie anaestahiki kuombwa radhi. Mume akikosea amuombe radhi mkewe na mke akikosea amuombe radhi mume. Je unajua utamu wa neno samahani kwa mke au mume pale wanapokosana. Hebu jaribu kutumia fursa ya kuombana radhi kila punapokosana ili muifanye ndoa yenu iwe imara. Na inapendeza zaidi mmoja wao akimuomba mwenzake samahani huku akimpa zawadi kwa uwezo alojaaliwa bila ya kujikalifisha, au mke kumpikia mume chakula kizuri. Na wewe unaeombwa samahani usirejeshe samahani kurudi tupu msamehe kwani kusameheana ni wema katika uislamu na unapata thawabu kwa wema huo.

4- Kujenga mapenzi baina ya majirani na kupelekea kuishi kwa amani katika nyumba zetu.

Majirani wale waliokosana wasameheane kwa yale yaliyotokezea. Na msamehe jirani ikiwa amekuomba radhi au hajakuomba radhi. Jirani ana haki kubwa sana ndani ya uislamu na muislamu ajue pale jirani yake anapokosa kusalimika kutokana na maneno yake au vitimbi vyake basi hatoingia peponi kwa ushahidi wa hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)  Mtume (swalla Allaahu alayhi wasallam) aliulizwa,“Mwanamke fulani namkumbuka kwa wingi wa Swalah zake, Saumu zake na sadaka zake azitoazo lakini anawaudhi jirani zake kwa ulimi wake.Mtume (swalla Allaahu alayhi wasallam) akajibu, ‘Kwa hakika yeye ni mtu wa motoni”. Imepokea na Imam Ahmad  . Hivyo ndugu yangu wa kiislamu msamehe jirani yako kwa kosa alilokufanyia kwa kujua au kutokujua, kwa kukuomba radhi au kutokuomba radhi.

5- Kusameheana baina ya waislamu wawili kunapelekea kujiepusha na makatazo ya Allah

Kusameheana vipi kutatufanya tujiepushe na makatazo ya Allah ? Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) anasema “ Si halali kwa muislamu amhame ndugu yake wa kiislamu zaidi ya siku tatu, hata wanapokutana huyu anamgeuzia (uso) huyu na huyu anamgeuzia (uso) huyu. Na aliye mbora wao ni yule anayeanza kutoa salaam”.Bukhari na Muslim.  Na katika riwaya nyengine "Atakayemhama (mwenzake) zaidi ya siku tatu akafariki, basi ataingia motoni" Abuu Daud. Hivyo basi ndugu zangu wa kiislamu kwanza tuwe wenye kuombana radhi pale tunapokosana na pia tuwe wenye kusameheana na ikiwa ndugu yako amekukosea na kama hajakuomba radhi basi msamehe ili uwe mbali na kumuasi Allah (subhanahu wataala).

6- Kupata kivuli cha Allah (subhanahu wataala)

Haya yameelezwa na Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) pale alipowafundisha waislamu awe mwenye kumvumulia ndugu yake muislamu kutokana na deni au amsamehe basi atapata kivuli siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila cha Allah. Imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah(radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtume  wa Allaah (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: "Atakayemuakhirishia mwenye usiri (wa kulipa deni) au akamsamehe, Allah Atamfunika kivuli Siku ya Qiyaamah chini ya kivuli cha Arshi yake, siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli Chake. Attirmidhy. Na Allah (subhanahu wataala) anasema “Na ikiwa (mdaiwa) ni mwenye hali ngumu, basi (mdai) angoje muda wa kufarijika (anayemdai).  Na  mkitoa swadaqah (deni mnalodai)  basi ni kheri kwenu mkiwa mnajua” (2:280).

Mwisho kabisa nimalizie mada yangu kwa kisa kinachotufunza kuhusu kusameheana.

Vijana watatu walikwenda mbele ya Khalifa  wa  Waislamu Umar bin Al Khattab (Radhiya Llahu anhu) wakiwa wamemkamata mtu waliyemfunga kamba. Wakasema kumwambia Umar (Radhiya Llahu anhu):

"Mtu huyu amemuuwa baba yetu na amekiri juu ya jambo hilo, isipokuwa ametuomba tumpe siku tatu ili aweze kusafiri kwa wanawe kwa ajili ya kuwajulisha juu ya hazina aliyoifukia mahala ambapo hapana anayepajuwa isipokuwa yeye peke yake". Sahaba mmoja aitwae Abu Dhar Al Ghafariy (Radhiya Llahu anhu) akamdhamini mtu huyo juu ya kuelewa kwake vizuri kuwa iwapo mtu huyo hatorudi basi atauliwa yeye badala yake. Mtu huyo hakurudi mpaka baada ya kukaribia sana kumalizika muda wa siku tatu hizo, na watu wakawa na wasi wasi asije Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu) akauliwa badala yake.

Dakika za mwisho za siku ya tatu akawasili mtu huyo akiwa amejaa vumbi na huku uso wake ukionesha dalili za kuchoka sana. Umar (Radhiya Llahu anhu)akamuuliza: "Ilikuwaje ukarudi wakati ungeweza kukimbia?" Akajibu: "Nilihofia pasije pakasemwa kuwa; Watu wenye ahadi za kweli hawapo tena."

Kisha Umar (Radhiya Llahu anhu)akamgeukia Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)na kumuuliza: "Na wewe ilikuwaje ukakubali kumdhamini mtu huyu wakati humjuwi?" Abu Dhar (Radhiya Llahu anhu)akasema: "Nilihofia pasije pakasemwa; Wakarimu na wenye moyo wa kishujaa hawapo tena."

Ndipo wale vijana watatu wakasema: "Na sisi tumemsamehe mtu huyu ili pasije pakasemwa; 'Hawapo tena watu wenye kusamehe juu ya kuwa na uwezo wa kulipa kisasi."

Familia,majirani,marafiki au baina ya waislamu ombaneni msamaha na kila mmoja amsamehe mwenzake kwa yaliyopita. Na yafanyeni hayo kwa ajili ya Allah (subhanahu wataala).

Allah atujaalie tuwe kuyafahamu haya yote tuliyoyaeleza. Na tuchukue manufaa yake kwa kusameheana baina yetu ili tuweze kuishi kwa mapenzi na salama baina yetu. Aaamin

Monday, 2 June 2014

KUUNGA UDUGU KATIKA UISLAM


Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Makala yetu itazungumzia suala zima la kuunga udugu katika uislam. Tambua ewe ndugu yangu muislam ya kuwa udugu upo wa namna mbili. Nao ni :
1-Udugu wa Kiimani
2-Udugu wa damu.
Udugu wa kiimani ni ule ambao unatukutanisha pale tunapokiri ya kuwa hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah na Muhammad ni Mtume wa Allah.Allah subhanahu wataala amesema “..Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.”( 49:10)
Ama udugu wa pili ni udugu wa damu ambao ndio niliopenda kuuzungumzia leo kwa Tawfiq ya Allah Subhanahu Wataala.

Uislam ni dini ambayo imetuwekea mfumo wa kiibada kuanzia kuzaliwa kwetu mpaka kufa kwetu na hili ni kwa kutambua kuwa lengo letu kuu hapa duniani ni kumuabudu Allah na si vinginevyo.Kwa kutambua hilo, Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam ametufundisha ibada kimatendo na kimaneno katika kila kipengele cha maisha yetu ili tupate kuutumia vizuri uhai wetu na tusiwe katika watakao juta siku utakapo katika uhai huu. Na katika ibada hizo miongoni mwao ni hii ya kuunga udugu.

Kuunga udugu ni ibada iliyojengeka kimaneno na kivitendo. Ni miongoni mwa ibada ambayo imetiliwa mkazo kwa malipo mengi kwa mwenye kuifanya na vilevile kuahidiwa kwa adhabu kali kwa mwenye kuiacha. Kwa masikitiko makubwa wengi wetu tumekua tukiipuuza ima kwa kujua au kutojua. Allah Subhanahu Wataala anasema “ Muabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri” (4:36).

Aya hii imeanza kwa kutaja Tawhiid kisha kufuatanishwa na suala la kuunga udugu nako ni kuwafanyia wema wazazi na ndugu wa karibu. Hii ni kuonyesha nafasi kubwa ya ibada hii na ikaonyesha pia kuwa mwenye kulipinga jambo hili Allah anamchukia kwani hua ana kibri na ni mwenye kujifakharisha.

Umuhimu wa Kuunga Udugu

Kwanza ni alama ya kuwa na Imaan. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam : ((..Na mwenye kumuamini Allah na Siku ya mwisho basi na aunge udugu wake..)) Bukhari na Muslim.

Pili kuunga Udugu ni miongoni mwa matendo anayoyapenda Allah Subhanahu Wataala. Aliulizwa Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam, Ni amali gani bora mbele ya Allah? Akajibu ((Swala kwa Wakati wake)) akaulizwa tena kisha ipi? Akajib ((Kuwafanyia wema wazazi)) kisha ipi?? Akasema ni Jihaad katika njia ya Allah)) Bukhariy na Muslim.

Tatu ni sababu ya kuongezewa Rizki na Umri. Amesema Mtume Swalla Llahu Alayhi Wasallam: ((Mwenye kupenda kukunjuliwa katika rizki yake na kuongzewa Umri wake, basi na aunganishe udugu wake)) Bukhary na Muslim.

Nne ni sababu ya kuingizwa peponi.Kuna Mtu alimfata Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam akamwambia, Ewe Mtume wa Allah nijulishe jambo ambalo litaniingiza peponi,akasema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam : (( Muabudu Allah Usimshirikishe na chochote, Simamisha Swala, Toa zaka na Unga Udugu)) Bukhari na Muslim.

Je Vipi tutauunga udugu ?

Zipo njia nyingi za kuunga udugu ila nitazungumzia kwa ujumla tu kama kwa kuwatembelea wakiwa wazima au wagonjwa, kuwasaidia wanapopatwa na shida, kuwaheshimu, kuwafurahisha kwa kila njia kwa maneno na vitendo kama kuwapa maneno mazuri na pia kuwapa zawadi na mengine mengi yanayopendwa na familia yako pendelea kuwafanyia kwa kadri ya uwezo wako.

UBAYA WA KUVUNJA UDUGU

1..Hulaaniwa na Allah. Amesema Allah Subhanahu Wataala “ Basi yanayo tarajiwa kwenu mkitawala ndio mfisidi katika nchi na muwatupe jamaa zenu? Hao ndio Mwenyezi Mungu alio walaani, na akawatia uziwi, na akawapofoa macho yao.” ( 47 :22-23).

2..Haingii peponi mwenye kukata ukoo. Amesema Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam. ((Haingii peponi mwenye kukata udugu) Bukhary na Muslim.

Tunapoongelea kuunga udugu wazazi tusiwasahau kuwa wao ndio wenye nafasi ya kwanza..kama anavyosema Mtume Swalla ALlahu Alayhi Wasallam: ((Ameangamia mtu, Ameangamia mtu,
Ameangamia mtu...Mwenye kuwakuta wazazi wake wapo hai, mmoja wao au wote wawili na hakuingia peponi.)). Hadithi hii inaonyesha ni namna gani uislam unavyohizima kuwafanyia wema wazazi wetu kiasi ya kwamba Mtume Swalla Allahu alayhi wasallam amesisitiza maangamizo yake mara tatu. Na pia katika sUala la kuunga udugu tunatakiwa tuunge udugu hata bila ya kuangalia kama wazazi au ndugu zetu ni waislam au laa... ni wema au waovu..kama anavyotusimulia Bibi Asmaa bint Abubakar radhi za Allah ziwe juu yao. Anasema "Alinijia mama yangu hali ya kuwa ni mshirikina katika enzi za Mtume, Nikamtaka ushauri Mtume Swalla Allahu Alayhi Wasallam; Amenijia Mama yangu nae ni mwenye shida, Je nimuunganishe ? Akasema (( Muunge Mama yako)) Bukhari na Muslim. Na maana ya kumuunga yani nimtendee wema..

Baada ya kuona faida za kuunga udugu na ubaya wa kuacha kufanya hivyo. Nitapenda kumalizia mada hii kwa kuwakumbusha na kuwatanabahisha mambo ambayo huvunja udugu ili tupate kuepukana nayo. Miongoni mwa hayo ni :

a- Kutojua fadhila za kuunga udugu na adhabu za kuvunja udugu.
b-Kibri
c-Choyo na Ubakhili
d-Husda
e-Talaka
f-Kuoa au kuolewa na mume au mke muovu ambae atakuzuia kuwa karibu na ndugu zako.
g- Mali.
h-Kazi.
i-Masafa baina yako na familia yako.

Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayosababisha watu kuvunja udugu Allah atujaalie tuwe ni wenye kuunga udugu wetu ili tupate malipo hapa duniani na kesho akhera. Na wale ambao wamehasimiana basi waondoshe tofauti zao na tujue kuwa kuunga ukoo ni amri kutoka kwa Allah. Takriban kila familia siku hizi za kiislamu watu huhasimiana na wanasahau kuwa kuunga udugu ni katika amri zake Allah subhanahu wataala.
Tunamuomba Allah atujaalie miongoni mwa wale wanaoambiwa mema na kuyafanyia kazi na kukatazwa maovu na kuywacha. Aaamin.

*Msitusahau kwenye dua zenu**

NA ALLAH NDIE MJUZI ZAIDI.

USISAHAU KUSAMBAZA UJUMBE HUU