Wednesday, 2 July 2014

TUNAKUOMBA UDHURU RAMADHAN


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Ni wajibu wetu kuiomba msamaha Ramadhan na ni haki yake kutusamehe au kututosamehe,kukubali udhuru wetu au kuukataa udhuru wetu.

Kwanini tuiombe msamaha Ramadhan? Ni kwasababu ilipokuja mwaka jana, tuliazimia kufanya mengi, na baada ya kutushinda kuyatekeleza, tukaazimia kuyafanya tena mwaka huu, na kujiapiza kua tutayatekeleza kwa hali yoyote ile. Lakini ndio hiyo inaendelea kwenda kumalizika bila ya kutekeleza hata nusu ya tuliyoyaazimia.

Tunarejea makosa yaleyale tuloyayafanya Ramadhan zilopita. Tunarejea kukosa sala za jamaa, na kutosheka mtu kusali ndani ya wakati tu,tunarejea kosa la kuzungumza maneno maovu, na kusahau kua tunatakiwa tusifunge matumbo yetu tu, bali hata midomo yetu na viungo vyenginevyo. Tunarejea tena kosa la kutosoma Qur-an, na anaesoma hazingatii maana yake.

Je tunajua kwanini tunashindwa kuyatekeleza hayo yote na kutoipa Ramadhan haki yake? Ni kwasababu moja tu; na si nyengineo nayo ni kua TUNATAKA KUFANYA MAMBO AMBAYO HATUKUZOEA KUYAFANYA KABLA YA RAMADHAN. Hatukuzoea kusimama usiku kusali alau rakaa moja ya witri. Hatukuzoea kusoma Qur-an alau juzuu moja kwa siku, na tukakhitimisha baada ya mwezi,hatukuzoea kukaa miskitini katika vikao vya kheri na kusikiliza darsa,na hatukuzoea kusali sala za sunnah, hivyo tunashindwa kudumu na tarawehe. Hatukuzoea kua na khushui ndani ya swala hivyo hata anaeswali tarawehe na sala za usiku haathiriki na kinachosomwa kwani akili haipo, na ipo kwenye mechi ya leo nani atakua mshindi. Hatukuyazoea yote hayo na ndio yanatushinda kuyafanya, na anaefanya hushindwa kudumu nayo.

Tunahitaji kuiomba radhi Ramadhan kwa sababu kwa wengi imekuja wakati sio, kwani tumeghafilika na kutizama kandanda, na kupanga mechi, hivyo hatuhitaji kushughulishwa na jengine. Na hivyo ndivyo itakavyokua hali mpaka kinapomjia mtu kiama chake kidogo, (kutokwa na roho) au kikubwa atakua ameghafilika. Amesema Allah subhanah katika Suratul-Anbiyaa aya ya 1-3 “IMEWAKARIBIA WATU HESABU YAO, NA WAO WAMEGHAFILIKA NA KUPUUZA.HAYAWAJII MAWAIDHA MAPYA KUTOKA KWA MOLA WAO, ILA HUYASIKILIZA HALI YAKUA WANACHEZA. ZIMEGHAFILIKA NYOYO ZAO………..”. Hivyo Ramadhan una haki kutusamehe au kutotusamehe, lakini udhuru wetu ndio huo.

Amesema Mtume rehma na amani ziwe juu yake kuwabashiria maswahaba zake ilipoingia Ramadhan:“Umekujieni mwezi wa Ramadhan,mwezi wenye Baraka. Mumefaradhishiwa ndani yake Funga.Milango ya pepo hufunguliwa, na kufungwa ya moto. Ndani yake kuna usiku bora kuliko miezi elfu,atakaeharamishiwa kheri za usiku huo basi uyo ameharamishiwa. (kikweli kweli ameharamishiwa kheri zote)” (Nasai).

Jee sisi tunabashiriana kwa lipi? Au tunabashiriana kwa ushindi wa timu zetu? Amesema Mtume wa Allah katika hadith inayosimuliwa na Jaabir “Pua lake lirambe mchanga, (amepata hasara), anaeidiriki Ramadhan, kisha asisamehewe dhambi zake” . Lakini Jee kusamehwa dhambi ni kwa kila mtu atakaefunga?. Laa hasha wa kalla. Yule atakaefunga kwa Imani na kutarajia malipo, akajiepusha na mambo ya kipuuzi na kusema maneno yasiyokua ya kheri, huyo ndio iliyokamilika funga yake, kwani ameyafunga na kuyazuia matamanio ya tumbo lake,utupu wake, ulimi wake na viungo vyenginevyo.

Hivyo ndivyo walivyokua waja wema waliotangulia kuanzia maswahaba matabiina na wengineo,kwao wao mwaka mzima ulikua Ramadhan. Walijiandaa kuipokea Ramadhan, na wakimuomba Allah miezi sita awafikishe Ramadhan, na miezi sita baadae kuomba wakubaliwe waloyoyatenda Ramadhan.Walijua thamani ya funga itoshe hadithi ya Rasuul kua “Atakaefunga siku moja katika njia ya Allah, ataepushwa na moto mwendo wa miaka sabini”(Muttafaqun alayhi).

Walidumu na funga si za Ramadhan tu, bali na za Sunnah. Ramadhan waliipa haki yake, na ndipo wakaweza kufunga na za Sunnah. Sayyidina Uthmaan radhia Allahu anhu ameuwawa hali ya kua amefunga, na alikua akisoma Qur-an, ni kweli mtu hufa kwa amali aloizoea kuifanya.

Inasimuliwa kua Ibnu Umar yeye na baba yake radhia Allahu anhuma walikua hawafungi wanapokua safarini, na walikua hawali wanapokua nyumbani ,zaidi ya siku zilizoharamishwa kufunga. Lakini jee sisi tunaweza hayo au ndio tunatamani Ramadhan iishe ili jukumu la kufunga lituishie? Wengine kufikia kusingizia maradhi ya vidonda vya tumbo, ili tusifunge. Tumesahau kua aliefaradhisha Funga, ni mwenye kusikia na mwenye kuona, na anajua kila kitu,hakifichiki kwake kitu kama anavosema “…Na anajua yaliyomo barani na baharini,na halianguki jani ila anajua,wala punje katika giza la ardhi(ila anajua)…” (An-am :59).

Wengine wakafikia kuhama miji yao, na kwenda miji ya makafiri kwa kukimbia funga.Kwa kweli tunahitaji kuiomba radhi si ramadhan pekee bali na aloileta Ramadhan.

Allah ameeleza Lengo la kutufaradhishia funga, na si jengine zaidi ya kutaka tuwe wacha-mungu, kwa maana nyengine tumuogope yeye subhaanah,lakini je tumelifikia lengo hilo? Ramadhan ngapi zishapita na bado hatujalifikia lengo hilo. Kiukweli tunahitaji kuiomba msamaha Ramadhan.

Ramadhan ni mwezi ulioteremshwa Qur-an, na fadhila za kusoma Qur-an tumeona katika makala mbali mbali na kuzungumizwa na masheikh wengi, lakini Je tumezingatia fadhila hizo au ndio tuko na mashughuli ya kidunia na kusahau Akhera?. Kiasi Mtume wa Allah atushtaki pale aliposema “Na akasema Mtume:Ewe Mola wangu,hakika watu wangu wameihama Qur-an” (Fur-qaan 30). Na sisi hatufai kutushtakiwa kwa kuihama Qur-an tu, bali tunahitaji kushtakiwa kwa kutoipa hadhi yake stahiki Ramadhan.
Ramadhan ni mwezi wa maghfira,na toba na kuwachwa huru na moto. Lakini je tumayakimbilia haya?
Ramadhan ni mwezi wa subra na sadaka, na kuhurumiana baina ya watu na kuunganisha koo Lakini jee tunayafanya haya?

Ramadhan ni mwezi kushkuru na kuomba dua, na ndio mwezi wa ushindi,kwa waislamu kama tutakavyoona katika mada ya “Matukio muhimu ndani ya Ramadhan,”basi kwa nini wasifurahi waumini kwa hili na wanafurahia mengine?

Ramadhan ni mwezi wa adhkaar,itikafu,qiyamul-layl,tarawehe na kuengezewa mema na kufutiwa madhambi. Tunayafanya haya? au ndio tumeigeuza kuwa ndio mwezi wa kula na kunywa na kuchezacheza. Amesema Allah kumwambia Mtume wake “Waachie wale, na wacheze na yawapoteze matamanio na karibuni watajua”(Hijri 3). Tumeilizangatia onyo hili? Kwani ndo hali yetu wengi,tunakula,tunakunywa na kuchezacheza.

Maswahaba waliyafahamu haya, na ndio wakaipa Ramadhan thamani stahiki. Waliufahamu wasia wa Mjumbe wa Allah, na kama alivyosema swahaba wake mtukufu Abu-Dardai radhia Allahu anhu nilikua mfanya biashara mashuhuri, niliekua na mafanikio katika biashara zangu alipotumwa Muhammad, nikaona biashara na ibada haviendani, (kutokana na mishughuliko ya kibiashara) nikaamua kuchagua ibada na kuacha biashara. Amesema kweli Allah pale alipowasifu watu kama hawa na mfano wake: “Wanaume ambao haiwashughulishi biashara wala mauzo,(kuwasahaulisha) kutokana na kumkumbuka Allah,na kusimamisha sala,na kutoa Zakka,na wanaiogopa siku zitakapobadilika nyoyo na macho (Qiyamah)”( Nuur 37) .
Hii ndo ilikua hali yao, basi ni ipi hali yetu ? Jee sisi tumechagua nini; Ramadhan au Mashughuliko ya kidunia? Tusameh Ramadhani

No comments:

Post a Comment