Saturday, 19 July 2014

HALI ZA WEMA WALIOPITA NDANI YA RAMADHAN

Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Kutoka kwa Abi Hurayra (radhiya Allahu anhu), Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ““Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”. Bukhari na Muslim.

Katika makala hii leo tutaelezea vipi Mtume (swalla Allahu alayhi wasalla), maswahaba,matabiina na wema wengine waliopita walivyokuwa wakiuthamini mwezi wa Ramadhan. Na vipi walikuwa wakijitahidi katika kufanya ibada ndani ya Ramadhan ili waweze kufikia malengo ya Ramadhan pamoja na kupata ujira mkubwa kutoka kwa Allah (subhanahu wataala) ikiwemo kusamehewa dhambi zao zilizopita.

Wengi wetu tunafunga ila bidii inayotakiwa ambayo tuifanye ndani ya Ramadhan hatuioneshi au haitoshelezi na ndio maana kila mwaka tunafunga na hatuoni matunda ya funga zetu wala hatuoni raha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa ni mwenye kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kufunga sana ndani ya mwezi wa Shaaban. Pia unapoingia mwezi wa Ramadhan alikuwa ni mwingi wa kufanya ibada na zaidi huzidisha pale linapoingia kumi la mwisho pia hukaa iitikafu. Amesema Bibi Aisha (radhiya Allahu anha) "Zilipokuwa zikiingia siku kumi za mwisho (za Ramadhan), Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akiuhuisha usiku kwa kufanya ibada, akiamsha familia yake usiku, na akikaza Izaar yake (shuka inayovaliwa kiunoni makusudio hapa ni kuwa alikuwa akijibidiisha sana). Bukhari na Muslim.
Pia  imepokewa kutoka kwa Aisha (Radhiya Allaahu anhaa) kwamba: Mtume (swalla Allaahu alayhi wa sallam) alikuwa akifanya Itikaaf kila Ramadhaan siku kumi, ulipofika mwaka wake wa kuaga dunia alifanya Itikaaf siku ishirini" Bukhari

Pia  alikuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) akisoma Quraan pamoja na kuja kusomeshwa Quraan na mwalim wake Sayydina Jibri. “Mtume (Swalla Allaahu alayhi waaalihi wasallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) kwa watu, na alikuwa mbora zaidi katika Ramadhan kwa sababu Jibril alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhaan akimfundisha Qur-aan” Al-Bukhaari

Huyu ndie aliekuwa kipenzi cha Allah (subhanahu watala) akifanya matendo kama hao. Kipenzi ambae ameshasamehewa dhambi zake zilizopita na zijazo. Je vipi mimi na wewe?

Vipi yalikuwa mapokezi ya wema waliopita kwa ajili ya Ramadhan? Wema waliopita walikuwa wakiupokea mwezi wa Ramadhan kwa furaha pamoja na maandalizi mazuri na makubwa ya kuupokea mwezi mtukufu wa Ramadhan.  Anasema Muala Ibn Fadhwal “ Walikuwa watu wema miezi sita wakimuomba Allah (subhanahu wataala)  awafikishe Ramadhan ”

Wema waliopita walizifahamu hadithi hizi na ndio maana nao walijibidiisha katika kufanya mazuri ndani ya Ramadhan. Dua zao njema walizielekeza kwa Allah (subhanahu wataala) awafikishe mwezi wa Ramadhan wakiwa ni wazima ili waweze kufunga na kutekeleza ibada mbali mbali ndani ya Ramadhan. Pia walikuwa wakimuomba Allah (subhanahu wataala) daima wawe katika uongofu ili isije ikaingia Ramadhan na wao hawako katika utiifu wa Allah (subhanahu wataala). Pia wakimuomba Allah (subhanahu wataala) awatakabalie saumu zao watakazokuja kuzifunga.

Ukiangalia ni namna gani ambavyo walikuwa wakiuthamini mwezi huo. Mtu huanza kuupokea kwa dua za kumuomba Allah awafikishe miezi sita kabla ya kuingia Ramadhan na miezi iliyobaki hujibidiisha na kufanya Ibada. Sisi umma wa sasa tunasubiri karibu Ramadhan kufika ndio tunaanza kujiandaa nao tena kwa kuwaza vyakula tena kufanya israfu na sio vipi mtu atajipanga kwa ajili ya Ibada.

Wema waliopita waliitumia Ramadhan kwa kufanya matendo mema. Matendo yale yale ambayo alikuwa akiyafanya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) kwani walifahamu kuwa kigezo chao ni Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) na wakajibidiisha katika kumfuata.

Sasa tuangalie mifano hai vipi waliingia kwenye milango ya Kheri ya ndani ya Ramadhan :

Kusoma Quraan

Mwezi wa Ramadhan ni mwezi wa Quraan na ndio mwezi ambao imeteremshwa Quraan. Mtume(swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa mwingi wa kusoma Quraan ndani ya Ramadhan na  wema waliopita walitumia Ramadhan kwa kusoma Quraan.

Sayyidina Othmaan Ibn Affan alikuwa akimaliza msahafu kila sik umara moja.
Az zuhr mmoja ya wema waliopita wakati ilipokuwa ikiingia Ramadhan alikuwa akiacha kusoma hadithi na elimu nyengine alikuwa akiutumia muda wake wote kuisoma Quraan.

Qatadah alikuwa akimaliza kusoma Quraan kikawaida kila siku 7 mara moja lakini ndani ya Ramadhan kila baada ya siku 3 mara moja.

Kusali sala za Usiku

Kama tulivyoona kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa ni mwenye kusali usiku na alikuwa akiwaamsha watu wake katika kumi la mwisho. Ummul Muuminina Aisha (Radhiya Allaahu anhaa):“Msiwache kuswali usiku (Qiyaamul Layl), kwani hakika Mjumbe wa Allah (Swalla Allaahu alayhi waaalihi wasallam) alikuwa hawachi kuswali usiku, na alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama anaumwa au anaona uvivu huswali kwa kukaa.” Imepokelewa na Ahmad.

Hivyo hivyo na watu wema nao walimfuata Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam). Amepokea Zayd bin Aslam kutoka kwa baba yake kuwa:“Alikuwa Umar bin Al-Khattwaab (Radhiya Allaahu anhu) akiswali usiku  Anavyomjaaliya Allah, hadi inapokuwa Aakhirul Layl -mwisho wa usiku– huwaamsha ahli zake kwa Swalah; huwaambia: Swalah Swalah, kisha husoma Aayah hii: “Na waamrishe watu wako Swalah, na ufanye subira kwa hayo. Sisi hatukuombi wewe riziki, bali Sisi ndio tunakuruzuku. Na mwisho mwema ni kwa mcha Mungu” (Twaahaa: 132). Imepokelewa na Maalik, katika Al-Muwattwa

Na katika Hadiyth ya nyengine ya Abdullaah bin Abi Bakr (Radhiya Allaahu anhu) amesema: Nimemsikia baba yangu Abu Bakr (Radhiya Allaahu anhu)- akisema:” Tulikuwa tukimaliza -Qiyaam- katika Ramadhaan basi tunawaharakisha wasaidizi kwa chakula kuchelea Alfajiri (isitukute)” Imepokelewa na Maalik katika Al-Muwattwa.

Kutoa Sadaka na Kumfturisha aliyefunga

Siku moja Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wasallam) aliulizwa Swawm ipi bora baada ya Ramadhaan? Akajibu: “Shaban… pakaulizwa Sadaka ipi bora? Akajibu: “Sadaka katika Ramadhaan” .Imepokelewa na At-Tirmidhiy.

Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam): “Atakayemfuturisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake -aliyefunga- bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga.” Imepokelewa na Ahmad

Masahaba na wema waliopita walijitahidi sana katika kutoa sadaka pamoja na kuftarisha wenziwao kwa kujua fadhila na utukufu wa jambo hili.

Imepokewa Abu As-Siwar Al adwi amesema “ Kundi la wanaume katika kabila la la Bani Adi walikuwa wakisali msikitini. Na hakukuwa na hata mmoja aliyekuwa akifungua peke yake. Akimuona mtu wa kula pamoja nae alikuwa anakula pamoja nae na ikiwa atakosa basi anakwenda na chakula chake msikitini ili ale chakula chake pamoja na wenzake.

Huu ni kwa uchache vipi watu wema walikuwa wakijibidiisha katika kupata matunda ya mwezi wa Ramadhan.

Nasaha kwako ewe msomaji jitahidi kuiga mifano hii ya watu wema ili nawe uwe ni mwenye kupata matunda ya mwezi wa Ramadhan kwa uwezo wake Allah (subhanahu wataala).

No comments:

Post a Comment