Saturday, 19 July 2014

KWA NINI HATUATHIRIKI NA FUNGA ZETU?

Makala Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Allah (subhanahu wataala) ametufaradhishia juu yetu kufunga. Na pale alipotufaradhishia akatuambia kuwa lengo kuu la kutufaradhishia funga ni kupata uchamungu(Taqwa). Pale aliposema “Enyi mlio amini! Mmeandikiwa Saumu, kama waliyo andikiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuchamngu.”(2:183).
Analolisema Allah (subhanahu wataala) lazima tuliamini na mwenye kuwa na shaka na kauli za Allah (subhanahu wataala) basi huyo anatoka kwenye uislamu. Funga kwa uhakika lengo lake ni kutufanya sisi tuwe wachamungu. Lakini masuali ya kujiuliza Je kweli tunakuwa wachamungu? Je tunaathirika na funga zetu? Malengo mengine ya saum Je tunayafikia?

Majibu ni wachache wenye kufikia hayo na kutambua hayo. Ila ni yapi hasa matatizo yanayotufanya tusifikie malengo ya funga?. Leo katika makala hii tutaelezea miongoni mwa sababu ambazo zinapelekea waislamu kutopata matunda ya funga zetu na kutoathirika nazo.
Ama sababu zwenyewe ni :

1-KUTOWEZA KUTAMBUA THAMANI YA MUISLAMU KUIDIRIKI RAMADHAN
Mwanadamu anapojua thamani ya kitu huwa ni mwenye kukithamini kitu kile pia na kuwa na tahadhari ya juu ili kitu kile kisiweze kupata madhara. Chukulia mfano mtu amepata Almasi vipi atakuwa mwenye kuithamini? Kwa vile anajua thamani ya almasi ni kubwa hivyo atakuwa na tahadhari ya hali ya juu asije kuitupa hali kadhalika atakuwa ni mwenye furaha kwani anajua kuwa almasi ile inaweza kuwa sababu ya kuondoka umasikini wake.

Tuje kwenye Ramadhan wengi wetu hatujui thamani ya Ramadhan na ndio maana hatuuthamini au wenye kujua thamani ya mwezi huo basi hawaupi ile thamani inayostahiki. Nizungumzie mawili tu katika mengi ambayo tunayapata ndani ya Ramadhan. La kwanza ni usiku wenye cheo. Anasema Allah (subhanahu wataala) “Hakika Sisi Tumeiteremsha (Qur-aan) katika Laylatil-Qadr (usiku wa cheo). Na nini kitakachokujulisha ni nini huo (usiku wa) Laylatul-Qadr? (Usiku wa) Laylatul-Qadr ni (usiku) mbora kuliko miezi elfu Wanateremka humo Malaika na Ruwh (Jibriyl) kwa idhini ya Mola wao kwa kila amri (jambo). (Usiku huo ni) Amani mpaka kuchomoza Alfajiri. (Al-Qadr: 97). Ni nani asiyeutaka usiku huu umkute ikiwa yumo ndani ya Ibada? Tunatambua uzito wake ila hatuoneshi thamani yake kivitendo. Bali vitanda vyetu ndivyo tunavyovithamini.

Ama jambo la pili ni kutoka katika hadithi sahihi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) iliyopokelewa na Bukhari,Muslim na Nasai Rahimahumullah na kusimuliwa na Abu-Hurayra radhiallahu anhu :“Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”.

Wako wasiyoyajua haya ndio maana hawauthamini na wako wenye kujua ila hawafanyi bidii za kuonesha thamani ya mwezi wa Ramadhan.
Hivyo basi Yule mwenye kutaka kupata uchamungu basi kwanza authamini. Na kuuthamini kwenye kuwe kwa vitendo vyema na ibada hapo ndipo mja ataweza kufikia lengo la funga.

2-KUTOJIANDAA NA KUIPOKEA MWEZI WA RAMADHAN

Ramadhan inahitaji maandalizi. Maandalizi yanayoihitaji kwanza ya kielimu. Ni lazima mwenye kutaka kufunga ajue nguzo za funga,yanayobatilisha funga,yaliyo sunna kwa mwenye kufunga. Mambo haya mtu akiyajua basi alau atakuwa anajua nini anachokifanya ndani ya funga.

La muhimu zaidi katika yaliyosahaulika na ni ambalo lenye kufunguza ajue maneno machafu na kusema uongo pia nayo yanafunguza.. Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) inayosema " Yule ambae haachi kusema uongo na haachi vitendo viovu. Allah (subhanahu wataala) hana haja na funga yake." Bukhari na Muslim. Ikiwa mwenye kufunga hayajui haya vipi ataweza kuyachunga ikiwa kusema uongo ni haramu halafu yeye ndio imekuwa ada yake? Vipi unadhani mtu kama huyu anaweza kufikia malengo ya funga?

Maandalizi mengine ni ya kimwili. Wako baadhi ya watu miili yao imeshalemaa haiwezi kabisa kuamka usiku. Haiwezi kabisa kuacha vitanda na kumuabudu Allah (subhanahu wataala) katika thuluthi ya mwisho ya usiku. Lazima mwanadamu auzoeshe mwili wake kutopenda kitanda na awe ananyanyuka kusali usiku kabla ya Ramadhan kuingia ili ramadhan ikifika awe ni mwenye kuendelea tu na ibada.

Jambo hili la maandalizi wengi wetu yamekuwa ni madogo bali tumekuwa ni wazuri wa kujiandaa na vyakula na nguo za sikukuu na tunaisahau kabisa Ramadhan. Tusikubali kutekwa na nafsi zetu lazima turejeshe mioyo yetu kwa ajili ya kupata kheri za Ramadhan.

3-KUTOKUWA NA MAAMUZI YA KIUKWELI YA KUBADILIKA NAFSI ZETU

Maamuzi ya kikweli yanakosekana ndani ya Ramadhan. Mtu husema ndani ya nafsi yake Ramadhan hii ikifika nataka nijibadilishe kabisa. Lakini maneno haya huwa ni kutoka katika ulimi tu ila ndani ya moyo huwa hayapo.

Mwenye kutaka kubadilika kwa haki basi lazima atakuwa na bidii ya hali ya juu. Na mwenye kujitahidi katika njia ya Allah basi lazima atafanikiwa. Allah (subhanahu wataala) anasema “Na wanao fanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema” (Ankabut : 69).

Maneno ya Allah ni ya kweli na daima yataendelea kubakia kuwa ni ya kweli. Suali la kujiuliza ikiwa Allah (subhanahu wataala) ametuambia hayo je kweli sisi tunayo dhamira ya kweli katika kubadilika? Au kutaka kubadilika kwetu huwa ni maneno tu kutoka katika vinywa vyetu na sio kutoka ndani ya nyoyo zetu?

Vipi mwenye kutaka kubadilika bado anaendelea kuyafanya yale ya haramu anayotaka kuyawacha. Vipi mwenye kutaka kubadilika bado anaendelea kukaa na marafiki waovu? Vipi mwenye kutaka kubadilika hajihimizi na vikao vya kheri,kusoma Quraan?

Mwezi wa Rehma wenye fadhila nyingi ni miongoni mwa sababu kubwa ya kumfanya mja aweze kubadilika. Tusikose kuitumia fursa hii kwani hatujui kuweza kufika ramadhan ijayo.

4-KUJISHUGHULISHA ZAIDI NA DUNIA NA KUSAHAU IBADA

Unapoingia mwezi wa Ramadhan muislamu lazima ajipange vizuri ili adumishe ibada. Ila sisi dunia imetuteka na ndio maana hatufikii malengo ya funga. Mfanyabiashara anajua ndio mwezi wa kuchuma pesa akili yote ipo katika kuutafuta mzigo wa kuuza, wengine ndio wanaona mwezi wa kuwakomoa watu na bei. Wanunuzi nao wanawaza kwenda kununua na ndio maana kwenye maduka watu wanajaa katika mwezi  wa Ramadhan.

Sisemi watu wasinunue na wasiuze bali wajipangie vizuri ili wapate na alau muda wa mtu kufanya ibada. Mfanyabiashara daima ajiweke vizuri mapema kabla ya kuingia Ramadhan ili ikifika ramadhan asiwe mwenye kushughulishwa. Na mnunuzi nae ajipangie vizuri. Unapohangaika kutwa nzima bila ya kupumzika basi usidhanie kama utapata alau muda wa kumuabudu Allah kwani machofu yatatawala katika mwili wako.
Pia mambo yote ya haramu tunayaweka usiku baada ya kumaliza kuftari. Sasa vipi mtu anafunga lakini baada ya funga tu magharibi anayakimbilia maasi. Huku ni kuipenda dunia na kusahau akhera.
Tusipe thamani kubwa dunia itatupeleka pabaya enyi ndugu zangu wa kiislamu. Daima tuwe wenye kujishughulisha na ibada kwani ndizo zitakazotufaa siku ya Qiyama.

5-KUPOTEZA WAKATI KATIKA MAMBO YASIYOKUWA NA MSINGI

Wakati ni jambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu ndio maana Allah (subhanahu wataala) ameapa na wakati ndani ya sura mbali mbali. Mwanadamu unapokwisha wakati wake wa kuishi duniani ndio mauti yake yamefika na anaondoka katika dunia.

Ni wachache kati yetu wenye kujua thamani ya wakati na kuutumia vizuri wakati wetu. Wengi kati yetu tumekuwa ni wenye kuupoteza wakati wetu katika mambo yasiyokuwa na maana. Funga na malengo yake ili tuweze kupata fadhila zake na kufikia malengo yake ni lazima tuutumie wakati wetu katika kheri kwa kufanya ibada na kusoma Quraan,na ibada nyengine za kheri.

Sasa ikiwa tunafunga ili tufikie lengo la kumcha Allah (subhanahu watala), kwa nini waislamu wanatumia wakati wao katika michezo ya kipuuzi ikiwemo kuangalia mipira, kuangalia sinema zisizokuwa na maana, kucheza makeram, karata, zumna nk. Sasa vitu hivi vinatupelekea kusahau lengo  la funga kwa sababu ya kupoteza wakati mwingi katika mambo hayo. Kwani wakati huo ungetafuta la kheri ungekuwa umejichumia thawabu ngapi? Na wengine husema kabisa anafanya hayo ili wakati upotee funga yake isiwe tabu kwake.

Kwa hiyo ndugu zangu wakiislamu hatutaathirika na funga kwa sababu tuanaendekeza anasa za kidunia na tunaacha  mambo yanayotupelekea tupate huo uchamungu tuliouelezea.

Lau tungejua yale ambayo yamo ndani ya mwezi wa Ramadhan tusingeiwacha hata sekunde moja ndani ya mwezi huu itupite bila ya mtu kufanya kheri.

Nasaha kwenu enyi ndugu zangu wakiislamu lengo la funga ni kumcha Allah kama alivyosema Allah katika Quraan Uchamungu hauji tu kwa kutamani bali kuna sababu nyingi zitakazo kufanya uupate uchamungu. Sababu zenyewe pale unapofunga basi uwe ni mwenye kudumisha ibada za faradhi na unajishughulisha na kufanya ibada mbali mbali za sunna, kama kusoma Qur-an, kuswali sala za sunna,kutoa sadaka, kuleta dhikri nk. Na hizi ndizo ibada zitakazokupelekea upate lile lengo la funga.

Tujitahidini kuzifanya kwa hima na tumuombe Allah (subhanahu wataala) atuwafikishe katika hayo.

No comments:

Post a Comment