Monday, 30 June 2014

WASIA KWA WENYE KUFUNGA RAMADHAN

Imeandaliwa na RAUDHWAH ISLAMIC GROUP

Ilipokaribia kuingia Ramadhan Mtume swalla Allahu alayhi wassalam aliwausia masahaba zake kuhusu Ramadhan, wasia tutakaouona katika mada zijazo Inshaa Allah. Na sisi tukiwa tumeuanza mwezi huu mtukufu ni muhimu kukumbushana yafuatayo ili uwe wasia wetu kwa ajili ya kufaidika na Ramadhan.
1-Kumshukuru Allah subhanahu wataala kwa kutuwafikisha kuidiriki Ramdhan. Hakika kushukuru ni miongoni mwa ibada azipendazo  Allah, na akaahidi kwa waja wake wakimshukuru basi atawaongeza neema alizowapa. Amesema Allah subhanahu wataala“Na alipotangaza Mola wenu : Kama mtanishukuru nitakuzidishieni, na mkikufuru hakika adhabu yangu ni kali sana” (Suratu Ibrahim: 7) na akasema tena katika Suratul Baqarah aya ya 152 “….na nishukuruni wala msinikufuru”.

Uhakika hatuwezi kufikia upeo wa kushukuru neema za Allah, kwani neema zake hazihesabiki wala hazipimiki. Amesema  Ibnul Qayyim rahimahullah: “Kuwafikishwa kushkuru neema za Allah, nayo ni neema inayohitaji shukrani, na kuwafikishwa kushkuru neema ya shukrani, ni neema nyengine inayohitaji shukrani, na hivyo hivyo inaendelea kua muislamu aendelee kumshkuru Allah mpaka mwisho wa pumzi zake”. Miongoni mwa neema hizo ni kuwafikishwa kuidiriki ramadhan, alau siku moja na usiku wake, kwani wangapi walitamani alau waweze kufunga lakini maradhi yamewaweka vitandani, hawawezi kufunga, na kula yao mpaka watumie mirija? Wangapi walitamani waidiriki ramadhan na family zao, lakini sasa wako kaburini ima katika viwanaja vya pepo au mashimo ya moto? Hatutojua neema mpaka ikiondoka. Tumepewa nafasi ya kujirekebisha matendo yetu ,kwa kuitumia vizuri Ramadhan,ili siku ya Qiyama tupate ujira mkubwa apatao mfungaji, ujira ambao mimi na weye wakati huu tumewafikishwa na Allah kuupata,na tuukimbilieni huku tukiomuomba Allah atuwafikishe tuimalize Ramadhan kwa salama, asitunyime ujira wake wote, na atuwafikishe tuidiriki Ramadhan inayokuja. Tumshukuruni Allah si kwa maneno tu, bali na kwa matendo kwa kuonesha kuithamini Ramadhan.

2-Kufunga kwa Imani na kutarajia malipo

Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)katika hadith sahihi, iliyopokelewa na Bukhari,Muslim na Nasai rahimahumullah na kusimuliwa na Abu-Hurayra radhiallahu anhu :“Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”.

Kufunga kwa Imani ni kukiri kua funga ni amri ya Allah, na ni miongoni mwa nguzo za kiislamu, atakaesimamisha basi atakua ameusimamisha uislamu wake, na atakaevunja basi atakua kaubomoa uislamu wake. Allah hataki kula yetu na wala hana haja ya kukaa na njaa kwetu lakini anachotaka ni ibada na kama anavyosema katika lengo la funga ni kuwa anataka watu wawe wacha-Mungu yani wamuogope yeye Subhanah.
Kutarajia malipo ni kutaraji kuwa kutokana na funga tunayofunga basi kuna malipo mazuri yaliyoandaliwa kwa wafungaji,na malipo ya mwanzo ni kusamehewa dhambi na mengine yanafuatia Akhera. Ni madhambi mangapi tumeyafanya ya dhahiri na siri,makubwa na madogo yote hayo yatasamehewa kwa atakaefunga kwa imani na kutaraji malipo. Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika Hadith inayosimuliwa na Anas(radhia Allahu anhu) :“Hakuna amali kwa asiekua na nia na hakuna na malipo kwa asiyeyatarajia” . Na tumkumbukeni Allah na ukubwa wake na kwamba akatayarisha malipo mazuri kwa wafungaji na papo hapo tuyatarajie malipo hayo.

3-Kuchunga ulimi na mambo ya kipuuzi.

Anasimulia kwamba amesema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi iliyopokewa na Bukhari na Abu-Daud na kusimuliwa na Abu-Hurayra:“Yoyote asiewacha maneno ya upuuzi, na kuyafanyia kazi,basi Allah hana haja ya kuacha chakula chake na kinywaji chake”.  Je tumeizingatia hadithi hii tukafumba midomo yetu?

Amesema Mtume wa Allah  (swalla Allahu alayhi wasallam) kuwa “Yoyote anaemuamini Allah, na siku ya mwisho basi na aseme la kheri au anyamaze” .(Muttafaqun alayhi). La kusikitisha Ramadhan ndio imekua mwezi wa porojo,Ramadhan imekua ndio mwezi wa kusengenyana, Ramadhan ndio mwezi wa watu kukaa barazani na kuanza kutaja sifa za wapita njia,na wengine kukaa maskani na kuhadithiana uongo. Tumejiweka wapi na hadithi hii?

Tokea hapo mwanzo Allah hahitaji chakula chetu wala kukaa  kwetu na njaa lakini analolitaka ni ucha-mungu,na haupatikani kwa kuzungumza ovyo,na kwa mwenye kusema uongo na kufanya upuuzi mwengine basi ni bora kwake kula kwani Allah hahitaji kulifungia tumbo akauwachia ulimi,kama kufunga basi na viungo vyote vifungwe. Hatopata hasara anaenyamaza kimya lakini hasara kwa asiweza kuumiliku ulimi wake.

Kumiliki ulimi ni jambo alousiwa Muadh bin Jabal na kaambiwa kuumiliki ulimi ndio itakua sababu ya kutengenea matendo yote iwe sala,swaumu,hajj na hata Jihad. Aliulizwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam):” Ni kipi kitachowaingiza wengi motoni ? Akajibu kua ulimi na utupu ndivyo vitakaowaingiza wengi motoni. Na akasema atakaenidhamini viungo hivyo basi na yeye amemdhamini Jannah,(Hadith imepokewa na Bukhari). Basi na tuanze kumdhamini Mtume wa Allah viungo hivi ndani ya Ramadhan hii kwa kutosema uongo,kutosengenya,kutukana na porojo nyenginezo.

4-Kutia nia ya kuzidisha kheri, na kushindana katika mazuri.

Muumini wa kweli hatasheki na kufunga tu ndio ikawa basi,wala hatosheki na kusali sala zake tano, kisha ikawa ndio kishamuabudu Allah. Kumuabudu Allah hakutoshi kwa dakika 25 kwa sala zote tano, ndani ya masaa 24. Allah hahitaji kupangiwa au kutengewa muda kwani muda wote ni wake na anastahiki muda wote kuabudiwa. Alipotaja pepo na starehe zake akamalizia kwa kusema na washindane wenye kushindana(Muttafifin :26) na kwengine akasema Kwa mfano wa haya nawatende watendao. (swaaffaat :61). 

Pepo inahitaji kushindaniwa kwani kama anavyosema Rasuul (swalla Allahu alayhi wasallam) kuwa “….Hakika bidhaa ya Allah ni ghali na bidhaaa ya Allah ni pepo.(Tirmidhy).  Ikiwa kushindana kwenyewe sisi ndio tutaenda na sala tano tu ambazo hazina khushui ndani yake, na haikutimizwa rukuu wala sijdah, mbele ya wale ambao wanaswali mpaka kuvimba miguu yao, na kuroa ndevu zao kwa kulia na kukesha usiku mzima, kwa kumuabudu Allah hivi tutakua sawasawa? Au ndo sisi tunashindana kwa aina za vyakula na nani kapika vingi na vizurii?

Wengi wetu kabla ya Ramadhan tulitia nia ya kuzidisha kufanya kheri, na wengine baada ya kufanya vibaya Ramadhan zilopita, tukajiapiza Ramadhan ijayo nitafanya vizuri, na nitamuabudu Allah kikamilifu, lakini tunayakumbuka haya au pia tunasubiri ya mwakani, ili tufanye vizuri kwa kua Ramadhan hii tuko na mishughuliko ya world cup, hatuna muda wa kumuabudu Allah.

Na tuipambeni Ramadhan yetu kwa Qur-an na qiyamul-layl. Adhkaar na madarsa na vikao vya kheri,Tutieni nia ya kuzidisha kheri na miongoni mwa mambo tunaotakiwa kuyaazimia kuyafanya  ni kutekeleza sunna ya itikafu, sunna ambayo hakuiachapo Mtume baada ya kuhamia Madina na mwaka aloiwacha ikabidi ailipe lakini ndio sunna iliyokimbiwa na wengi.

5-Kuwahurumia wanyonge na kuacha israfu.

Anasema Allah (subhanahu wataala) “…. Na amewanyanyua daraja baadhi yenu juu ya wengine ili akufanyieni mtihani kwa hayo alokupeni…” (An-aam 165).Na akasema tena katika Suratu-Nahli aya ya 71 “Na Allah amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika rizki, Je wale walofadhilishwa,hawarejeshi rizki zao,kwa wale wanaowamiliki kwa mikono yao ya kulia?”.

Kutofautiana kwa kipato ni dalili za uwepo wa Allah kuonesha anampa amtakae na humnyima amtakae na kwamba kupata si kwa utashi wa mtu, bali ni mipango ya Allah. Na akawataka waja wake wasaidiane. Bila shaka miongoni mwa jamii za kiislamu tunazoishi nazo wako wanaofunga lakini wasijue wataftari nini, na wanafunga hawana daku ya kula ili waweze kufunga vizuri.

Wanafunga kwa kua ni amri ya Allah (subhanahu wataala) lakini kipato chao na uwezo wao hauwaruhusu kufanya hivyo.  Watu aina hiyo wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la huruma na wale wenye uwezo. Si vibaya kila siku kumlisha maskini mmoja kwani sadaka ya kulisha chakula ina thamani kubwa mbele ya Allah (subhanahu wataala). Na Amesema Mtume wa Allah katika hadithi inayosimuliwa na Saad bin Khalid:”Atakaemfutarisha aliefunga, basi atapata ujira sawa na wake, pasi na kupungua ujira wa mfungaji chochote”(Tirmidhy,Nasai na Ibnu-Majah). 

Ikiwa ni hivyo basi na kuftarsha kwetu tusiwasahau maskini na sio shughuli zetu za kuftarisha kujazwa matajiri na wenye uwezo wao ambao hata hicho chakula hawakihitaji. Kwa kutumia kiyasa ya hadith ya Rasuul inayosimuliwa na Abu-Hurayrah kua chakula kibaya ni chakula cha harusini, kwani wanaalikwa wasiokihitaji; basi na ftari zetu kesi ndio hiyohiyo, tunawasahau maskini na wote wanaoalikwa hawakihitaji. Tusitosheke na thawabu za kuftarisha mtu bali tutake na thawabu za kulisha maskini kwani tukialika matajiri tutapata thawabu za kuftarisha tu lakini kualika maskini itakua ni thawabu za kuftarisha na za kulisha maskini.
           Ama kuhusu israfu tumeona maudhui yake katika mada zilopita

6-Kukumbuka njaa na kiu siku ya Qiyamah.

Moja kati ya mambo walohusishwa Mitume na ndo ikawa kama zawadi yao hapa duniani amesema Allah subhanah “Hakika tuliwachagua kwa lile jambo zuri kabisa la kuikumbuka Akhera” (Swaad :46). Ni zawadi ambayo imewafanya kutojali maisha ya dunia ni kutoshughulishwa na starehe za duniani.

Amesema Allah (subhanahu wataala) hii kuonesha kua kila kitu chao walikua wakifiri akhera.Na hivyo ndio anavyotakiwa muislamu wa kweli awe. Awe anafikiri akhera,kwani nguzo zote za kiislamu kuanzia sala,swaumu na hata hajji vinamkumbusha mtu mambo yatakayotokezea siku ya kiyama. Funga inatakiwa imkumbushe mtu njaa na kiu, kitakachowakuta watu wa motoni na kutokana na kiu hiyo wataomba kwa watu wa peponi kama anavyotusimulia Allah (subhanahu wataala) katka suratu A’raf  aya ya 50 “Na watanadi watu wa motoni kuwaita wa peponi: Tumiminieni maji au chochote katika alivyokuruzukuni Allah. Watasema watu wa peponi: Hakika Allah ameviharamisha vyote viwili (yani chakula na maji) kwa makafiri”. Hivyo basi mtu anapokaa na njaa na kiu akumbuke kua akhera watu waovu watakaa na njaa na kiu.(Allah atuhifadhi)

Allah atuwafikishe kuyatekeleza haya na mengineyo ya kheri.

Sunday, 29 June 2014

Fadhila za kusali Dhuhaa

Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Imesimuliwa na Abu-Hurayra -radhi za Allah ziwe juu yake- amesema:"Ameniusia Kipenzi changu(swalla Allahu alayhi wasallam) mambo matatu: Kufunga siku tatu kila mwezi,Rakaa mbili za Dhuha na kusali witri kabla ya kulala" Imepokelewa na Bukhari na Muslim na pia Mtume swalla Allahu alayhi wassalam alimuusia hayo hayo swahaba wake mwengine Abuu-Dardai radhia Allahu anhu katika hadityhi ilopokelewa na Imam Muslim na Abu-Daud

Ndugu zangu wa kiisalamu, sala ya dhuha ni sala yenye ujira mkubwa lakini ni katika swala ambazo zimesahaulika katika jamii ya kiislamu, na hata wengine hawajui kama kuna sunna hiyo, hii ni kutokana na kuwa na mishughuliko mingi ya kidunia kwani swala hii huswaliwa robo saa mara baada ya kuchomoza  jua mpaka kabla ya adhuhuri, hivyo watu huwa katika mishughuliko yao, na kusahau kusali sala hii, Anasimulia swahaba Abdullah bin Amr bin Aas -radhiallahu anhu kua mara moja maswahaba walirud katika vita hali ya kua wamepata ngawira nyngi na wamerudi katika muda mfupi sana, wakawa watu wanazungumzia kuhusu habari yao, Mtume akawauliza"Jee nikutajien kitu chenye thamani kuliko hata hizo ngawira na chenye kutosheleza muda? Maswahaba wakasema ndio. Akawaambia:Mwenye kutawadha akaelekea msikitini na kusali dhuhaa basi huyo kapata zaidi kuliko hata hizo ngawira" Imepokelewa na Imam Ahmad

Atakaeswali Dhuhaa kachukuliwa dhamana na Allah ya kusimamiwa mambo yake kwa siku ile kama anavyosema Mtume swallahu alayhi wassalam katika hadithi ilopokelewa na Uqba bin Amir radhia Allahu anhu kua "Amesema Allah kumwambia mwanadamu:Ewe mwanadamu nitosheleze mwanzo wa mchana kwa rakaa nne nami nitakutosheleza mwisho wa mchana" Imepokelewa na Imam Ahmad

swala ya dhuhaa ina rakaa mbili mpaka nane na muda wake ni robo saa baada ya kuchomoza jua na kabla ya adhuhuri , ina fadhila nyingi Allah atuwafikishe kuisali na atulipe ujira kamili
Wallahu a'alam.

Usisahau kusali DHUHA

VIPI TUTAIPOKEA RAMADHANI


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Kwa hakika mwezi wa Ramadhani tayari umeshafika. Na baada ya muda mchache tutaingia katika mwezi huo mtukufu. Mwezi uliokuwa bora. Mwezi ambao ni shamba la watenda wema ili kuchuma mazuri yatakayowafaa kesho akhera. Ni mwezi wa kuomba tawba tukasemehewa dhambi zetu. Ila suala la muhimu kabisa ni vipi fursa hii ya Ramadhani tunaweza kuitumia? Ni lazima uweke maandalizi ambayo yatakuja kukufaa na kuyafanya ndani ya mwezi wa ramadhani.

Kwa nini tuuthamini mwezi huu wa Ramadhani? Na kwa nini inamlazimu muislamu kuwa na makusudio na jitihada maalum ndani ya Ramadhani. Kwanza tuangalie hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) inayosema “ Kutoka kwa Abdul rahmaan Bin Sakhar Al dausy (Abuu Huraira) (radhi za Allah ziwe juu yao)  amesema RASOUL  (swalla Allahu alayhi wasallam) “UMEPEWA UMMAH WANGU MAMBO MATANO KATIKA RAMADHANI HAUKUWAHI KUPEWA UMMAH WOWOTE KABLA YAKE.
1-HARUFU INAYOTOKA KWENYE KINYWA CHA ALIYEFUNGA INAPENDEZA ZAIDI MBELE YA ALLAH KULIKO HARUFU YA MISKI.
2- MALAIKA HUWAOMBEA MSAMAHA WAJA HAO MPAKA WAFTARI.
3- ALLAH HUIANDAA NA KUIPAMBA PEPO YAKE KILA SIKU NA HUIAMBIA JANNAH KWA WAKARIBIA WAKATI AMBAPO WAUMINI WATATUPULIA MBALI MITIHANI MIKUBWA YA DUNIA NA KUKUINGIA.
4-SHETANI HUFUNGWA MINYORORO ILI WASIWATIE UOVU KAMA AMBAVYO HUFANYA MIEZI MENGINE.
5-USIKU WA MWISHO WA RAMDHANI WAFUNGAJI HUSAMEHEWA MADHAMBI YAO”  (Imepokelewa na Ahmad na Baihaqi)

Ndani ya mwezi wa ramadhani kuna makumi matatu. Rasoul swalla Allahu alayhi wasallam anasema ya kwamba mwanzo wake ni rehma katika yake ni magh-firah na mwisho wake mja kuepushwa na moto.
Mwezi wenyewe ndio unakaribia kutufikia bila shaka mambo mazuri kama hayo kila mtu anahamu ayapate lakini unahitaji maandalizi sasa mimi na wewe je! vipi tutaweza kuupokea mwezi mtukufu wa ramadhani.

1-Kwanza kabisa muislamu ahakikishe anajua elimu kamili juu ya funga. Kuanzia  sharti za kusihi kwa wafunga, yanayobatilisha funga, nani anaruhusika kufungua au kutofunga, yaliyo sunna kwa mwenye kufunga na mengineyo.

Ikiwa muislamu atayajua hayo atakuwa na tahadhari ya kuichunga funga yake ili asije akawa anakaa na njaa ila hana chochote katika funga yake.

2- Kuchukua tahadhari zaidi na dhambi zinazotokana na ulimi. Katika viungo ambavyo Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema yeyote atakaemdhamini viungo hivyo kwa maana kuvitumia katika kheri na akajiepusha na haramu basi anamdhamini pepo. Kutoka kwa Sahli bin Saad (Radhiya Allaahu anhu) amesema: Mtume (Swalla Allaahu alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Atakayenidhaminia kilichomo baina ya taya zake [yaani ulimi] na kilichomo baina ya miguu yake (yaani tupu au sehemu za siri) nami nitamdhamini Pepo" (Al-Bukhaariy na Muslim)

Suali litakuja je ulimi unaweza kumfanya mtu asiwe na funga? Tuangalie hadithi ya Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) inayosema " Yule ambae haachi kusema uongo na haachi vitendo viovu. Allah (subhanahu wataala) hana haja na funga yake." Bukhari na Muslim.

Hadithi ya hapo juu inaonesha wazi ikiwa mtu hatofunga pamoja na kuuzuia ulimi wake na maasi basi hatokuwa na funga. Hivyo muislamu aupokee mwezi huu kwa kukusudia hasa kuwa mbali na dhambi kama za kusengenya,kusema uongo,matusi basi ajue Allah hana haja na funga yake na anakaa na njaa tu. Allah atujaalie wale ambao watazizuia ndimi zao na dhambi hizo na mfano wa hayo.

3- Muislamu aweke nia na azma ya kufunga ramadhani kwa uzuri na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (subhanahu wataala). Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) : "Atakayefunga Ramadhaan kwa imani na kutaraji malipo atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia " Bukhaariy na Muslim.

4- Kuhakikisha muislamu kuwa anasali sala za faradhi kwa wakati na kujihimiza sana na kusali sala za sunna. Miongoni mwa sala za sunna ni rakaa 12 za sunna (Qabliya na Baadiyah), sala ya dhuha,sala ya witri na sala ya tarawehe.

5-Kushikamana na kusoma quran kwani mwezi wa ramadhani ndio ulioteremshwa Quraan. Allah (subhanahu wataala) anasema "Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur'ani kuwa ni uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. "(Baqara :185).

Hata Jibril alikua akishuka kila mwaka katika mwezi wa ramadhani kwa kumdurusisha Quraan Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)  sio kua hajui kusoma ila ni kuonesha ubora na umuhimu wa ibada hiyo ndani ya mwezi wa Ramadhani.

Kusoma Quraan kuna faida nyingi sana. Miongoni mwa faida hizo ni mtu kupata thawabu kwa kila herufi atakayoisoma. Imetoka kwa Abdullahi bin Masuud (Radhiya Allahu anhu) kwamba Mtume (Swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: "Atakayesoma herufi moja katika kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja, na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, wala sisemi "Alif-Laam-Miym" ni herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miym ni herufi moja))  At-Tirimidhiy.

Pia Quraan itakuwa kiombezi kwa watu wa Quraan. Watu waliokuwa wamedumu kusoma Quraan kwa mazingatio na kuifanyia kazi. Imetoka kwa Abu Umaamah (Radhiya Allahu anhu)  kwamba Mtume (Swalla Allahu alayhi wasallam)  amesema "Someni Qur-aan kwani itakuja siku ya Qiyaamah ikimuombea   mwenye kuisoma" Muslim.

Hivyo basi muislamu azidishe kusoma Quraan na ajitahidi aisome kwa mazingatio.

6- Kuhudhuria katika sehemu mbali mbali za kujifunza kama katika mihadhara na madarsa mbali mbali.  Jambo hili leo hii wengi wetu tumeliwacha na tumekuwa tukitumia muda wetu mwingi ndani ya whatsapp,facebook na mitandao mengineyo pamoja na vibaraza vyenye mazugumzo yasiyokuwa na manufaa. Na mtu anapoambiwa ahudhurie sehemu za kheri basi hutoa sababu zisizo na msingi ila yote hayo tumeghafilika na mauti na imetuhadaa dunia.
Sehemu za kujifunza na kukumbushana yaliyo mema ni nzuri sana katika kuufanya moyo wa mja uwe unaathirika na maneno ya Allah. Na hii itamfanya daima awe anakumbuka wajibu wake kama kiumbe wa Allah(subhanahu wataala) katika ulimwengu huu.

Mwisho kwa kumalizia tujitahidini kuyafanyia kazi haya tuayokumbushana kabla ya ramadhani ,ndani ya ramadhani na baada a ramadhani ili tuweze kuzitafuta radhi za Allah hapa duniani na kesho akhera.
Tunamuomba Allah (subhanahu wataala) atujaalie wale ambao watafika ramadhan na watafunga na kupata ujira mkubwa kutoka kwa Allah (subhanahu wataala) pamoja na kusamehewa dhambi zetu. Aaamin.

MALIPO YA MWENYE KUFUNGA SIKU YA QIYAMAH


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subuhanahu wata‘ala) Muumba wa wanaadamu na viliyomo duniani na akhera na baina yake na akavikadiria maisha yao. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).
Ndugu wa Kiislamu, Allah (subuhanahu wata‘ala) ametuwekea namna mbali mbali za ibada ili kutujenga kiroho na kimwili kuwa ndani ya twa‘a yake wakati wote. Swaum (funga) ni moja ya ibada hizo na ni nguzo ya nne katika Uislamu kama anavyosema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Uislamu umejengwa kwa nguzo tano: Kushuhudia kuwa hapana Mola apasae kuabudiwa isipokuwa Allah na Muhammad ni mja wake na mjumbe wake, Kusimamisha Swala, Kutoa zaka, Kufunga Ramadhaan, na Kwenda Makka kuhiji kwa mwenye uwezo.” Bukhary na Muslim.
Na imethibiti kufaradhishwa kwake ndani ya mwezi wa Ramadhaan pale Allah Aliposema: “Enyi mlio amini! Mmefaradhishiwa Saumu, kama waliyo faradhishiwa walio kuwa kabla yenu ili mpate kuwa wachaMungu.” [Al-Baqara 2 : 183].
Swaum ni ‘amali yenye kumpatia mja malipo mengi makubwa makubwa wakati ambao amefunga kwa matendo mbali mbali ya ibada anayoyafanya akiwa ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhaan. Kwa leo in sha Allah, tutazungumzia malipo ambayo Allah (subuhanahu wata‘ala) amemuandalia mfungaji siku ya Qiyamah.
Swaum ni kiombezi. Swaum itakuja kumuombea shifaa mwenye kufunga siku ya Qiyama kama ilivyothibiti hadithi kutoka kwa Abdullah ibh Amr (radhi za Allah ziwe juu yake), Amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Funga na Quran ni  viombezi viwili vya mja wa Allah siku ya Qiyamah, Funga itasema: Ewe Mola, nilimzuia na chakula na matamanio wakati wa mchana, niruhusu nimuombee. Na uombezi wao utakubaliwa.” Ahmad.
Swaum ni sababu ya kumuingiza mtu Peponi. Mwenye kufunga na akaitimiza funga yake na akajiepusha na maovu na machafu yanayopunguza fadhila za swaum, Allah amemuandalia pepo kwa ajili yake. Abuu Umamah amesema: “Nilienda kwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) nikamwambia: Niamrishe ‘amali ambayo itaniwezesha kuingia peponi. Akasema: “Jilazimishe na kufunga kwani hakuna iliyo sawa na hiyo.” Baadae nikaja tena kwake na Akasema: “Jilazimishe na kufunga.” Ahmad, An-Nasai na Al-Hakim.
Allah atawafadhilisha wenye kufunga kwa kuwaingiza Peponi kupitia mlango maalum uitwao Rayyaan. Amesimulia Sahl ibn Sa‘ad (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Kuna mlango wa kuingilia Peponi uitwao Rayyaan, siku ya Qiyama utasema: wako wapi walokuwa wakifunga? Akishapita wa mwisho kuingia (mlango) utafungwa.” Bukhary na Muslim.

Swaum humsaidia mfungaji kuwekwa mbali na mashimo ya moto wa Jahannam. Imesimuliwa na Abu Said al-Kudry (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Hakuna mja atakaefunga siku moja katika njia ya Allah isipokuwa Allah atamuondoshea moto umbali wa miaka sabiin na uso wake.” Imepokewa na kundi la watu wa hadithi isipokuwa Abu Daud.
Swaum ni ‘amal yenye malipo makubwa kiasi kwamba Allah (subuhanahu wata‘ala) amesema kuwa ‘amali hii ni kwa ajili yake na yeye ndiye atakayeilipa pasi na kubainisha ukubwa wa malipo yake. Kutoka kwa Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake), Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: Allah amesema: Kila ‘amali anayoifanya mwanaadam ni kwa ajili yake isipokuwa funga, kwani hiyo ni kwa ajili yangu, na Nitatoa malipo kwa ajili yake (funga). Funga ni ngao, ikiwa mtu amefunga asitumie lugha chafu, asinyanyue sauti yake, au kufanya vitendo viovu. Ikiwa mtu atamtolea maneno au kupigana naye aseme “mimi nimefunga” ... ” Muslim, Ahmad na An-Nasai.
Ndugu wa Kiislamu, hayo  ni katika baadhi ya Aliyotuandalia Allah (subuhanahu wata‘ala) endapo tutaitekeleza ibada hii kwa usahihi wake na kujiepusha na yale yote yenye kupunguza fadhila za swaum kama kucheza game wakati mtu amefunga au karata au kutizama filamu na tamthilia zinazokwenda kinyume na maadili ya Uislamu.
Tunamuomba Allah (subuhanahu wata‘ala) atuwezeshe kuifunga Ramadhani hii na zijazo kwa namna anayoiridhia na kuifurahia na atuwezeshe kupata malipo yote aliyowaandalia wafungaji. Amin.

FAIDA ZA MWENYE KUFUNGA HAPA DUNIANI


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.

Allah Subhaanahuu Wataala ametufaradhishiya funga sisi tulioamini, ili tupate uchamungu pamoja na faida mbali mbali zinazopatikana katika funga. Na tujue funga hii ni ile iliyofungwa kwa kujua na kutambua sharti, sunna na yale yanayobatilisha funga kwa mfungaji, ndipo tutakapopata uchamungu na   faida nyingi.
Hivo basi Kwa mwenye kufunga anapata faida za kiroho, za kijamii na katika siha yake. Kama zifuatazo:
Miongoni mwa faida za kiroho ni kule kuwa na subra na kuijenga khasa katika nafsi yake, na anajifunza kuifunga nafsi na kuisaidia kuwa katika hali hiyo.

Na atailea nafsi katika Taqwa na uchamungu, kwani uchamungu ndio lengo kubwa la funga. Allah anasema: “Hakika mumuefaradhishiwa funga kama walivofaradhishiwa walio kabla yenu ili muwe wachamungu” 2:183
Faida nyengine kwa mwenye kufunga ni kukubaliwa dua yake.

Hadithi aliyoipokea Imam Al Tirmidhy Radhi za Allah ziwe juu yake amesema : “Watu watatu hukubaliwa dua zao; aliyefunga mpaka aftari, kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa”
Pia akasema tena Mtume Swalla Allahu alayhi wassalam “Dua ya aliyefunga hupokelewa pale anapoftari” (Imepokelewa na Ibnu Maajah).

Angalia kwa namna gani faida na fadhila tunazopata pale tunafunga hapa hapa duniani.
Ama faida za kijamii kwa mwenye kufunga ni:
Kuurejesha umma au jamii katika nidhamu na umoja, na kupenda uadilifu na usawa.
Na kuengeza na kuzidisha kwa waumini upole na huruma, na tabia ya kuwa na ihsani, pale jamii inapojifunga na kuzuiya kufanya mambo ya shari na ufisadi wakati wote wa funga.

Na katika faida nyengine ya funga ni:
Faida ya kisiha na kupata afya kwa mwenye kufunga, kwani anasafisha mfumo wake wa chakula na kupumzisha tumbo, kuusafisha mwili kutokana na vidudu na minyoo inayoleta maradhi. Maana vidudu hivi hupata nguvu na pale mwanadamu anapokuwa anakula (parasites).

Na kupunguza kiwango kikubwa cha mafuta na uzito katika tumbo, kwa maana kisayansi mwili wa mwanaadamu unatakiwa usipungue kiwango cha glucose au sukari katika damu, kiwango hichi huwa sawa pale mwanadamu anapokula chakula, hivo mda anaofunga chakula na kiwango cha sukari hupungua mwilini ila mwili unajaribu kuangalia sehemu ama chakula kilichohifadhiwa na kukivunja na kukitumia ili mwili uwe sawa na kuwa na nguvu. Ndipo mwili huvunja mafuta yaliyohifadhiwa katika mwili na kuweka ustawi mzuri bila kuhisi uchovu.
Na katika hadithi mtume Sallahu alayhi wassallam  anasema: “Fungeni mtapata siha na afya” (imepokelewan na imam zubayd) katika kitabu cha “ITHAAFU SAADAT EL-MUTTAQYBA” 401:7
Na ameitaja Mundhiry katika kitabu chake cha “ATTARGHYBU WATTARHYB” 83:2

EWE ALLAH ULIETUKUKA TUPE KHERI NA FAIDA ZINAZOPATIKANA NDANI YA RAMADHANI.
WAFFAKANALLAHU FIYMA YUHIBUHUU WARDHWAA.

YALIYO SUNNAH KWA MWENYE KUFUNGA


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subhanahu wata‘ala) Mola wa viumbe vyote vyenye kuonekanwa na visivyoonekanwa. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba zake.
Ndugu wa Kiislamu, kama ilivyo katika ibada ya swala kuwa kuna baadhi ya matendo ya sunnah hufanywa ndani yake ili kuengeza fadhila na daraja ya swala hiyo, kadhalika katika ibada ya swaum (funga) kuna matendo ya sunnah amabayo mfungaji akiyafanya hupata fadhila zaidi katika funga yake na kupata ujira maradufu.

Katika makala hii in sha Allah, tutazungumzia baadhi ya mambo yaliyo sunnah kwa mwenye kufunga kuyafanya. Miongoni mwa mambo hayo ni haya yafuatayo.

Kula daku

Daku ni chakula kinacholiwa mwishoni mwa usiku kwa ajili ya kutekeleza sunnah ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) na pia kumfanya mfungaji awe mchangamfu na mwenye nguvu hali itakayompelekea kutokushindwa kufanya harakati zake za maisha kama ilivyo kawaida yake katika siku za kula mchana. Imethibiti hadithi kutoka kwa Anas bin Malik (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Kuleni daku kwani katika daku kuna baraka.” Bukhary na Muslim.

Kuchelewesha kula daku
Pia imesuniwa kuchelewesha kula daku hadi karibu na swala ya asubuhi kama ilivyopokewa hadithi na Anas kutoka kwa Zayd bin Harith (radhi za Allah ziwe juu yake) ambae amesema: “Tulikula daku na Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) kisha tukainuka tukaswali.” Nikasema: “Kulikuwa na muda gani baina ya adhana na daku?” Akasema: “Ni muda wa kusoma aya hamsini (50).” Bukhary

Kuharakisha kufutari (kufunguwa)
Vile vile ni sunnah kuharakisha kufunguwa mara tu baada ya jua kuzama kama alivyokuwa Akifanya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam), tofauti kabisa na wafanyavyo baadhi ya ndugu zetu ambao husubiri mpaka wamalize kuwali magharibi pamoja  na sunnah yake ya baadiyah. Kufanya hivi sio sahihi kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume wetu. Imepokewa hadithi kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Watu wataendelea kuwa katika hali nzuri maadam wanaharakisha kufunguwa (funga zao).” Bukhary na Muslim.


Kufunguwa kwa kula tende
Ni sunnah kwa mwenye kufunga kufutari kwa kula tende mbichi, ikiwa atakosa basi kwa tende kavu na ikiwa atakosa basi na afungue kwa kunywa mafunda ya maji. Kama ilivyopokewa kutoka kwa Anas (radhi za Allah ziwe juu yake) ambae amesema: “Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) alikuwa akifunguwa kwa tende mbichi kabla ya kuswali, ikiwa hamna tende mbichi basi kwa kavu na ikiwa hamna basi hunywa mafunda machache ya maji.” Abu Daud na Tirmidhy.

Kuomba dua kwa wingi
Vile vile inahimizwa kuomba dua kwa wingi wakati mtu akiwa amefunga na kabla ya kufutari kwani mtu aliyefunga ni katika watu ambao hukubaliwa dua zao, kama ilivyokuja hadithi ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) isemayo: “Dua za watu watatu hazirejeshwi (hazikataliwi), dua ya baba (kwa mwanawe), dua ya mtu aliyefunga, na dua ya msafiri.” Imepokewa na Al-Bayhaky kutoka kwa Anas (radhi za Allah ziwe juu yake).

Kujitenga na mabishano na majibizano
Mtu aliyefunga hatakiwi kuanzisha mabishano na malumbano, na kama mtu atakuja kwa ajili ya kugombana naye au kutaka kupigana naye basi ni wajibu wake kujizuia na kusema kuwa “mimi nimefunga” ili kuepukana na kuiharibu funga yake na kupunguza fadhila za funga yake.
Amesema Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam): “Funga ni Pepo hivyo kusiwe na mazungumzo machafu na tabia chafu. Ikiwa mtu atampiga au kumtukana (aliyefunga) na aseme, “Mimi nimefunga” mara mbili. Naapa kwa yule ambaye roho yangu iko Mikononi Mwake, harufu itokayo kinywani mwa mtu aliyefunga ni bora mbele ya Allah kuliko harufu ya miski. (Allah anasema:) “Ameacha chakula chake, kinywaji na matamanio yake kwa ajili Yangu. Funga ni kwa ajili Yangu Nami nitailipa, na matendo mema hupata malipo mara kumi yake.” Bukhary na Muslim.

Ndugu wa Kiislamu, ni muhimu pia juu yetu kuzidisha kufanya ‘amali nyingi tukiwa tumefunga kama vile kutoa sadaka, kuwasaidia wahitaji na kutumia muda wetu mwingi kuisoma Quran na kuhudhuria madarsa ili kujifunza maana yake, kwani bila ya kujifunza maana yake hatutoweza kuishi kwa mujibu wa Quran na kupelekea kuishi maisha ambayo Allah haridhiki nayo na hatimae kuingia katika adhabu za Allah.

Ni muhimu pia kuendeleza yale yote ya kheri tunayoyafanya katika mwezi mtukufu wa Ramadhaan katika miezi myengine khassa kuhudhuria madarsa na kujifunza dini yetu. Kwani bila ya elimu hakuna litakalofanywa kwa usahihi wake.

Tunamuomba Allah atuwezeshe kuyafanya haya na mengine ya kheri hadi mwisho wa maisha yetu na Atuweze kupata Rehma zake na Kutuingiza katika Pepo yake. Amin.

SHARTI ZA KUSIHI KWA FUNGA- SEHEMU YA PILI


Makala imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

3 – KUJIZUIA KUFANYA TENDO LA NDOA KWA MAKUSUDI NA KUJITOA MANII

Ikiwa mtu atafanya jimai bila ya kukusudia basi mtu huyo atakuwa amesameheka. Kwa kauli ya Allah: “Lakini ipo lawama katika yale ziliyo fanya nyoyo zenu kwa makusudi.” (Suratul Ahzaab : 5).

Ama yule ambae atafanya jimai kwa makusudi basi huyo funga yake itabatilika na itamlazimu kwake yeye kuilipa funga hiyo pamoja na kutoa kafara. Kafara kwa yule ambae atafanya tendo la ndoa katika mchana wa Ramadhani ni :

i. Kuacha huru mtumwa.
ii. Kufunga miezi miwili mfululizo.
iii. Alishe maskini 60 kila mmoja kibaba kimoja.

Ikiwa mke au mume mmoja wao amemlazimisha kwa nguvu mwenzake kufanya tendo la ndoa ndani ya mchana wa Ramadhan na wamo katika funga basi yule aliemlazimisha mwenzake ndio itamuwajibikia kutoa kafara.

Na mwanamke hatakiwi akubali kufanya tendo la ndoa wakati amefunga ndani ya Ramadhani. Na  maulamaa wengine wakaengeza kwa kusema hata ikiwa anaweza kupigana na mume wake basi ampige. Kuonesha uzito wa funga. Na wala mtu asitumie kivuli kuwa amelazimishwa kujitetea ajue kuwa Allah (subhanahu wata‘ala) anajua kila kilichomo ndani ya nafsi ya mja wake.

Ikiwa mtu atafanya tendo la ndoa hali ya kuwa amefunga ndani ya Ramadhani kwa siku mbili tofauti basi ni juu yake kafara mbili. Kila funga moja basi na kafara yake moja.

Pia ikiwa mtu anafanya tendo la ndoa na baadae ikambainikia kuingia kwa alfajiri basi kinachotakiwa ni kuacha tendo la ndoa hapo hapo akakoge janaba na aendelee na funga yake.

Je ni wakati gani jimai ya mchana wa Ramadhani inaruhusika?

Ikiwa mke na mume wote wana dharura za kisheria za kutofunga kwa mfano wote wamesafiri basi hakuna ubaya na hawatotoa kafara. Kwani awali ruhusa ya kutofunga ishakuwepo kwao wao.

Ikiwa mume amerudi safari na mke wake hakufunga siku hiyo kwa sababu ya hedhi na ametwaharika baada ya funga kuanza, basi tendo la ndoa kwao wao linaruhusika kwani mume hajafunga na mke hakufunga.

Ama kinyume na hali hizo wakifanya tendo la ndoa ndani ya mchana wa Ramadhani wakiridhia wenyewe basi kwa kila mmoja juu yake kafara ama mmoja amemlazimisha mwenzake basi yule aliyemlazimisha mwenzake ni juu yake kutoa kafara.

Kujitoa maniii kwa makusudi kunabatilisha funga. Hivyo basi yeyote ambae amefunga anatakiwa ajizuie na kujitoa manii kwa makusudi. Na mfano wa kujitoa manii kwa makusudi ni puunyeto, au kwa kumkumbatia au kumchezea mkewe au mwanamke mpaka akatokwa na manii.

1-SUALI
Walifanya jimai kabla ya kuanza kwa funga na baadae hawakuwahi kukoga janaba wakalala mpaka ikaingia alfajiri. Je nini hukmu ya funga yao?
JIBU
Ikiwa walitia nia ya kufunga basi funga yao itasihi. Kinachowalazimu ni kukoga janaba ili waweze kuswali na waendelee na funga yao. Na hili ni kwa ushahidi wa hadithi ya Bibi Aysha na Ummu Salamah (radhiya Allahu anhuma) “kwamba Mtume (Swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akiamka na janaba kutokana na kukutana kimwili na wake zake, kisha anakoga na kufunga.” (Al Bukhariy na Muslim).

2-SUALI
Alifanya jimai bila ya kujua kwamba alfajiri imeingia. Na baadae akajua kuwa alifanya jimai wakati tayari alfajiri ishaingia. Nini hukmu yake?

Ikiwa wakati anafanya hajui kama wakati umeingia basi atakoga na ataendelea na funga yake. Kwani hakuna kosa kwa mtu kutojua.Ama akifanya kwa kusudi basi funga itabatilika funga yake na itamlazimu kutoa kafara na kuilipa funga hiyo.

4-KUEPUKANA NA HEDHI NA NIFASI

Ni lazima kwa mwanamke anaetaka kufunga awe ametoharika kutokana na hedhi na nifasi. Na pindi mwanamke anapokuwa na hedhi au nifasi basi huwa ni wajibu kwake kuacha kufunga. Na hii ni amri kutoka kwa Allah (subhanahu wata‘ala) na mwanamke akitoharika ataendelea na kufunga. Pia siku ambazo ameziacha kwa kutofunga atakuja kuzilipa baada ya Ramadhani.

SUALI
Bado muda mdogo sana kumalizika kwa funga. Mwanamke akapatwa na hedhi. Je itahesabika funga yake ile?

JIBU
Hapana, haitohesabika funga ile kwa sababu wakati haujatimia. Na itamlazimu mwanamke huyo aje kuilipa funga hiyo baada ya kumalizika kwa Ramadhani.

SUALI
Mwanamke amepatwa na maumivu au dalili nyengine za kuonyesha atapatwa na hedhi ila hakupata wala hakutokwa na damu. Nini hukmu yake?
JIBU
Hatowajibika kuilipa na funga yake itakuwa sahihi.

SUALI
Ikiwa mwanamke siku zake za hedhi zimekaribia. Akaona matone ya damu ila damu haikutoka. Nini hukmu ya funga yake?
JIBU
Lazima ailipe funga hiyo kwani matone hayo ya damu yatahesabika kama ni damu ya hedhi.

SUALI
Miaka yote Ramadhan napata kufunga siku 10 tu au 11. Na zinazobaki nakuwa katika siku za hedhi. Sipati kufanya ibada ambazo zina fadhila kubwa kuliko miezi mingine. Nakuwa mnyonge kutokana na hali hiyo.
Je naweza kutumia vidonge vya kuzuia hedhi ?

JIBU
Kuhusu hedhi muda wake wajuu kabisa ni siku kumi na tano, zikizidi hapo huwa ni ugonjwa, kwa maelezo yako unakuwa ukitokwa na damu kwa takriban siku 20, hii inaonesha una tatizo jitahidi kutafuta tiba ya ugonjwa huo.
Ama ikiwa zitabaki siku 15 au chini ya hapo tutaizingatia kuwa ni hedhi, na kipindi unachokua ndani ya hedhi kuacha yale sheria iliokutaka kuyaacha ni ibada, hivyo ibada iliyokuzuilia kufanya ibada nyengine fadhila zake ni kubwa zaidi kwa wakati huo.
Pili.
Kuhusu kutumia vidonge vya hedhi wako maulamaa wanasema kuwa haifai kutumia vidonge hivyo kwani vimethibitika vina madhara.

Ama tukisema havina madhara basi ushauri wetu ni bora kuiacha hedhi katika utaratibu wake ndio bora zaidi kiibada na kiafya pia. Kwani ndio maumbile yake mwanamke alivyoumbwa na Allah (subhanahu wata‘ala). Na Allah ndie mjuzi zaidi.

SUALI
Ikiwa mwanamke amemaliza nifasi kwa siku chache mfano siku saba je anaweza kufunga?
JIBU
Ikiwa kweli imesita damu ya nifasi mwanamke huyo anaweza kufunga. Na Allah ni mjuzi zaidi.

SUALI
Ni ipi hukmu ya funga kwa mwanamke aliyeharibu mimba?
JIBU
Ikiwa mimba imeharibika kabla ya mtoto kuumbika basi damu hiyo si damu ya nifasi na mwanamke atakoga kujisafisha na kuendelea na funga yake.
Ikiwa mimba imeharibika baada ya mtoto kuumbika basi damu hiyo itakuwa ni ya nifasi na itambidi ajizuie kufunga mpaka pale itakaposita damu ya nifasi. Na Allah ni mjuzi zaidi.

SUALI
Mwanamke ametoharika kabla ya kuanza kwa alfajiri ya kweli. Akatia nia ya kufunga ila akachelewa kukoga josho. Je anaweza kufunga?
JIBU
Ndio anaweza kufunga. Kitakachomlazimu ni kukoga josho kabla ya kutoka kwa swala ya alfajiri ili asiache swala na ataendelea na funga yake. Na Allah ni mjuzi zaidi.

Hayo ndio masharti ambayo yanalazimika kutimizwa ili funga ya Muislamu isihi. Na kinyume cha masharti hayo ni kubatilika kwa funga hiyo. Na kama tulivyoeleza itamuwajibikia mtu huyo kulipa. Ama yule ambae kwa sababu ya kufanya tendo la ndoa yeye itamuwajibikia kulipa pamoja na kafara. Na Allah ni mjuzi zaidi.