Monday, 31 March 2014

Matumizi Ya ‘In Shaa Allaah’ Ndani Ya Du’aa


Shaykh Swaalih Al-Fawzaan

Imetafsiriwa na ‘Abdun-Naaswir Hikmany

Haifai, pale Muislamu anapomuomba Allaah kusema, “Ee Allaah nisamehe iwapo utapenda!” Pindipo unapoomba kitu kutoka kwa Allaah, mtu asifanye du’aa yake kuwa na shaka katika uwezo wa Allaah, lakini kinyume chake ni lazima awe na uhakika wa dhana njema kwamba Allaah Ataijibu du’aa yake. Imenukuliwa kutoka Hadiyth sahihi iliyosimuliwa na Abu Hurayrah akisema:

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Asiseme mmoja wenu ‘Ee Allaah! Nisamehe iwapo Unapenda; Ee Allaah, kuwa na Rahmah kwangu iwapo Utapenda,’ lakini ni lazima awe na matumaini kwa Allaah yenye uhakika, kwani hakuna mtu anayeweza kumlazimisha Allaah kufanya kitu dhidi ya Uwezo Wake.)) [Imepokewa na Muslim]

“Kuomba kwa Allaah pamoja na yakini” inamaanisha kwamba mtu asimuombe Allaah kwa maneno ya ‘lakini’ au ‘iwapo’ lakini anatakiwa afanye maombi ya uhakika na kutilia mkazo katika jambo hilo. Inakatazwa kutumia maneno kama hayo kwa hoja mbili:

· Hakuna mtu mwenye nguvu ya kumlazimisha Allaah kufanya kitu Asichokitaka; Anafanya tu kile Anachokitaka. Tofauti na Allaah, waja wanaweza kulazimika kufanya vitu kutokana na hofu na mfano wa hayo.

· Kufanya maombi katika hali ya kuwa na shaka kwa Uwezo wa Allaah inaonesha udhaifu wa maombi na ukosefu wa hamu ya kuipaita du’aa hiyo jibu; ukosefu wa yakini katika hapa unamaanisha kwamba mtu hana haja ya Allaah.

Katika simulizi nyengine iliyopokewa na Muslim, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anathibitisha kwamba du’aa ifanywe kwa yakini kamilifu, na mtu asisitize moja kwa moja hamu yake (mbele ya Allaah) ndani ya du’aa zake, kwani hakuna baraka iliyo kubwa kwa Allaah itakayomshinda kubariki (juu ya waja Wake), hata kama baraka hii itaonekana kuwa ni kubwa mno mbele ya macho ya wengine. Allaah, Mtukufu, Anasema:

{{Hakika amri Yake anapotaka chochote (kile kitokee) ni kukiambia: ‘Kuwa’, basi mara huwa.}} [Yasiyn: 82]

Hivyo, Muislamu anahitajika kuwa na ufahamu wa kina kuhusiana na masharti ya imani ya kweli na halikadhalika mambo yanayobatilisha tawhiyd, ili kwamba aweze kumuabudu Allaah katika misingi thabiti.

Imechukuliwa kutoka Kitabu cha Shaykh Swaalih Al-Fawzaan ‘Muongozo Wa  Itikadi Sahihi’ Guide to Muslim Creed, chapa ya mwaka 2005, ukurasa wa 139 -141.

No comments:

Post a Comment