Imetayarishwa na www.alhidaaya.com
Tutakuwa pamoja nanyi tukizungumzia moyo wenye huruma, moyo wenye ulaini, moyo ulio umbiwa huruma. Tutakuwa tukizungumzia moyo ambao umeumbwa siku ulipoumbwa, ukapandikizwa huruma, tutakuwa na moyo wenye kuhurumia hata kama unafanyiwa ukali. Je, mmeufahamu moyo huo? Hakika si mwingine bali moyo huo ni mama.
Tunamzungumzia mama ambaye maadui wa Allaah wamemuwekea siku moja tu na wakaiita "siku ya mama" na hili si katika Uislamu kwa chochote. Uislamu umeamrisha kumfanyia wema mama (kila siku) mwaka mzima.
Huyo ndiye mama enyi waja wa Allaah. Kiumbe ambaye ameendelea kuwa mbele na mshindi daima.
Mama yako enyi waja wa Allaah, ni mara ngapi amehuzunika (ameingia katika jambo la kumhuzunisha) ili wewe ufurahi, na akashinda au kulala njaa ili ushibe, na akalia ili ucheke, na akakesha ili ulale, na akabeba mambo magumu na mazito katika njia ya furaha yako (ili ufurahi). Unapokuwa umefurahi naye ndipo hufurahi, na ukihuzunika, umemhuzunisha, ukipatiwa na mfadhaiko, basi maisha yake yako katika shida kubwa. Matumaini na matarajio yake, yako katika shida kubwa. Matumaini na matarajio yake (yote) ni wewe uishi maisha ya kiungwana (matukufu) ya kuridhisha yenye kuridhiwa.
Mama kiumbe dhaifu ambaye hutoa bila kutaraji malipo yoyote. Anayemimina (kheri zake zote kwako) bila kutumai shukrani zozote kwako. Je umewahi kumsikia kiumbe anayekupenda kuliko mali yake? Hapana, bali zaidi kuliko dunia yake? Hapana bali zaidi kuliko nafsi yake iliyopo kati ya mbavu zake? Ndio, anayekupenda zaidi kuliko nafsi yake, hakika huyo si mwengine bali ni mama yako, mama pekee ndio alama ya huruma.
Hebu fikiria kwa makini ewe ndugu yangu mpendwa, hali uliyokuwa nayo udogoni mwako (fikiria) kumbuka udhaifu wa uchanga wako, hakika alikubebea mimba tumboni mwake miezi tisa kwa hali ya unyonge (udhaifu) juu ya unyonge. Amekubebea mimba kwa taabu na akakuzaa kwa taabu, kuendelea kukua kwako tumboni mwake kulimzidishia udhaifu na anabeba mzigo (taabu) zilizo nje ya uwezo wake, na mama (kama alivyo mwanamke mwengine) ni mdhaifu wa kiwiliwili, mnyonge wa nguvu, na wakati wa kujifungua huyaona mauti mbele ya macho yake, machozi na masikitiko, vikwazo na machungu, lakini yeye anajilazimisha kusubiri (mpaka anakuzaa) na pale tu anapokuona u-pembeni mwake na akakukumbatia kifuani mwake, na akashumu (akanusa) harufu yako, na akazihisi pumzi zako zikikariri (kuingia na kutoka), basi husahau maumivu yake yote, na husahau machungu yake yote.
Anakuona na kufungamanisha matumaini yake yote kwako. Na huona kwako uzuri wa maisha na mapambo yake, kisha anageukia kukuhudumia mchana wa maisha yako na usiku wake. Akikulisha kwa ajili ya siha yako, na akikukuza kwa kujichakaza (kujizeesha) yeye, na kukuimarisha (kukutia nguvu) kwa kujidhoofisha yeye, chakula chako ni chuchu zake, nyumba yako ni mapaja yake, na gari lako ni mikono yake (au mgongo wake). Amezunguka na kukuchunga (usipatwe na balaa lolote). Yuko radhi yeye abaki na njaa ili wewe ushibe, na akeshe ili ulale, na yeye kwako ni mwenye huruma nyingi. Na ana uchungu mwingi juu yako, akikaa mbali nawe (kidogo tu) unamuita, na akikupa nyongo unamuomba akuelekee. Na likikupata la kukuchukiza unaomba wokozi kwake. Unadhani kheri zote (kila jambo zuri) ziko kwake tu. Na unadhani shari haitokufikia akikukumbatia kifuani mwake, au akiwa anakuangalia kwa jicho la mazingatio.
Na baada ya kutimia kuacha kwako ziwa ndani ya miaka miwili (mara nyingi), na ukaanza kutembea huanza kuuzungusha umuhimu wake wote kwako, na macho yake hukufuatilia (popote uendapo). Hukufuatilia haraka nyuma yako kwa kukuhofia (kuanguka na mengineyo) kisha ukakua, na kuchukua kwako miaka. Ikampata na kumuingia shauku na huruma, sura yako ni nzuri zaidi mbele yake kuliko mwezi unapokamilika (duara lake), sauti yako kwake ni tamu zaidi masikioni mwake kuliko sauti za bulbul na nyimbo za ndege wengine. Harufu yako inanukia vizuri zaidi kwake kuliko manukato yote na maua yote, utukufu wako ni kitu cha ghali sana kuliko dunia, lau itapelekwa kwake pamoja na mapambo yake yote hakuna kitu ghali, bali kila kitu ni rahisi kwake katika kuhakikisha unapata raha. Mpaka hata nafsi yake iliyopo kati ya mbavu zake mbili si lolote si chochote, na huchagua kufa ili wewe uishi salama salimini mwenye afya tele!!
Ni Mama Yako Ewe Mja Wa Allaah
Hebu sikiliza kwa makini ewe mja wa Allaah, na ujue ya kwamba aliyenyimwa kheri, aliyepotea na kuruka patupu (kula hasara) duniani na Akhera, ni yule atakayepoteza haki za wazazi wawili na hasa hasa mama.
Amepokea Hadiyth Imaam Ahmad na An-Nasaaiy na Ibn Maajah, kutoka kwa Mu'awiyah Ibn Jahimah As-Salamiy (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema. Nilimuendea Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (siku moja) na nikamwambia; Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi nahitaji kupigana jihadi pamoja nawe, nikitaraji kupata radhi za Allaah na nyumba ya akhera, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma (Usifanye Hivyo), hivi yuko hai mama yako?)) Nikasema: Ndiyo. Mtume akasema: ((Rudi ukamfanyie wema usiende kupigana Jihadi)). Kisha nikamuendea kupitia upande mwingine, nikamuambia: Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi nataka kupigana Jihadi pamoja nawe, nikitafuta kwa hilo radhi za Allaah na nyumba ya akhera, Mtume akasema ((Nakuhurumia, usifanye hivyo, je mama yako yu hai?)). Nikasema ndiyo ewe Mtume wa Allaah. Mtume akasema: ((Rudi kwake ukafanye wema)). Kisha nikamuendea kwa mbele yake nikasema: Ewe Mtume wa Allaah, hakika mimi nataka kupigana jihadi pamoja nawe, nikitafuta kwa hilo radhi za Allaah na nyumba ya akhera, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma, usifanye hivyo, Mtume akasema: ((Nakuonea huruma, jilazimishe na mguu wake hapo ndipo palipo na pepo)), Hakika mama ni pepo namuapa Mola wa al-Kaabah, Lazimiana (shikamana) na mguu wake hapo ndipo ilipo pepo)).
Imepokewa Hadiyth (nyingine) kutoka kwa Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: Mtu mmoja alimjia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na akasema: Ewe Mtume wa Allaah, mimi nimekuja nataka kupigana jihadi pamoja nawe nikitaraji radhi za Allaah na nyumba ya akhera, na kwa hakika nimekuja, huku wazazi wangu wawili wanalia; Mtume akasema: ((Rudi kwao ukawachekeshe kama ulivyowaliza)). [Ameisimulia Ibn Maajah na akaisahihisha Al-Albaaniy].
Na kutoka kwa Anas bin Nadhwiri Al-Ashijainiy amesema: Siku moja mama yake Ibn Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anha) alitaka maji ya kunywa na ilikuwa usiku – kwa mwanawe Ibn Mas'uud, akaenda kumletea maji, kurudi akamkuta keshalala, Ibn Mas'uud akabaki amesimama na maji mbele ya kichwa chake mpaka asubuhi, na walipofika Abu Muusa Al-Ash'ariy na Abu 'Aamir kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakampa Bay'ah (kiapo cha utii) na wakasilimu. Mtume akawauliza (amefenya nini yule mwanamke, miongoni mwenu aitwaye kadhaa wa kadhaa? Mtume akasema: (Kwa sababu ya kumtendea mama yake akasema, alikuwa ana Mama bibi kizee, mara akawajia muonyaji akisema, hakika adui anakusudia kuwadhuruni, Mama huyu (Mama Ibn Mas'uud) akambeba mama yake mgongoni mwake, akichoka anamtua chini (anapumzika) kasha anakutanisha tumbo lake na tumbo la Mama yake (yaani anambeba kwa kumkumbatia tumboni) ikawa miguu yake iko chini ya miguu ya Mama yake kutokana na kumkinga na joto kali, mpaka akaokoka na adui yule). [Ameitoa 'Abdur-Razaaq katika Muswannaf yake].
Huyo ndiye Mama, ewe mwenye kutaka kuokoka, basi lazima ana miguu yake, hapo ndipo ilipo pepo yake.
Waja Wema Na Kuamiliana Kwao Na Mama
Siku moja Ibn 'Umar alimuuliza mtu mmoja, je, unaogopa kuingia motoni? Na unapenda kuingia peponi? Yule mtu akasema ndiyo. Ibn 'Umar akamwambia: Basi mfanyie wema Mama yako, kwani namuapa Allaah, Kama utamlainishia maneno na ukamlisha chakula, hakika utaingia peponi endapo utajiepusha na madhambi makubwa yenye kuangamiza.
Hakika kuwafanyia wema wazazi wawili ni tabia ya watu wema, na ni mwendo wa wacha-Mungu. Inasimuliwa kuwa siku moja Ibn Al-Hasan At-Tamiymiy alimpiga Ng'e akaingia shimoni na yeye akaingiza kidole chake nyuma yake ndani ya hilo tundu, ng'e akamgonga kwa mwiba wake wa sumu; akaulizwa kuhusu jambo hilo? Akasema: "Nilihofia asije akatoka na kumgonga mama yangu''
Na amesema Muhammad Ibn Siyriyn: ''Ulifikia mtende mmoja wakati wa Khalifa 'Uthmaan kuuzwa kwa Dirhamu elfu moja. Usaamah bin Zayd akajitahidi akanunua mtende mmoja akautoboa na kutoa utomvu wake akamlisha Mama yake. Watu wakamuliza, ni kipi kilichokupelekea kuuchezea mtende namna hii na wewe unaona mtende umefikia kuuzwa ghali namna hii; dir'hamu alfu moja? Akasema: "Hakika mama ameniomba. Na hawezi Mama yangu kuniomba kitu chochote ninachokiweza isipokuwa nitampa).
'Abdullaah bin 'Awn nae siku moja aliitwa na mama yake, na yeye akanyanyua sauti yake ikawa juu ya sauti ya mama yake. Kwa kosa hilo tu akaamua kuadhibu nafsi yake kwa kuacha huru watumwa wawili!
Na Zaynul-'Aabidiyn (pambo la wacha Mungu) naye alikuwa ni mtu mwenye kufanya wema sana kwa mama yake. Lakini hakuwa akila naye sahani moja, siku moja akaulizwa mbona wewe ni mwenye kufanya wema kwa mama yako kuliko watu wote lakini hatukuoni ukila nae sahani moja? Akajibu akasema: "Ninaogopea mkono wangu kutangulia kufika pale mahali lilipotangulia kuona jicho lake hivyo nikawa nimemvunjia heshima" Hakika washatangulia mbele yetu watu hawakuwa akirefusha mmoja wao nyumba yake kupita kimo cha mama yake!!
Hakika ni pepo, ewe mtafuta pepo lazimiana (shikamana) na nyayo zake hapo ndipo ilipo pepo.
Amepokea Hadiyth hii At-Tirmidhiy na akaisahihisha kutoka kwa Abu Dardaa (Radhiya Allaahu 'anhu) amesema: nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: ((Mzazi ni mlango wa katikati ya milango ya pepo, ukitaka upoteze mlango huo au uhifadhi)).
Na katika At-Tirmidhiy, kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Radhi za Mola zinatokana na radhi za mzazi, na chuki zake zinatokana na chuki za mzazi))
Amesema Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhu): "Hakuna Muislamu yeyote mwenye wazazi wawili Waislamu akaamka akitaka thawabu kwa Allaah kupitia kwao, isipokuwa Allaah Hufungua milango miwili – yaani katika pepo na ikiwa ni mmoja basi utafunguliwa mmoja, na akimkasirisha mmojawapo, Allaah Hatomridhia mpaka mzazi amridhie). Akaulizwa hata kama wamedhulumu? Akasema: Hata kama wamedhulumu.
Anasema mshairi mmoja:
Mama yako ana haki kubwa sana kwako lau ungejua,
kingi chako wewe huyu mbele yake ni kichache.
Ni masiku mangapi amekesha akishitakia shida zako,
kwake akakesha akiungulia moyo wake na kupiga makelele.
Na wakati wa kujifungua hujui mazito yanayompata,
hivyo kwa yanayomkwaza nyoyo zinakaribia kuruka.
Na ni mara ngapi amekuoshea uchafu kwa mkono wake wa kulia,
na halikuwa paja lake kwako ni kitanda.
Na ni mara ngapi amepata njaa na akakupa chakula chake,
kwa sababu ya huruma na uchungu kwako ukiwa mdogo.
Ukamtupa pale ulipomfanyia ubaya katika hali ya ujinga,
na likarefuka kwako jambo na hali ya kuwa yeye ni mfupi.
Majuto ni kwa yule aliyeelewa (ubora wa mama) lakini akafuata matamanio,
na majuto ni kwa kipofu wa moyo hali ya kuwa macho yanaona.
Basi jipendekeze katika kukithirisha kumuombea dua,
kwani wewe unaloliomba una haja nalo zaidi.
Siku moja Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) alimuona mtu mmoja M-yemen akitufu Al-Ka'abah huku amembeba mama yake mgongoni mwake huku akisema: Hakika mimi ni ngamia wake aliyedhalilishwa, ikiwa abiria wake watamkorofisha, basi mimi siogopi, Allaah ndiye mola wangu mwenye utukufu mkuu, nimembeba mara nyingi zaidi kuliko alivyonibeba, Je, ewe Ibn 'Umar unahisi nitakiwa nimeshamlipa? Ibn 'Umar akasema: ''Hapana, hujamlipa hata pumzi moja''
Nasaha kwa wale wanaowafadhilisha (wanaowatanguliza) wake zao kuliko mama zao;
Na kwa wale wanaowapa wake zao na kuwanyima mama zao.
Usimtii mke ukamkata mama juu yako, ewe kijana wa ndugu yangu umepoteza umri wako.
Ni vipi unamkana mama wakati mimba yako kaibeba yeye, tena umegaragara mapajani mwake kwa uzito.
Na akauguza maumivu ya nafsi kwa ajili yako na ni kwa kiasi gani, alifurahi alipozaa mtoto wake akawa ni mwanamme.
Na hakuonyesha mpaka miaka miwili iliyokamilika, na huku akitaka kunyeshelezwa katika kifua chake na matiti yake ya lulu.
Na kile ulichokinyonya kutoka kwake unakitoa na kumchafua, bila yeye kulalamikia uvundo wa uchafu.
Na ameamiliana nawe kwa wema na malezi mema mpaka, umelingana sawa na mpaka umekuwa namna unavyojiona.
Hivyo usimfadhalishe mke kuliko yeye milele, na wala usiache moyo wake ukivunjika kwa kumtenza nguvu.
Mzazi ndio mlezi wa kwanza hilo halipingiki, mlinde hasa hasa akifikia utu uzima.
Huwezi kumtekelezea haki zake zilizo juu yako hapo, juu ya macho yako amehiji nyumba tukufu na akafanya 'Umrah.
Enyi waumini, ni masaa mangapi Muislamu ametumia kuwatimizia haja wazazi wawili, kwa hilo Allaah Amekuondolea mawazo ya kufadhaisha shida, ni wangapi katika mtoto wa kiume mwema kwa wazazi wake au msichana mwema kwa wazazi wake, wamesimama mbele ya wazazi wao baada ya salamu au maneno mazuri au zawadi kwa unyenyekevu, huku imefunguliwa milango ya mbingu kwa ajili ya maombi yao yenye kujibiwa kutoka kwa wazazi wao wawili walio dhaifu waliozeeka.
Hivyo mcheni Allaah kwa wazazi wawili, hasa hasa wanapofikia umri mkubwa na uzee kiasi walipofikia, na kudhoofika kwao mifupa, na kichwa kuwaka mvi, watakapokuwa wamefikia hali waliyoifikia na wakawa wanakuangalia muangalio ambao unangojea tonge kwa furaha au kipawa cha malipo.
Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) anasema katika Qur-aan Suratul Al-Israai aya ya 23 kwamba:
{{Amehukumu mola wako kuwa asiabudiwe (yeyote) isipokuwa Yeye (tu) na wazazi watendewe wema, kama mmoja wao amefikia uzee (naye yuko) pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata aah! Wala usiwakemee, na useme nao kwa msemo wa heshima}}
Hali Ya Mama Na Watoto Wake Katika Maafa Ya Moto
Anahadithia mmoja wa askari wanaofanya kazi katika kitengo cha ulinzi wa mji (zimamoto) akasema: "Hakika wao walifika katika nyumba moja inayowaka moto na ndani yake alikuwepo mama mmoja na watoto wake watatu. Moto ulianzia katika moja ya vyumba (vya nyumba ile) akajaribu yule mama kutoka kupitia milangoni lakini akakuta milango (yote) imefungwa. Akapanda haraka pamoja na watoto wake watatu mpaka sehemu ya juu ya nyumba ili atokee kupitia mlango huo, akaukuta umefungwa vile vile. Akajaribu kila njia bila mafanikio, akarudia rudia mpaka akachoka. Moshi nao ukapaa na kuenea nyumba nzima, wakawa wanahema kwa taabu. Mama akaamua kuwakumbatia watoto wake akawakumbatia kifuani mwake, na hali ya kuwa chini ili usije ukawafikia moshi mzito. Na mama wa huruma anauvuta moshi huo yeye (lakini si wanae). Baada ya kufika vikundi vya uokozi juu ya nyumba wakamkuta amedondoka (amelalia) tumbo lake, wakamyanyua mara wakawaona watoto wake watatu chini yake wakiwa maiti!!. Kama vile ndege anayewafunika mbawa vifaranga vyake akiwaepusha na hatari. Akiwakinga na adui mvunjaji. Wakakuta ncha za vidole vya mkono wake vimevunjika, kwani alikuwa mara akijaribu kufungua mlango, kisha anarudi kwa watoto wake ili kuwakinga na muwako wa moto na mpalio wa moshi kwa mara nyingine, mpaka akafa na watoto wake wakafa!
Katika picha inayopamba uzuri wa kujitoa muhanga, katika ubao uliohifadhiwa kwa rangi za huruma na kunakishiwa na unyoya wa upole na huruma. Pamoja na kujitolea na juhudi zote hizi na aina mbalimbali za kuhifadhi na ulinzi ambao mama anautoa kwa mwanae na kwa kipande cha ini lake, mpaka akasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika kubainisha ukubwa wa haki ya mama pamoja na baba: ((Mtoto hawezi kumlipa mzazi wake kwa wema aliomtendea isipokuwa, amkute akiwa mtumwa na kumnunua kisha amwache huru)). [Ameisimulia Imaam Muslim].
Pamoja na mapenzi yote haya yenye kububujika na upole mwingi na huruma yenye kuchupa tunasikia na tunaona aina mbalimbali za ugomvi na ukanaji wa wema, na ususuwavu wa moyo wa kushangaza, na ukali wa kutisha, na ubaya wa matendo, na ubaya wa kuamiliana (na wazazi) kiasi cha kutokuingia akilini (akili yoyote) wala kubebwa na moyo wowote (kuvumiliwa).
Barua Ya Mama Kwa Mwanawe
Hebu soma hii barua iliyoandikwa kwa wino wa machozi kutoka kwa mmoja wa akina mama.
Barua yenyewe hii hapa aliyoiandika Mama mmoja kwa wino wa machozi yake. Barua ameituma "Mama Makluumah" kwa kijana wake ambaye ni kama manukato ya moyo wake, maskini yule mama anasema:
"Ewe kijana wangu, tangu miaka ishirini na tano (iliyopita) ilikuwa ni siku yenye mwanga katika maisha yangu pale aliponifahamisha Daktari wa kike kwamba mimi ni mja mzito. Na akina mama ewe mwanangu, wanajua vizuri maana ya hili neno (uja uzito) nalo linaleta maana ya kuchanganyika na furaha na ni mwanzo wa matatizo na mabadiliko ya kinafsi na ya kimwili kwa mama na baada ya ishara hii ya kuwa mja mzito ewe mwanangu-nikakubeba miezi tisa tumboni mwangu kwa furaha, (nilitaka kusimama) nasimama kwa taabu na ninalala kwa shida, na ninakula udongo, na ninapumua kwa uchungu, lakini yote hayo hayakunipunguzia mapenzi yangu kwako na furaha yangu kwako, bali yakamea mapenzi ya kukupenda kadri siku zinavyosonga mbele.
Na ikakuwa shauku kwako. Nimekubeba ewe mwanangu juu ya uchungu, isipokuwa mimi pamoja na yote hayo nilikuwa nikifurahi na kufurahi kila ninapohisi kutingishika kwako ndani ya tumbo langu, na ninafurahi kwa kuongezeka uzito wako pamoja na kwamba ni mzigo mzito sana kwangu, hakika yalikuwa ni mateso ya muda mrefu, mara ikafika baada ya hayo yote Alfajiri ya usiku ule ambao sikulala ndani yake, na wala sikufumba jicho, na ukanikuta uchungu na shida na hofu na woga ambao kalamu haiwezi kuandika (kusifia) wala ulimi kuelezea, na nikaona kwa mboni ya jicho langu- namuapa Allaah ewe mwanangu nikayaona mauti yakinijia mara nyingi, mpaka ukawa umetokea duniani! Yakachanganyika machozi ya kilio chako na machozi ya furaha yangu. Na yakaondoka machungu yangu yote na majeraha yake. Ewe mwanangu, ikipita miaka katika umri wangu nikiwa nakubeba, moyoni mwangu na ninakuosha kwa mkono wangu, nikajaalia mapaja yangu kuwa kitanda chako. Na kifua changu kuwa ni chakula chako, nimekesha usiku wangu ili ulale, nimetaabika mchana wangu ili uwe muungwana, utukuke, matamanio yangu ni kuona tabasamu lako, na furaha yangu kila wakati ni kukuona unanitaka nikufanyie kitu chochote. Huo ndio mwisho wa utukufu wangu. Siku zikapita na mausiku yakapita nami nikawa katika hali hiyo, nikawa mtumishi bila kupunguza utumishi wangu. Na nikawa mnyonyeshaji asiyesimamisha huduma yake. Na nikawa mfanyakazi asiyechoka, mpaka ikakomaa miguu yako na kulingana sasa ujana wako, na zikaanza kuonekana kwako alama za kiume, mara nikaanza kwenda mbio kulia na kushoto ili kukutafutia mke umtakae, ukafika muda wa ndoa yako, moyo wangu ukakatika na yakatirizika machozi yangu kwa furaha kwa ajili ya maisha yako mapya yenye utukufu, na nikawa mwenye huzuni kwa kutengana na wewe. Yakapita masaa mazito, mara wewe sio yule mwanangu niliyemjua. Hakika umenikana na umejisahaulisha haki zangu, yanapita masiku sikuoni na wala sisikii sauti yako, umeshindwa kumuelewa mtu aliyesimama kidete kwa ajili yako, umemsahau Mama yako.
Ewe mwanangu sihitaji kwako ila kitu kidogo tu. Nifanye mimi ni katika marafiki zako na machoni kwako, na wengine wasogeze hatua moja mbele yako.
Nifanye Mimi ewe mwanangu, ni moja ya vituo vya maisha yako ya mwezi ili nikuone humo japo kwa dakika chache. Ewe mwanangu, mgongo wangu umepinda, na viungo vyangu vimedhoofika, na maradhi yamenikondesha, na yamenitembelea maradhi, sisimami ila kwa taabu, na sikai ila kwa mashaka, na haukuacha moyo wangu ukizingazinga kwa mapenzi yako, kama angekukirimu mtu yeyote siku moja ungemsifu kwa kitendo chake kizuri alichokufanyia. Na ewe mwanangu Akulinde Mola wangu, mama amekufanyia wema (ihsani) ambayo huioni, na wema ambao hutaki kuulipia; hakika amekutumikia na kulisimamia jambo lako miaka na miaka, basi yako wapi malipo yake?! Umefikia upeo huu na kuwa na moyo mgumu kiasi hiki, na masiku yakakuzuia kiasi hiki kuja kuniona?!
Ewe mwanangu, kila nikifahamu kwamba wewe ni Muungwana katika maisha yako, furaha yangu huzidi, lakini naona ajabu na hali yakuwa wewe ni bidhaa iliyotengenezwa na mkono wangu, na kujiuliza ni kosa gani nimelifanya mpaka nimekuwa adui yako huwezi kuniona na kuwa mzito kwangu?!
Siwezi kupelekea mashtaka yako kwa Allaah, wala huzuni zangu kwa sababu nikiyapeleka juu ya mawingu na kuyakokota mpaka katika mlango wa mbingu, utapatwa na shari ya kugombana na wazazi, na adhabu itakuteremkia, na utashuka nyumbani kuwa kipande cha ini langu na manukato ya maisha yangu na furaha ya dunia yangu.
Zinduka ewe mwanangu, mvi zimeanza kuenea kichwani mwako, na itapita miaka kisha utakuwa baba mzee, na malipo yanategemea matendo, utakuja andika barua nyingi kwa mtoto wako, kwa wino wa machozi kama nilivyokuandikia mimi barua hii. Na kwa Allaah watakusanyika wagomvi wote ewe mwanangu, mche Allaah kwa Mama yako, mfutie machozi yake, na mpungizie huzuni yake, ukitaka baada ya hapo chana barua yake, na elewa ya kwamba yeyote mwenye kutenda wema, ni kwa ajili ya manufaa ya nafsi yake na mwenye kufanya ubaya ni kwa madhara yake mwenyewe.
(Imetokana na khutbah ya Maazin At-Tuwayjiriy amesema; "nilimuuliza Al-Hasan Al Baswriy: "Ni ipi dua (maombi) ya mzazi kwa mwanae? Akasema Al-Hasan "Ni kuokoka" akasema, nikamuliza tena na kwake (kwa mzazi)? Akasema: "Kuangamia kwake (Yaani mzazi humuombea mwanae kuokoka na kila balaa, lakini mtoto humuombea mzazi wake afe haraka ili apumzike na kero zake)!
Haki Za Mama Yako Anazodai Kwako
Hakika haki za mama kwa mtoto ni kubwa mno, usimuite kwa jina lake, bali muite kwa jina analolipenda au kun-yah (yaani 'mama fulani') usikae kabla yake, na wala usitembee mbele yake, kutana nae kwa uso mchangamfu, busu kichwa chake na shum mkono wake, na ukimnasihi basi ni kwa mema bila ubaya (usimuudhi) itika wito wake pindi akuitapo bila kumkemea au kumkirihisha. Zungumza naye kwa maneno laini, mlishe akiwa na njaa, au akitamani kitu japo utafika mbali katika kutafuta mletee, mpe zawadi kabla hajakuomba chochote, hisi anachokipenda umpe, kuwa mtumishi mtiifu kwake, mtii katika mambo ambayo si maasi, usimtanulie katika kula au kunywa, umfurahishe kwa kumuombea usiku na mchana rehema na msamaha, funga jicho lako kuhusu makosa yake na kuteleza kwake, usisikitike au kumhadithia makosa yake na kwa mtindo wa kumshtaki au kumshinda.
Muheshimu Mama yako na umkirimu, usimfanyie kibri wewe si chochote si lolote mbele yake kwani uliishi kati ya mapaja yake na mikono yake. Muingizie furaha, kaa naye kwa wema, taka dua kwake kwani milango ya mbingu hufunguliwa kwa ajili yake.
Mama Yako Baada Ya Kifo Chake
Ndugu yangu mpendwa, jua Akurehemu Allaah ya kwamba, hakika kuwatendea wama wazazi wawili hakuishi kwa kifo chao, kwani imepokelewa Hadiyth kutoka kwa Abu Usaydi As-Sa'adiy amesema: "Wakati sisi tuko mbele ya Mtume, mara ghafla akamjia mtu mmoja kutoka kwa Banu Salimah akasema: "Ewe Mtume wa Allaah, je, kumebakia chochote katika wema kwa wazazi wangu wa kuwafanyia baada ya kifo chao? Mtume akasema: ((Ndiyo! Ni kuwaombea rahma kwa Allaah na kuwaombea msamaha na kutekeleza ahadi zao baada yao, na kuunga undugu ambao hauungwi kwa wao, na kuwaheshimu marafiki zao))
Wema kwa wazazi wawili unaendelea katika kizazi cha mwanadamu na kinachofuata baada yake, imepokelewa kutoka kwa Ibn 'Umar, amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((wafanyieni wema wazazi wenu, nanyi watoto wenu nao watajiheshimu))
Vile vile wema kwa wazazi wawili unazidisha umri (Akipenda mwenyewe Allaah) kwani imepokewa kutoka kwa Sahal bin Mu'aadh, ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Yeyote atakayewatendea wema wazazi wake wawili, kheri nyingi sana ni zake yeye, Allaah Atamzidishia umri wake))
Tunamuomba Allaah Atusaidie kuwafanyia wema wazazi na kuwatii na kuwafanyia Ihsani wakiwa hai na wakiwa wamekufa, na asitufishe isipokuwa pale atakapokuwa Yu radhi na sisi, na tunamuomba Allaah Azishushe Rahma na Baraka na Amani Zake kwa Muhammad na kwa ahli zake na Maswahaba.