Muhammad Baawazir
Ndugu Waislam, baada ya kuuaga mwezi mtukufu wa Ramadhwaan, ambao umejaa fadhila nyingi na kheri zisizopatikana katika miezi kumi na moja iliyobaki, kuna umuhimu mkubwa wa kuendeleza zoezi hili la Funga baada ya mwezi huu mtukufu hususan, na kwa mwaka mzima kwa ujumla In shaa Allaah.
Swawm kwa ujumla na Swawm za Sunnah haswa ni jambo kubwa sana la ki-'Ibaadah. Na ni bora sana ieleweke ndugu zangu, kuwa Swawm si 'Ibaadah ifanyikayo katika mwezi wa Ramadhwaan pekee, bali ni jambo ambalo linalofanyika mwaka mzima katika nyakati mbalimbali kama tutakavyoona katika makala haya.
Kama ilivyo katika ‘Ibaadah ya Swalah, kuna Swalah za Sunnah au Rawaatib au Nawaafil, ambazo ndizo zitakazokuwa viraka siku ya Qiyaamah wakati zile Swalah za Fardh zitakapopelea katika Mizani. Nazo Swawm za kujitolea au za Sunnah, ndizo zitakazomuongezea mja thawabu na ujira pamoja na ile Swawm yake ya Fardh ambayo ni Ramadhwaan.
Hapa chini tutaziorodhesha Swawm za SUNNAH ambazo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kazipendekeza kwetu tuzitekeleze:
SWAWM YA SIKU SITA ZA MWEZI WA SHAWWAAL
Swawm hii inafuatia moja kwa moja baada ya mwezi wa Ramadhwaan na siku ya 'Iyd ul Fitr. Na Mtume(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
((من صام رمضان ثم أتبعه ستاً من شوال كان كصيام الدهر)) رواه مسلم و الترمذي و ابن ماجه, أبو داود وأحمد
((Atakayefunga mwezi wa Ramadhwaan, kisha akafuatia kwa kufunga siku sita za mwezi wa Shawwaal, basi atapata ujira wa aliyefunga mwaka mzima)).Imepokewa na ma-Imaam Muslim, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah, Abu Daawuud na Ahmad.
'Ulamaa wanachambua sababu ya kulipwa mja ujira wa mwaka mzima kwa atakayefunga Ramadhwaan na siku sita hizo za Shawwaal, kwa kusema: Jambo zuri hulipwa ujira mara kumi, kwa hiyo mtu akifunga siku 30 za Ramadhwaan atapata ujira mara kumi; nazo zitakuwa 300, ukijumlisha na siku sita za Shawwaal ambazo zikilipwa mara kumi, huwa 60. Kwa hivyo 300 + 60 = 360, mtu atapata hesabu ya mwaka mzima.
Kwa mantiki hii, tunaona kuna umuhimu na ubora mkubwa wa kuifunga Swawm hii ndugu zangu.
SWAWM YA SIKU YA 'ARAFAH (Kwa wale wasio katika Hajj)
Hadiyth ifuatayo inaonyesha uzito na muhimu wa Swawm ya siku hiyo:
عنْ أَبي قتَادةَ رضِي اللَّه عَنْهُ ، قالَ:سئِل رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِوسَلَّم: عَنْ صَوْمِ يوْمِ عَرَفَةَ؟ قال:يكفِّرُ السَّنَةَ المَاضِيةَ وَالبَاقِيَةَ رواه مسلمٌ
Imetoka kwa Abu Qataadah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba aliulizwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Swawm ya 'Arafah akasema ((Inafuta madhambi ya mwaka uliopita na mwaka uliopo)) [Imepokewa na Muslim].
SWAWM YA SIKU TATU KATIKA KILA MWEZI 'AYAAMUL-BIYDHW'
Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
((من صام ثلاثة أيام من كل شهر فذلك صوم الدهر فأنزل الله عز وجل تصديق ذلك في كتابه {من جاء بالحسنة فله عشر أمثالها} فاليوم بعشرة أيام)) رواه الترمذي قال الشيخ الألباني : صحيح
((Yeyote atakayefunga kila mwezi siku tatu,ni sawa amefunga mwaka mzima, kisha Allaah Akashusha Aayah ithibitishayo maneno ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo: {{Atakayetenda jambo zuri basi malipo yake ni mara kumi mfano wake}}. Siku moja kwa malipo ya siku kumi))[Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni Sahihi].
Ukiitazama Hadiyth hii, utakuta makusudio yaliyotajwa kuwa malipo ya Funga hiyo ya siku tatu za kila mwezi, ni sawa na ya mwaka mzima, ni kuwa, ukipiga hesabu ya hizo siku tatu za kila mwezi, mara miezi kumi na mbili ya mwaka, ni sawa na siku 36. Na siku hizo 36 mara 10 ambazo ndizo malipo ya kila siku kwa mara kumi, basi utapata jumla ya siku 360 ambazo ni takriban idadi ya mwaka mzima wa Kiislam. Fadhila zilizoje na Ujira mrahisi kiasi gani wa kuuchuma ndugu watukufu.
Masiku haya matatu, Masiku Meupe ''Ayaamul-Biydhw'', yametajwa katika Hadiyth ifuatayo:
Abu Dharr Al-Ghifaariy anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:
((يا أبا ذر إذا صمت من الشهر ثلاثة أيام فصم ثلاث عشرة وأربع عشرة وخمس عشرة)) رواهالترمذي. قال الشيخ الألباني: حسن صحيح
((Ee Abu Dharr! Endapo utafunga siku tatu za kila mwezi, basi funga siku ya 13, ya 14, na ya 15)) (Hizi huitwa 'Ayaam ul Biydhw' Masiku Meupe kwa sababu katika masiku hayo kunakuwa kweupe zaidi kwa mwanga wa mbalamwezi). [Imepokewa na At-Tirmidhiy na kasema Shaykh Al-Albaaniy kuwa ni Sahihi].
SWAWM YA JUMATATU NA ALKHAMIYS
عن أبي هريرة رضي الله عنه قال: كان رسول الله صلى الله عليه وسلم يصوم الإثنين والخميس وعندما سئل قال: (( تُعْرَضُ الْأَعْمَالُ يَوْمَ الِاثْنَيْنِ وَالْخَمِيسِ فَأُحِبُّ أَنْ يُعْرَضَ عَمَلِي وَأَنَا صَائِمٌ })) رواه الترمذي وقال حديث حسن
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) anasimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akifunga Jumatatu na Alkhamiys. Alipoulizwa sababu ya Swawm katika siku hizo, akajibu: ((Matendo ya Wanaadam huwekwa mbele ya Allaah kila siku ya Jumatatu na Alkhamiys, nami napenda matendo yangu yawekwe mbele ya Allaah nikiwa nimefunga)). [Imepokewa At-Tirmidhiy na kasema ni Hadiyth Hasan].
SWAWM YA SIKU YA TAASU'AANA 'AASHURAA
Hizi ni Swawm za siku ya tisa na ya kumi ya mwezi wa Muharram (Mwezi wa kwanza katika kalenda ya Kiislam). Hizi ni Swawm kwa kumbukumbu na kumshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) kwa kumuokoa Nabii Muwsaa (‘Alayhis-Salaam) pamoja na watu wake, kutokana na balaa la Fir’awn na jeshi lake.
SWAWM NYINGINEZO
Swawm katika mwezi wa Muharram zina fadhila nyingi kama Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alivyomwelezea Abu Hurayrah. pia Swawm katika mwezi wa Sha'abaan, ambapo mama wa waumini 'Aaishah (Radhiya Allaahu 'anha) anasema kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akikithirisha sana kufunga.
NIYYAH
Swawm kama amali zingine, ni lazima kuwepo na Niyyah ndani yake. Niyyah pahala pake ni moyoni, na si kutamka, ukishapitisha uamuzi wa kufunga, basi hiyo yatosha na si kukariri maneno au kutafuta mtu akufundishe namna ya kuitamka Niyyah kwa Kiarabu au vinginevyo kama wanavyodhania baadhi ya watu.
Wa Allaahu A’lam