Mwezi wa Shaaban ni mwezi wa nane katika miezi ya kiislamu. Mwezi huu upo kati ya Rajab na Ramadhan. Rajab na Ramadhan ni katika miezi mitukufu. Ni mwezi ambao Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya ibada. Pia ni mwezi ambao mja autumie katika kujiandaa zaidi na Ramadhani ili asiweze kupoteza fursa ya
Ramadhani ikiwa Allah atamjaalia kufika. Pia husemwa kuwa umeitwa kwa jina la Shaaban kwa sababu ya waaarabu kutawanyika kwao katika kutafuta maji au katika mashambulizi baada ya kutoka mwezi wa Rajab.
Miongoni mwa mambo ambayo yamependekezwa sana mja ayafanye ndani ya mwezi wa Shaaban ni kufunga. Kabla ya kuangalia ubora wa funga ndani ya Shaaban na vipi imethibiti, kwanza tuangalie umuhimu wa mja kufunga siku tu kwa ajili ya Allah. Imepokewa na Abi said Al Khudri (Radhi za Allah ziwe ju yake) amesema: “Amesema Mtume wa Allah "Hakuna mtu yoyote anayefunga siku yeyote katika njia ya Mwenyezi Mungu Mtukufu isipokuwa Mwenyezi Mungu huuweka mbali uso wake na moto kwa siku hiyo aliyofunga miaka sabiini ". Imepokelewa na Bukhari na Muslim. Pia imepokewa na Amri Ibn Abass (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Amesema Mjumbe wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) "Mwenye kufunga siku yeyote katika njia ya Allah moto huwa mbali naye kwa mwendo wa miaka mia moja”.Imepokelewa na Attbraniy
Hadithi tulizozitaja hapo juu zinaonesha wazi uzito wa mja kufunga siku moja tu kwa ajili ya Allah (subhanahu wata‘ala). Hivyo ndugu yangu Muislamu usiwe mzito kwa kusema hizi funga za sunna tu. Kimbilia funga za sunna ili uweze kupata kheri kama hizo. Na zifunge saumu zako kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah (subhanahu wata‘ala).
KUPENDEKEZWA KUFUNGA KATIKA MWEZI WA SHAABAN NA FADHILA YA FUNGA HIYO
Kutoka kwa Bibi Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akifunga hadi tukadhani kuwa hatofungua kamwe, na alikuwa akiacha kufunga hadi tukadhani hatofunga tena. Sijamuona Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) kufunga mwezi mzima kama alivyokuwa akifunga Ramadhaan, na sijamuona akifunga mara nyingi kama alivyofunga katika Shaabaan” Bukhaariy na Muslim.
Kwa hakika Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) alikuwa akikithirisha zaidi kufunga ndani ya mwezi wa Shaaban kuliko miezi mengine yoyote ukitoa mwezi wa Ramadhan. Na katika hili Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) mwenyewe alieleza ni kwa nini hufunga zaidi ndani ya mwezi wa Shaaban. Imepokewa kutoka kwa Usama Ibn Zaid (Radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: Nilisema ewe Mjumbe wa Allah sikukuona ukifunga katika mwezi wowote katika miezi kama siku unazofunga katika mwezi wa Shaaban? Akasema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) Huo ni mwezi ambao watu wameghaflika nao baina ya Rajab na Ramadhan nao ni mwezi ambao (hurufaishwa) hupandishwa ndani yake amali za watu kwa Bwana wa Viumbe na napenda zipandishwe amali zangu na hali ni mwenye kufunga.” Imepokelewa na An-nasai.
Huyu ni kipenzi cha Allah ambae amesamehewa dhambi zake zilizopita na zinazokuja ila alikuwa akijihimu kwa kufunga ili a’amali zake zipelekwe kwa Allah hali ya kuwa amefunga. Je vipi mimi na wewe ambao daima ni wenye kumkosea Allah? Kwa nini na sisi tusijikurubishe kwa Allah kwa kufunga sana ndani ya mwezi wa Shaaban? Isitupite fursa hiyo na tujihimize katika suala zima la kufunga sisi wenyewe pamoja na watu wetu.
JE MTU AKITAKA KUFUNGA MWEZI MZIMA WA SHAABAN INASIHI?
Katika kauli yenye nguvu zaidi wanazuoni wanasema kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kamili ambao ni sunna kufunga. Na hili linatokana na ushahidi kuwa imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas (radhi za Allah ziwe juu yake ) amesema "‘‘Mtume wa Allaah (swalla Allahu alayhi wasallam) hakuwahi kufunga mwezi wowote kikamilifu isipokuwa Ramadhan." (Al-Bukhaariy).
MLANGO WA KUKATAZWA KUFUNGA NUSU YA MWISHO YA SHAABAN
Imekatazwa kufunga katika mwisho wa Shaban kwa nia ya kutozikosa siku za mwanzo wa Ramadhani. Na hili linathbitishwa kuwa imeripotiwa katika Sahihi Bukhari kutoka kwa Abu Hurayrah (radhi za Allah ziwe juu yake) kuwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema: “Kufunga katika mwisho wa Shaaban kumekatazwa ili kuweka tofauti kati ya Swawm za Sunnah na Swawm za faradhi.”
TANBIHI
Wale wenye tabia na mpangilio wa kufunga na ikawa siku za mwisho za Shaaban zimetokezea sambamba na siku ambazo mtu yule kawaida huwa anafunga, kama vile za Jumatatu na Alhamis, au funga ya Nabii Daud au imemkuta akiwa anaendelea kulipa saum ya deni basi hawa wao wanaruhusika kufunga.
MLANGO WA KUKATAZWA KUITANGULIA RAMADHANI KWA SAUMU YA SIKU MOJA AU MBILI
Imepokewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhi za Allah ziwe juu yake) kutoka kwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema : “Asiitangulie mmoja wenu Ramadhani kwa saumu ya siku moja au mbili isipokuwa akiwa mtu alikuwa akifunga saumu yake basi na aifunge siku hiyo” Bukhari na Muslim.
Amesema Tirmidhi (3/69) na wanavyuoni wanaitumia hadithi hii, kwa kuchukia mtu kufanya haraka kufunga kabla kuingia mwezi wa Ramadhani. Ila mwenye kuzoea kufunga siku za jumatatu na alhamisi au siku tatu za kila mwezi au saumu ya Nabii Daud, ikawafiki saumu yake siku hiyo basi na afunge kama kawaida yake kwa sababu makatazo hayamuelekei yeye, kinyume cha mwenye kuanzia kufunga hali ya kuwa si wajibu kwake na wala hatakiwi kulipa wala si ada kwake, haitakiwi kwake kufunga.
Pia Yaumu Shakka kumekatazwa mtu kufunga. Yawmu Shakk (siku yenye shaka) ni ile siku ambayo watu hawana uhakika juu ya kuanza kwa Ramadhan, kwa sababu ya hali ya mawingu kufunga na mwezi kutoonekana au sababu nyinginezo.
Imepokewa kutoka kwa Swila Ibn Zufar “Tulikuwa kwa Ammar Ibn Yaser akaletewa mbuzi wa kuchoma akasema" Kuleni " akakaa mbali mmoja katika watu akasema “Hakika mimi ni mwenye kufunga” akasema Ammar “mwenye kufunga siku ambayo watu huitilia shaka basi amemuasi Abal Qassim (swalla Allahu alayhi wasallam). Bukhari.
Pia Muislamu anatakiwa ajihimu katika kufanya mambo mengine mbali mbali ya kheri kama kuswali swala za sunna, kuleta istighfaar na adhkaaar nyenginezo kwa wingi, kutoa sadaka kwa wingi na kheri nyengine. Haya yote mwenye kuyafanya yatamuandaa katika kuitumia Ramadhani yake vile ipasavyo.
UKUMBUSHO
Wale wote wenye madeni ya swaumu, basi wasiwache kulipa madeni yao. Kwani hairuhusiwi mtu kuchelewesha kulipa deni la Ramadhani hadi ikaingia Ramadhani nyengine. Na mtu anaweza kuzilipa funga hizo ndani ya Shaaban kwa ushahidi kutoka kwa Mama wa Waumini Aysha (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema : “Ilikuwa ninazo siku za kulipa za Ramadhaan na sikuweza kuzilipa isipokuwa (katika mwezi wa) Shaaban.” Al-Bukhaariy.
Yeyote aliyekuwa na uwezo wa kulipa Swawm zilizompita kabla ya Ramadhaan (ya pili) kuingia na asifanye hivyo, basi atalazimika kuzilipa baada ya Ramadhaan (ya pili), pia analazimika kutubia na kumlisha maskini mmoja kwa kila siku iliyompita. Huu ni msimamo wa Imam Maalik, Ash-Shafi’iy na Ahmad.
Ama kuhusu Nisfu Shaaban tutakuja kuelezea katika siku zitakapokaribia in shaa Allah.
Na Allah ni mjuzi zaidi.