Imeandaliwa Na Kuandikwa Na Swaalih Fallaah Al-Mawraqy
Bismi Allahi alrrahmani alrraheemi
KWA JINA LA MWENYEZI MUNGU MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.
Hakika ya kumuomba Mola aliyetukuka aliye juu ni katika vitendo vitukufu na vilo bora.
Amesema Mola aliyetukuka katika ubora wake:
{{Yalaiti iwajiapo adhabu wangenyenyekea kwa kuomba du’aa lakini zimekua ngumu nyoyo zao hazina imaan; Na wamepambiwa na shaytwaan kwa yale wayafanyao.}} [Al-An’aam: 43]
Na akasema Aliyetukuka:
{{Sema kuwaambia hamukukithirisha; kufanya kwa wingi; wala kuzingatia lau mungenyenyekea na kumuomba Yeye katika shida; hakika mumekanusha; mumekataa; kwanini adhabu isiwe lazima kwenu? Mwastahili kuadhibiwa.}} [Al-Furqaan: 77]
Yaani lau musingejali kwa kuomba na kufanya ‘ibaadah kwa wingi.
Na Hadiyth iliyopokewa na at-Tirmidhiy akiisahihisha Shaykh Al-Albaaniy; amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakuna kitu kitukufu kuliko du’aa; kuomba du’aa.))
Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kutaka kujibiwa du’aa na Mwenyezi Mungu wakati wa shida na dhiki, na azidi kufanya kwa wingi wakati wa raha zake kuomba.)) [Imepokewa na at-Tirmidhy akasema Shaykh Al-Albaaniy ni Hasan]
Na imepokewa na Daylamiy kutoka kwa Anas bin Maalik amesema: Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hamfungulii Mola mja Wake kuomba kisha akamfungia mlango wa kujibiwa, Mola ni Mtukufu hawezi kufanya hivyo.))
Na akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Mwenye kushindwa katika watu (yaani mpungufu ama dhaifu) ni yule anayeshindwa katika du’aa (mpungufu ama dhaifu wa kuomba du’aa).)) [Imepokewa na at-Twabraaniy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]
Na amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakuna kinachorudisha hukumu ya Mola isipokuwa du’aa.)) [Imepokewa na At-Tirmidhiy na akaipendezesha Shaykh Al-Albaaniy]
Na Hadiyth hii ni dalili ya kuwa Mola Aliyetukuka na Aliye juu, kulingana na thamani ya du’aa ya kinga aliyo hukumu Mola kwa mja Wake.
Kwa hivyo amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ((Du’aa yanufaisha kwa yaliyoteremka na yasiyoteremka, kutoka kwa Allaah.)) [Imepokewa na al-Haakim kutoka kwa Ibnu ‘Umar]
Na amesema Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuusisitiza Ummah wake katika kuomba kwa kila kitu:
((Hakika ataomba mmoja wenu Mola wake haja zake mpaka uzi wa viatu vyake.)) yaonyesha hatodharau kumuomba hata kwa kitu kidogo mfano gani ataomba. [Imepokewa na at-Tirmidhiy na Ibnu Hibbaan kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ‘anhu).]
Na kujibiwa kwa du’aa kuna sababu nyingi, mwenye kushikana nazo kwa uwezo wa Mola Aliyetukuka na Aliye juu ni sababu ya kuondolewa mazito yake na kutekelezewa haja zake.
Tutazitaja sehemu katika hizo tukitaraji kwa Mola kukubaliwa na kunufaisha.
1) Du’aa uinukapo usingizini usiku ni sababu katika sababu za kujibiwa du’aa. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Imaam Al-Bukhaariy kutoka kwa ‘Ubaadah bin Swaamit (Radhiya Allaahu ‘anhu) zimfikie: Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema:
((Mwenye kuinuka usiku akasema laa ilaaha illa Allaah wahdahu laa shariyka lahu, lahul mulku wa lahul hamdu wa huwa ‘alaa kulli shay-in qadyr, wala hawla wala quwwata illa biLlaah, kisha akasema ee Mola nisamehe, ama aombe atakalo atajibiwa, na akitawadha na kuswali itakubaliwa Swalah yake.))
2) Na katika sababu ya kukubaliwa du’aa ni neno: Hakuna Mola isipokuwa Wewe, umetakasika, hakika mimi nimekuwa katika madhaalimu. Imetoka kwa Sa’ad bin Abi Waqaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema:
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Uombezi wa Dhannuun alipoomba naye yupo tumboni mwa samaki ni:
La ilaaha illa anta subhaanaka inniy kuntu mina dhw dwaalimiyn
Hataomba kwa du’aa hiyo Muislam yeyote kwa neno hilo ila atajibiwa du’aa yake.)) [Imepokewa na Tirmidhiy]
3) Kujiepusha na haraam katika kula kunywa na mavazi. Hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa na kutofanya hilo ni sababu ya kutojibiwa. Kwa kujivisha maasi hiyo ni katika sababu kubwa ya kutojibiwa du’aa.
Amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
((Hakika Mola ni mzuri na hakubali isipokua mazuri... kisha akamtaja mtu aliyekuwa safarini mwake ndefu aliyejawa na vumbi, akainua mikono yake mbinguni: Ee Mola, Ee Mola, na chakula chake ni cha haraam na kinywaji chake haraam, na mavazi yake haraam na nyama yake ya mwili imekuwa kwa haraam. Vipi Mola Aijibu du’aa yake.)) [Imepokewa na Muslim]
Amemuweka mbali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mtu huyu kuwa hatojibiwa du’aa hata akiomba vipi. Kule kuwa mbali kwake na kujibiwa du’aa ni kuwa katika haraam.
Ameifasiri Ibn Rajab Hadiyth hii kuwa ni dalili kubwa kuwa haikubaliwi ‘amali yoyote wala haitakaswi isipokuwa kwa kula halali. Na kula haraam huharibu kitendo cha mtu na kukataza kupokelewa du’aa na Allaah Aliyetukuka.
Imepokewa na Ikrimah bin ‘Ammaar kutoka kwa Asfar kuwa amesema: Aliambiwa Sa’ad bin Abi Waqaas: Kwa nini du’aa zako katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni zenye kujibiwa? Akasema: “Sitii mdomoni kwangu tonge isipokuwa niijue imetoka wapi, na imekuja kivipi.”
Kutoka kwa Wahaab bin Manbah amesema:
“Mwenye kutaka kujibiwa du’aa yake na Mwenyezi Mungu, kiwe halali chakula chake.”
Fanya pupa ewe ndugu Muislam kiwe chakula chako, kinywji chako, na mavazi yako yawe halali, ili upate kujibiwa du’aa yako na uepuke na moto.
4) Kuomba kwa (kutawasali) du’aa zako kwa kuziunganisha na vitendo vyema, basi hiyo ni sababu ya kujibiwa du’aa.
Dalili ya hilo ni Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika swahiyh yake: Kutoka kwa Ibnu ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma): Kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Walikuwa watu watatu wakitembea, ikawanyeshea mvua wakajisitiri katika pango, likafunikika mahali pa kutokea jiwe kubwa katika jabali, wakasema wao kwa wao: Angalieni vitendo vyema mulivyofanya mumuombee navyo Mwenyezi Mungu, huenda Akatufariji. Akasema wa kwanza wao: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na wazazi wawili na mke na watoto wadogo nikiwalea, niwaendeapo na maziwa huwaanzia wazazi wangu nikawanywesha kabla watoto wangu. Nilichelewa siku moja sikuja isipokuwa usiku nikawakuta wamelala nikasimama na maziwa kwa kuchukia kuwaamsha, na kuchukia kuwanywesha watoto kabla yao, nikaendelea kusimama mpaka Alfajiri, ikiwa nililifanya hilo kwa ajili yako tuokoe, likafunguka kiasi kidogo cha kuiona mbingu.
Akasema mwengine: Ee Mola hakika mimi nilikuwa na mtoto wa ‘ammi yangu nikimpenda sana kama vile mwanamume anavyokuwa na mapenzi kumpenda mwanamke. Nikamtaka akanikataa, mpaka siku alitaka dinaar mia, nikamkusanyia kwa taabu nikamletea, nilipotaka kumuingilia aliniambia: Muogope Mwenyezi Mungu ewe mja wa Mungu usiivae pete isipokuwa kwa haki, nikainuka. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, wakafunguliwa.
Akasema mwengine: Hakika mimi nilimuajiri mtu kwa kiasi cha kilo sita ya mchele malipo yake, alipomaliza kazi yake akasema: Nipe malipo yangu, nikampa malipo yake akayakataa, nikawa naikuza kiuchumi mpaka ikaleta faida ya ngo’mbe, akanijia akaniambia muogope Mola wala usinidhulumu haki yangu! Nikamwambia nenda kwa yule ngo’mbe, akaniambia muogope Mungu usinifanyie istihzai (shere), nikamwambia sikufanyii shere mchukue ngo’mbe. Akamchukua akaenda naye. Ikiwa nililifanya kwa ajili yako tuokoe, likafunguka lote na wakatoka Akawaokoa Mwenyezi Mungu
Amesema Wahab bin Manbah: Mfano wa yule anayeomba bila ya vitendo vyema ni kama mrushaji arushae chombo bila ya kamba. Akasema pia vitendo vyema huipeleka du’aa mbinguni. Kisha akasoma neno la Mola Aliyetukuka:
{{Kwake yeye yapanda kila maneno mazuri [mfano wa du’aa, tasbiih, adhkaar, usomi wa Qur-aan]; na vitendo vyema anavipokea, na kupata thawabu mtendaji.}} [Faatwir: 10] Amesema Qataadah: Hakubali Mwenyezi Mungu neno ila kwa kitendo.
5) Na katika sababu pia ni kuwafanyia wema na mazuri wazazi wawili. Lajulisha hilo kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiih yake kuwa: ‘Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu), alikuwa wamjiapo watu wa Yeman anawauliza je hapo kuna Uways bin ‘Aamir? Mpaka alipojiwa na Uways, akamwambia wewe ni Uways bin ‘Aamir, akasema ndio, unatoka Muraad kisha Qarn? Akasema ndio, akasema ulikuwa na mambalanga ukapoa isipokuwa sehemu kama mfano wa dirham? Akasema ndio, akasema una mama? Akasema ndio, akasema nimemsikia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
((Atawajia nyinyi Uways bin ‘Aamir pamoja na watu wa Yeman, kutoka Muraad kisha Qarn, yeye ana mambalanga akapozwa na Mwenyezi Mungu isipokuwa sehemu kama dirham, ana mama anamfanyia wema, lau atawaombea kwa Mwenyezi Mungu atapokelewa du’aa yake, ukiweza akuombee msamaha lifanye hilo.)) nikataka kuombewa msamaha akaniombea.
Na Hadiyth iliyokuja katika Swahiyh Muslim katika Hadiyth ya watu wa Jabalini waliotajwa zamani, walikuwa kuna katika wao wanaojikaribisha kwa Mwenyezi Mungu kwa wema wao wa wazazi wawili, ikawa ni sababu ya kujibiwa du’aa.
6) Katika sababu za kujibiwa du’aa ni kumuombea mtu ndugu yake kwa siri. Yajulisha hilo kupitia kwa Hadiyth iliyopokewa na Muslim katika Swahiyh yake kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Du’aa ya mtu kumuombea ndugu yake kwa siri inajibiwa kupitia kwa Malaaikah aliowakilishwa kuwa kila amuombeapo ndugu yake kwa wema, mazuri, anasema Malaika: “Aamiyn nawe upate mfano wake”.))
Hadityh ni nyengine ni ile iliyopokewa na Abu Daawuud katika Sunan yake: Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Hakika du’aa inayojibiwa kwa wepesi, haraka ni ile inayoombwa kumuombea mtu kwa siri.))
7) Na du’aa katika safari hairudishwi kama ilivyopokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Maombi matatu ni yenye kujibiwa, haina shaka ndani yake: Du’aa ya mwenye kudhulumiwa, du’aa ya msafiri na du’aa ya mzazi kwa mtoto wake.)) [Imepokewa na Al-Bukhaariy]
Imekuwa du’aa ya msafiri ni yenye kukubaliwa, kwa kule kupata mashaka safarini, taabu na upungufu wa kila kitu akifanyacho kumfanyia Mola wake Aliye na cheo Mwenye nguvu.
8) Kuamrisha mema na kukataza mabaya ni katika sababu za kujibiwa du’aa. Hili linathibitishwa kupitia Hadiyth ya Hudhayfah bin al-Yamaan kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Naapa kwa Yule nafsi yangu ipo mikononi mwake, mtaamrishana mema na kukatazana mabaya, ama atawaunganishia kwa kuwapa mfano wake Mwenyezi Mungu na kuwateremshia nyinyi adhabu itokayo Kwake, kisha mumuombe Yeye na asiwajibu du’aa zenu.)) [Imepokewa na at-Tirmidhiy na akaisahihisha Shaykh Al-Albaaniy]
Imepokewa na Ahmad na al-Bazzaar kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Enyi watu, hakika Mola Aliyetukuka Aliye juu Anawaambia nyinyi: Amrishaneni mema, na mukatazane mabaya kabla haijafikia kuniomba na nisiwajibu du’aa zenu, na mutake kwangu nisiwapatie, na mutake nusra kwangu nisiwanusuru.))
Amesema Ibnu Rajab katika Jaami’ul ‘Uluum Wal-Hikam “Hakika kufanya vitendo vilivyoharamishwa kwa kuendelea, kunazuia kujibiwa du’aa, na hivyo hivyo kuacha yaliyolazimishwa kama vile Hadiyth ilivyotuelekeza kuacha kuamrisha mema na kukataza mabaya ni sababu ya kuzuia kujibiwa du’aa, na yajulisha kufanya kila liloamrishwa inafanya du’aa kujibiwa.”
9) Na sababu ya kujibiwa du’aa ni kurudia Yaa Rabb, Yaa Rabb. Nalo ni jambo kubwa linalotakiwa katika du’aa. Amesema Yaziyd Ruqashiy kutoka kwa Anas: “Hakuna mja yoyote atakaesema: Yaa Rabb, Yaa Rabb, Yaa Rabb isipokuwa humwambia Mola wake nakuitikia, nakuitikia, nakuitikia.”
Imepokewa na Abu Dardaa na Ibnu ‘Abbaas kuwa wao wawili walikuwa wakisema: Jina kubwa la Mwenyezi Mungu Rabb, Rabb.
Kutoka kwa Atwaa amesema: “Hatosema mja Yaa Rabb, Yaa Rabb mara tatu, isipokuwa Mola humuangalia yeye, akasema je hamusomi Qur-aan? Kisha akasoma neno lake Mola Aliyetukuka:
{{Wale ambao wanamkumbuka kwa kumtaja Mwenyezi Mungu wakiwa wamesimama, wameketi, wamelala kwa ubavu na wanafikiria uumbaji wa mbingu na ardhi wakasema: Ee Mola wetu hukuumba hizi bure bure umetakasika tukinge na adhabu ya moto.}} Mpaka katika neno lake: {{Akawajibu wao Mola wao: Hakika Yangu Mimi sipotezi kitendo cha mtendaji kati yenu.}} [Al-‘Imraan: 191- 195]
Amesema Ibnu Rajab na mwenye kuzingatia du’aa zilizotajwa katika Qur-aan, atazikuta du’aa nyingi zimeanza kwa jina la Rabb kama neno lake:
{{Na katika wao wanaosema Mola wetu, tupe sisi katika dunia mema na Akhera mema na utukinge na adhabu ya moto.}} [Al-Baqarah: 201]
Na neno Lake:
{{Mola wetu usizigeuze kwa kuzipoteza nyoyo zetu baada ya kuziongoza, na tupe sisi rahmah itokayo Kwako, hakika Yako Wewe ni mwema kwa kutoa.}} [Al-‘Imraan: 8]
10) Na pia imepokewa na AbU Dunya katika kitabu cha Mujaabiyna Fiy Du’aa kutoka kwa Hasan amesema: “Alikuwa mtu katika Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Answaar amebandikwa jina la Aba Mu-uliq. Alikuwa mfanyabiashara kwa mali yake na wengine akienda nao safarini alikuwa akiinamisha kichwa kwa uchaji Mungu. Siku moja alitoka akakutana na mwizi aliyebeba silaha, akamwambia: Toa ulicho nacho, nitapigana na wewe, akamwambia kwanini waitaka damu yangu? Unalolitaka ni mali, akasema ama mali ni yangu sitaki ila damu yako, akamwambia ikiwa hilo ni lengo lako niwache niswali rakaa nne, akamwambia swali ikiwa huna budi kufanya hilo, akatawadha akaswali rakaa nne, akasema katika sijdah yake ya mwisho kwa kuomba: “Ee Mwenye mapenzi, Mwenye kiti cha enzi, Mtendaji kwa ulitakalo, nakuomba kwa cheo Chako kisichomalizika, na ufalme Wako usio na dhulma, na mwangaza wako uliojaa nguzo za ‘Arshi Yako, unikinge na shari ya mwizi huyu, ewe Msaidizi nisaidie, ewe Msaidizi nisaidie, akasema mara tatu, akatokea mpanda farasi amebeba silaha za vita ameziweka katika farasi wake, alipomuona mwizi alimuelekea akamchoma (akamdunga) na akamuua.
Kisha akamuendea akamwambia inuka. Akamuuliza wewe ni nani, hakika Ameniokoa Mwenyezi Mungu kwa njia yako leo. Akamwambia mimi ni Malaika wa mbingu ya nne uliomba kwa du’aa yako ikagonga mlango wa mbinguni kwa mshindo wake, kisha ukaomba mara ya pili ikasikika vilio vya watu wa mbinguni, kisha uka omba mara ya tatu, nikaambiwa du’aa ya mwenye dhiki. Nikamuomba Mwenyezi Mungu Anipe mimi uwezo wa kumuua. Amesema Hasan: “Mwenye kutawadha akasali rakaa nne na akaomba kwa du’aa hii atajibiwa du’aa yake, mwenye dhiki ama awe hana dhiki (shida).”
11) Na katika sababu za kujibiwa du’aa ni kuchunguza (kujua) wakati wa kujibiwa, na kuwa mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka na kuulinganisha moyo wako unapoomba du’aa - uwe moyo wako upo hapo.
Amesema Ibnu Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu cha Jawaabul-Kaafiy “Yatakapoungana mambo mawili kwa muombaji - kuuhudhurisha moyo wake na kupata wakati wa kujibiwa katika wakati sita nao; - thuluth ya mwisho ya usiku, na wakati kunapoadhiniwa, na baina ya adhaan na iqaamah, na mwisho wa kila Swalah tano za faradhi, na apandapo Imaam katika mimbari siku ya Ijumaa mpaka Swalah imalize kuswaliwa, na saa ya mwisho baada ya alaasiri siku ya Ijumaa, na ikapatikana unyenyekevu moyoni na kujiweka chini mbele ya Mola wake, na kuwa mnyonge, dhaifu, kujielekeza kwa Mola, na kuelekea Qiblah, na akawa ametawadha (yuko twahara), na akainua mikono yake kwa Mola wake, na akaanza kumshukuru Mola na kumsifu, kisha akafuatiliza kumswalia Muhammad mja Wake na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kisha akazitanguliza haja zake, kwa kutubia na kuomba msamaha, kisha akajilazimisha katika kuomba, kwa kujipendekeza kwa Mola wake, katika du’aa zake kwa kuwa na hima na hicho, kwa kuziunganisha kwa majina ya Mola, na sifa Zake, pamoja na kumpwekesha, na akawa du’aa zake anazifuatanisha na Swadaqah, hakika du’aa hii haitokuwa ni yenye kurudishwa kabisa.
Na rahmah na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad na aali zake na Maswahaba zake na amani.